• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mwalimu Magreth Komba azungumzia mambo ya elimu

    (GMT+08:00) 2009-04-10 17:38:45

    Bi. Magreth Komba ni mzaliwa wa Tanzania katika mkoa wa Ruvuma ambao uko kusini mwa Tanzania. Alisomea masomo yake ya ualimu katika chuo kikuu cha Mpwapwa. Baadaye akahamia chuo cha ualimu cha Dar es Salaam kwa mafunzo ya diploma, kwa hiyo alipata stashahada nzuri ya kumwezesha kuwa mkufunzi wa chuo cha ualimu na shule ya sekondari. Baada ya hapo, alipata kazi ya kufundisha walimu wa daraja la kwanza ambao ni walimu wanaojiandaa kufundisha watoto wa shule ya msingi. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo aliweza kuhitimu shahada yake ya kwanza ya ualimu ya masomo ya arts, kwa hiyo baada ya hapo alikwenda kufundisha Chuo cha ualimu cha Dar ambacho kwa wakati ule kilikuwa kinaitwa Chang'ombe TTC. Aliwafundisha kwa muda wanafunzi ambao watakuwa walimu wa sekondari. Baada ya kufundisha akaweza kuendelea na masomo ambapo aliweza kusoma shahada ya pili. Baadae alipata udhamini wa masomo na kuja kusoma udaktari wa ualimu na mitaala. Alifika hapa Beijing tarehe 5 Septemba mwaka 2007, na ameshakaa hapa mwaka mmoja na miezi saba sasa.

    Ingawa Bi. Komba yupo chuoni sasa, lakini ana uzoefu wa kufundisha wa miaka kumi, alipotuelezea kwa ufupi historia yake ya kufundisha alisema,

    "Kwanza kabisa, niliwahi kufundisha wale watoto wadogo kabisa wa chekechea, lakini nilifundisha kwa muda mfupi sana, muda kama wa miezi mbili tu. Nilikuwa nafanya mazoezi ya kufundisha, kwa hiyo nilifundisha katika shule moja ya ya Kibangu ya Kimataifa iko Dar es Salaam, Tanzania. Baadae niliajiriwa kufundisha Chuo cha ualimu cha Ifunda kilichoko mkoani Iringa. Katika Chuo hicho cha ualimu wakati ule kinatoa walimu wale wa daraja la tatu niliweza kuwafundisha mbinu za kufundishia na mitaala katika elimu na pia niliwafundisha maeneo ya utafiti, upimaji na tathmini. Na pia niliweza kufundisha somo la uraia. Niliwahi pia kufundisha shule ya sekondari ya wazazi ya Tegeta katika mkoa wa Dar es Salaam. Baada ya hapo nilifundisha chuo cha ualimu cha Dar es Salaam kinachotoa mafunzo ya stashahada ambapo nilifundisha masomo ya upimaji na tathmini pamoja na uraia."

    Mwalimu Komba anaipenda sana kazi yake ya kufundisha sana, ambapo kazi hii pia imemletea mafanikio mengi na fuaraha nyingi.

    "Kwanza kabisa, ni ile raha ninayojisikia mwenyewe moyoni mwangu kwamba nimeweza kuwafundisha watu, na sasa hivi nao wamepata kazi zao, wanajitegemea na wengine wanaweza kuwa na familia. Pia nina furaha kwani baadhi ya wanafunzi wangu wameenda kusoma vyuo vikuu, wengine walienda kufanya kazi katika sehemu mbalimbali nchini kwetu. Baadhi yao wachache wameweza kusoma katika nchi za nje. Na hiyo inanipa furaha sana, kwa sababu mimi nimeweza kuchangia katika maisha yao ya kujitegemea. Kwa hivyo hiyo inanipa moyo kwa sababu lengo ni kujenga taifa letu la Tanzania, kwa hiyo naweza kufanya kazi ambayo matunda yake nayaona."

    Lakini katika ufundishaji wake alikumbwa na matatizo mengi, anaona masuala mengi ya elimu yanapaswa kutatuliwa nchini Tanzania.

    "Vifaa vya kufundishia ni tatizo, labda uwezo wa serikali yetu wa kuandaa vifaa sio mkubwa, kwa hiyo kuna ukosefu wa vifaa. Inakuwa ngumu hasa kutumia njia au mbinu nzuri za kufundishia kwa sababu mtu hawezi kufundisha wanafunzi labda mia moja kwa kutumia vitabu vinane. Vifaa vya kufundishia siyo vitabu tu, kuna vitu vingi. Lakini sisi hatuna maabara mzuri, hatuna chumba cha kijiografia. Na pia kuna tatizo la usafiri, hasa kwa shule zile za kutwa kwamba wanafunzi wanaenda shule na kurudi nyumbani. Nchi yetu haina magari mengi sana, kwa hiyo wanafunzi wetu wanapata shida katika usafiri."


    1 2
    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako