• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kuanzisha shughuli barani Afrika ili kampuni zijiendeleze kwa kasi

    (GMT+08:00) 2009-05-01 20:54:14

    Kadri msukosuko wa fedha wa dunia ulioanzia nchini Marekani unavyozidi kuwa mbaya, ndivyo athari yake inavyozidi kuwa kubwa katika sehemu nyingi na mambo mengi duniani. Katika msukosuko huo uchumi wa China hauwezi kuepuka na athari hizo hasa katika sekta ya uuzaji bidhaa nje. Ingawa kampuni zote zinakabiliwa na hali mbaya ya uchumi, lakini baadhi yao ziliendelea kupata faida kubwa. Hivi karibuni mwandishi wa habari alitembelea kampuni ya Sunda ya Guangzhou inayojiendeleza vizuri.

    Asubuhi na mapema, meneja mkuu wa kampuni ya Sunda ya Guangzhou Bw. Shen Yanchang alipokea simu ya ripoti ya kazi iliyopigiwa na mkuu wa tawi la kampuni hiyo la Tanzania. Mkuu huyo alisema katika simu hiyo kuwa, tawi jipya la mkoa wa Arusha lililoanzishwa mwezi Septemba mwaka jana linaendeshwa vizuri, na tawi la mkoa wa Dar es Salaam pia linaendelezwa haraka, hivyo thamani ya uuzaji bidhaa ya mwaka 2008 ya kampuni ya Sunda huko Tanzania inatarajia kuongezeka kwa kiasi kikubwa hadi dola za kimarekani milioni 15 kutoka milioni 8 ya mwaka 2007.

    Kampuni ya Sunda ya Guangzhou ilianzishwa mwaka 2000, na ni kampuni inayoshughulikia kuuza vyombo vya kaure, vifaa vya ujenzi, vifaa vya bafuni, vifaa vya elektroniki na bidhaa za viwanda vidogo za matumizi ya kila siku. Hivi sasa, kampuni hiyo imejenga matawi sita katika nchi za nje, na matano kati yao yako barani Afrika. Bw. Shen alisema, sababu kubwa ya kampuni ya Sunda kupata mafanikio ya leo ni kuanzisha shughuli barani Afrika.

    Bw. Shen mwenye umri wa miaka 35 alipohitimu masomo yake kutoka chuo kikuu mwaka 1997 alikwenda kufanya kazi katika kampuni ya Hongkong nchini Nigeria. Wakati ule, wachina wengi hawakujua hali ya Afrika, na wachina waliokwenda kufanya kazi barani Afrika walikuwa ni wachache sana. Bw. Shen alipata matumaini ya kufanya biashara katika kazi ya miaka miwili barani Afrika. Alisema,

    "Niliwahi kuishi nchini Nigeria kwa miaka miwili, naliona ukosefu wao wa vitu. Kama bidhaa zilizotoka China zinaweza kukidhi mahitaji ya soko hazitakumbwa na shinikizo la uuzaji."

    Mwaka 1999 Bw. Shen aliyepata uzoefu wa kazi na uhusiano na wateja alijiuzulu kutoka kampuni hiyo ya Hongkong, na kurudi nchini China kufanya maandalizi ya kuanzisha kampuni yake binafusi. Mwezi Aprili mwaka 2000, Kampuni ya Sunda ya Guangzhou ilianzishwa, na Bw. Shen aliweka mwelekeo thabiti wa biashara katika nchi za Afrika. Kwa wakati ule jamaa na marafiki zake hawakuweza kumkubalia, kwa sababu waliona kuwa soko la nchi za Ulaya na Marekani lilikuwa na fursa nyingi zaidi kuliko soko la Afrika lisilopevuka. Pia waliona kuwa kufanya biashara katika nchi za Afrika hakutakuwa na mustakabali mzuri. Lakini takwimu za baadaye za mfululizo zimethibitisha kuwa uamuzi wa Bw. Shen ni sawa. Alisema,

    "Thamani ya uuzaji bidhaa ya kampuni yetu kwa mwaka 2004 ilikuwa dola za kimarekani milioni 5.3, na mwaka 2005 iliongezeka hadi dola za kimarekani milioni 11, mwaka 2006 iliongezeka hadi dola za kimarekani milioni 27, mwaka 2007 iliongezeka hadi dola za kimarekani milioni 44, na mwaka huu inatazamiwa kuwa dola za kimarekani milioni 80 hivi."

    Bw. Shen anaona kuwa sababu kuu ya mafanikio ya kampuni yake ni kuchagua soko linalofaa na kuthubutu kupanua soko lake barani Afrika linalodhaniwa kuwa sio zuri. Maoni yake ni kwamba, ingawa soko la nchi za magharibi limepevuka, lakini ni soko linalochaguliwa na wafanya biashara wengi ambapo mashindano ya biashara yatakuwa makali sana. Na soko lisilopevuka lina uwezo mkubwa zaidi.

    "Kusema kweli, soko la Afrika lina uwezo mkubwa, kwa sababu msingi wake wa uchumi zamani ulikuwa mdogo. Miaka ya hivi karibuni uchumi wa dunia umeendelea kwa haraka hasa nchi zinazoendelea, na hali ya usalama wa jamii na siasa inaelekea kuwa ya utulivu. Mazingira hayo ya uchumi, siasa na maisha yanafaa kwa kampuni zetu kuanzisha shughuli na kujenga mtandao wetu wa uuzaji bidhaa katika nchi za nje."

    Licha ya uchaguzi wa soko, Bw. Shen anaona kuwa urafiki wa jadi kati ya China na nchi za Afrika pia ni sababu muhimu ya mafanikio ya kampuni yake. Alisema,

    "Urafiki wa jadi kati ya China na nchi za Afrika umeweka msingi mzuri kwa kampuni zetu kuanzisha shughuli barani Afrika. Tunaweza kusema kwamba sisi tunanufaika na juhudi za watangulizi. Kampuni zetu zinaendeshwa kwa kufuata sheria za huko, na wenyeji wa huko wanatutendea kirafiki sana sisi wachina. Nchi nyingi za Afrika zilitawaliwa kikoloni na nchi za magharibi, na historia hiyo haiwezi kusahaulika. Lakini waafrika wanaweza kukumbuka zaidi urafiki wa jadi kati ya China na nchi za Afrika. Kwa hiyo katika mambo yote barani Afrika, tunaweza kuona urafiki wa waafrika, na wenyeji wa huko wanatuheshimu sana."

    Bw. Shen alisema kuanzisha shughuli barani Afrika ni lazima kuiheshimu na kuichangia Afrika. Afrika inatoa jukwaa kubwa la kujiendeleza kwa kampuni ya Sunda, na njia ya kampuni hiyo ya kutoa mchango wake kwa Afrika ni kuifanya kampuni iwe ya huko. Hayo ni mahitaji ya mendeleo ya kampuni, na pia ni mchango wa kampuni hiyo wa kuchangia kuongeza nafasi za ajira na kuwaandaa wafanya biashara wa huko. Alisema,

    "Kwa kawaida tunatuma wasimamizi watatu au wanne katika nchi za nje, na wafanyakazi wengine wote wanaajiriwa huko. Tawi moja lina wasimamizi wanne na wafanyakazi 40 wa huko. Sisi tunafuata kanuni ya kuwatendea wafanyakazi wa huko kwa usawa, na tunawaelekeza na kuwafundisha katika kazi hata katika maisha. Tunaishi vizuri pamoja na wafanyakazi wa huko."

    Kampuni ya Sunda pia imeweka utaratibu wa kuwaleta wafanyakazi wa nchi za nje kupata mafunzo nchini China. Na kwa wafanyakazi wazuri wa huko wa tawi la nchi za nje, kampuni inawaandalia mafunzo ya mwezi mmoja nchini China. Na katika mafunzo hayo, wafanyakazi wanapata fursa ya kutalii nchini China na kujionea maendeleo na utamaduni wa China.

    Safari moja ya kuomba viza katika miaka kadhaa iliyopita inakumbukwa na Bw. Shen mpaka sasa. Ofisa mmoja wa Tanzania aliyeshughulikia viza alimwambia kuwa kampuni yake inakwenda kuwekeza na kutoa nafasi za ajira nchini Tanzania, sio tu inasaidia kuongeza nafasi za ajira, bali pia itasaidia kuboresha maisha ya wafanyakazi wa huko. Hivyo kila atakapowaajiri watu 40, inamaanisha analisha familia 40 hivi, huu ndio mchango mkubwa sana.

    Bw. Shen alimhadithia kila mfanyakazi wa kampuni ya Sunda kuhusu jambo hilo na anataka kila mmoja aweze kujua kwamba wanapofanya biashara wanabeba wajibu mkubwa. Kwa kufuata maendeleo ya shughuli za nchi za nje, kampuni hiyo inaweza kutoa nafasi nyingi zaidi za ajira kwa wakazi wa huko.

    Ingawa Kampuni ya Sunda ya Guangzhou imepata faida kubwa mwaka huu, lakini Bw. Shen Yanchang anakiri kwamba msukosuko wa fedha unaoikumba dunia hakika utaathiri uchumi wa nchi za Afrika na uuzaji bidhaa wa kampuni, lakini hatarudi nyuma katika juhudi za kutafuta fursa ya kujiendeleza barani Afrika. Alisema,

    "Kwa wakati huu tutafanya juhudi za kuimarisha usimamizi wa ndani ya Kampuni. Na muskosuko wa fedha wa dunia utakaposhuka hadi kiwango cha chini kabisa, tutaendelea kwenda nchi za nje, na kutumia fursa nzuri ili kuharakisha maendeleo ya kampuni yetu. Tutaendelea kupanua soko letu barani Afrika, tunataka kuanzisha shughuli zetu miaka miwili ijayo katika nchi nyingine nyingi za Afrika zikiwemo Cote d'Ivoire na Cameroon."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako