• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Shakespeare wa nchi za mashariki" Guan Hanqing

    (GMT+08:00) 2009-05-01 18:30:56

    Mwandishi mkubwa wa michezo ya kuigiza katika zama za kale nchini China Bw. Guan Hanqing anasifiwa kama ni "Shakespeare wa nchi za mashariki".

    Zama alipoishi Bw. Guan Hanqing zilikuwa mbele kwa miaka 300 kuliko miaka ya Shakespeare,Guan Hanqing ni mwanzilishi wa aina moja ya mchezo wa kuigiza iitwayo Yuanqu ambayo ilistawi sana katika Enzi ya Yuan miaka zaidi ya 700 iliyopita nchini China. Yuanqu ilichanganya mashairi, nyimbo na misemo vilivyoenea miongoni mwa watu, ni tamthilia iliyopendwa sana kutokana na mtindo wake wenye vichekesho na kumithilisha hali ya jamii. Yuanqu inachukua nafasi muhimu katika hisotria ya fasihi ya China.

    Ustawi wa michezo ya kuigiza ya Yuanqu ni matokeo ya kuanzishwa kwa Enzi ya Yuan katika karne 13 na utaratibu wa kugawa watu kwa matabaka katika enzi hiyo. Kabla ya enzi hiyo wasomi walikuwa wanaweza kupata nyadhifa kwa kupitia mitihani ya kifalme, lakini katika Enzi ya Yuan utaratibu huo ulifutwa, wasomi walikuwa wakidhalilishwa hadi kwenye ngazi ya tisa ambayo ni ya mwisho katika jamii. Kutokana na hali hiyo, wasomi wengi walikuwa hawana budi kuwasiliana na watu walioshughulika na michezo ya kuigiza ambao walikuwa kwenye ngazi moja na kuwaandikia tamthilia ili kujipatia riziki. Kwa sababu ya wasomi hao kujiunga na watu wenye shughuli za michezo ya kuigiza, Yuanqu ilipata ustawi, na Guan Hanqing alikuwa mmoja wa wasomi hao.

    Bw. Guan Hanqing alikulia katika mji wa Dadu ambao ulikuwa mji mkuu wa Enzi ya Yuan. Hapo awali alikuwa daktari wa hospitali ya kifalme, lakini shauku yake juu ya michezo ya kuigiza aina ya Yuanqu ilikuwa kubwa kuliko kazi yake ya kutibu. Wakati huo wananchi waliishi maisha mabaya sana kutokana na utawala mbovu, msukosuko wa jamii na uonevu. Bw. Guan Hanqing kwa kutumia michezo ya kuigiza alifichua giza lililogubika jamii nzima na kueleza matumaini yake mema, mwishowe akawa mwandishi mkubwa wa michezo ya kuigiza aina ya Yuanqu.

    Bw. Guan Hanqing ni mtu mwenye akili nyepesi na ucheshi, elimu yake ni pana, yeye ni mtu mwenye huruma na kutetea haki. Tamthilia yake licha ya kulilia haki pia inahamasisha mapambano dhidi ya uonevu. Katika wimbo mmoja alijieleza hivi, kwamba yeye ni njegere ngumu ya shaba ambayo haiwezi kuwa laini kwa mvuke, haiwezi kuiva kwa kuchemshwa, haiwezi kuwa bapa kwa kugongwa na haiwezi kupasuka kwa kukaangwa. Bw. Guan Hanqing pia alikuwa hodari kwa kupiga muziki, kuimba mashairi, kucheza ngoma na kuwinda, na mara nyingi alisaidia waigizaji namna ya kuigiza na aliwahi kushiriki maonesho. Katika tamthilia yake, wahusika wenye tabia na hadhi tofauti waliigizwa tofauti kwa maneno na vitendo.

    Katika miongo kadhaa Bw. Guan Hanqing aliandika tamthilia zaidi ya 60, na kati ya tamthilia hizo, 18 zinaendelea mpaka leo ambazo ama kwa idadi au kwa sifa, zote zilizishinda zile za waandishi wengine wa Enzi ya Yuan. Mbali ya michezo ya kuigiza ya aina ya Yuanqu Bw. Guan Hanqing pia alitunga nyimbo nyingi. Maandishi ya Guan Hanqing yamechangia sana hadithi zilizosimuliwa kwa kuimba miongoni mwa watu, na watu ambao si matajiri au maskini wote walipenda.

    Maandishi ya michezo ya kuigiza ya Bw. Guan Hanqing yametafsiriwa katika lugha nyingi za Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kijapani, amepata heshima kubwa katika historia ya fasihi na sanaa duniani na kusifiwa kuwa ni "Shakespeare wa nchi za Mashariki".

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako