• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mchoraji mkubwa wa China Bw. Wu Guanzhong

    (GMT+08:00) 2009-05-20 20:50:20

    Hivi karibuni majumba matatu ya sanaa ya uchoraji ya Beijing, Shanghai na Singapore kwa ushirikiano yalifanya maonesho ya picha zilizochorwa na mchoraji mkubwa wa China Bw. Wu Guanzhong, picha hizo ni zawadi aliyoitoa kwa ajili ya majumba hayo. Mzee Wu Guanzhong amekuwa na umri wa miaka 90, ni mchoraji aliyechangia sana maendeleo ya uchoraji wa picha nchini China.

    Maonesho hayo yanayojulikana kwa jina la "Kupalilia na Kuchangia" yalianza mwishoni mwa Februari mjini Beijing. Maonesho hayo licha ya kuonesha picha zaidi ya 180 alizochora Bw. Wu Guanzhong, pia yanaoneshwa maandishi husika na picha za video ambazo kwa pande zote zimeonesha jinsi mzee huyo alivyopalilia sanaa yake kwa miaka zaidi ya 70. Naibu mkuu wa Jumba la Sanaa la Beijing Bw. Qian Linxiang alisema,

      "Bw. Wu Guanzhong anaithamini sanaa ya uchoraji kama uhai wake, katika miongo kadhaa iliyopita popote alipokuwa hakuwahi kuacha kuendeleza sanaa yake ya uchoraji. Mzee Wu Guanzhong ni mchoraji anayeheshimika sana katika karne ya 20 na ametoa mchango mkubwa katika kuunganisha uchoraji wa mtindo wa Kichina na wa Kimagharibi."

    Bw. Wu Guanzhong alizaliwa mwaka 1919 katika familia ya wakulima. Alianza kujifunza sanaa alipokuwa na umri wa miaka 18, na alipokuwa na miaka 23 alihitimu Shule ya Sanaa mjini Hangzhou nchini China. Mwaka 1946 alipelekwa na serikali nchini Ufaransa kuendelea na masomo yake, mwaka 1947 akajiunga na Chuo Kikuu cha Sanaa ya uchoraji cha Paris akifundishwa na Profesa Jean Souverbie uchoraji wa picha za rangi. Bw. Wu Guanzhong alipozungumza na waandishi wa habari wa televisheni alisema,

      "Profesa huyo aliniambia kwamba kuna njia mbili katika sanaa, moja ni njia finyu, sanaa inayofuata njia hiyo inafurahisha macho tu, njia nyingine ni pana, sanaa inayofuata njia hiyo inatetemesha sana moyo. Kwa hiyo nimechagua njia pana."

      Baada ya kuhitumu Bw. Wu Guanzhong angeweza kubaki nchini Ufaransa kwa sababu ya kiwango chake cha uchoraji, lakini baadaye alighairi. Mwaka 1950 Bw. Wu Guanzhong alirudi nyumbani China.

      Katika miaka mitatu ya masomo alipokuwa huko Ufaransa alipata roho ya uchoraji wa picha za Ulaya, na kutokana na utafiti wa utamaduni wa jadi wa China amepata kiini cha uchoraji wa picha za Kichina. Bw. Wu Guanzhong alijaribu kuunganisha mitindo ya aina mbili aliyopata katika uchoraji wake.

      Bw. Wu Guanzhong aliwahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Sanaa ya uchoraji cha China, kitivo cha ujenzi cha Chuo Kikuu cha Qinghua, Chuo Kikuu cha Sanaa cha Beijing na Chuo Kikuu cha Sanaa ya Mikono nchini China. Mwaka 1970, kutokana na athari ya mazingira ya jamii ya wakati huo nchini China, alilazimishwa kufanya kazi za kilimo vijijini. Katika muda wa miaka mitatu vijijini alikuwa anaendelea na sanaa yake ya uchoraji, alichora picha nyingi zilizoonesha maisha ya wakulima.

      Mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, utamaduni nchini China ulianza kufufuka, Bw. Wu Guanzhong alipata kipindi chake kizuri cha kuendeleza uchoraji wake. Kutokana na ujasiri alichora picha nyingi ambazo ni tofauti na mtindo wa Kimagharibi na mtindo wa Kichina.

      Mwaka 1991 Wizara ya Utamaduni ya Ufaransa ilimteua kuwa "msanii mwenye heshima kubwa wa Ufaransa". Mwaka 1992 Jumba la Makumbusho la Uingereza lilifanya maonesho kwa jina la "Bw. Wu Guanzhong----Mchoraji Mkubwa wa China katika Karne ya 20". Hii ni mara ya kwanza kwa jumba hilo kufanya maonesho kwa ajili ya mchoraji wa China. Mwaka 2000 Bw. Wu Guanzhong alichaguliwa kuwa msanii wa Chuo cha Sanaa cha Ufaransa, hivyo amekuwa mchoraji wa kwanza kabisa wa China kupata heshima hiyo na pia ni msanii wa kwanza kabisa wa Asia katika miaka karibu 200 tokea chuo hicho kianzishwe.

      Picha alizochora Bw. Wu Guanzhong zina thamani kubwa katika soko la kimataifa, lakini Wu Guanzhong alisema picha zilizouzwa hajihusishi nazo, na picha ambazo anaridhika nazo zote amezawadia majumba ya sanaa ya uchoraji ya kiserikali. Bw. Wu Guanzhong alipoulizwa na waandishi wa habari namna ya kudumisha juhudi za uchoraji, alisema,

      "Kwanza, kutoogopa hali ya umaskini, kimaisha usiwe na tamaa, na ni lazima kutoa moyo wote kwenye sanaa ya uchoraji."

      Mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, Bw. Wu Guanzhong aliandika makala moja akisema "Kama ukiiga uchoraji wa kale, hutakuwa na maendeleo". Makala hiyo ilisababisha malumbano makali katika nyanja ya wachoraji. Miaka mingi imepita sasa, Bw. Wu Guanzhong anaendelea na msimamo huo. Alisema,

      "Hakuna namna maalumu za kuonesha hisia. Mradi tu unaweza kuonesha hisia zako basi namna zote ni sawa, kinyume chake ukiiga tu wengine namna ya kuonesha hisia bila ya hisia zako mwenyewe ni sawa na kusema uwongo, na picha zako ni sawa na sifuri !"

      Katika maonesho hayo, pembeni mwa picha moja yaliandikwa maneno yasemayo, "Picha ni lugha ya kimataifa, haziwezi kuonesha uwongo, hisia za kweli au za uwongo picha yenyewe inaonekana wazi."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako