• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Sikukuu ya Duanwu ya jadi ya Wachina

    (GMT+08:00) 2009-06-01 16:41:50

    Bw. Quyuan

    Tarehe 28 Mei ambayo kwa kalenda ya kilimo ya China ni tarehe 5 ya mwezi wa 5 ni sikukuu ya Duanwu, hii ilikuwa siku ya Wachina ya kumkumbuka Qu Yuan ambaye ni mshairi mzalendo wa China katika zama za kale. Katika siku hiyo Wachina wana desturi ya kufanya mashindano ya mbio za mashua zilizochongwa kwa sura ya dragoni, kuvaa shingoni mifuko midogo iliyotiwa dawa za mitishamba inayonukia na kula Zongzi, chakula ambacho kinapikwa kwa mchele uliofungwa kwa majani ya matete. Siku ya Duanwu imekuwa siku ya mapumziko kitaifa.

      Hapo awali sikukuu hiyo ilianza kwa ajili ya kumkumbuka mshairi mzalendo aliyejiua kwa kujitupa ndani ya mto miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita. Wakati huo nchini China kulikuwa na madola mengi madogo yaliyokuwa yakipigana vita kwa miaka mingi kwa ajili ya kugombea utawala wa China nzima. Dola la Chu iliyokuwa karibu na Mto Changjiang na kupakana na Dola la Qin upande wa kaskazini magharibi ilikuwa ni moja kati ya madola hayo, wakati huo madola hayo mawili yalikuwa yakipambana. Mshairi Qu Yuan aliyetoka ukoo wa heshima alikuwa ni mtu wa Dola la Chu. Ili kuimarisha dola lake na kulishinda Dola la Qin alimsaidia mfalme wake kwa kumpa ushauri, lakini ushauri wake ulipingwa na maofisa wahafidhina. Maofisa hao walimtweza na kumsengenya mshairi huyo mbele ya mfalme, matokeo yake mfalme alimpuuza. Qu Yuan aliyekuwa na moyo wa kuliokoa taifa na wananchi wenzake alipuuzwa na kutoaminika badala ya kuthaminiwa, kutokana na uonevu huo alishindwa kuvumilia hasira zake, akaandika mashairi mengi kueleza moyo wake wa kulitumikia taifa.

      Baadaye Qu Yuan alifukuzwa na mfalme na kupelekwa sehemu ya mbali ya Mto Miluo mkoani Hunan kwa hivi leo, huko aliheshimiwa na kupendwa sana na wenyeji. Muda si mrefu baadaye Qu Yuan alipata habari kwamba mji mkuu wa dola lake ulikaliwa na jeshi la Qin, dola lake liliangamizwa. Kutokana na hasira na huzuni Qu Yuan alijitupa ndani ya Mto Miluo, siku hiyo ilikuwa ni tarehe 5 ya mwezi wa 5 mwaka 278 K.K kwa kalenda ya kilimo ya China.


    1 2 3
    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako