• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mwimbaji mashuhuri wa opera wa China Bi. Zhang Liping

    (GMT+08:00) 2009-06-08 16:56:31

    Hivi sasa mwimbaji mashuhuri wa China Bi. Zhang Liping anajitokeza mara kwa mara kwenye jukwaa la kimataifa la opera.

    Opera ya "Tosca" ni tungo muhimu ya mwanaopera mkubwa Puccini, ambayo inaeleza hadithi inayohusu mapenzi, siasa, chuki na hila. Opera hiyo inavutia kiasi kwamba imeoneshwa katika muda wa zaidi ya miaka mia moja, na bado watazamaji hawapungui. Opera inaeleza hadithi ya ajabu ambapo mwanamke wa kawaida Tosca anasababisha vifo vya watu watatu. Waimbaji huona fahari kama wakiweza kuigiza mhusika mkuu wa opera hiyo Tosca. Zhang Liping kwa kutegemea uzoefu alioupata jukwaaani katika miaka mingi, alifuzu kuigiza mhusika huyo kama alivyotarajia. Alisema,

    "Nimejiandaa kuigiza mhusika mkuu wa opera hiyo Tosca kwa miaka mingi, nina uelewa wangu kuhusu mhusika huyo. Mimi ni Mchina, na Tosca ni mwanamke wa Italia wa miaka zaidi ya mia moja iliyopita. Pengine utasema wanawake wa hivi leo na wa miaka mia moja iliyopita wana mitazamo tofauti kuhusu mapenzi, lakini mimi naona hawatofautiani, wote huwa wakatili wakinyanyaswa kimapenzi. Tosca ni mwanamke katili ndio maana alifanya kitendo cha ukatili. Hii ina mafunzo kwa jamii ya hivi leo."

    Kabla ya hapo Bi. Zhang Liping aliwahi kualikwa na majumba mengi ya opera kuigiza mhusika Tosca kwenye maonesho ya opera, lakini alikataa kwa sababu aliona kuwa hajajiandaa vizuri kuigiza mhusika huyo. Mwimbaji anayeigiza mhusika Tosca kwenye maonesho ya opera anatakiwa pale anapoanza kuimba tu hali ya kusikitisha ya opera hiyo itawale muda wote wa maonesho, sauti yake lazima iwe na nguvu ya kutosha na idhibitiwe vizuri.

    Bi. Zhang Liping alijikita sana katika maonesho yake ya uigizaji na uimbaji, ambao ulijaa hisia, uhakika na utulivu, alisema alijihisi kama mtu aliyekufa. Anaona kwamba mvuto wa opera hiyo ni muunganisho kamili wa opera yenyewe na muziki wake ambao umeonesha wazi jinsi kabwela alivyonyanyaswa. Bi. Zhang Liping anaona kwamba Tosca ni mwanamke wa kawaida kabisa kama wanawake wengine wengi.

    Bi. Zhang Liping ambaye aliwahi kuimba opera zaidi ya 20, alisafiri sehemu mbalimbali duniani, kila alipofika alisifiwa na watu kwa uimbaji wake. Kutokana na uhodari wake alialikwa kuwa profesa na kuwa mkurugenzi wa somo la uimbaji katika Chuo Kikuu cha Muziki cha China.

    Bi. Zhang Liping ni mwimbaji wa kwanza wa China na pia ni mwimbaji pekee muhimu aliyewahi kuingia katika jumba la ngazi ya juu kabisa la opera duniani, Royal Opera House nchini Uingereza. Katika jumba hilo aliwahi kuwa mwimbaji muhimu katika opera za "Turandot", "Madam Butterfly" na nyinginezo. Bi. Zhang Liping alizaliwa miaka 40 iliyopita mkoani Hubei. Alipokuwa mtoto alipenda sana kuimba, kutokana na kuathiriwa na baba yake ambaye pia alipenda opera ya kibeijing. Alisema,

    "Nilipokuwa mtoto baba yangu mara kwa mara alinichukua kwenda kutizama opera za kibeijing, lakini kilichonivutia zaidi ni jinsi waigizaji walivyoimba."

    Bi. Zhang Liping alitizama opera ya kimagharibi kwa mara ya kwanza alipokuwa na umri wa miaka zaidi ya kumi, opera hiyo inaitwa "Madam Butterfly", ingawa hakuhafahamu maneno yaliyoimbwa, alivutiwa na mazingira ya opera hiyo hata alitokwa na machozi. Tokea hapo alianza kupenda opera. Bi. Zhang Liping alihitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Muziki cha China mwaka 1989, mwaka 1990 aliendelea na masomo yake katika Chuo Kikuu cha Muziki cha Vancouver nchini Canada, na mwaka 1992 alipata sifa ya msanii. Baada ya kuhitimu masomo katika chuo kikuu hicho alishiriki kwenye mtihani wa jumba moja la opera nchini Canada na kufaulu mtihani huo, tokea hapo akaanza kuonekana katika jukwaa la kimataifa.

    Mwaka 2004 kwa mara ya kwanza alialikwa na Jumba la Opera la Marekani, The Metropolitan Opera, kuigiza Bibi Cio Cio San, ambaye ni mhusika muhimu katika opera ya Madam Butterfly. Opera hiyo ilitungwa na mwanaopera mkubwa wa Italia Bw. Puccini, mhusika mkuu wa opera hiyo ni msichana Cio Cio San wa Japan ambaye aliacha imani yake ya dini na kuolewa na mwanajeshi wa Marekani, lakini muda si mrefu baadaye mwanajeshi huyo alioa mwanamke mwingine. Kutokana na hasira na huzuni Cio Cio San aliamua kujiua. Mwaka 1904 opera hiyo ilioneshwa kwa mara ya kwanza huko Milan nchini Italia na mara ikaanza kuoneshwa katika majumba mbalimbali ya opera duniani. Mhusika Cio Cio San aliwahi kuigizwa na waimbaji wengi, lakini Bi. Zhang Liping aliiga vingine kutokana na uelewa wake wa ndani, sauti yake iligusa hisia za watazamaji kwa kueleza vilivyo hisia za bibi huyo. Watazamaji wa nchi za magharibi wanamwita Zhang Liping kuwa ni "Madam Buterfly". Bi. Zhang Liping alisema,

    "Kinachogusa hisia za watazamaji sio ustadi wa kuimba bali ni muziki, watazamaji wanaweza kuhisi kama unaimba kwa ustadi au kwa moyo."

    Bi. Zhang Liping anaimba opera katika nchi tofauti na kuigiza wahusika tofauti kwa kushirikiana na wasanii wa mataifa tofauti, kwa hiyo changamoto kubwa kwake ni upweke, kila afikapo jukwaani watu wote pembezoni mwake huwa ni wageni kwake, hivyo namna ya kushirikiana nao na namna ya kuigiza vizuri ni tatizo ambalo anatakiwa kulitatua ili kuwaridhisha watazamaji. Alisema,

    "Nimeimba opera kwa zaidi ya miaka 20, napenda kuimba opera, naithamini opera kama ninavyothamini uhai wangu."

    Kila mwaka Bi. Zhang Liping anaimba katika nchi za nje kwa zaidi ya nusu mwaka, anapanda ndege wakati wa usiku na anapoamka huwa hafahamu aliko. Kila anapoondoka nyumbani anakuwa na masikitiko kumwacha mtoto wake mwenye umri wa miaka tisa. Lakini anaona faraja kwamba mtoto wake anamwelewa. Mtoto wake alisema, ingawa hayuko na mama yake lakini anapata matunzo mazuri kutoka kwa baba na bibi yake. Asipokuwa na shughuli za maonesho Bi. Zhang Liping huwa anawafundisha waimbaji katika chuo kikuu au kueneza elimu ya opera ya magharibi nchini China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako