• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 0616

    (GMT+08:00) 2009-06-16 16:44:13

    Baada ya kuanzishwa kipindi cha chemsha bongo kuhusu maadhimisho ya miaka 45 tangu Jamhuri ya watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zianzishe uhusiano wa kibalozi, tumepata barua kutoka kwa wasikilizaji wetu ambao wanasifu chemsha bongo hii.

    Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah Alghassani P.O. BOX 52483 DUBAI

    United Arab Emirates ametuletea barua akisema, ni matumaini yangu makubwa kwamba nyote hamjambo na mnaendelea na kuchapa kazi hapo Radio China Kimataifa Idhaa ya Kiswahili. Ingawa ni muda mrefu umepita bila kuwa na mawasiliano nanyi, lakini hali hiyo haikumaanisha kuwa urafiki wetu wa muda mrefu kati yangu nanyi umevunjika la hasha !!!

    Leo ningependa kutoa pongezi zangu za dhati kwa Idhaa ya Kiswahili ya CRI kwa kuandaa shindano kabambe la Chemsha Bongo kwa mwaka huu wa 2009 ambalo linaambatana na maadhimisho ya miaka 45 ya uhusiano kati ya China na nchi yangu ya Tanzania.

    Kwa kweli kuandaa Chemsha Bongo yenye kumbukumbu kama hiyo ya urafiki kati ya China na Mataifa yetu ya Afrika kwa maoni yangu kunasaidia sana kuboresha hali ya udugu baina ya pande mbili , pamoja na kujenga nguzo imara za kuendeleza mahusiano na udugu baina ya Wachina na Waafrika.

    Bila shaka yoyote kumbukumbu za uhusiano wa China na Jamhuri ya Tanzania ni mfano mmoja tu unaotudhihirishia jinsi gani Jamhuri ya Watu wa China ilivyoweza kujitolea kwake kulisaidia Bara letu la Afrika punde tu mataifa yetu yalipoweza kujikwamuwa katika minyororo ya Kutawaliwa na Wakoloni na kujipatia Uhuru wake.

    Ni matumaini yangu makubwa kwamba Chemsha Bongo hiyo ya Maadhimisho ya miaka 45 ya uhusiano kati ya China na Tanzania itakuwa ni yenye faida kubwa kwa Wasikilizaji wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa bila kujali wanakotokea , kwani ni wazi kabisa Chemsha Bongo hiyo inatoa nafasi zaidi kwa Wana Afrika Mashariki kujikumbusha na kujielimisha zaidi juu ya Historia ndefu ya uhusiano wa Jamhuri ya Watu wa China na bara letu la Afrika.

    Msikilizaji wetu Franz Manco Ngogo wa Tarime Tanzania ametutumia barua pepe akisema, maisha yamezidi kwenda yakipendeza! Angalia tunavyoenda na wakati na mashindano ya chemsha bongo yanamiminika na zawadi lukuki. Hongera CRI na wadhamini wenu;ofisi zote mbili za ubalozi wa China na Tanzania. Tunakuja kwa maandalizi ya kushiriki vizuri sio lazima kushinda. Ila nitafarijika iwapo shindano litakutanisha wasikilizaji wote wa CRI , tuonane uso kwa uso.

    Bw. Mogire O. Machuki Bogeka village s.l.p. 646, kisii Kenya ametuletea barua akisema, maoni na tathmini yangu ya jumla kuhusu urafiki kati ya mataifa haya mawili...

    uhusiano baina ya China na Tanzania wa miaka 45 umeleta maendeleo ya muda mrefu yenye afya na ya kasi tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili.

    Kwa mtazamo wangu naona kuwa uhusiano kati ya Tanzania na China umepitiliza kutoka kwa serikali za jadi hadi kuingia kwenye mawasiliano ya mara kwa mara kati ya serikali hizo mbili na kuingiza pia ushirikiano baina ya wananchi wa mataifa hayo mawili, hadi kufikia kiwango ambacho watu wa Tanzania na wale wa China huitana "rafiki".

    Urafiki kati ya China na Tanzania sio tu umeleta manufaa kwa watu wa tanzania pekee bali hata sisi majirani wa karibu Kenya tumenufaika kwa kiasi kikubwa na uwekezaji wa China nchini Tanzania. urafiki huu sharti uwe wa kudumu kwa manufaa ya vizazi vya baadaye la msingi ni kuwa nchi ya China imedhihirisha kuwa inawajali sana watu wa maeneo yote duniani. ni nchi gani ambayo inaweza kutumia fedha na raslimali zake kufadhili miradi ya taifa la pili? China twaipenda na kuithamini mno.

    Uhusiano wa Tanzania na China umejidhihirisha tena hivi karibuni wakati wa ziara ya rais wa China, Hu Jintao, jumamosi, februari 14, alipotembelea nchi hizi za Afrika Mashariki, ziara iliyoelezewa kama "yenye lengo la kuimarisha urafiki baina ya mataifa hayo mawili".

    kuna mambo mengi ya kufanyika mwaka huu ili kukuza zaidi urafiki kati ya Tanzania na China, kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, ikiwa ni pamoja na kufaidisha wachina wanaofanya kazi na biashara nchini Tanzania.

    Kulingana na balozi huyo, baada tu ya uhuru wa Tanganyika na Zanzibar, wataalam wa kilimo, ujenzi na madini walifika kusaidia wenzao wa Tanzania katika fani zao. baadae, mamia kwa maelfu ya wafanyakazi wa reli walifika kujenga kilomita 1,860 za reli ya Tanzania hadi Zambia, ambayo inajulikana zaidi kama TAZARA. reli hii ina na alama ya kudumu kati ya China na Tanzania. ni kumbukumbu ya kipekee ambayo nailinganisha na miradi ambayo China imewekeza hapa kenya kama vile uwanja wa kisasa wa kasarani ambao ulijengwa na serikali ya China na barabara kadha za kisasa ambazo zimefadhiliwa na mfuko wa serikali ya China...tuna mengi ya kujivunia.

    Takwimu zaonyesha kuwa biashara kati ya mataifa hayo mawili, imeongezeka zaidi ya mara 10 tangu kuanza kwa karne hii, kutoka thamani ya dola milioni 93.44 mwaka 2001 hadi zaidi ya dola milioni 900 mwaka jana, na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya 15 miongoni mwa washirika 60 wa biashara wa China katika bara la afrika.

    Mimi mwenyewe nimewahi kufika sehemu kadha za Tanzania na nilipokuwa huko niliwahi gundua kwamba asilimia kubwa ya bidhaa wanazotumia watanzania asili yake ni China. Hili laonyesha kuwa urafiki huu ulianzia mbali na unazidi kuendelea.biashara kati yamataifa haya mawili inazidi kuimarishwa.

    Takwimu za mwaka 2007 za biashara kati ya Tanzania na China ilifikia thamani ya dola milioni 290, ambapo kati ya hizo bidhaa za China nchini zilifikia thamani ya dola milioni 180 wakati iliagiza kutoka Tanzania bidhaa za thamani ya dola milioni 110.

    Bidhaa zinazouzwa na China nchini Tanzania ni pamoja na vyakula, magari, nguo, bidhaa za viwandani, vipuri vya magari na mitambo mingine,vifaa vya umeme na vile vya chuma. Tanzania inauza samaki nchini China, ngozi mbichi, magogo, shaba na vifaa vya mbao. Katika safari yangu ya Musoma Tanzania mwaka 2002 niligundua kwamba watanzania wanavipenda sana vitu kutoka china kutokana na thamani ya pesa.. maumbo ya bidhaa hizo ya kupendeza na pia bidhaa hizo ni madhubuti.

    Mbali na biashara na uchumi, China pia imeendelea kutoa misaada mbalimbali kwa Afrika Mashariki. Zaidi yaaminika kuwa Tanzania ndio inayoongoza kwa kupokea misaada mingi kutoa China barani Afrika. Katika ziara yake ya Tanzania jirani ya nchi yangu Kenya , rais Hu alisaini mkataba wa dola milioni 21.9 kusaidia sekta za kilimo, mawasiliano na ushirikiano wa kiufundi. Mbali ya msaada huo, Hu alishiriki katika uzinduzi wa uwanja mpya wa michezo ambao ulijengwa kwa msaada wa China kwa mamilioni ya dola. Uwanja wenye uwezo wa kuingia watazamaji 60,000 wakiwa wameketi, unaelezewa kuwa wa kisasa zaidi katika Afrika mashariki. Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete alishukuru sana kwa hili kwa niaba ya wananchi wa Tanzania.

    China na Tanzania zina msimamo unaofanana katika masuala mengi, hasa katika kutafuta amani duniani na masuala ya maendeleo. tangu China ijiunge na shirika la WTO kweli imepata mafanikio mengi na nia ya China kuwekeza miradi yake kwenye mataifa kama Tanzania ni jambo la kutia moyo sana.

    Naona sisi hapa Afrika maisha yatakuwa duni kabisa bila misaada ya kila wakati kutoka China ambayo inaendelea kufurika hapa. takribani nchi ya China ndio inayoongoza kwa misaada barani Afrika na imewezesha sekta ya biashara na uchumi kushamiri.

    Udumu urafiki kati ya China na Tanzania. udumu urafiki kati ya China na Afrika.

    Shukurani za dhati wasikilizaji wetu na wasomaji wetu wa mtandao wetu, kweli tunafuraha kubwa sana kwa kupokea maoni mbalimbali kuhusu chemsha bongo ya maadhimisho ya miaka 45 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania, hili ni jambo la faraja sana kuona kweli mnafuatilia chemsha bongo, uhusiano na maendeleo ya nchi hizi mbili. Na tunaendelea kusisistiza kuwa bado tunapokea majibu ya chemsha bongo na pia tunakaribisha maoni mengine mbalimbali kutoka kwenu wasikilizaji wetu kuhusu chemsha bongo hii.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako