• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Dastan" sanaa ya kuimba na kuongea ya kabila la wakhazak mkoani Xinjiang China

    (GMT+08:00) 2009-06-30 14:33:52

    Mzee Kazim Alman

    Katika sehemu ya Altay, kaskazini mwa mkoa wa Xinjiang China, wanaishi watu wa kabila la wakhazak, ambapo sanaa ya jadi iitwayo Dastan ya kuimba na kuongea imeenea sana miongoni mwao. Dastan ni fasihi simulizi, hivi sasa imekuwepo kwa miaka zaidi ya elfu moja. Mzee Kazim Alman ni mrithi wa sanaa hiyo, sasa tusikie maelezo kuhusu mzee huyo.

      Mzee Kazim Alman anaimba, "Wewe ni ua kwenye kilele cha mlima; Nataka kukupata lakini magenge yananizuia; Niko radhi kupoteza mifugo yangu yote ili niishi nawe pamoja; Naimba wimbo kuelezea mapenzi; Napiga kinanda nikitumai kuwa utapenda muziki."

      Kabila la Wakhazak ni kabila la wafugaji lenye historia ndefu, wanahamahama wakifuata maji na malisho ya mifugo katika sehemu ya Altay, kaskazini mwa mkoa wa Xinjiang. "Dastan" ni aina moja ya fasihi simulizi ya asili katika utamaduni wa kabila hilo. Katika lugha ya Kikhazak, neno "Dastan" maana yake ni utenzi, Dastan ilianza tokea kati ya karne ya 9 na 10 hivi, mambo yanayosimuliwa katika Dastan yanahusu mashujaa na historia. Msanii anaweza hata kutumia mchana na usiku kuimba Dastan moja kutokana na hadithi ndefu akiwa anaimba na kuongea na huku akipiga kinanda mwenyewe.

      Mzee Kazim Alman ana umri wa miaka 77, yeye ni mwenyeji wa wilaya ya Fuhai katika sehemu ya Altay. Mwaka 1943 alipokuwa na umri wa miaka 11 alianza kujihusisha na sanaa ya Dastan wakati alipokuwa kwenye mkusanyiko wa watu, alivutiwa sana na jinsi msanii alivyosimulia hadithi za mashujaa kwa kuimba na kuongea. Mpaka sasa anakumbuka sana alivyokuwa kwenye mkusanyiko huo. Alisema,

      "Mwaka 1943 nilipokuwa njiani nikitafuta malisho ya mifugo nilibahatika kusikiliza Dastan katika mkusanyiko wa watu. Dastan iliyosimuliwa ilikuwa ndefu yenye kiasi cha beti zaidi ya 400. Baada ya kusikiliza Dastan hiyo nikaweza kuihifadhi moyoni mwangu. Tokea hapo nilianza kujifunza Dastan, wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 11 tu."

      Akili ya mzee Kazim Alman ni nzuri sana na ya ajabu, anaweza kuimba Dastan moja ndefu sana bila kusoma maandishi, kutokana na uhodari huo anasifiwa kuwa ni mtaalamu wa Dastan. Mkoani Xinjiang mzee huyo ni msanii pekee mwenye uwezo wa kuimba Dastan nyingi zaidi. Kati ya Dastan 200 zilizohifadhiwa sasa, mzee huyo anaweza kuimba 104.

    Tokea alipoanza kujihusisha na Dastan kwa mara ya kwanza aliipenda sana sanaa hiyo, aliwatembelea wasanii wote mashuhuri wa sanaa hiyo na kujifunza kutoka kwao. Mzee huyo anaona kwamba utamaduni wenye historia ya miaka zaidi ya elfu mbili uko katika sanaa hiyo na haifai kuachwa, kwani huu ni utambulisho wa kabila la Wakhazak. Alisema,

    "Kwenye sanaa Dastan kuna utamaduni, historia, mambo ya siku za kale na ya leo ya kabila la Wakhazak. Hapo zamani kabila letu lilikuwa halina lugha ya kuandikwa, tulitegemea Dastan kuwaeleza watoto wetu utamaduni wetu wa jadi."

    Mzee Kazim Alman alipokuwa mtoto alikwenda shule kwa miezi mitatu tu kutokana na hali mbaya ya elimu wakati huo, lakini hata hivyo hakukwamishwa kujifunza Dastan, aliposikia tu wengine wakiimba Dastan fulani, mara aliweza kuimba Dastan hiyo. Licha ya kujifunza, Mzee huyo pia alitunga Dastan yake kwa mujibu wa mambo yaliyomkuta maishani mwake. Kutokana na umaarufu wake, wenyeji wa kijiji chake na vijiji vingine mara kwa mara walimwalika kuimba Dastan katika sherehe zao. Mzee Kazim Alman alisema,

      "Mara nyingi naimba kwa wiki na hata nusu mwezi katika sherehe mbalimbali za harusi, jando, kuwapatia watoto majina na sikukuu. Mwaka 1956 kwenye tamasha la Altay niliimba kwa usiku na mchana. Kama nikianza kuimba sasa basi naweza kumaliza kesho."

      Kutokana na uimbaji wake wa Dastan mzee huyo alijipatia mke mzuri. Alipokuwa na umri wa miaka 20 kijiji cha jirani kilifanya karamu, alialikwa kwenda huko kuimba Dastan. Kwenye karamu hiyo, alivutiwa na msichana mmoja mrembo, na msichana huyo pia alivutiwa na kijana Kazim Alman, hao wawili walianza kupendana mara walipokutana. Cha ajabu ni kwamba kaka wa msichana huyo alikuwa ni msanii wa Dastan wa kijiji chake. Ili aweze kumwoa msichana huyo Kazim Alman alifanya kazi huku akijitahidi kujifunza Dastan kutoka kwa kaka huyo. Kazim Aliman alikumbuka akisema,

      "Kaka wa msichana huyo alikuwa msanii mashuhuri wa Dastan katika kijiji chetu, kwa kuwa nilijifunza kwa kaka huyo nilipata fursa kubwa ya kukutana na msichana huyo."

      Mara nyingi Mzee Kazim Aliman alijizamisha katika furaha yake ya kuimba Dastan bila kuchoka, na watu waliomsikiliza walifurahishwa pia. Ili kuonesha shukrani zao baadhi ya watu walimzawadia farasi, mbuzi au majora ya vitambaa. Lakini kitu alichotilia maanani sio mali wala pesa bali ni urithi wa sanaa ya kabila lake. Alisema,

      "Dastan ni utamaduni pekee wa kabila la Wakhazak, utamaduni huo lazima uhifadhiwe na urithishwe. Kwenye sanaa ya Dastan kuna hadithi za mashujaa wetu ambao wanatutegemea sisi wasanii kuwafahamisha vizazi vyetu."

      Kuna Dastan zaidi ya 200 zinazoenea miongoni mwa Wakhazak, lakini wanaoweza kuimba Dastan hizo wako wachache sana. Mzee Kazim Alman ana masikitiko kwa kukosa wasanii vijana. Alisema,

      "Nahofia sana sanaa hiyo isije kutoweka, hivi sasa vijana wengi wanashabikia muziki wa kisasa na kupuuza Dastan. Nasikitika sana."

      Mwaka 2008 serikali iliingiza sanaa ya "Dastan ya Kabila la Wakhazak" katika orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana nchini China na mzee Kazim Alman alichaguliwa kuwa mrithi wa sanaa hiyo. Ili kuhifadhi sanaa hiyo yenye historia ndefu, serikali ya mkoa imeanzisha idara maalumu na imerikodi Dastan zote 104 anazoweza kuimba mzee huyo na kumwalika afundishe katika vituo na shule. Mkuu wa Jumba la Utamaduni la Wilaya ya Fuhai Bi. He Yan alisema,

    "Mzee Kazim Alman amekuwa na umri wa miaka 77, licha ya kumtunza kiafya tunamwalika kufundisha katika vituo na shule zilizoanzishwa hivi karibuni na kila wiki tumempangia kipindi kimoja kufundisha vijana Dastan."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako