• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji 0629

    (GMT+08:00) 2009-06-30 14:43:24
    Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161 Bariadi Shinyanga Tanzania ametuletea barua akisema, Wapendwa wafanyakazi wa idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa, tarehe 12 mwezi wa tano mwaka uliopita wa 2008 ilikuwa ni siku ya huzuni na masikitiko makubwa kwa wakazi wa mkoa wa Sichuan, wananchi wote wa China na marafiki wa China na watu wote wapendao amani na maendeleo duniani. Ambapo tetemeko kubwa la ardhi lililosababisha maafa makubwa liliukumba mkoa wa Sichuan. Kama ilivyoripotiwa maelfu ya watu walipoteza maisha na wengine kupoteza makazi yao kutokana na tetemeko hilo.
    Tunapokumbuka tukio hilo la kimaumbile lililosababisha maafa makubwa mwaka mmoja uliopita, kwa mara nyingine tena ninawapa pole wakaazi wa mkoani Sichuan na wananchi wote wa China kutokana na tukio hilo la kusikitisha mno. Waraka maalumu kupitia Radio China Kimataifa ili kuwafariji walioathirika kwa njia moja ama nyingine na tetemeko hilo la ardhi. Aidha katika waraka wangu huo wa mwaka jana kuhusu tukio hilo nilisema kwamba kama ningepata fursa ya kutembelea China kwa mwaliko au kwa safari yangu binafsi, hata kama itakuwa imepita miaka kadhaa hivi tangu kutokea janga hilo la tetemeko la ardhi mkoani Sichuan, nitataka kufika huko na kutoa msaada wangu mdogo na kutia saini katika kitabu cha wageni kwa mamlaka za huko. Kwani "kutoa ni moyo si utajiri" na binadamu wote ni sawa na dunia ni moja. Juhudi na mikakati mingi na ya uhakika, ikiwemo ya dharura iliyofanywa na serikali kuu ya China, serikali za mikoa na mitaa pamoja na jumuiya ya kimataifa, asasi nyingine za kiraia nchini China zimetutia moyo sana katika utoaji misaada ya hali na mali kwa wahanga wote wa tetemeko la ardhi mkoani Sichuan.
    Radio China Kimataifa ilitoa taarifa na kuripoti kwa kina shughuli nzima ya uokoaji, utoaji misaada na ukarabati wa miundo mbinu ilivyoendelea. Ni imani yangu kwamba baada ya miaka michache hivi kupita, maisha ya wakazi wa mkoani Sichuan nchini China yatarejea katika hali ya kawaida na kuendelea na mchakato wa ujenzi wa taifa lao la China. Mwisho kabisa natoa shukrani nyingi kwa Radio China Kimataifa kwa ajili ya mfululizo wa vipindi kuhusu kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani Sichuan mlivyotutangazia mwezi Mei mwaka huu wa 2009. Asante sana.
    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Kilulu Kulwa kwa barua yako kuhusu tetemeko kubwa la ardhi lililotokea huko Wenchuan mkoani Sichuan, na sasa mwaka mmoja umepita toka litokee tetemeko hilo, baada serikali ya China kufanya juhudi kubwa, mafanikio makubwa yamepatikana katika ukarabati wa sehemu zilizoharibiwa vibaya katika tetemeko la ardhi, na watu wengi wamehamia kwenye nyumba mpya. Nawe tunakushukuru sana kwa imani na moyo ulionao, sisi huku tunakukaribisha kwa mikono miwili ili ukifika China uweze kukamilisha tumainio lako la kufika Sichuan na kutoa msaada wako.
    Msikilizaji wetu January Nchimbi wa P.O.Box 34573 Dar es Salaam Tanzania, anasema nianze kwa shukrani nyingi kwa serikali ya China kwa urafiki wa dhati na Tanzania, kwani rafiki wa kweli huonekana kwa matendo yake. Tunashukuru kwa uamuzi wa busara kwetu na kuanzisha matangazo kupitia Idhaa ya Kiswahili ya CRI ili nasi hapa Tanzania tushirikiane vizuri na wenzetu wa huko China kiuchumi, kiutamaduni, kielimu, kisiasa na shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii. Ninaomba Idhaa ya Kiswahili ya CRI iweke mikataba na Radio za FM zilizopo hapa Tanzania ili kuongeza wasikilizaji wake na pia muda wa matangazo uongezeke kutokana na mahitaji ya wasikilizaji wenu. Mimi mwana-taaluma wa habari niko tayari kujitolea kuwatumia habari toka hapa Tanzania. Ninawaunga mkono daima.
    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu January Nchimbi wa Dar es Salaam kwa barua yako, maoni yako tumeyapokea na tunakutaarifu tu kuwa hivi sasa Redio China Kimataifa iko mbioni kushughulikia suala hilo la kuanzisha matangazo yake nchini Tanzania kupitia redio za FM, hivyo usiwe na hofu kuhusu hilo na kuhusiana na kuongeza muda wa vipindi na kututumia habari pia tumesikia ila tutakapoanza matangazo yetu huko naamini mambo mengi tu yatafanyika.  
    Gasto F. Mkawe  P. O. Box 11091, Arusha, Tanzania. Anasema nawapongeza sana wachina na serikali yenu. mnafanya vizuri sana katika sekta ya ujenzi. hivi sasa hapa Tanzania kuna makampuni mengi sana ya ujenzi yanafanya kazi nzuri katika kujenga barabara na majengo mbalimbali.HONGERA.Watanzania tujifunze
    Shukrani Bw. Gasto F. Mkawe wa Arusha. Kwanza tunasema ahsante sana kwa pongezi hizo ulizozitoa, China ikiwa mwenza mkubwa wa Tanzania katika mambo mbalimbali kila siku itakuwa mstari wa mbele katika kuisaidia Tanzania kwani urafiki na ushirikiano wa nchi hizi mbili umeanzia toka enzi na enzi.
    Amin NAJMI amony_hi_22@yahoo.com ametuletea barua pepe akisema,napenda sana sura mpya ya tovuti yenu kwenye mtandao wa ineternet, nimeona maelezo kuhusu chakula kitamu cha China, kweli napenda sana kula chakula cha kichina. Jana nilijaribu kupika chakula cha Chunjuan ambacho ni kama sambusa ya Tanzania, ni chakula kitamu kweli, watu wa familia yangu na marafiki zangu wote walipenda sana Chunjuan cha kichina. Naona vyakula vyote vya kichini ni vitamu.
       Tunamshukuru sana bwana huyo aliyetuelezea hayo ambayo yanatufurahisha sana. Ni matumaini yetu kuwa marafiki wengi watapata fursa ya kuonja chakula cha kichina.
    Msikilizaji wetu Ras Manko Ngogo wa Kemogemba Club P.O.BOX 71  Tarime Mara Tanzania, yeye barua yake pepe ameigawa katika sehemu mbili kwanza anatoa maoni yake na pili ametuandikia shairi zuri mno. Tukianza na maoni anasema Ni jambo la kujivunia kuona kuwa nchi mbili zinakuwa na urafiki unaopamba moto kiasi, licha ya kutopakana wala kuwa hata katika bara moja. Moyo wa kusaidiana kwa maendeleo ya binadamu bila kujali rangi ama itikadi ya mtu mwenyewe. Chanzo kikubwa ni mfumo wa siasa ya ujamaa na kile kilichoitwa kuwa watu wote ni sawa, na utajiri wa taifa na rasilimali zote ni mali ya umma na sio kwa kundi la watu. Nawapa pongezi za dhati viongozi wa wakati huo wa mwanzo wa uhusiano na urafiki ulioleta mahusiano ya kibalozi miaka 45 iliyopita. Mwl. Nyerere na wenzake, rais Abeid Karume ni watu pekee waliofanikisha tukio hili, kabla ya nchi hii kuitwa Tanzania. Ziara ya waziri mkuu wa China wa kipindi hicho Bw. Zhou Enlai hapa nchini na kuleta maendeleo yanayoonekana hadi sasa ya ujenzi wa reli ya TAZARA yenye urefu wa 1860km, hata kidogo haiwezi kusahaulika. Ushahidi na kumbukumbu nyingi zipo hadi leo hii, nazo ni  watoto wengi hapa Tanzania walioitwa CHINA ambao  leo hii ni watu wazima wenye familia na wajukuu. Binafsi mimi nilishuhudia kwa macho na masikio yangu mwenyewe, nilipokuwa na umri wa miaka 8-10 kuwa Wachina wapo katika hospitali za wilaya na mkoa wetu wa Mara kwa matibabu ya hali ya juu kwa wagonjwa.   Sifa hizo, zilimwagika kwa kushukuru juhudi na ujuzi wao waliouonesha. Imedhihirika wazi kuwa mzazi mmoja awapo na urafiki kwa mzazi mwingine ni rahisi sana kwa watoto wao kujenga urafiki. Mfano huo halisi,umeonekana kwa Tanzania na China, pale tu zilipodumisha urafiki wao na mara moja miji miwili ya nchi hizo kuwa marafiki na kuendeleza urafiki huo hadi sasa;Haikou na Zanzibar leo hii ni kioo kwa miji mingine kuweza kuona kuwa urafiki unapodumishwa faida yake ni nini. Maendeleo ya urafiki wa China na Tanzania yatazidi kushamiri sana kwa jinsi ishara inavyoonyesha kuwa,wanafunzi wa Tanzania na China wamekuwa wakibadilishana kwa kwenda kusoma China na Tanzania tangu 1960 hadi sasa. Na ahadi nyingi kutolewa na rais Hu Jintao, akiwataka wanafunzi wengi zaidi kutoka Tanzania kupata mwaliko wa kwenda kusoma nchini China. Hilo tutaona kuwa ni wajibu,kwani kawaida ni kama sheria, na hili ndilo pekee litakalosaidia na kudumisha urafiki na ushirikiano wa nchi mbili. Kitendo cha China kutoa msaada wa ujenzi wa reli ya TAZARA na uwanja wa michezo wa Taifa, ni alama pekee inayoelekea kufanya mengi mazuri katika kipindi hiki cha urafiki na ushirikiano. Mbinu za usimamizi wa biashara na uchumi ni moja ya mambo ambayo tutazidi  kushirikiana na kusaidiana, hususani katika nyanja ya utalii. Ningefurahia kuona ushirikiano unaendelea kwa kujali watu wote wa nchi zote mbili. Mfano, rais Hu Jintao alipotoa mwaliko kwa wanafunzi wa Tanzania kwenda kusoma China, bado nionavyo, haijakidhi mahitaji ya wananchi.  Wakulima ni watu ambao wangepata fursa ya kutembelea China na kuona jinsi wenzao wanavyofanya na kuendesha shughuli za kilimo na kuiga mkakati wa watu wa China ambao hawana muda wa kupiga gumzo tu bila shughuli ya msingi.  Wasimamizi wa sehemu ya utalii na vivutio mbalimbali nao wachukuliwe hadi nchi rafiki kwa mwanga zaidi wa jinsi gani wenzao wanasimamia miradi na hawana viti vya kukaa na kubweteka kazini kwao,bali wanawasimama na kuwahudumia wateja kwa ukarimu na tabasamu iliyojaa ufundi wa kumridhisha mteja, ilimradi aridhike na kufurahia huduma. Madaktari nao watumwe kwenda China kuona mwito na huruma inayotumiwa na madaktari wa China kuokoa maisha ya wanadamu wenzao. Wahandisi nao wapate mwanya wa kwenda kusoma namna ya kusimamia na kubuni mifumo mizuri ya miundo mbinu na ujenzi kwa ujumla na wala sio kujali ufanisi wao binafsi na maendeleo ya jamaa zao pekee mbali na taifa. SHAIRI: WATANZANIA MARAFIKI WA WACHINA 1. Chonde chonde wachina,  rafiki wa Tanzania,     Kwa moyo bila hiyana, rafiki kujivunia,     Ni vigumu kuachana,tangu tulikoanzia,  Marafiki wa Wachina,ni wote Watanzania. 2.Toka Mara na Mtwara, sherehe twashangilia, Visiwani hata Bara, sote tunashuhudia, Tumeiweka shajara,tarehe ya kuingia, Marafiki wa Wachina ni wote Watanzania. 3. Hakika walisifika,dawa walizotibia,Sifa nyingi kuziweka,kila walipofikia,Jina China lasikika,kule walikopitia, Marafiki wa Wachina,ni wote Watanzania, 4. Amini heko nawapa,maanani kutilia,Si papara wala pupa, mazuri kuyapania, Majukumu tunajipa,ushirikiano pia. Marafiki wa Wachina,ni wote Watanzania 5. Misaada twapokea, wanafunzi kujuzia, TAZARA kutujengea,na uwanja zingatia, Kwa vitendo waongea,hatuna la kujutia, Marafiki wa Wachina,ni wote Watanzania. 6. Na hapa sina pa kwenda,Beijing natarajia,Dar Zenji nitadunda,sherehe kuhudhuria, Nafasi nzuri nawinda,mengi nije hadithia, Marafiki wa Wachina,ni wote Watanzania. 7. Urafiki umedumu,miaka mingi tangia, Kwenye sekta muhimu,mengi wamesaidia, Kwetu sisi ni walimu, sayansi teknolojia, Marafiki wa Wachina,ni wote Watanzania.8. Ngogo hapa ninakacha,moyo ukifurahia,Tuishi bila kuficha,mabaya yakidunia, Tukae kama mapacha,mema yatatujiria.Marafiki wa Wachina,ni wote Watanzania. Na mwisho anamalizia kwa kusema ahsanteni sana kwa yote mnayotuletea ikiwa ni pamoja na Chemsha Bongo Maalumu.
    Nawe msikilizaji wetu Ras Manko Ngogo tunakushukuru sana kwa maoni yako pamoja na shairi mwanana la kumtoa nyoka pangoni, mengi umeeleza kuhusu uhusiano na urafiki wa nchi hizi mbili tuombe urafiki huu uendelee kudumu milele.

    Wasikilizaji wapendwa, sasa tunawaletea maelezo aliyotuletea mwandishi wetu wa habari kutoka Nairobi Kenya.
    Wasikilizaji wapendwa, salamu mlizosikia ni za watoto wa kupendeza waliopo kwenye maktaba moja maalumu iliyopo kwenye eneo kubwa zaidi la watu wenye maisha ya chini mjini Nairobi. Jina la maktaba hiyo ni "Nicofeli Club", vilevile inaitwa "The hope library".
    Mapema ya mwaka 2008, maktaka hiyo ndogo ilianzishwa kwenye eneo hilo la kibera kutokana na taabu wanayokumbana nayo watoto ya kupata vitabu na kusoma. Na muda mfupi baadaye, idadi ya vitabu iliongezeka na kuwa 1200, na vitabu hivyo ni vya aina mbalimbali, kwa mfano kuna vitabu vya historia, mambo ya kiroho yanayoathiriwa na siasa za kijografia (geopolitics spirituality), mafunzo ya wanawake, hadithi na vinginevyo.
    Karani wa maktaba hiyo Bw. Osir Caleb na mwenyekiti Bw. Evans Otira, walitujulisha kwa nyakati tofauti hali ya maktaba hiyo, wakisema,

    Hivi sasa kwa ujumla kuna watoto zaidi ya 50 ambao wanakwenda kwenye makataba hiyo kusoma vitabu mbalimbali. Mtoto ambaye ni mdogo zaidi anayekwenda kwenye maktaba hiyo ana umri wa mwaka mmoja na nusu tu, na mkubwa zaidi ana miaka 17. Delta Sanjika ni miongoni mwa watoto hao, alisema,

    Watoto hao hawasomi vitabu tu kwenye maktaba hiyo, bali pia wanafundishwa kuimba na kutoa hadithi,

    Na msichana mrembo aitwaje Winnie Line alituonesha uwezo wake wa kutoa hadithi aliyofundishwa jana yake.
    Karani Osir Caleb alijulisha kuwa, maktaba hiyo haifurahiwi na watoto tu, bali hata wazazi wa watoto hao pia wanaifurahia sana maktaba hiyo, Osir alisema,

    Kwa bahati nzuri, kwenye maktaba hiyo pia tulikutana na mama wa mtoto aliyeimba ambaye anaitwa Kristina Nyango, Bi  Kristina alisema,

    Msichana huyo aliyewaongoza watoto kuimba anaitwa Anumu Ikale. Yeye ni mfanyakazi anayejitolea kufundisha kwenye maktaba hiyo. Kama ilivyo kwa watoto hao wote, naye pia anaishi kwenye maeneo hayo ya Kibera.

    Winnie Line alituambia, wakati atakapokuwa mtu mzima, angependa kuwa mwimbaji mashuhuri. Kwa kweli, kila mtoto kwenye maktaba hiyo ana ndoto yake mwenyewe. Na maktaba hiyo ndiyo mwanzo wa kutekeleza ndoto zao. Mwenyekiti wa maktaba hiyo Bw. Evans Otira alitoa mwito wake akisema,

    Wasikilizaji wapendwa, mliosikia ni hadhiti kuhusu makataba ndogo iliyopo kwenye maeneo ya Kibera aliyotuletea mwandishi wetu wa habari huko Nairobi Kenya.
    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako