• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mwimbaji mashuhuri Bi. Guo Shuzhen

    (GMT+08:00) 2009-07-06 16:26:15

    Katika mwaka huu wa lugha ya Kirusi nchini China tumeandaa maelezo kuhusu watu mashuhuri wa China waliowahi kusoma Russia, leo tunawajulisha mwimbaji mwenye umri wa miaka 82 Bi. Guo Shuzhen.

      Bi. Guo Shuzhen alizaliwa mwaka 1927 katika mji wa Tianjin. Baba yake alikuwa hajui kusoma wala kuandika, na mama yake alikuwa na sauti nzuri, ambapo watu walimwita "kengele". Wazazi wake waliendesha maisha kwa kufanya biashara ndogondogo, ingawa maisha yao yalikuwa magumu lakini wazazi wake walifahamu umuhimu wa kusoma, walikaza mkanda na kumsomesha binti yao wakiwa na matumaini kuwa atakuwa na maisha mazuri baadaye. Lakini bila ya kutarajia, binti yao Guo Shuzhen baada ya kuhitimu masomo katika shule ya sekondari aling'ang'ania kujiunga na shule ya michezo ya sanaa ya serikali iliyopo mjini Beijing, badala ya kujiunga na chuo kikuu. Wakati huo waimbaji na waingizaji wa michezo ya sanaa walikuwa wanadhalilishwa nchini China, hata hivyo Bi. Guo Shuzhen alishikilia uamuzi wake. Alisema,

    "Napenda kuimba toka nilipokuwa mtoto, mji wa Tianjin una bandari, hivyo biashara ilistawi, maduka mengi yalikuwa yanaweka vipaza sauti vya radio nje ili kuvutia wateja, kwa hiyo nyimbo na opera za aina mbalimbali zinasikika kila upitapo. Kwa sababu sauti yangu ni nzuri kama ilivyo ya mama yangu, nilipenda kuimba, lakini aliyenifundisha kuimba ni mwalimu wangu wa muziki nilipokuwa darasa la nne katika shule ya msingi, mwalimu huyo alinipenda sana."

    Guo Shuzhen alifaulu mtihani wa kujiunga na shule ya michezo ya sanaa, lakini baba yake alimkataza kwenda shule hiyo, mwaka wa pili Guo Shuzhen alifanya mtihani tena, mtahini alipomwona alishangaa akisema "si ulifanikiwa mtihani mwaka jana wewe?" Baada ya kumweleza kisa chenyewe mtahini alimwambia "Huna haja ya kufanya tena mtihani, umepokelewa." Kutokana na kushawishiwa na majirani, mwishowe baba yake alikubali kwa shingo upande binti yake asome katika shule hiyo.

      Katika shule hiyo, mwalimu wake wa kwanza alikuwa mwimbaji wa Marekani, na baadaye akapata mwalimu Mchina Bw. Zhao Meibo aliyewahi kusoma Ulaya, mwalimu huyo alimwekea msingi imara wa uimbaji.

      Tumaini alilokuwa nalo Bi. Guo Shuzhen alipokuwa mtoto lilitimizwa kutokana na juhudi zake. Mwaka 1953 serikali ya China ilituma kundi la kwanza la wasanii wanafunzi kwenda Russia kusomea muziki na uchoraji, Bi. Guo Shuzhen alikuwa mmojawapo katika kundi hilo. Katika miaka mitano aliyosoma katika Chuo Kikuu cha Muziki cha Tchaikovsky huko Moscow alifanya juhudi kubwa isiyo ya kawaida. Alisema anakumbuka kwamba katika miaka hiyo kila wiki siku sita ni muda wa masomo. Siku moja jioni mwalimu wake alimpa karatasi ya muziki na siku ya pili alitakiwa kuimba darasani, hili lilikuwa kazi gumu, lakini Guo Shuzhen alifanikiwa. Siku ya pili mwalimu wake alishangaa na kufurahi, lakini hakujua jinsi gani Guo Shuzhen alifanya juhudi katika usiku uliopita.

       Jasho lake halikupotea bure, muda si mrefu baadaye uhodari wa Bi. Guo Shuzhen ukaonekana. Katika Tamasha la Kimataifa la Vijana lililofanyika nchini Poland mwaka 1955, alipata medali ya shaba kwenye mashindano ya kuimba; mwaka 1957 kwenye mashindano ya kuimba huko Moscow, alipata nafasi ya kwanza kwa kuimba nyimbo nyingi kwa lugha za Kifaransa, Kiitalia, Kiczech na Kirusi, nyimbo zake ziliwashangaza majaji wa mashindano waliotoka nchi mbalimbali. Alisema,

    "Mashindano hayo yalikuwa ya kiwango cha juu kabisa, washiriki walikuwa wengi, na majaji walikuwa ni waimbaji mashuhuri duniani na mwenyekiti wao alikuwa Mtaliana ambaye alijulikana kote barani Ulaya tangu miaka ya 30 ya karne iliyopita."

    Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Mchina kupata nafasi ya kwanza katika mashindano ya kuimba ya kimataifa. Bi. Guo Shuzhen alisema, wakati huo wazazi wake waliokuwa nyumbani huko Tianjin walizungukwa na waandishi wengi wa habari. Kutokana na ushindi huo jina lake lilichongwa kwenye kibao cha shaba cha majina ya wanafunzi hodari katika chuo hicho. Baada ya kuhitimu masomo wanafunzi wenzake wa China walirudi nchini, lakini Guo Shuzhen alibaki chuoni nchini Russia, katika muda wa nusu mwaka hivi alifanya maonesho ya kuimba nyimbo katika nchi mbalimbali za Ulaya mashariki. Alisema,

      "Kutokana na urafiki uliopo kati ya China na Russia, baada ya kuhitimu masomo, nilipangiwa kufanya maonesho huku na huko kwa nusu mwaka nchini Russia, mimi nilifurahi kupata fursa hiyo ya kuonesha shukrani zangu kwa nchi rafiki. Nilifanya maonesho mawili ya opera huko Leningrad na Ukraine nikiigiza wahusika muhimu wawili katika opera mbili".

      Muziki wa opera hizo mbili ulitungwa na mwanamuziki mkubwa Tchaikovsky, nyimbo katika opera hizo zimekuwa nyimbo za lazima kwa Guo Shuzhen kuimba katika maonesho ya kila mara nchini China na nchi za nje.

    Baada ya kurudi nchini China, licha ya kufanya maonesho amekuwa mwalimu katika Chuo Kikuu cha Muziki cha China akifundisha kuimba opera, katika miongo kadhaa iliyopita, amewaandaa waimbaji wengi hodari. Hivi sasa amekuwa mwalimu wa wanafunzi wa shahada ya uzamili zaidi ya kumi. Mmoja wa wanafunzi wake wa mwaka wa tatu Zhang Jiajia alisema,

      "Tumebahatika sana kumpata mwalimu huyo. Anatufundisha mengi toka muziki mpaka mavazi na jinsi tunavyotakiwa kuwa jukwaani. Uzoefu wake mkubwa unatusaidia moja kwa moja.

      Tarehe 10 Julai mwaka huu "Maonesho ya Muziki ya Wanafunzi wa Guo Shuzhen" yatafanyika katika Ukumbi Mkuu wa Jumba la mikutano ya umma la Beijing, ili kuadhimisha miaka 62 tangu Bibi Guo Shuzhen afundishe muziki, hivi sasa wanafunzi wake wako mbioni kuyaandaa maonesho hayo. Bi. Guo Shuzhen alisema, amefanya kazi ya kufundisha katika miongo kadhaa iliyopita, na kazi hiyo pia imeongeza mambo katika maisha yake.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako