• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 0707

    (GMT+08:00) 2009-07-07 16:52:51

    Kuimarika kwa nguvu na uwezo wa nchi ya China katika miaka 60 iliyopita

    Wasikilizaji wapendwa, huu ni mwaka wa 60 tangu Jamhuri ya Watu wa China ianzishwe. Katika miaka 60 iliyopita, China imeendelezwa kuwa nchi yenye ustawi na neema kutoka nchi maskini na iliyoko nyuma kimaendeleo. Katika makala ya kwanza ya Chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Miaka 60 ya Jamhuri ya Watu wa China, tunapenda kuwakumbusha njia ya kujiendeleza ya China katika sekta ya uchumi, na kuangalia mabadiliko gani yametokea katika maisha ya wachina miaka 60 iliyopita.

    Kabla ya kusoma makala hii, tunatoa maswali mawili ili muweze kusikiliza makala na muweze kujibu vizuri maswali. Swali la kwanza: Hivi sasa thamani ya jumla ya uchumi wa China inachukua nafasi ya ngapi duniani? Maonesho ya kimataifa ya mwaka 2010 yatafanyika katika mji gani nchini China?

    Tarehe 8 Agosti mwaka 2008, Michezo ya Olimpiki ya 29 ilifunguliwa Beijing, mji mkuu wa China, ambapo wanamichezo kutoka nchi na sehemu 204 duniani walikusanyika, na watu wapatao bilioni kadhaa duniani waliburudishwa na furaha iliyotokana na michezo hiyo.

    Siku 16 baadaye, Michezo ya Olimpiki ya Beijing ilifungwa kwa mafanikio. Kwenye sherehe ya kufungwa kwa michezo hiyo, mwenyekiti wa kamati ya Olimpiki ya kimataifa Bw. Roge alisifu sana michezo ya awamu hii akisema:

    "Baada ya michezo ya Olimpiki ya awamu hii, dunia imejua mengi zaidi kuhusu China, na China pia imeelewa zaidi kuhusu dunia. Hii ni Michezo ya Olimpiki iliyofana!"

    Kwa wachina wapatao milioni 1.3, siku hizo 16 zilikuwa siku ambazo watazikumbuka daima. Mwenyekiti wa Kamati ya elimu ya utamaduni na Michezo ya Olimpiki katika Kamati ya Olimpiki ya kimataifa Bw. He Zhenliang alisema, siku hizi 16 ni mchakato wa kutimiza ndoto. Alisema:

    "Kuandaa Michezo ya Olimpiki kulikuwa ni ndoto ya wachina kwa miaka mingi, lakini zamani ndoto hiyo haikuweza kutimizwa. Kwani kuandaa Michezo ya Olimpiki kunatakiwa kutoa nguvu kubwa za watu na mali. Kabla ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, sisi tulikuwa tunaweza kuota ndoto tu, hakukuwa na uwezekano hata kidogo."

    Kama alivyosema Bw. He Zhenliang, ni lazima kuwa na uwezo wa hali na mali kwa kuandaa Michezo ya Olimpiki. Wakati wa kuandaa Michezo ya Olimpiki ya Beijing, China ilitenga Yuan bilioni 310 kwa ajili tu ya kujenga viwanja na majumba ya michezo na kukarabati miundo mbinu. Zamani China ilikuwa haina uwezo wa kutenga fedha nyingi namna hii kwa ajili ya kuandaa Michezo ya Olimpiki.

    Jamhuri ya Watu wa China ilipoanzishwa mwaka 1949, kutokana na vurugu za vita za muda mrefu, mambo ya uchumi yalifika kwenye ukingo wa kufilisika, na pato la kila mtu kwa mwaka lilikuwa ni dola 50 za kimarekani, maisha ya raia yalikuwa na taabu kubwa. Bibi Liu Guixian mzee mwenye umri wa miaka 77 alisema:

    "Wakati ule watu wengi waliishi maisha ya umaskini, mimi nilikuwa na watoto wengi, lakini pato la familia yangu ni la chini, tulikuwa tunakumbwa na taabu ya kupata chakula kila mara, hata wakati wa majira ya baridi, watu 7 wa familia yangu tulikuwa na mifarishi miwili tu kwenye vitanda."

    Katika kipindi cha mwanzo baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya watu wa China, wachina waliokuwa na matumaini ya kuwa na utandawazi wa viwanda nchini, walifanya juhudi kubwa za kujenga miradi mikubwa ya kimsingi zaidi ya 100, miradi hiyo iliweka msingi mzuri kwa ajili ya kupata maendeleo ya nguvu na uwezo wa nchi wa jumla. Lakini miradi mingi kati yao ni ya viwanda vizito, hivyo utoaji wa vitu kwa ajili ya maisha ya kila siku kwenye masoko ya nchi nzima ulikuwa na upungufu mkubwa.

    Balozi wa zamani wa Palestina nchini China Bw. Mustafa Safarini alikuja China mwaka 1968 kwa mara ya kwanza, lakini hapendi kukumbuka hali ya siku za baridi za mwaka huo nchini China. Alisema:

    "Wakati ule mimi nilikuwa sipendi siku za baridi, kwani hali ya wakati ule siyo kama ya sasa, tunaweza kununua na kuvaa nguo nzito za aina mbalimbali, hatuwezi kuona baridi. Lakini wakati ule, China ilikuwa na upungufu wa vitu vya lazima, hata watu walikuwa wanapaswa kutumia kuponi zilizotolewa na serikali kununua nguo nzito."

    Wakati ule China ilikuwa katika kipindi cha uchumi wa mipango, na kutekeleza utaratibu wa kuweka kikomo kwa utoaji wa vitu mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya kila siku zikiwemo nguo nzito kwa wakazi wa mijini, ambapo wakazi walipewa kuponi kwa ajili ya kununua vitu hivyo.

    China ilianza kufanya mageuzi na ufunguaji mlango mwaka 1978, ambapo iliweka mkazo katika ujenzi wa uchumi ili kupata maendeleo ya nchi. Tangu hapo China imepiga hatua kubwa kuelekea kwenye ujenzi wa mambo ya kisasa.

    Tarehe 30 Septemba mwaka 1980, Bibi Liu Guixian tuliyemtaja hapo kabla alifungua mkahawa mmoja mdogo mjini Beijing. Siku ya kuanzishwa kwa mkahawa wake, baada ya kupigwa kwa fataki za kusherehekea, msururu wa watu ulitokea nje ya mlango wa mkahawa huo, kwani mkahawa huo ulikuwa wa kwanza kuanzishwa na mtu binafsi nchini China. Mama mzee Liu alisema:

    "siku ile msururu huo ulikuwa na zaidi ya watu mia moja, ambapo mvua ilinyesha, hivyo watu wote walikuwa na miavuli. Mwanzoni hata mimi nilikuwa na wasiwasi, niliogopa kuwa huenda hakuna mtu ambaye angekuja kwenye mkahawa wangu kula chakula. Lakini baada ya kupiga fataki, watu wengi waliambiwa kuwa mkahawa wangu ni mkahawa binafsi, wengi walikuja.

    Mkahawa huo ulimletea mama mzee Liu Guixian maisha mazuri aliyokuwa akiyatamani kwa miaka mingi. Hivi sasa yeye na mume wake wamenunua nyumba kuishi kwa furaha na utulivu maisha yao ya uzeeni.

    Baada ya kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, mabadiliko makubwa yalitokea katika China nzima, ambapo mfumo wa uchumi ukabadilika hatua kwa hatua kuwa mfumo wa uchumi wa sokohuria badala ya mfumo wa uchumi wa mipango. Mabadiliko hayo yametia uhai mkubwa kwa maendeleo ya uchumi wa China, bidhaa zinazotolewa kwenye soko zimekuwa nyingi za aina mbalimbali. Balozi wa zamani wa Palestina nchini China Bw. Safarini bado anaishi nchini China baada ya kustaafu, hivi sasa anachukulia soko la China kuwa ni soko huria halisi. Alisema:

    "Hivi sasa wakati unapoingia kwenye soko au maduka nchini China, unaweza kuona bidhaa nyingi za aina mbalimbali, ambapo wafanyabiashara wanaoongea Kiingereza, kirusi na lugha nyingine wanafahamisha aina na sifa za bidhaa zao kwa wateja wa China na wa nchi mbalimbali, na wewe unaweza kugombea nao bei za vitu."

    Hivi sasa China imeagana kabisa na zama zile zenye ukosefu mkubwa wa bidhaa. Familia nyingi kabisa nchini China zinatumia televisheni, majokofu, mashine za kufulia nguo na kompyuta, vyombo hivyo vya umeme nyumbani vilichukuliwa kuwa ni vyombo vya anasa. Hata familia nyingi zimenunua magari madogo, zamani wachina wengi hata hawakuthubutu kutarajia kuendesha magari yao binafsi. Mtumishi wa kampuni moja Bw. Ma Yunliang ana umri wa miaka 27 tu, lakini alinunua gari mwezi uliopita. Alisema:

    "Hivi sasa watu wengi wamenunua magari, nadhani mapato ya mwaka mmoja hadi miaka miwili yanatosha kununua gari moja, nimenunua gari naweza kwenda kutalii vijijini, na sina haja kupanda basi lenye msongamano wa watu."

    Tukiangalia takwimu zilizokusanywa, tunaweza kuona kuwa thamani ya jumla ya uzalishaji nchini kwa mwaka 2008 iliongezeka kwa zaidi ya mara 400 kuliko ile ya mwaka 1952, utoaji wa jumla wa kiuchumi unachukua nafasi ya 4 duniani, na wastani wa pato la taifa kwa kila mtu pia umezidi dola za kimarekani 3,000.

    Maisha yameboreshwa, wachina wengi wamenunua nyumba mpya na magari madogo, pia wanapenda kutalii nchini China na katika sehemu mbalimbali duniani. Bw. Hao Xin anayependa sana kwenda nchi za nje kutalii anasema:

    "Kwa kawaida, naweza kwenda nchi za nje kutalii kila baada ya mwaka mmoja au miaka miwili, nimewahi kwenda Uingereza, Singapore, na Malaysia. Kabla ya miongo kadhaa iliyopita, wachina walioweza kupata fursa ya kwenda sehemu nyingine nchini kutalii ndio waliohusudiwa na watu, zamani watu wa kawaida hawakuwa na uwezo wa kifedha kwenda nchi za nje kutalii."

    Lakini mwaka kesho Bw. Hao hataki kwenda nchi za nje kutalii, amepanga kwenda Shanghai kutembelea Maonesho ya kimataifa.

    Katibu wa Kamati ya chama ya mji wa Shanghai ambaye pia ni mkurugenzi wa Kamati ya utendaji ya Maonesho ya kimataifa ya Shanghai Bw. Yu Zhengsheng alisema, mji wa Shanghai umetenga Yuan karibu bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya subway na barabara, pamoja na ujenzi wa majengo ya umma kwenye eneo la maonesho hayo. Alisema:"Mwezi Machi mwaka kesho, njia itakayopitwa na reli ya subway mjini Shanghai itakuwa na urefu wa kilomita 400 kutoka zaidi ya kilomita za mraba 200 ya mwaka jana. Kuboreshwa kwa mawasiliano kutakuwa na msukumo mkubwa sana katika kuboresha maisha ya wananchi na maendeleo ya uchumi.

    Sasa tunarudia maswali yetu mawili: Swali la kwanza: Hivi sasa thamani ya jumla ya uchumi wa China inachukua nafasi ya ngapi duniani? Maonesho ya kimataifa ya mwaka 2010 yatafanyika katika mji gani nchini China?

    Barua za wasikilizaji

    Msikilizaji wetu M.J wa Kemogemba Club" Urafiki kati ya China Na Tanzania utaimarishwa endapo China na Tanzania zitaboresha sekta ya elimu na hususani elimu ya juu yaani vyuo vikuu.Watoto wa kitanzania kufundishwa somo la Kichina na Watoto wa China wakifundishwa Kiswahili.Hilo litaambatana na uboreshaji wa tamaduni zetu, kwa maana kwamba somo la kichina lifundishwe mashuleni nchini Tanzania na Kiswahili vilevile kifundishwe kule China mashuleni.

    Vilevile yatupasa kutangaza sekta ya utalii ndani ya nchi hizi mbili China na Tanzania, pale ambapo vitu vya zamani na mabaki vito vya thamani vyaweza kuonyeshwa , wanyama wanaopatikana katka nchi hizi mbili watangazwe huku na kule.Mfano wanyama wa ajabu wa Tanzania watangazwe nchini China na chochote kilichopo China kitangazwe nchini Tanzania. Kwa njia hiyo naamini watalii wanaweza kuleta neema kubwa katika urafiki na ushirikiano huu.

    Kwa kuinua sekta ya Afya, basi watanzania waende China kama madaktari wakiongozwa na vikosi vya madakitari wa China ili kujifunza mengi kutokana na huduma zitolewazo na hospitali za huko,hivyo urafiki kati ya China na Tanzania utaimarishwa milele.

    Mbali na hapo ili kuimarisha na kuboresha urafiki kati ya China na Tanzania ni lazima tuwe tunaikumbuka tarehe 26 Aprili ya mwaka 1964, ili kujenga umoja ,ushirikiano na kuimarisha urafiki. Hivyo ni bora zaidi ikiwa nchi za China na Tanzania kuwa wanasherehekea kwa pamoja ili kudumisha amani, uhusiano na urafiki. Sherehe hizo ziwe zinafanyika kwa zamu; yaani mwaka wa kwanza nchini China na mwaka wa unaofuata nchini Tanzania.Ingawa tarehe hiyo hiyo huwa na sherehe za MUUNGANO wa Zanzibar na Tanganyika lakini sio vibaya zikiwa sherehe mbili kwa pamoja na marais wote wawili au wawakilishi wao wahudhurie.Pia wafanyakazi wa miradi iliyojengwa na China nao wahudhurie.

    Kubwa zaidi ni kusajili makampuni ya kitanzania kuwekeza nchini China na makampuni ya China kuwekeza nchini Tanzania na kuwepo na taratibu za kuajiri wafanyakazi wazalendo nusu na nusu nyingine wawe wageni.

    Baada ya muda kutokana na hayo ya kufundisha lugha za nchi hizi mbili basi kuwepo na ushirikiano wa matangazo ya radio kurushwa kupitia vyombo vya habari vya hapa Tanzania kwa lugha zote za kichina na kisawhili na vilevile matangazo ya radio ya Tanzania yarushwe kupitia radio ya china huko kwa lugha mbili.Matangazo haya yatasaidia kudumisha urafiki na ushirikiano kuendelea miaka nenda rudi.

    Shukrani Bw. M.J kwa maoni yako mbalimbali uliyoyatoa ambayo kwa kweli ni changamoto kwa nchi zote mbili, na endapo yatafanikiwa yote hayo basi nchi hizi mbili zitakuwa mfano wa kuigwa zaidi kuliko nchi nyingine.

    Msikilizaji wetu Juma S. Chamkwata wa Chuo Kikuu cha Sokoine sanduku la posta 3130, Morogoro Tanzania ametuandikia barua akisema, madhumuni ya barua yake ni kuomba kutumiwa gazeti la picha zinazohusu maendeleo ya shughuli za kilimo nchini China. Anasema zamani kwenye miaka ya 67 na 68 mpaka 71 alipokuwa mwanafunzi mdogo alikuwa mwanachama msomaji wa magazeti hayo. Na alifurahi sana kuona jinsi China ilivyokuwa inajiendeleza katika nyanja ya kilimo. Hasa kilimo cha mpunga na Bustani za mbogamboga. Na vilevile mambo ya viwanda na matibabu, au maendeleo ya China kwa jumla. Magazeti hayo yalikuwa yanatoka kila mwezi, na vile vile anakumbuka kuwa alikuwa anapokea hata zawadi ndogondogo kama vitabu na beji zenye picha za Mao Zedong.

    Mwisho anasema, kwa kuwa sasa hivi amekuwa mtu mzima atafurahi sana kama atatumiwa vitabu vya kilimo cha mpunga na Bustani za mbogamboga kwani hivi sasa hizo ndio shughuli zinazomwingizia kipato. Anasema tena kuwa atafurahi sana kama atapata mafunzo na kuelimishwa kupitia China Gazeti la picha. Kwani Nilikuwa Naletewa gazeti hili bure kila mwezi.Anakumbuka kuwa alikuwa akitumiwa gazeti hilo bila malipo yoyote, na sasa kwa kuwa yeye ni mkulima mwenye kipato cha chini kutoka Morogoro vijijini sehemu moja inaitwa Mvuha Kisaki, anaomba sana atumiwe gazeti hili bila malipo.

    Kwanza kabisa tunamshukuru sana msikilizaji wetu Juma S. Chamkwata wa huko Mvuha Kisaki. Tunavutiwa sana na moyo wako wa kufuatilia maendeleo ya China na kuwa mfuatiliaji wa matangazo ya Radio China Kimataifa na hata una kumbukumbu na majira uliyokuwa unapokea katika miaka iliyopita. Hata hivyo tunapenda kukuarifu kuwa, kutokana na mabadiliko yaliotokea hapa China, shirika lilikokuwa linafanya kazi ya kuchapisha magazeti hayo, na idara iliyokuwa ikifanya kazi ya kutafisiri na kutoa nakala za kiswahili sasa haipo tena. Shughuli zake zimechukuliwa na idara nyingine ambayo haichapishi magazeti kwa wingi na kwa lugha tofauti kama zamani. Siku hizi magazeti yanayochapishwa yanaitwa China Pictorial na China Today na bahati mbaya ni kuwa huwa yanatolewa kwa nakala chache tu ambazo hatuwezi kuwatumia wasikilizaji wetu wote. Hata hivyo, kama tukiweza kupata gazeti lolote lenye picha kuhusu shughuli za kilimo, au gazeti lolote linaloweza kuwa na picha zinazoonesha jinsi wakazi wa kijijini wanavyojiendeleza kimaisha tunaweza kukutumia. Endelea kutusikiliza na kuwasiliana huku tukiendelea kukutafutia.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako