• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wuzhong, sehemu inayopendeza zaidi kwenye ziwa Taihu

    (GMT+08:00) 2009-07-13 18:22:51

    Maonesho ya kimataifa ya mwaka 2010 yatafanyika Shanghai, mji ulioko sehemu ya mashariki ya China. Kamati ya maandalizi ya maonesho ya kimataifa inakadiria kuwa, wakati huo idadi ya watalii kutoka sehemu mbalimbali za dunia watakaotembelea maonesho hayo itafikia milioni 70. Mbali na kutembelea maonesho hayo, watalii kama watapenda kutembelea sehemu nyingine zenye vivutio karibu na Shanghai, basi Suzhou, iliyoko umbali wa saa 1 kwa gari ni chaguo moja zuri. Hivi sasa, utalii wa utamaduni wa milimani, ziwani na vijiji vya kale vya sehemu ya ziwa Taihu ya Suzhou umethibitishwa na kamati ya maandalizi ya maonesho ya kimataifa ya Shanghai ya mwaka 2010 kuwa "utalii wa uzoefu wa maonesho ya kimataifa".

    Wachina wana msemo mmoja wa "kwenye anga kuna pepo, duniani kuna Suzhou na Hangzhou", maana yake ni kuwa miji ya Hangzhou na Suzhou ni mahali pazuri kama peponi. Toka zamani za kale Suzhou ilikuwa maarufu sana kutokana na mandhari yake nzuri, sehemu ya Wuzhong iliyoko kusini mwa mji wa Suzhou inavutia watu zaidi kwa kuwa na ziwa Taihu.

    Wapendwa wasikilizaji, mliosikia ni wimbo unaopendwa na wachina wengi, kinachoelezwa katika wimbo huu ni mandhari nzuri ya ziwa Taihu. Kwenye sehemu ya ziwa Taihu, tarafa na vijiji vingi vya kale bado vimehifadhiwa vizuri hadi hivi sasa, ambavyo vinaonekana kama lulu zilizoko kwenye milima na maji, na kuunganishwa pamoja na vijito vingi vya ziwa Taihu.

    Suzhou na Shanghai ni miji jirani, na mawasiliano kati ya miji hiyo ni rahisi sana. Mtu akisafiri kutoka Shanghai, anaweza kufika sehemu mbalimbali zenye vivutio za Suzhou kwa kiasi cha saa 1 kwa gari. Kwa hiyo, ifikapo siku za likizo na sikukuu, mara kwa mara kuna wakazi wengi wa Shanghai wanaokwenda na magari yao kupumzika Suzhou, kutembelea ziwa Taihu na vijiji mbalimbali vya kale vya Suzhou na kukaa huko kwa siku chache na kuishi maisha ya utulivu.

    Mwishoni mwa mwezi Mey mwaka huu, ilikuwa sikukuu ya jadi ya kupiga makasia kwenye mashua zenye vichwa vya dragon (Dragon Boat Festival), mwandishi wetu wa habari katika mji wa Suzhou alikutana na mkazi wa Shanghai Bw. Chen, ambaye aliendesha gari akiwa na watu wa familia yake kutembelea tarafa ya kale ya Luzhi. Alimweleza mwandishi wa habari mawazo yake kuhusu Suzhou, alisema,

    "Ni karibu sana, tulifika hapa kwa saa 1 tu. Utulivu wa Luzhi na maisha ya kipekee ya tarafa ya kale yananivutia sana. Nilifika hapa mara nyingi, sasa ni likizo la siku kuu, hivyo nimewachukua watu wa familia kutembelea mtaani na kunywa chai kwenye mkahawa, leo tumepumzika vizuri."

    Sawa na tarafa ya Luzhi, Mudu iliyoko kwenye sehemu ya magharibi ya mji wa Suzhou pia ni tarafa maarufu ya kale. Mudu ni tarafa ya kale iliyo karibu zaidi na mji wa Suzhou, vilevile ni mashuhuri kwa kuwa na bustani nyingi binafsi za kale za China. Bustani hizo zaidi ya 30 zilijengwa katika enzi za Ming na Qing kati ya karne ya 14 na karne ya 19. Bustani nzuri za kupendeza, utamaduni maalumu wa jadi pamoja na hadithi nyingi za kihistoria za tarafa ya Mudu, zinawavutia watalii laki kadhaa wa nchini na wa nchi za nje kwenda kuitembelea tarafa ya Mudu kila mwaka.

    Mbali na mandhari ya kimaumbile na bustani za kupendeza, wanawake wa Suzhou wanajulikana kwa kuwa na akili nyingi na ni hodari kwa kazi, hususan katika kazi za kutarizi, utengenezaji wa nguo za pamba na hariri, utengenezaji wa majani ya chai, na wamekuwa ni uti wa mgongo katika sekta hizo, baadhi ya wanawake walikuwa mashuhuri sana kwenye kuendesha mashua, kutarizi, kupiga vinanda, ufugaji wa wadudu wa nyuzi za hariri, kupanda maua, kuimba, kuchora, kukamata kombe wa majini, pamoja na utengenezaji wa nguo, majani ya chai, vipepeo, taa za jadi, wanawake hao wanasifiwa kama ni "wanawake 12 hodari wa Suzhou".

    Ili kuwawezesha watalii wafahamu zaidi utamaduni wa jadi wa Suzhou, kampuni ya utalii ya Mudu imeanzisha shughuli za "kuwatembelea wanawake 12 hodari". Katika shughuli hizo, wasichana wa Suzhou wa zama zetu wanajishughulisha na kazi mbalimbali za kale wakivaa nguo za jadi, wako kwenye mitaa na mito mbalimbali ya tarafa ya kale ya Mudu, wakati watalii wanapojiburudisha kwa mandhari nzuri ya tarafa ya kale ya Mudu, wanaweza kuwaona "wanawake 12 hodari", hii inawaonesha watalii hali ya ustawi na uzuri wa mji wa kale wa Zuzhou wa zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Ofisa wa mpango wa maendeleo wa kampuni ya utalii ya Mudu Bi. Yang Li alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari, alisema, wanatarajia watalii hususan wa nchi za nje wafahamu utamaduni wa tarafa ya kale ya Mudu kutokana na shughuli hizo. Alisema,

    "Tunatarajia kuongeza utamaduni wa Suzhou kwenye vivutio vyetu, hivyo licha ya kuona mandhari nzuri, watalii pia wanaweza kuona vitu vya kiutamaduni."

    Mtalii Bibi Xu alisema amekwisha waona "wanawake 8 hodari" kati ya wale 12. Alisema,

    "Nimewaona wanawake hodari wa uendeshaji wa mashua, utarizi, utengenezaji nguo, chai, vipepeo, taa za jadi, wa uimbaji na wa kukamata kombe wa majini. Nitaendelea kuwatafuta wengine. Ninapenda sana shughuli hizo, licha ya kuona mandhari nzuri, nimefahamu utamaduni wa hapa."

    Mbali na kuanzisha mambo mapya ya utalii, Suzhou inafanya kazi nyingi katika kuboresha usimamizi na utalii ili kuwapokea watalii wa nchini na wa nchi za nje watakaotembelea maonesho ya kimataifa ya Shanghai. Naibu mkurugenzi wa idara ya utalii ya sehemu ya Wuzhong Bw. Xu Min alisema,

    "Hivi sasa, tumewaalika wataalamu wa usimamizi wa hoteli, watathmini wa ngazi ya taifa kuhusu viwango vya hoteli pamoja na wataalamu wa usimamizi kuhusu ujenzi wa sehemu ya mandhari waje kutoa mafunzo kamili kwa wasimamizi wa sekta ya utalii ya Wuzhong kuhusu ubora wa huduma na mapokezi kwa watalii ili kujenga msingi imara kwa ajili ya kuinua kiwango cha utalii wa ziwa Taihu la Wuzhong na kutoa huduma nzuri kwa maonesho ya kimataifa ya Shanghai. Baada ya hapo, tutawaalika wataalamu maarufu wa nchini na nchi za nje wa usimamizi wa ubora wa utalii waje kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu, ili kuanzisha mazingira ya utalii ya usalama na yenye utaratibu mzuri wa ziwa Taihu la Wuzhong.

    Mkurugenzi Xu Min pia kupitia CRI alipenda kutoa mwaliko kwa watalii wa nchini na wa nchi za nje waende kutembelea Suzhou baada ya kutembelea maonesho ya kimataifa ya Shanghai ya mwaka 2010.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako