• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 0714

    (GMT+08:00) 2009-07-14 16:50:05

    Bi Halima Ijeiza wa Sanduku la barua 14 Ndori, Kenya ametuandikia barua akitusalimu na kusema kuwa ana matumaini sote hatujambo na tunaendelea vizuri na kazi za kila siku. Anasema yeye pia hajambo na anaendelea vyema na pilikapilika za kila siku, huku akiendelea kusikiliza matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China. Pia anasema anapenda kutumia fursa hii kutoa pole zake za dhati kwa watu wa mataifa yote ambayo yameathiriwa na homa ya mafua ya H1N1aina ya A, ikiwa ni pamoja na marafiki wa China.

    Anasema jambo ambalo limemtia dukuduku na kumfanya aandike barua hii, ni kwamba sasa hivi dunia inakumbwa na magonjwa ya ajabu kama Ukimwi, homa ya mafua ya ndege na sasa homa ya H1N1, ambayo mwanzoni ilikuwa inaitwa homa ya mafua ya nguruwe! Anaona ni kama sasa wanasayansi wamezidiwa na kazi ya utafiti ili kupata tiba ya magonjwa haya! Anashauri tuwe makini kujilinda na kujiepusha na hatari za magonjwa hayo.

    Na kuhusu matangazo yetu, anasema anafurahia sana kusikiliza vipindi vilivyoboreshwa, hususan kipindi cha salamu zenu na habari. Mbali na hayo, pia anasema anafurahia sana na sauti nzuri za watangazaji, na kama ikiwezekana angependa kutumia picha za watangazaji. Anasema kwa ujumla anaridhika na matangazo yetu na anashukuru sana.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Bi Halima Ijeiza kwa barua yako na maoni yako ambayo yanadhihirisha hofu uliyonayo kutokana na majanga mbalimbali yanayoikumba dunia hususan magonjwa yanayoibuka kila siku, ni kweli hivi sasa dunia imekumbwa na taharuki kubwa ya ugonjwa huu wa HINI aina ya A, lakini tunapaswa pia kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuutibu ugonjwa huu na pia kupatikana kinga yake ukilinganishwa na ukimwi na kama ulivyosema ni muhimu kuwa makini kujilinda na kujiepusha na hatari za magonjwa hayo.

    Msikilizaji wetu mwingine Bw. Ali Hamisi Kimani, S.L.P169-40602,Ndori KENYA, naye anaanza kwa salamu kwa watangazaji na wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa. Anatumai kuwa tu wazima tukiendelea kuchapa kazi kama kawaida, yeye pia anasema ni mzima kabisa kama gogo. Anasema anapenda kutumia fursa hii kutoa shukrani zake za dhati kwa kuweza kudumisha mawasiliano mazuri ya mara kwa mara kupitia njia ya posta na radio pia. Anasema ama kwa kweli anafurahia sana kwa kuwa tumewawezesha na kuwarahisishia kutuma salamu kwa jamaa na marafiki na hata kutuma maoni na dukuduku zao juu ya matangazo yetu kwa njia mbalimbali.

    Anasema atakuwa mtovu wa shukurani, kama hajampongeza Rais Hu jintao na serikali ya China kwa misaada wanayotoa mara kwa mara kwa serikali ya nchi yake ya Kenya, ili kuanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali ya kuinua uchumi. Anasema anapenda uhusiano huu mwema uendelee kwa manufaa ya nchi zote mbili. Vilevile anasema angependa kuipongeza serikali ya China kutokana na mbinu murua inazochukua za kukabiliana na homa kali ya H1N1 aina ya A, ambayo wengine wanafikiria kwa kubadilisha jina hili badala ya homa ya mafua ya nguruwe basi huenda mambo yatabadilika. Anasema hana mengi, zaidi ya kututakia kila la heri katika kazi zetu za kila siku.

    Shukrani za dhati Msikilizaji wetu Ali Hamisi Kimani kwa maoni yako, ni kweli serikali ya China iko mstari wa mbele katika kusaidia nchi mbalimbali hasa zilizopo barani Afrika na hii ni kutokana na usuhuba uliopo kati ya China na nchi za Afrika, hili ni jambo jema la kupigiwa mfano, jambo muhimu ni kuzidisha mshikamano uliopo kati ya wananchi wa China na Afrika kwa jumla. Na kuhusu mbinu zilizochukuliwa na China za kukabiliana na homa ya H1N1 aina ya A, kweli ni murua kama ulivyosema na hii ni kwasababu ya bidii za viongozi pamoja na wananchi wa China za kupambana na ugonjwa huo, na serikali isipofanya hivyo inaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ikizingatiwa kuwa China ni nchi yenye watu wengi ingawa kuna baadhi ya nchi waliiilaumu China kwa hatua inazochukua.

    Msikilizaji wetu mwingine Bi. Zuhura Khavere wa sanduku la posta 34 40602, Ndori Kenya ametuletea barua akianza kutusalimu. Anasema ni matumaini kuwa sote tu buheri wa afya, na kama kawaida tunaendelea kuchapa kazi, na yeye huko aliko hana neno na anaendelea vyema kabisa na masomo yake.

    Bi Zuhura anasema ameandika barua hii akiwa na furaha kubwa kutokana na zawadi ndogo ndogo tunazomtumia mara kwa mara. Inagawaje zawadi hizi kwa ukubwa zinaonekana ndogo, lakini kwake yeye ni zawadi zenye thamani kubwa sana, kwani ni ishara ya uhusiano wa ushirikiano mwema baina yake na Radio China kimataifa. Anasema hivi karibuni tulimtumia zawadi za bahasha zilizolipiwa gharama za stempu, kadi za salamu, kalenda ya mwaka huu wa 2009, picha za wanyama mbalimbali na picha zinazoonyesha Ukuta Mkuu wa China. Anashukuru sana, na anataraji kuwa siku moja atatunukiwa zawadi nono katika maswali ya chemshabongo. Anamaliza barua yake kwa kutupongeza sote kwa kazi za kila siku. Pia anasema kuna nyakati huwa anapata matatizo kidogo kusikia matangazo yetu kupitia masafa mafupi, lakini hana budi kukaa na kusubiri kwa hamu..

    Tunakushukuru sana Bi. Zuhura Khavere kwa barua yako nasi pia tunasema tumefurahi kuona zawadi tunazotuma zinafika kwa wasikilizaji wetu, waswahili wanasema pokea zawadi japokuwa dhaifu kwa hiyo hata kama ni ndogo tunashukuru umepokea na umeifurahia.

    Na msikilizaji wetu mwingine Bw Geophrey Wandera Wamachi wa kampuni ya Everyday Security, sanduku la posta SF 333 Nairobi Kenya, ametuletea barua akisema, kila mara yeye huwa anapenda sana kufuatilia kipindi cha mazungumzo kati ya Mama Chen, Bwana Fadhili pamoja na Jane kwenye mawimbi ya 91.9 FM hapa jijini, Nairobi. Kipindi ambacho huwa kinaangazia maswala ya mila desturi na vilevile utamaduni wa wachina. Kipindi ambacho wachambuzi wa kihistoria walikichambuwa wiki hii ni kile cha mapishi mbalimbali ya vyakula vya kichina.

    Anasema kwa mujibu wa matangazo hayo, Mama Chen alisema mapishi ya Wachina yanaambatana na dhamira ya mila, desturi, na utamaduni wa kila kabila. Naye Bwana Fadhili alitoa mfano wa Upishi wa nyama, alisema watu wa kusini mwa China wakipika nyama, itakuwa na ladha tofauti na upishi wa watu wa kasikazini mwa China. Hivyo hivyo watu wa magharibi pia upishi wao ni tofauti na wale wa mashariki. Inagawa wote wamepika nyama, lakini desturi zao za upishi zitafanya nyama iwe na ladha tofauti. Jambo ambalo lilinifurahisha katika kipindi hiki cha mazungumzo ni kuwa, kwa Wachina kuna vyakula fulani vinavyopikwa kwa sababu maalumu.

    Bw Wamachi anasema mama Chen ambaye ni mwenyeji wa China alisema wakati wa ndoa kuna chakula maalumu kinachopikwa kwa sababu ya ndoa, hivyo hivyo kuna chakula maalumu kinachopikwa kwa ajili ya harusi, pia kuna chakula kinachopikwa kwa ajili ya kuzaliwa mtoto. Vilevile kuna chakula cha mazungumzo, na pia inajulikana kuwa upishi nchini China unaambatana na dhamira ya mila, desturi, na utamaduni wa kila kabila. Hata hivyo upishi huo unazingatiwa sana kulingana na wakati maalumu. Anasema amefurahia sana kujua mambo haya, kwani yamemfunza mengi kuhusu mapishi na mila za utamaduni za China. Mwisho anatoa pongezi kwa kipindi na vilevile pongezi mara dufu kwa wandaaji wa makala hizi za mazungumzo kwenye 91.9FM.

    Shukrani msikilizaji wetu Geophrey Wandera kwa barua yako, inaonekana unapenda sana mapishi hasa ya kichina, kweli wachina ni watu ambao wana mambo mengi sana na hii si kwenye mapishi tu bali hata kwenye mambo mengine, lakini kwa vile umezungumzia mapishi ni sawa kabisa kwani kila sherehe ina upishi wake maalum kwa ajili ya sherehe hiyo na kila chakula kinakizidi kingine kwa utamu hayo ndio mapishi ya China ingawa unaweza kukuta ladha tofauti lakini vyote ni vitamu kupita kiasi.

    Mafanikio ya ujenzi wa mfumo wa sheria nchini China katika miaka 60 iliyopita

    Wasikilizaji wapendwa, leo tunawaletea makala ya pili ya chemsha bongo kuhusu miaka 60 ya Jamhuri ya watu wa China, kuhusu mchakato wa China katika ujenzi wa mfumo wa utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria.

    Kabla ya kuwasomea makala hii tuwaletea maswali mawili ili muweze kusikiliza vizuri makala na kuyajibu maswali. Swali la kwanza: China ilikuwa imepata maoni mangapi kuhusu katiba yake ya kwanza kutoka kwa raia wake? Swali la pili: Hivi sasa nchini China kuna sheria ngapi zinazofanya kazi?

    Tarehe 1 Oktoba mwaka 1949, sauti ya mwenyekiti Mao Zedong ya kutangaza kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China ilishangiliwa kwa furaha na watu waliotoa vifijo na vigelegele kwenye uwanja wa Tian An Men mjini Beijing. Tangu hapo ukurasa mpya wa historia ya taifa moja lililokumbwa na vurugu za vita kwa miaka mingi ukafunguliwa.

    Utawala mpya wa Jamhuri ya Watu wa China ulikuwa tofauti kabisa na mfumo wa jamii wa zamani, si kama tu madaraka yote ya nchi yaliwekwa chini ya wananchi wote, bali pia ulilenga malengo ya juu na ya mbali ya kutokomeza unyonyaji, kuondoa pengo na kutafuta utajiri wa pamoja. Katika mwaka wa 5 baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, "Katiba ya Jamhuri ya Watu wa China" ilitolewa. Kabla ya kutolewa kwa katiba hiyo, mswada wa katiba ulikabidhiwa kwa wananchi wote ili ujadiliwe kwa miezi mitatu, ambapo China ilikuwa imepata maoni milioni 1.38 kuhusu katiba yake ya kwanza kutoka kwa raia wake, katiba hiyo ikatolewa baada ya kurekebishwa kwa mujibu wa maoni hayo ya raia, na athari nzuri ya katiba hiyo kwa mchakato wa mfumo wa utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria wa China mpaka sasa unasifiwa na wanasheria wa China. Mtaalamu maarufu wa elimu ya sheria wa China Bw. Li Buyun alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alizungumzia kanuni mbili zilizowekwa kwenye katiba hiyo. Alisema:

    "Tuliwahi kutoa katiba ya nchi mwaka 1954, katiba hiyo ilikuwa nzuri, kwani kuna kanuni mbili kwenye katiba hiyo, kanuni hizo ni: utekelezaji huria wa sheria na utungaji wa sheria wa kidemokrasia."

    Lakini "mapinduzi makubwa ya utamaduni" yaliyodumu kwa miaka 10 ambayo yalitokea bila kutazamiwa, yalikwamisha ujenzi wa utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria nchini China. Bw. Li Buyun alisema:

    "Baada ya kukumbwa na mapinduzi hayo makubwa ya utamaduni, watu wa chama kizima na nchi nzima wamepata mafunzo na kutambua kuwa, bila ya kufuata sheria, utawala wa nchi utashindwa. Kutawala nchi kwa mujibu wa sheria ni nia ya watu, kanuni za historia, matakwa ya lazima ya kujipatia maendeleo ya ustaarabu wa jamii ya binadamu, na ni moyo wa zama za hivi sasa".

    Mwaka 1978 ulikuwa mwaka usioweza kusahaulika katika historia ya Jamhuri ya Watu wa China. Sera ya mageuzi na ufunguaji mlango iliyoanza kutekelezwa mwaka huo iliifanya China ishike njia ya kujiendeleza ili kuwa nchi yenye nguvu, ambapo China ilidhihirisha bayana kuwa, ni lazima "kuendeleza demokrasia ya ujamaa na kujenga utawala wa nchi ya ujamaa kwa mujibu wa sheria." Kufuatia kutolewa kwa sheria mbalimbali kuhusu uhalifu wa kijinai, ujenzi wa mfumo wa kisheria nchini China ukaingia katika kipindi kizuri.

    Hivi sasa mfumo wa sheria wa kijamaa wenye umaalum wa kichina umeundwa kimsingi, na kiini cha mfumo huo ni katiba ya nchi. Kanuni mbalimbali kuhusu "watu wote kuwa sawa chini ya sheria", "kutawala nchi kwa mujibu wa sheria", "taifa kuheshimu na kulinda haki za binadamu", na "mali za raia haziruhusiwi kuvamiwa" zote zimeandikwa kwenye katiba ya nchi, na kuwa kanuni za katiba. Kanuni ya "kuitawala nchi kwa mujibu wa sheria" imekuwa mkakati wa kimsingi wa nchi kuanzia mwaka 1999. Mtaalamu wa elimu ya sheria Bw. Li Buyun anajivunia sana na kazi yake alisema:

    "Katika maisha yangu ya kushughulikia elimu ya sheria, mambo mawili yanastahiki kutajwa, moja ni kutetea utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria, lingine ni kutetea haki za binadamu, masuala hayo mawili yote yamewekwa kwenye katiba ya nchi."

    Hivi sasa "katiba ya nchi" na "sheria kuhusu utungaji wa sheria" nchini China vimekuwa na mfumo wa utungaji wa sheria wa kisayansi ulio wa pamoja na kugawanywa kwenye ngazi tofauti, ambapo katiba na sheria kuhusu katiba, sheria kuhusu raia na biashara, sheria ya utawala wa nchi, sheria ya uchumi, sheria ya jamii, sheria ya uhalifu wa jinai, sheria ya utaratibu wa kutoa mashitaka au kutotoa mashitka na kadhalika zimefikia 231 kwa hivi sasa, ambapo mambo yote yanayohusu uchumi, siasa, utamaduni na maisha ya jamii yanaweza kufanyika kwa mujibu wa sheria, kiwango cha utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria kimeinuka sana.

    Mafanikio yaliyopatikana katika ujenzi wa utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria hayawezi kuhesabiwa. Kwa mfano maendeleo makubwa yamepatikana katika elimu ya sheria, hivi sasa vyuo na vyuo vikuu vya elimu vimezidi 600 kote nchini; maendeleo makubwa yamepatikana katika utafiti wa elimu ya sheria, ambapo vimechapishwa vitabu vingi kuhusu taalum za sheria za nchini na nje. Aidha umetolewa utaratibu wa kuhakikisha kazi ya kutunga sheria kwa njia ya kisayansi na kidemokrasia, hivi sasa baada ya kutungwa kwa mswada wa sheria, kusikiliza maoni ya watu wa jamii imekuwa ni desturi; na kazi ya kuhimiza serikali iwe serikali ya utoaji wa huduma, na kuhimiza mageuzi ya mfumo wa sheria kumewawezesha wananchi wa China wajionee kuwa kiwango cha serikali cha kufanya mambo ya utawala kwa mujibu wa sheria, na kutekeleza sheria kwa haki pia kinainuka siku hadi siku, utekelezaji wa sheria umeimarisha hali ya kudhibiti na kusimamia matumizi ya madaraka.

    Mtaalamu wa elimu ya sheria Bw. Li Buyun anafurahia hali nyingi akisema:

    "Kutawala nchi kwa mujibu wa sheria na haki za binadamu, ni mitizamo miwili inayofuatwa na kutumiwa na umati wa watu na makada, na imekuwa silaha yao ya kifikra, hii imenitia moyo sana."

    Bw. Li Buyun anaona kuwa, katika miaka 60 iliyopita tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, haki za binadamu walizo nazo wachina zimehakikishwa kisheria, nchini China maneno kuhusu "kuheshimu na kuhakikisha haki za binadamu, na kusukuma mbele maendeleo ya pande zote ya mambo ya haki za binadamu" yanasisitizwa na kuzungumzwa zaidi na watu kwenye jamii, na maneno kuhusu "taifa kuheshimu na kuhakikisha haki za binadamu" yameandikwa kwenye katiba. Hivi sasa sheria zinazohusiana na kuhakikisha haki za bindamu pamoja na mikataba ya kimataifa iliyoidhinishwa nchini China zimefikia zaidi ya 250, haki na maslahi ya wanawake, wazee, watoto, walemavu na watu wa makabila madogomadogo yanalindwa kwa sheria mbalimbali maalum.

    Bw. Li Buyun akiwa mtafiti wa sheria anaona kuwa, katika ujenzi wa mfumo wa sheria miaka 60 iliyopita, China imepiga hatua moja baada ya nyingine, na kupita kipindi kimoja hadi kingine vyenye vipengele, kutoka kutilia maanani kazi ya kuimarisha utawala wa serikali mpya hadi kuzingatia kwa makini uendeshaji mzuri wa utawala wa nchi, hadi kujenga mazingira mazuri ya utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya mageuzi na ufunguaji mlango na uchumi wa soko huria, mpaka kulinda mamlaka ya nchi, maslahi ya taifa, maslahi ya jamii na maslahi ya raia binafsi. Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao alisema:

    "Ujamaa hautengani na demokrasia na utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria. Naona demokrasia, utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria, uhuru, haki za binadamu, usawa, na upendo kwa watu wote, hayo yote siyo tu mambo ya ubepari tu, bali ni matokeo ya ustaarabu ulioundwa katika mchakato wa historia ndefu ya dunia nzima, pia ni mtizamo wa pamoja wa binadamu juu ya thamani ya mambo."

    Ufahamu juu ya utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria umetia mizizi miyoni mwa watu siku hadi siku nchini China, na China itaendelea kushika njia hiyo. Wataalamu wengi wa sheria wa China wanaona kuwa, ujenzi wa mfumo wa sheria wa China ni wenye umaalum wa kichina, lakini hauko katika hali ya kutengwa, kadiri mambo ya mageuzi na ufunguaji mlango yanavyofanyika kwa kina nchini China, ndivyo upeo wa kutupia macho dunia nzima unaonekana dhahiri siku hadi siku katika ujenzi wa mfumo wa sheria nchini China.

    Wasikilizaji wapendwa, sasa tunarudia maswali yetu mawili: Swali la kwanza: China ilikuwa imepata maoni mangapi kuhusu katiba yake ya kwanza kutoka kwa raia wake? Swali la pili: Hivi sasa nchini China kuna sheria ngapi zinazofanya kazi?

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako