• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Walimu wa Chuo kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing wafanya juhudi katika ufundishaji na utafiti wa lugha ya Kiswahili

    (GMT+08:00) 2009-07-17 14:40:12

    Pro Sun Baohua

    Kiswahili ni lugha inayotumiwa na watu wengi sana barani Afrika, na kuanzia miaka ya 60 ya karne iliyopita hadi leo, vyuo vikuu vingi vya China vimeanza kufundisha lugha ya Kiswahili, na kuwavutia vijana wengi wanaoipenda Afrika.

    Wapendwa wasikilizaji, mliyosikia ni sauti ya wanafunzi wakisoma vitabu katika darasa la Kiswahili la chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing. Vijana hao walijiunga na chuo hicho mwezi Septemba, mwaka 2008, na hii ni mara yao ya kwanza kugusa lugha hiyo ya Afrika. Mwanafunzi mmoja kati yao anayeitwa Ning Yi alisema,

    "Kiswahili ni lugha nzuri sana. Naona wachina na waafrika ni marafiki wakubwa sana, kama tunaweza kujifunza lugha hii vizuri, tutaweza kupata habari mbalimbali kuhusu Afrika, pia katika siku za baadaye tutaweza kuwasiliana nao vizuri. Utamaduni wa Afrika unavutia sana, na mandhari yake ni nzuri sana. Sisi wananfunzi tunaipenda Afrika na tunakipenda Kiswahili."

    Nchi za Afrika zilipata uhuru katika miaka ya 60 ya karne iliyopita. Na kiswahili kikiwa lugha ya kienyeji ya Afrika, nafasi yake iliinuka sana. Ili kuimarisha mawasiliano na nchi za Afrika na watu wake, mwaka 1961 chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing zilianzisha kozi ya Kiswahili. Katika karibu nusu karne iliyopita, chuo hicho kimeliandalia taifa wahitimu wenye ujuzi wa lugha ya kiswahili 200 hivi ambao wametoa mchango mkubwa katika kuzidisha urafiki, mawasiliano na ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika Mashariki.

    Pro. Sun Baohua wa Chuo hicho ni mwalimu mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 30 wa kufundisha Kiswahili, alipojulisha hali ya ufundishaji wa Kiswahili katika chuo hicho alisema,

    "Somo la Kiswahili hufuata utaratibu wa kufundisha kwa miaka 4. Miaka miwili ya kwanza tunakiita kama kipindi cha kuwawekea msingi wanafunzi ambapo tunafungua somo rasmi la Kiswahili, somo la maongezi, somo la kusikiliza na somo la ziada. Na miaka miwili ya pili tunaweka kipindi cha kuinua uwezo wa lugha na wanafunzi wanatakiwa kufundishwa somo la magazeti ya Kiswahili, somo la ukalimani, somo la kutafsiri, somo la fasihi ya Kiswahili pamoja na somo la habari za nchi za Afrika Mashariki."

    Pro. Sun aliwahi kusoma na kufanya kazi kwa miaka 7 nchini Tanzania na Kenya, katika kipindi hicho alitambua umuhimu wa kutunga vitabu vya kufundisha Kiswahili vinavyowafaa wanafunzi wa China, alisema,

    "Kwa maoni yangu ufunguo wa kufanikisha katika ufundishaji wa lugha za kigeni unahusiana na mambo matatu, ambayo ni walimu hodari, wanafunzi wenye bidii na nia dhati ya kujifunza, na vitabu vya kufundishia. Sasa tuyaweke kando mambo mawili ya mwanzo, tuzungumzie vitabu vya Kiswahili. Pengine huwezi kunipinga kama nikisema vitabu vya kufundishia Kiswahili ni muhimu sana ama kwa mwalimu au kwa mwanafunzi. Historia yetu imetuambia kuwa bila ya vitabu vya kufundishia ni vigumu sana kufundisha Kiswahili vizuri. Bila ya vitabu mwalimu huwezi kupata mtiririko au mfuatano wa lugha na sarufi za Kiswahili anaweza akajisikia kama anatembea kwenye aponji na vile vile mwanafunzi hawezi kupewa mazoezi ya kutosha na ya kisayansi."

    Kutokana na juhudi za prof. Sun na wenzake wawili wakiwemo prof. Cao Qin na prof. Feng Yupei, utungaji na uhariri waseti ya kwanza ya vitabu vya mafunzo ya Kiswahili nchini China uilikamilika mwaka 1989. Seti hiyo ina vitabu vinne, Vitabu viwili vya kwanza vinatumika katika miaka miwili ya mwanzo na vingine vinatumiwa katika mwaka wa tatu na wa nne. Vitabu viwili vya mwanzo vinalenga ufundishaji wa matamshi, sarufi za kimsingi na misamiati na uwezo wa kuongea Kiswahili, na vitabu vingine viwili vina mazoezi mbalimbali ya maongezi, kisarufi na ukalimani.

    Hadi sasa kwa kufuatia maendeleo na mabadiliko ya siasa, uchumi na jamii ya sehemu ya Afirka Masharika, lugha ya Kiswahili inaendelezwa kwa kasi. Walimu wa chuo hicho wamegundua kuwa seti ya vitabu hivyo iliyohaririwa miaka ya 80 ya karne iliyopita inatakiwa kufanyiwa marekebisho. Prof. Sun alisema,

    "Baada ya kuvitumia miaka 17 hivi tumeona kuwa iko haja ya kufanya marekebisho katika baadhi ya sehemu ambazo zimepitwa na wakati na tumemaliza kazi ya kuziba viraka vyake. Mambo ambayo tumeongeza kwenye vitabu hivi sana sana ni utamaduni wa waswahili, watu mashuhuri wa Kenya n.k hata vikachapiswa tena katika mwaka 2007 na 2008. Vitabu vingine viwili vimo mbioni kutayarishwa pengine vitachapishwa mwakani."

    Licha ya kuongeza misamiati mipya, vitabu vipya hivyo vimeongeza vitu vingi vipya vikiwemo mila na desturi na utamaduni wa Afrika Mashariki, na makala inayohusu naibu waziri wa mazingira na maliasili wa Kenya Bi. Wangari Maathai aliyepata tuzo ya Nobel.

    Mbali na hayo, chuo hicho kinashirikiana na vyuo vikuu vya nchi za Afrika Mashariki, na kinawatuma wanafunzi kusoma nchini Tanzania na Kenya. Bi. Li Yike ni mwanafunzi aliyewahi kusoma katika chuo kikuu cha Dar es Salaama kwa mwaka mmoja, anaona kuwa njia hii ya kupelekana wanafunzi inamsaidia sana. Alisema,

    (Sauti 5)

    "Niliposoma nchini Tanzania, nilipenda na kuvutiwa sana na mila na desturi za Afrika Mashariki na mandhari yake nzuri. Naona kusoma kwangu huko kumenisaidia sana, na kuniwezesha nifahamu zaidi utamaduni na historia ya Tanzania. Nakishukuru sana chuo kikuu chetu na chuo kikuu cha Dar es Salaam kutoa nafasi hizo nzuri kwa sisi wanafunzi."

    Nusu karne imepita, wanafunzi 200 waliohitimu somo la kiswahili wa chuo hicho wanafanya kazi zao katika idara mbalimbali za mawasiliano kati ya China na nchi za Afrika Mashariki. Hasa katika kazi za ufundishaji wa Kiswahili, katika vyuo vikuu vinne vinavyofundisha lugha hiyo kuna wahitimu wa chuo hicho wanaofanya kazi ya kufundisha kiswahili. Mwalimu wa chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Tianjin Bi. Rui Jufen pia ni mmoja kati ya wahitimu hao, alimwambia mwandishi wetu akisema,

    (Sauti 7)

    "Baada ya kuhitimu masomo nilikwenda Tanzania, mandhari nzuri ya Tanzania na Kenya, ukarimu wa wenyeji wa huko viliniachia picha nzuri isiyosahaulika. Sasa ninafanya kazi ya kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha lugha za Kigeni cha Tianjin, nimenuia kueneza Kiswahili na utamaduni wa waswahili kadiri niwezavyo, maana ninaipenda ardhi hiyo ya Afrika ya Mashariki kwa moyo wote."

    Wasikilizaji wapendwa, mliyosikia ni maelezo kuhusu "Walimu wa Chuo kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing wanavyofanya juhudi katika ufundishaji na utafiti wa lugha ya Kiswahili", kipindi hiki cha Daraja la Urafiki kati ya China na Afrika kwa leo kimeishia hapa, asanteni kwa kuwa nasi, kwa herini.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako