• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mfasiri mkubwa Bw. Gao Mang

    (GMT+08:00) 2009-07-20 15:11:26

    Mfasiri Gao Mang na mkewe

    Mfasiri Gao Mang mwenye umri wa miaka 83 mwaka huu, alianza kazi ya kutafsiri maandishi ya fasihi ya Russia tokea miaka ya 40 ya karne iliyopita. Katika miongo kadhaa iliyopita amepata mafanikio makubwa katika kazi ya kutafsiri, kuhariri na kufanya utafiti kuhusu fasihi ya Russia. Kutokana na mafanikio hayo alitunukiwa nishani na rais wa Russia. Bw. Gao Mang licha ya kuwa mfasiri mkubwa pia ni mchoraji, picha alizochora za wanafasihi wengi mashuhuri wa Russia zimehifadhiwa katika majumba ya makumbusho ya fasihi za nchi za nje.

    Bw. Gao Mang alizaliwa mwaka 1926 katika mji wa Harbin mkoani Heilongjiang, kaskazini mashariki mwa China. Alipokuwa na miaka saba alijiunga na shule iliyokuwa inaendeshwa na wamisionari, na kwa kuwa wanafunzi wenzake wote walikuwa wanaongea Kirusi na walimu pia walifundisha kwa Kirusi, hivyo Bw. Gao Mang aliathiwa na mvuto wa lugha ya Kirusi toka alipokuwa mtoto. Hali kadhalika, Bw. Gao Mang aliwahi kufundishwa na wachoraji wakubwa watatu wa Russia, na hata alipokuwa na umri wa miaka kumi hivi aliweza kushiriki kwenye maonesho ya picha. Mwaka 1937 shule yake ilipofanya maadhimisho ya miaka 100 tangu mshairi mkubwa wa Russia Sergeevich Pushkin afariki dunia, aliombwa achore picha ya mshairi huyo ili itundikwe darasani. Bw. Gao Mang alisema,

      "Nilipoona picha niliyochora imetundikwa darasani nilikuwa sijui nieleze vipi hisia zangu, tokea hapo nilikuwa naitupia macho picha hiyo mara kwa mara hata kama nikiwa katika masomo, ingawa picha hiyo niliichora kwa kuiga tu lakini inaonesha upendo wangu, nikifikiri hatimaye nitachora picha yake kwa mujibu wa nionavyo moyoni mwangu."

    Tafsiri yake ya kwanza kabisa ilichapishwa mwaka 1943 wakati huo Bw. Gao Mang alikuwa na umri wa miaka 17, hii ilikuwa ni tafsiri ya shairi lililoandikwa na Sergeevich Turgenev liitwalo "Mawaridi Haya Yalikuwa na Uzuri Ulioje". Bw. Gao Mang alisema,

      "Wakati nilipotafsiri shairi hilo nilikuwa nimesoma katika shule hiyo kwa miaka 10, na nilianza kupenda fasihi ya Russia. Shairi hilo lilikumbusha maisha ya mshairi aliyekuwa Ufaransa wakati alipokuwa mzee, lugha ya shairi hilo ni tamu sana, ingawa shairi hilo si refu, lakini liligusa hisia zangu, basi niliamua kujaribu kulitafsiri."

      Shirika la gazeti lililochapisha shairi hilo lilidhani kuwa Bw. Gao Mang ni bingwa wa kutafsiri, likamwomba atafsiri mashairi mengi zaidi, basi tokea hapo akaanza kushika maisha ya kutafsiri fasihi ya Russia.

    Mwaka 1947 Gao Mang alitafsiri kitabu cha tamthilia cha Russia cha "Pavel Korchagin", hii ni tamthilia iliyohaririwa kwa mujibu wa riwaya iliyoandikwa na mwandishi wa vitabu asiyeona Nikolai Ostrovsky inayoelezea "Jinsi Chuma na chuma cha Pua kilivyofuliwa". Ushupavu wa mhusika mkuu katika riwaya hiyo wa namna alivyopambana na hali ngumu bila kukata tamaa uligusa sana hisia zake. Bw. Gao Mang alisema,

      "Kwa mara ya kwanza niliposoma kitabu cha tamthilia hiyo nilivutiwa sana, nilishangaa kuona mtu shupavu kama Pavel Korchagin. Wakati huo wavamizi wa Japan walikuwa wameanzisha serikali ya kiharamu katika Manchuria kaskazini mashariki mwa China, wananchi walinyanyaswa kama watumwa, nikifikiri ni jambo muhimu sana kupata watu wanaopigania kishupavu uhuru wa umma kama Pavel Korchagin, kutokana na wazo hilo nilitafsiri kitabu hicho, wakati huo maandishi kama hayo ya uzalendo na kuhamasisha wananchi yalikuwa yanahitajika sana."

      Baadaye tamthilia "Pavel Korchagin" aliyotafsiri ilioneshwa katika majumba mbalimbali ya michezo ya sanaa nchini na ilikuwa na athari kwa vijana kizazi hadi kizazi. Cha kufurahisha ni kuwa, tamthilia hiyo ilipooneshwa kwa mara ya kwanza, mwigizaji wa kike wa kwanza wa mhusika mkuu wa tamthilia hiyo ndio akawa mke wa Gao Mang baadaye, wakitegemeana na kusaidiana maishani mwao.

      Mwaka 1946 alipokuwa na umri wa miaka 20 Gao Mang alijiunga na Shirikisho la Urafiki wa China na Russia mjini Harbin. Kwa sababu alipenda kutumia majina tofauti kuchapisha maandishi yake kwenye magazeti, mtafiti mashuhuri wa fasihi ya nchi za nje Bw. Ge Baoquan alipoona huko Harbin kulikuwa na watu wengi wanaotafsiri na kutafiti fasihi ya Russia aliwaalika kwenye mkutano, kumbe aliyekwenda mkutanoni alikuwa Gao Mang peke yake tu, kwani majina yote yaliyotumika katika magazeti yalikuwa ni majina yake ya uandishi.

      Jamhuri ya watu wa China ilianzishwa Mwaka 1949, tokea hapo Bw. Gao Mang akaanza kujitosa katika maingiliano ya kifasihi kati ya China na Russia na kazi ya kutafsiri. Mwaka 1997 alipokelewa kuwa mwanachama wa heshima wa Shirikisho la Waandishi wa vitabu wa Russia, na mwaka huo alitunukiwa nishani na aliyekuwa rais wa Russia Boris Yeltsin kutokana na mchango wake mkubwa katika maingiliano ya kifasihi kati ya China na Russia.

      Bw. Gao Mang alitumia miaka yote kufanya utafiti wa fasihi ya Russia na amepata mafanikio makubwa, lakini alipokuwa mzee amekuwa mtu wa kwanza kabisa nchini China kueleza utamaduni wa makaburi ya Russia. Kwa mara ya kwanza Bw. Gao Mang alikwenda Moscow kuzuru makaburi ya miaka ya 50 ya karne iliyopita na hatimaye kwa mara kumi kadhaa alizuru makaburi mengi nchini humo ikiwa ni pamoja na makaburi ya watu mashuhuri, mwishowe katika mwaka 2000 alifanikiwa kuandika kitabu chake cha "Makazi ya mwisho ya roho---Utamaduni wa Makaburi Nchini Russia". Kitabu hicho kinaeleza historia na maisha ya watu mashuhuri waliofariki, sanamu zao na thamani ya makaburi hayo, ndani ya kitabu kuna picha nyingi alizochora. Kitabu kilipozinduliwa tu mara kiligombewa na wasomaji, wakiona kuwa kitabu hicho kimeonesha utamaduni unaong'ara wa taifa kubwa kutokana na mtazamo usio wa kawaida.

      Mwaka huu Bw. Gao Mang ameandika kitabu kipya kiitwacho "Jiwe la Kaburi na Peponi" kikielezea kuhusu waandishi wa vitabu na wasanii wakubwa zaidi ya 80 wa Russia walivyokuwa na uhusiano na China na ushawishi wao nchini China. Bw. Gao Mang amejihusisha na kazi ya kutafsiri kwa miongo kadhaa, anaona kwamba kutafsiri lugha ni taaluma ngumu, kwa hiyo kuweka mwaka wa lugha ya Kirusi nchini China ni jambo lenye mtazamo wa mbali. Alisema,

      "Hii ni mara ya kwanza kuwekwa mwaka huu kuwa ni mwaka wa lugha ya Kirusi katika historia ya China na Russia, maana yake ni kuinua lugha hiyo kwenye nafasi muhimu, hayo yatakuwa ni mafanikio makubwa kama tukiweza kuandaa wafasiri wengi wapya. Tumetambua umuhimu wa lugha, na tumeona lugha inaendelea siku zote, shughuli hiyo itasaidia kustawisha maingiliano ya kifikra moja kwa moja."

      Bw. Gao Mang alisema, mwaka 1999 mshairi mkubwa Sergeevich Pushkin alipotimiza miaka 200 tangu azaliwe alichora picha ya mshairi huyo ikiwa ni zawadi kwa jumba la makumbusho la Pushkin huko Moscow. Kutokana na utafiti wake wa miaka mingi, Bw. Pushkin alikuwa na hamu kubwa ya kuitembelea China na alitaka kutembelea Ukuta Mkuu, kwa hiyo katika picha hiyo Bw. Gao Mang alimsaidia Bw. Pushkin kutimiza matumaini yake, kwamba alichora picha yake yenye mazingira ya Ukuta Mkuu.

      Aidha, Bw. Gao Mang alisema mwanafasihi mashuhuri wa Russia Leo Tolstoy alipokuwa hai alikuwa akifanya utafiti juu ya falsafa ya China ya zama za kale, siku hizi Bw. Gao amekuwa akichora picha ya mwanafasihi huyo mashuhuri akiwa anazungumza na Confucius. Bw. Gao Mang alisema fasihi ya Russia ina historia ndefu sana, anaona kwamba muda si mrefu baadaye wimbi jipya la wasomaji wa fasihi ya Russia litatokea nchini China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako