• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 0721

    (GMT+08:00) 2009-07-21 17:00:37

    Mafanikio ya kilimo yaliyopatikana nchini China katika miaka 60 iliyopita

    Wasikilizaji wapendwa, leo tunawaletea makala ya tatu ya Chemsha bongo kuhusu miaka 60 ya Jamhuri ya Watu wa China, kuhusu Mafanikio ya kilimo yaliyopatikana nchini China katika miaka 60 iliyopita. Katika miaka 60 iliyopita, serikali ya China siku zote imefanya juhudi katika ujenzi wa vijiji, ambapo si kama tu imetatua suala la chakula kwa wananchi wake bilioni 1.3, bali pia imeweza kuyafanya maisha ya wakulima yawe na mabadiliko makubwa sana.

    Kabla ya kuwasomea makala hii, kwa tunatoa maswali mawili: Swali la kwanza, China inalisha watu wake ambao idadi yao inachukua 22 % ya watu wote duniani, kwa mashamba yake yanayochukua asilimia ngapi ya eneo la mashamba duniani? Swali la pili. Uzalishaji wa nafaka nchini China kwa mwaka 2008 ulikuwa ni tani ngapi?

    Suala la lishe lilikuwa suala kubwa nchini China. Bw. Long Yongtu aliyezaliwa mwaka 1943 huko Changsha, katikati ya China, sasa ni Katibu mkuu wa Baraza la Asia la Boao, yeye ni mtu mashuhuri. Alipokumbusha hali alipokuwa anakua alisema, wananchi wa rika yake wote waliwahi kukumbwa na hali ya njaa. Alisema:

    "Wachina wa rika yangu tulikuwa tunakumbwa na njaa, maisha yalikuwa magumu. Tulipokuwa na njaa tulikula maboga mengi, ndiyo maana sasa kila ninaponusa harufu ya boga nahisi kutaka kutapika."

    China ni nchi kubwa inayoshughulikia kilimo, idadi ya wakulima inachukua nafasi kubwa ya idadi ya jumla ya watu nchini China. Katika zama za miaka ya 40 ya karne iliyopita, kutokana na mbinu za kizamani za uzalishaji wa kilimo, pamoja na maafa ya ukame na mafuriko, uzalishaji wa kilimo ulizorota, ambapo mazao makuu ya kilimo yalikuwa na upungufu mkubwa, pamoja na kukumbwa na vurugu za vita zilizodumu kwa miaka mingi, hivyo watu wengi walikuwa na njaa na hawakuweza kupata nguo za kutosha. Mwaka 1949 kwa wastani, kila mkulima wa China alikuwa anaweza kupata nafaka kilo 180 tu.

    Baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949, China ilitumia miaka mitatu kufanya mageuzi ya ardhi, ambapo wakulima walipata ardhi, mifugo na vyombo vya kilimo ambavyo vingi vilikuwa miongoni mwa mabwana shamba, sera hiyo iliungwa mkono na wakulima, ndiyo maana uzalishaji wa kilimo ukafufuliwa na kuendelezwa kwa kasi, na uzalishaji wa nafaka na pamba ukazidi ule wa awali. Baada ya mwaka 1952, China ilifanya tena mageuzi katika ujenzi mkubwa wa kimsingi kuhifadhi maji mashambani na ufundi wa kilimo, ikaifanya hali ya uzalishaji wa kililmo iboreshwe kidhahiri, na uzalishaji wa mazao ya kilimo ukaongezeka kwa kasi. Ilipofika mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, uzalishaji wa nafaka na pamba nchini China uliongezeka kwa zaidi ya mara moja kuliko ule wa mwaka 1952.

    Ingawa uzalishaji wa nafaka ulipata ongezeko kubwa namna hii, lakini kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya watu, mazao ya kilimo yalikuwa bado hayajaweza kujitosheleza vya kutosha nchini China. Mkulima wa Kijiji cha Bishen cha mji wa Chizhou mkoani Anhui Bw. Yang Jiliang alisema, suala la chakula siku zote lilichukuliwa kuwa ni jambo kubwa la kwanza katika kijiji chake. Alisema:

    "Katika miaka ya 60 na 70 ya karne iliyopita, nafaka za kutosha hazikuweza kupatikana, wakati huo hata tulikula mboga pori ili kuondoa njaa."

    Wakati huo, mashamba nchini China yaliendeshwa na kusimamiwa pamoja katika kila kijiji, na wanakijiji walipaswa kushiriki kazi kwa pamoja, na kugawana kwa usawa mavuno ya kilimo, hivyo hamasa za wakulima zilikuwa si kubwa. Mwishoni mwa mwaka 1978, wanakijiji wa Kijiji cha Xiaogang mkoani Anhui walitangulia kuamua kugawanya mashamba ya kijiji kwa kila familia ya wakulima ili walime mashamba wao wenyewe, matokeo ya uamuzi huo ni kwamba uzalishaji wa nafaka wa mwaka huo ulifikia mara nne ya wastani wa uzalishaji wa mwaka katika miaka 10 kabla ya hapo. Mwaka 1980, Serikali ya China iliamua kueneza njia hiyo ya Kijiji cha Xiaoga kote vijijini nchini China, ambapo kila familia ilisaini mkataba wa kulima mashamba. Mkulima Yang Jiliang alisema, kijiji chake pia kilitekeleza utaratibu huo, na kila familia ilipata mashamba na kusaini mkataba wa kuyatumia. Alisema: "Baada ya kuanza kutekeleza utaratibu huo, sisi wakulima tuliongeza juhudi za uzalishaji wa nafaka, hivyo suala la lishe limetatuliwa, kihalisi tumeondokana na njaa."

    Takwimu zilizokusanywa zinaonesha kuwa, toka mwaka 1978 hadi mwaka 1984, wastani wa ongezeko la uzalishaji wa mazao ya kilimo ulidumisha asilimia 8 hivi kwa mwaka nchini China. Tangu hapo, uzalishaji wa nafaka ukadumisha ongezeko la utulivu kila mwaka. Mwaka 2008 uzalishaji wa nafaka nchini China ulizidi tani milioni 500.

    Ofisa wa Idara ya nafaka ya taifa ya China anayeshughulikia mpango na malimbikizo ya nafaka Bibi Liu Dongchu alisema, wachina wakatatua suala la lishe kwa kupitia juhudi zao wenyewe, China inatumia mashamba yanayochukua asilimia 7 ya yale ya dunia kuwalisha idadi ya watu inayochukua asilimia 22 ya ile ya dunia, hii kweli ni hali ya kushangaza. Alisema:

    "China inashikilia sera ya kujitegemea katika suala la nafaka, na kuhakikisha utoaji wa nafaka nchini. Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya jumla ya matumizi ya nafaka inalingana kimsingi na idadi ya jumla ya uzalishaji wa nafaka nchini China, na China inadumisha kujitosheleza nafaka kwa zaidi ya asilimia 95.

    Ili kuhamasisha zaidi juhudi za wakulima za uzalishaji wa nafaka, serikali ya China iliongeza ruzuku ya uzalishaji wa nafaka na uunuzi wa vyombo vya kilimo kwa wakulima katika miaka kadhaa iliyopita, ilipofika mwaka 2007, ruzuku zilizotolewa na serikali ya China kwa wakulima zilifikia zaidi ya yuan bilioni 60. Serikali ya China pia iliongeza siku hadi siku ruzuku kwa kilimo, kuendelea kuinua bei ya ununuzi wa nafaka kutoka kwa wakulima kuongeza malimbikizo ya nafaka, mafuta ya kupikia na nyama za nguruwe; kuongeza msaada wa kifedha kwa sehemu muhimu za uzalishaji wa nafaka na kadhalika, ili kuhakikisha kazi ya kuwasaidia wakulima kuongeza mapato yao. Serikali ya China pia ilitoa sera ya kuendeleza kwa nguvu kubwa viwanda vya vijijini na kuwahamasisha wakulima walio ziada ya nguvukazi vijijini waingie mijini kufanya kazi za vibarua, ili kuongeza nafasi za ajira vijijini, na kusukuma mbele maendeleo ya uchumi vijijini. Aidha, China ilifuta kodi za kilimio hatua kwa hatua kuanzia kabla ya miaka minane iliyopita, ilipofika mwaka 2006, kodi za kilimo zilifutwa kwa pande zote, na kodi za wakulima zilizokuwepo kwa zaidi ya miaka 2600 nchini China zikakomeshwa kabisa. Kila mwaka hatua hii iliweza kupunguza mzigo wa zaidi ya yuan bilioni 130 kwa wakulima.

    Chini ya utekelezaji wa hatua hizo zote, wakulima wa China wameongeza mapato, na maisha yao yameboreshwa sana kuliko zamani. Mkulima Yang Jiliang alipozungumzia maisha ya hivi sasa katika kijiji cha Bishen alifurahi sana. Alisema:

    "Hivi sasa wanakijiji wenzangu wengi wamejenga nyumba mpya zenye ghorofa mbili, na baadhi yao wamenunua magari madogo. Nyumbani kwetu vitu vingi vimebadilika kuwa vipya, tunatumia taa na simu au simu za mkononi, maisha yetu kweli yameboreshwa."

    Hivi sasa wastani wa pato la kila mkulima wa China ni mara 30 kuliko lile la mwaka 1978. Idadi ya watu wenye hali ya umaskini kabisa imepungua na kufika chini ya milioni 5 kutoka milioni 250. Bw. Yang Jiliang alisema, serikali pia imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kuimarisha ujenzi wa miundo mbinu ya sehemu ya vijijini. Alisema: (...................6 )

    "kutokana na ufuatiliaji na uungaji mkono wa serikali, barabara, huduma za matibabu, nyumba za wakulima na kiwango cha maisha ya watu, vyote vimeboreshwa na kiwango chake kuinuka."

    Wakati huo huo, China imefanya juhudi kubwa katika kubadilisha njia ya uzalishaji wa kilimo na kuendeleza mambo ya kisasa ya kilimo. Hayo yameonekana kwenye kuinua kiwango cha utumiaji wa mashine za kilimo, na kuimarisha kazi ya kubana matumizi ya raslimali na kutumia raslimali kwa kazi ya jumla. Hivi sasa mashamba yanayolimwa kwa mashine za kilimo yamezidi asilimia 60 ya mashamba yote ya kilimo; njia za kilimo cha kisasa cha kumwagilia maji mashambaji zinaenea hatua kwa hatua katika sehemu zenye hali ya kufaa.

    Kutokana na mpango wa serikali ya China, ifikapo mwaka 2020, wastani wa pato la kila mkulima litaongezeka mara mbili kuliko lile la mwaka 2008, na matumizi ya wakulimayatainuka kwa kiwango kikubwa, na hali ya kuwa na umaskani kabisa itaondolewa kimsingi. Hivi sasa serikali ya China na wananchi wake wanafanya juhudi ili kutimiza lengo hilo.

    Wasikilizaji wapendwa sasa tunarudia maswali yetu mawili: Swali la kwanza, China inalisha watu wake ambao idadi yao inachukua 22 % ya watu wote duniani, kwa mashamba yake yanayochukua asilimia ngapi ya eneo la mashamba duniani? Swali la pili. Uzalishaji wa nafaka nchini China kwa mwaka 2008 ulikuwa ni tani ngapi?

    Barua za wasikilizaji

    Msikilizaji wetu Rurangwa Gerard barua yake pepe ni rurangwa gerard@yahoo.fr

    Ametuletea barua pepe akisema yeye ni mnyaruanda yuko nchini Rwanda tena ni mpenzi sana wa tovuti ya Kiswahili ya CRI kwenye mtandao wa internet, anasema kwa kweli kazi mnayofanya ni nzuri kabisa, anataka tuendelee hivyohivyo. Anasema yeye pia ni mtangazaji wa radio katika redio ya sauti ya Africa kwa lugha ya Kiswahili nchini Rwanda.

    Msikilizaji wetu mwingine ni Amin Najmi, barua yake pepe ni Shukrani nyingi wasikilizaji wetu Rurangwa Gerard na Amin Najmi, kwa maoni na masuali, na tunapenda kumfahamisha Amin kuwa mpango unaoupanga ni sahihi kabisa na maombi yako yamefika kwani tutakutafutia anuani ya chuo na baadaye tutakujibu kwa baruapepe. Na kuhusu suali lako la pili kama kuna shule inayofundisha Kichina nchini China ambayo inahusiana na zile zinazofundisha Kichina nchini Moroco, ni kwamba hapa yapo makao makuu ya chuo cha Confucious ambacho kinatoa mafunzo hayo ya lugha ya Kichina pamoja na utamaduni wa China ambacho kina matawi mengi tu duniani likiwemo hilo la Morocco, na hii ni kwaajili ya kuwarahishia wale wote wanaopenda kujifunza kichina ambao hawana uwezo wa kuja China, ushauri wetu ni kuwa kwa kuwa Morocco lipo tawi basi ungeanza kujifunza hukohuko kwa hatua ya mwanzo baadae ndio ukafanya

    utaratibu wa kuja huku ili kuongeza ujuzi zaidi.

    Msikilizaji wetu Bw. Mogire O Machuki wa Bogeka village S.L.P. 646, Kisii Kenya ametuletea barua pepe akisema salamu tele kutoka hapa Kisii Kenya. Mie ni mzima huku nikitumai kuwa nanyi pia ni wazima wa afya, nina furaha kuwaarifu kuwa hivi punde nimemaliza kusoma ukurasa wenu wa tovuti na miongoni mwa yale yaliyonivutia ni makala kadhaa mpya na za kupendeza, sehemu ya muziki wa kiafrika inapendeza sana na nimefurahi kuona kuwa mmetenga wiki hii hususani kwa ajili ya mwanamuziki wa Marekani aliyeaga dunia Michael Jackson. Vile vile heko kwa kuanzisha sehemu maalumu na mpya kabisa kuhusu kujifunza lugha ya kichina. Sehemu hiyo inavutia sana na naamini kuwa mtachapisha kitabu ambacho kitakuwa mwongozo kwa masomo hayo. Ni matumaini yangu kuwa mtazidi kuchapa kazi na mungu awazidishie kwa kazi yenu njema.

    Msikilizaji wetu mwingine ni Kiiza Mrashani wa P.O.Box 366 Karagwe, Kagera-Tanzania. Anasema China na Tanzania zina msimamo unaofanana katika masuala mengi, hasa katika kutafuta amani duniani na masuala ya maendeleo. tangu China ijiunge na shirika la WTO kweli imepata mafanikio mengi na nia ya China kuwekeza miradi yake katika mataifa kama Tanzania ni jambo la kutia moyo sana.

    Msikilizajio wetu Emmy barua yake pepe ni ellymbonica@yahoo.com. Anasema nimeumizwa sana na kifo Michael Jackson Mungu amlaze pema peponi

    Na msikilizaji mwingine ni Mchana John wa barua pepe ambaye yupo Morogoro Tanzania. Anasema kwanza nawashukuru wale wote waliohusika na uandaaji wa chemsha bongo ya miaka 45 tangu Tanzania na China zianzishe uhusiano wa kibalozi, kwani nimekuwa karibu kila siku kwenye vipindi hivyo. Inaelekea wengi wamehamasika sana kiasi kwamba wengi wao wana matarajio ya kuja China ama Tanzania. Hii ni changamoto

    Hasa kwa wale ambao wameachana na Radio China Kimataifa kwa muda mwingi sasa wazinduke huko walipo na tuweze kushirikiana kama zamani kwani chemsha bongo lengo ni kutuweka pamoja kama ndugu wa karibu. Ombi langu kwa CRI kutuletea vijarida vya tujifunze kichina kwani vitatusaidia vilivyotafsiriwa kwa kiswahili. Nawatakia safari njema kwa wale watakao bahatika kuchajaguliwa kwenda China na Dares Salaam Tanzania.

    Shukrani za dhati wasikilizaji wetu wote kwa maoni yenu pamoja na mchango mnaoutoa kwa CRI sisi tunakuombeni tu msichoke kusikiliza CRI kwani kuna mambo mengi mapya tunayoyatoa kila siku na tunafanya hivi ili kuwavutia zaidi wasikilizaji wetu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako