• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Watu washuhudia hali ya kupatwa kwa jua nchini China

    (GMT+08:00) 2009-07-23 16:29:14

    Hali ya kupatwa kwa jua ilitokea saa mbili asubuhi ya tarehe 22, kwenye eneo la mtiririko wa mto Changjiang nchini China, ambapo hali ya kupatwa kabisa kwa jua ilidumu hata kwa dakika 6 katika baadhi ya sehemu. Katika ukanda wenye urefu wa kilomita elfu 10 na upana wa kilomita 250, watu wapatao milioni 300 wa miji zaidi ya 50 nchini China waliweza kuangalia hali hii ya muujiza wa unajimu, ambao hutokea kila baada ya miaka 500. Katika kipindi hiki tunakuletea maelezo kuhusu tukio hilo.

    Mchakato mzima toka kuanza hadi kumalizika kwa hali hiyo ya kupatwa kwa jua ulichukua zaidi ya saa mbili, ambapo watu wengi walikusanyika kwenye viwanja, vituo vya uchunguzi wa sayari, na kwenye kando za milima, wakishuhudia hali hiyo ya ajabu.

    Kwa mujibu wa wanajimu, hali ya kupatwa kwa jua huwa inatokea katika sehemu za bahari, jangwa na milima zisizo na watu wengi, kwa hiyo mara nyingi ni vigumu kwa binadamu kushuhudia muujiza huo. Safari hii ukanda wa kutokea kwa hali ya kupatwa kwa jua nchini China ulikuwa ni sehemu wanakoishi watu wengi zaidi, ndiyo maana muujiza huo uliwavutia wakazi wengi wa sehemu hiyo na wageni kutoka sehemu nyingine za China na nchi za nje.

    Kwa bahati nzuri zaidi, abiria 156 wa safari ya ndege moja iliyotoka Chengdu, mji wa kusini magharibi kuelekea Wuxi, mashariki mwa China walishuhudia muujiza huo angani. Abiria mmoja alisema  "Kwa mujibu wa ratiba ya kutokea kwa hali ya kupatwa kwa jua, tuliamua kupanda ndege hiyo ya kwenda Wuxi kutoka Chengdu iliyofunga safari saa 1 na nusu asubuhi ya tarehe 22. Nilishuhudia muujiza huo wa unajimu, naona hali ya maumbile ni tukufu sana."

    Mbali na wanasayansi wa China, mamia ya wanajimu kutoka nchi za nje za Ufaransa, Russia, India, Korea Kusini na Misri walimiminikia nchini China kufanya uchunguzi wa kisayansi kuhusu hali hiyo ya kupatwa kwa jua. Mnajimu kutoka India Bw. Singh na timu yake walikuja na vifaa vya utafiti vyenye uzito wa tani 2 hivi, ambao waliweka kambi huko Anji, mkoani Zhejiang.

    Bw. Singh alisema "Latitudo ya Anji inafaa zaidi katika kuchunguza hali hiyo ya kupatwa kwa jua, mbali na hayo ina hali nzuri ya anga, ni safi sana ikilinganishwa na sehemu nyingine, kwa mfano Suzhou, ni sehemu yenye hali mwafaka ya kijiogrofia, lakini hali ya anga haikuwa safi kwa kiwango cha juu ikilinganishwa na Anji."

    Wanajimu walieleza kuridhishwa na uchunguzi waliofanya katika mchakato wa hali hiyo ya kupatwa kwa jua.

    Kutokea kwa hali hiyo ya kupatwa kwa jua pia kulitoa fursa ya kueneza ujuzi wa unajimu miongoni mwa watu wa kawaida. Mbali na vituo vya televisheni na radio, tovuti nyingi za mtandao wa Internet za China ikiwemo tovuti ya lugha ya Kichina ya Radio China Kimataifa zilitangaza moja kwa moja tukio hilo. Majumba ya makumbusho ya unajimu katika miji mbalimbali ya China ikiwemo Beijing, Shanghai na Nanjing pia yaliandaa semina za kueneza ujuzi unaohusika.

    Hivi sasa kuna mashirika karibu 100 ya mashabiki wa unajimu katika vyuo vikuu vya China, na klabu mbalimbali za uchunguzi wa sayari katika miji kadhaa mikubwa ya China.

    Mkuu wa jumba la makumbusho ya unajimu la Beijing Bw. Zhu Jin alisema, toka mwaka 2004 ujenzi wa jumba jipya la makumbusho kukamilika na kufunguliwa kwa jamii, jumba hilo la makumbusho limefanya kazi nyingi katika kuenzeza ujuzi wa unajimu miongoni mwa watu wa kawaida, na serikali ya mji wa Beijing inachangia Yuan zaidi ya milioni moja kila mwaka. Na mwaka huu, mbali na hali hiyo ya kupatwa kwa jua, bado kuna shughuli mbalimbali za kueneza ujuzi wa unajimu ambazo zitawavutia sana mashabiki wa sayari nchini China.

    Bw. Zhu Jin alisema  "Kwa jumla mwaka huu tutaandaa shuhguli kati ya 20 na 30 za kueneza ujuzi wa unajimu, shughuli hizo ni pamoja na semina na siku za kufungua vituo vya uchunguzi wa sayari kwa watu wa kawaida. Katika baadhi ya shughuli hizo, mashabiki wa sayari pia wataweka darubini zao za kitaaluma kando ya barabara, kuwaalika wapita njia waangalie sayari ya mwezi au vitu vingine angani kwa kutumia darubini hizo. Aidha tumeanzisha tovuti kwenye mtandao wa Internet ambayo inawavutia watu wengi."

    Hata hivyo Bw. Zhu Jin alisisitiza kuwa, idadi ya mashabiki wa unajimu nchini China bado ni ndogo, kwa hiyo kuna kazi nyingi zinazopaswa kufanyika katika kueneza ujuzi wa elimu hiyo miongoni mwa watu wa kawaida.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako