• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Pango la mawe la Yungang

    (GMT+08:00) 2009-07-27 17:13:51

    Datong ni mji maarufu wenye historia ya zaidi ya miaka 2,400 ulioko mkoani Shanxi, mji huu unasifiwa kama "mji mkuu wa sanamu wa China" kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya sanamu za kale. Katika mji wa Datong, pango la mawe la Yungang, ambalo ni moja kati ya mapango makubwa ya mawe ya dini ya kibuddha nchini China, ni kivutio kikubwa zaidi. Pango hilo pamoja na mapango mengine mawili ya Mogaoku ya mji wa Dunhuang na Longmen ya mji wa Luoyang yanachukuliwa kama ni maghala matatu ya vitu vyenye thamani kubwa vya sanaa.

    Mji wa Datong ni mmoja kati ya miji ya kundi la kwanza iliyothibitishwa na serikali kuwa miji maarufu ya kihistoria na kiutamaduni nchini China. Kutokana na hali yake maalumu ya kijiografia, katika historia ya China mji wa Datong ni sehemu yenye kuungana kwa utamaduni wa makabila madogo ya wafugaji yaliyoko sehemu ya kaskazini na utamaduni wa sehemu ya kati ya China, sehemu hiyo vilevile ni muhimu sana katika mambo ya kijeshi. Katika enzi ya Wei ya kaskazini (mwaka 386 --- mwaka 534), Datong ilikuwa mji mkuu kwa kipindi cha karibu miaka 100, katika enzi zilizofuata za Liao na Jin, Datong ilikuwa mji mkuu wa pili kwa miaka 200 hivi. Mwaka 1277, Marcopolo, msafiri maarufu wa Italia alipofika Datong, alisifu "Datong ni mji mkubwa na maridadi". Kitu kinachoshangaza zaidi katika mji huo ni sanaa ya sanamu, hususan ni pango la mawe la Yungang lililochimbwa kwenye mteremko wa mlima, magharibi mwa mji wa Datong. Mwelezaji kutoka taasisi ya utafiti wa pango la mawe la Yungang, Bi. Wang Jia alisema,

    "Pango la mawe la Yungang liko kwenye umbali wa kilomita 16 kutoka mji wa Datong, pango hili lilichimbwa kwenye mlima wa Wuzhou, pango hili lina urefu wa kilomita 1 kutoka upande wa mashariki hadi upande wa magharibi. Pango hilo lina mapango makubwa na madogo, mapango yaliyo muhimu yanafikia 45, pamoja na matundu 209 yaliyochimbwa kwenye mteremko wa mlima, na sanamu kubwa na ndogo zaidi ya 5,000.

    Sanamu kubwa kabisa kwenye mapango ya mawe la Yungang ina kimo cha mita 17 na ile ndogo zaidi ina kimo cha sentimita 2 tu. Sanamu zote zinaonekana kama ni watu wa kweli, baadhi yake zimekalishwa kwenye viti, na nyingine ni kama watu wanaocheza ngoma, au kupiga ngoma au kengele, vilevile kuna nyingi zinaonekana kama ni watu wanaopiga filimbi, ala ya muziki ya pipa huku wakitabasamu. Sura na nguo za sanamu za malaika wanaoruka angani zinafanana na wafanyakazi wa kale wa China wenye akili na bidii. Sanamu za Buddha na sanamu za wanamuziki wanafana na watu wa nchi ya nje. Juu ya msingi wa sanaa za uchongaji sanamu za jadi ya China, zilitumia sanaa za India na Uajemi, hii inaonesha akili ya kazi ya uvumbuzi, na vilevile ni ushahidi wa kihistoria wa maingiliano ya kirafiki kati yao na nchi za nje.

    Bi. Wang Jia alisema, mapango ya mawe ya Yungang yanasifiwa kama ni maajabu katika historia ya sanaa ya uchoraji, uchongaji na ufinyanzi ya China, kila mwaka kuna idadi kubwa ya watalii wanaotoka sehemu mbalimbali za dunia kwenda kuziangalia. Alisema,

    "ukitazama kutoka mbali, mlima huu si mkubwa sana, tena unaonekana kama ni wa udongo, lakini watu wanapoingia ndani ya pango, au kuwa karibu nalo hushangazwa sana. Kwani sanamu zote zilizoko kwenye pango la mawe zilichongwa vizuri sana, hususan baadhi ya wageni kutoka nchi za nje, wanashangaa sana."

    Mtalii Bw. Li kutoka sehemu ya kaskazini mashariki ya China, alisema,

    "Nilishangazwa mno, hata mara tu baada ya kuingia humu ndani, mambo ya dini ya kibuddha yaliingia nchini China, sanamu hizo ni vitu vya kihistoria, na ni vitu vyenye thamani kubwa kwa vizazi vijavyo. Urithi wa vitu vya kihistoria ni muhimu sana kwa watu wa baadaye kufahamu historia ya China, vitu vya kihistoria vikipotea havitaweza kuzalishwa tena, kwa hiyo vinatakiwa kuhifadhiwa vizuri."

    Pango la mawe la Yungang si kama tu linawavutia watalii wa sehemu mbalimbali za dunia, bali pia linawavutia sana wasanii wengi. Msanii maarufu wa uchoraji Bw. Han Meilin, hivi karibuni alifika kwa mara ya kwanza kwenye Yungang, aliuchukulia uchunguzi wake kama ni safari ya kuhiji katika mambo ya sanaa ya uchongaji sanamu. Alisema,

    "kinachonisikitisha sana ni kuwa sikufika hapa kabla ya zaidi ya miaka 20, 30 au 50 iliyopita. Nilisoma vitabu vingi, vitabu vyangu kuhusu Yungang pia ni vingi, lakini sikushangazwa kama leo. Nilifuta machozi sasa hivi, nimefurahia sana pango la Yungang. Liwe katika jinsi inavyoonekana au muundo wake, sanaa ya pango la mawe la Yungang ni nzuri sana katika historia, kwa hiyo nimevutiwa nayo sana, ninasikitika sana kwa kuchelewa kufika hapa."

    Mbali na pango la mawe la Yungang, katika sehemu kadhaa zenye vivutio vya kihistoria yakiwemo hekalu la Huayan na hekalu la Shanhua ya mji wa Datong, vilevile watu wanaweza kuona sanaa ya sanamu za kale za kabla ya miaka elfu moja iliyopita. Kutokana na kuweko rasilimali kubwa ya mabaki ya kihistoria ya sanamu za kale, na kuitikia wito wa watu mashuhuri wa sekta ya utamaduni ya China, mji wa Datong hivi karibuni ulianzisha "mpango wa Yungang mpya" ukilenga kuenzi "mji mkuu wa sanamu wa China" unaoonesha heshima ya sanaa za sanamu za kale na za kisasa. Meya wa mji wa Datong Bw. Geng Yanbo alisema,

    "Datong haina azma ya kuwania nafasi ya kwanza kwa ukubwa, lakini inataka kuwa na umaalumu na kuwa nzuri zaidi. Sanaa za uchongaji sanamu ni ua la kupendeza zaidi katika mji huo maalumu. Kutimiza lengo la kuwa mji mkuu wa sanamu wa China ni lengo la kimkakati la muda mrefu, tunatakiwa tufanye juhudi kwa watu wa vizazi kadhaa, hususan tunahitaji uungaji mkono wa mabingwa wasanii wa nchini na wa nchi za nje. Tunatakiwa kujitahidi kadiri tuwezavyo kuhimiza utekelezaji wa mpango wa Yungang mpya, na kuwafahamisha watu wa nchini na wa duniani kuhusu sanaa ya uchongaji sanamu ya Datong."

    Si vigumu kwenda Datong, mji wenye rasilimali kubwa ya utalii mkoani Shanxi, endapo unasafiri kutoka Beijing, unaweza kufika huko baada ya saa 4 kwa gari, tena Datong ina uwanja wa ndege, nchini China kuna njia kadha za ndege zinazofika huko moja kwa moja. Kama unataka kushuhudia haiba ya sanaa za jadi ya China, basi tafuta nafasi ya kwenda huko.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako