• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Sanaa ya utengenezaji wa vyombo vya udongo mweusi ya Nixi

    (GMT+08:00) 2009-07-30 16:37:13

    Sanaa ya utengenezaji wa vyombo vya udongo mweusi ni alama moja ya utamaduni wa kitibet. Sanaa hiyo ina historia ndefu sana. Katika sehemu iliyo kando ya mito ya Jinshajiang na Lancangjiang, vyombo hivyo vilivyotengenezwa miaka 2,000 iliyopita vimefukuliwa kutoka ardhini. Vyombo vya udongo mweusi bado vinaendelea kutumiwa na watu wa kabila la Watibet.

    Tarafa ya Nixi ya wilaya ya Shangri-la mkoani Yunnan inajulikana kwa utengenezaji wa vyombo vya udongo mweusi. Kati ya vyombo hivyo vinavyotengenezwa katika sehemu mbalimbali ya tarafa hiyo, vile vinavyotengenezwa na wasanii wa jadi wa kijiji cha Tangdui ni maarufu zaidi.

    Waandishi wetu wa habari hivi karibuni walitembelea katika karakana ya kutengenezea vyombo vya udongo mweusi katika kijiji cha Tangdui. Waliwaona wanaume kadhaa wa kabila la Watibet waliokuwa wakitengeneza vyombo vya udongo mweusi wamekaa chini kwenye ardhi, wakipigapiga udongo.

    Msanii anayetengeneza vyombo vya udongo mweusi Bw. Rachi Chucheng alisema, anapoupiga na kuukata udongo mweusi, hafikirii jambo lingine lolote ila kufanya vizuri kazi yake. Aliwaambia waandishi wetu wa habari kuwa, alirithishwa na babu yake ufundi wa kutengeneza vyombo vya udongo mweusi, na amefanya kazi hiyo kwenye karakana yake kwa miaka 13. Alisema anavitengeneza vyombo vyote kwa makani sana, kwani anaona furaha na majivuno kuwa amevibadilisha kutoka udongo na kuwa vyombo vizuri. Alisema,"Mimi ni mwanafunzi wa babu yangu, na napenda sana kutengeneza vyombo vya udongo mweusi. Ufundi wa kuchora kwenye vyombo vya udongo ulitithishwa kizazi baada ya kizazi, na ni kazi ngumu sana."

    Bw. Chucheng alijulisha kuwa, hivi sasa mafundi wa kijiji cha Tangdui bado wanatengeneza vyombo vya udongo mweusi kwa njia ya kijadi. Tokea kukusanya udongo hadi kukamilisha utengenezaji wa vyombo, inawachukua mafundi hao mwezi mmoja. Bw. Chucheng alisema, kwanza mafundi hao wanakwenda kutafuta udongo mweusi mzuri ambao unapatikana kwenye mlima ulioko kilomita kadhaa kutoka kijiji cha Tangdui, halafu wakipigapiga na kukatakata udongo kwa kutumia kibao mpaka uwe na umbo la vyombo, baada ya hapo, mafundi wanachora picha mbalimbali juu yao. Baada ya hatua hizo za mwanzo, vyombo hivyo vinawekwa ndani ya nyumba mpaka vikauke, halafu vinachomwa moto kwa kuni za msonobari. Hatua hii ni muhimu sana katika utengenezaji wa vyombo vya udongo mweusi, na mafundi wanapaswa kudhibiti vizuri moto, ili kupata vyombo vizuri. Baada ya kazi ya kuvisafisha na kusugua ambayo ni hatua ya mwisho, utengenezaji wa vyombo vya udongo mweusi unakamilika.

    Bw. Chucheng alisema ana matumaini kuwa, ufundi wake utarithiwa daima dawama. Alisema, "Nitaurithisha ufundi huo kwa watoto wangu, na watoto wangu watauritisha kwa watoto wao, hivyo ufundi wa kutengeneza vyombo vya udongo mweusi utarithishwa kizazi baada ya kizazi."

    Takwimu zinaonesha kuwa, karibu familia 60 kati ya familia zote zaidi ya 180 za kijiji cha Tangdui zinajishughulisha na uendelezaji wa vyombo vya udongo mweusi. Mwezi Juni mwaka 2005, kijiji hicho kilianzisha Kampuni ya Upanuaji wa Vyombo vya Udongo Mweusi, kazi yao ni kuvifunga ndani ya maboksi na kuviuza vyombo hivyo vilivyotengenezwa na wakulima mafundi. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na maendeleo makubwa ya shughuli za utalii katika sehemu ya Shangri-La, vyombo vya udongo mweusi vinapendwa sana na watalii kutoka nchini China na nchi za nje.

    Naibu meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Wangdu alisema, hivi sasa kampuni hiyo inauza vyombo vya udongo mweusi zaidi ya elfu 20 kwa mwaka. licha ya kuviuza katika sehemu wanayoishi watibet mkoani Yunan, kampuni hiyo pia imeanza shughuli katika sehemu nyingine nchini China, hata nchi za nje. Bw. Wangdu alisema,"Nchini China tunaviuza vyombo hivyo hasa katika miji ya Beijing, Guangzhou na mkoa wa Hainan. Pia tunaviuza nchini India na Nepal."

    Vyombo vya udongo mweusi vilivyotengenezwa katika sehemu ya Nixi vina aina zaidi ya 100, na pia vinagawanyika katika aina tatu kubwa, yaani vyombo vya kawaida vinavyotumiwa katika maisha ya watu, vyombo vinavyotumiwa katika shughuli za kidini, na vyombo vya mapamno vikiwa ni vitu vya kisanaa.

    Hivi sasa vyombo vya udongo mweusi vya Nixi vinajulinana duniani, ambapo wanakijiji wa Tangdui wanaovitengenezwa vyombo hivyo pia wametajirika. Kwa kuwa njia ya jadi ya kukausha vyombo vya udongo mweusi kwa kuwasha kuni inasababisha changamoto kwa mazingira ya asili, wanakijiji wa Tangdui wanatafuta njia nzuri ya kisasa. Bw. Wangdu alisema, "Naona kuwa vyombo vya udongo vinavyochomwa na moto wa gesi vitakuwa vizuri sana. Moto wa aina hiyo utakuwa mzuri na hautasababisha uchafuzi kwa mazingira. Tutajaribu njia hiyo baadaye."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako