• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Watu kutoka Korea Kusini wanaoishi mkoani Shandong China

    (GMT+08:00) 2009-08-06 17:00:25

    Mkoa wa Shandong wa China na Korea Kusini zinatenganishwa kwa bahari. Watu wa Korea Kusini wanapenda kusema, kama ukiamka mapema na hali ya hewa ni nzuri, ukiwa katika bandari ya Inchon ya Korea Kusini, unaweza kusikia sauti za jogoo kutoka Qingdao, mkoani Shandong China. Tangu enzi na dahari, watu wa sehemu hizo mbili wamekuwa wakiwasiliana kwa karibu katika mambo ya utamaduni na biashara. Katika miaka ya hivi karibuni, watu wengi wa Korea Kusini wamewekeza mkoani Shandong China, ambapo wanafanya kazi na kuishi kwa furaha. Katika kipindi hiki cha leo, tunakuletea maelezo kuhusu watu wawili kutoka Korea Kusini wanaoishi mkoani Shandong, China.

    Bw. Kim Sun Heung ni balozi mdogo wa Korea Kusini mjini Qingdao, yeye ni mwanadiplomasia mpole. Maisha yake yamekuwa yanahusiana na China tangu miaka zaidi ya 20 iliyopita alipokwenda Taipei China kujifunza lugha ya Kichina. Alisema "Nina uhusiano wa muda mrefu na China. Mwaka 1982 nilijifunza lugha ya Kichina kwa mwaka mmoja kwenye shule ya sekondari ya Taipei, miaka 20 baadaye nilifanya kazi kwa miaka miwili na nusu mjini Shanghai kabla ya kufika Shandong kufanya kazi. Kati ya watoto wangu watatu, wawili walizaliwa nchini China. Kwa hiyo naona nina uhusiano mkubwa na China."

    Bw. Kim Sun Heung alisema kuwa yeye anavutiwa na utamaduni wa China. Alivutiwa na riwaya za China aliposoma shule ya sekondari, hususan riwaya zinazohusu mashujaa wa Gongfu, pia anafahamu sana majina ya waandishi wa riwaya hizo. Alisema "Utamaduni wa Korea Kusini na wa Shandong unafanana katika mambo mengi. Katika muda mrefu kwenye historia, utamaduni wa Korea Kusini uliiga mambo mengi kutoka kwa utamaduni wa Shandong. Kwa mfano mawazo ya Confucius na mfuasi wake Mengzi ambao walitoka Shandong, pia ni msingi wa utamaduni wa Korea Kusini."

    Katika miaka 30 iliyopita, maendeleo makubwa yamepatikana mkoani Shandong katika mambo mbalimbali ya siasa, uchumi, jamii na utamaduni. Mkoa huo mkubwa wa pwani unawavutia watu wengi wa Korea Kusini kutokana na sifa yake ya kijiografia na mazingira mazuri ya uwekezaji.

    Bw. Kim Sun Heung alisema "Shandong inafanana na Korea Kusini katika hali ya hewa na vyakula, pia ina sifa nzuri ya kijiografia. Watu wa Shandong ni wakarimu sana. Wakorea Kusini wanaweza kuishi hapa Shangdong bila matatizo kama wapo nyumbani."

    Raia mwingine wa Korea Kusini Bw. Kim Jin Oo ana nyumba kwenye barabara ya Yan'erdao, mjini Qingdao, mji mkuu wa mkoa wa Shandong. Bwana huyo mwenye umri wa miaka 35 ameishi nchini China kwa miaka 15, anaongea vizuri Kichina na kuichukulia Shandong kama maskani yake ya pili.

    Mwaka 2005 Bw. Kim Jin Oo alianzisha kliniki moja ya matibabu ya Kichina kwenye barabara ya Yan'erdao. Kliniki hiyo yenye eneo la mita 60 za mraba ina wafanyakazi wanne. Bw. Kim Jin Oo alisema anavutiwa na Qingdao na nyumba yake nchini China kutokana na mandhari nzuri ya mji huo wa Qingdao, wakazi wa huko wenye moyo mwema na maendeleo yaliyopatikana mjini humo, hususan mustakabali mzuri wa matibabu ya jadi ya kichina. Alisema (sauti 4) "Napenda nyumba yangu iliyopo nchini China. Nilifika China mwaka 1994, wakati ambapo hata katika miji mikubwa, majengo ya ghorofa yalikuwa ni ya ghorofa mbili tu, na majengo mengine yalikuwa ya kawaida. Wakati huo watu walikuwa hawana ufahamu wa kutosha kuhusu afya na usafi, lakini hivi sasa hali hiyo imebadilika sana."

    Bw. Kim Jim Oo aliyevutiwa na utamaduni wa China tangu utotoni mwake, alipuuza pingamizi kutoka ndugu na marafiki zake, alifika China mwaka 1994 kujifunza taaluma ya matibabu ya jadi ya kichina. Katika kipindi cha mwanzo alipoanza kuishi nchini China, hakuzoea hospitali zenye vifaa vya hali duni, mawasiliano magumu, na idadi ndogo ya wahudumu wa hoteli na maduka walioweza kuongea lugha za kigeni. Katika miaka 8 aliposoma nchini China, Bw. Kim Jim Oo ameshuhudia jinsi China ilivyopata maendeleo ya kasi katika mambo ya uchumi na jamii, alisema "Hadi mwaka 1999 niliona mabadiliko makubwa ya China. Hospitali zina vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa. Hivi sasa katika hali ya kawaida vijana wanatumia simu za mkononi. Bidhaa za kisasa zinaagizwa kutoka nchi za nje na kuuzwa nchini China, na wananchi wanazimudu."

    Mwaka 2002 Bw. Kim Jim Oo alipata shahada ya pili ya taaluma ya matibabu ya kichina, alikwenda Vancouver nchini Canada kufanya kazi kwa muda mfupi. Katika kipindi hicho alijisikia bado anavutiwa na China, hali ambayo ilizidi kuongezeka kiasi kwamba aliamua kurudi China na kufanya kazi ya matibabu ya kichina.

    Alisema  "China inapata maendeleo kwa kasi. Naona miti mingi inapandwa nchini China, na watalii wanaokuja China wamekuwa wengi zaidi mwaka hadi mwaka. Michezo ya Olimpiki iliyofanyika mjini Beijing mwaka 2008 ilikuwa ni shughuli kubwa zaidi duniani kwa mwaka huu. China pia ilirusha satelaiti yake ya kuchunguza sayari ya mwezi. China ina raslimali nyingi za kiutamaduni, kihistoria na vitu halisi. Napenda wageni wengi zaidi waje China, au waje pamoja na watoto wao, ili wajifunze lugha ya kichina."

    Hivi sasa ni vigumu kumtofautisha Bw. Kim Jim Oo na wachina, yeye pia anafurahia wengine wamchukulie kuwa mwenyeji wa mkoa wa Shandong. Kutokana na kuwepo kwa mambo mengi yanayofanana katika utamaduni wa China na wa Korea Kusini, ni rahisi zaidi kwa watu wa Korea Kusini wanaoishi nchini China kuzoea maisha ya huko, ambao wanapenda kuchangia mawasiliano kati ya China na Korea Kusini.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako