• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ijue China 19

    (GMT+08:00) 2009-08-06 20:27:59

    Sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China ni sikukuu ya pamoja kwa watu wa makabila 56 wa China. Mbali na kabila la Wahan, watu wa makabila mengi madogomadogo pia wanasherehekea sikukuu hiyo kwa desturi zao maalum.

    Asubuhi ya tarehe 1 mwezi wa kwanza kwa kalenda ya kilimo Watong hupenda kuvua samaki na kuwaweka samaki hao hai kwenye meza ili kuonesha kuwa katika mwaka mpya familia itakuwa na baraka na chakula cha kutosha.

    Wazhuang hupenda kupika chakula cha kuliwa tarehe 1 mwezi wa kwanza kwa kalenda ya kilimo wakati wa mkesha wa mwaka mpya, ili kuomba mwaka unaofuata wapate mavuno mengi na baraka.

    Wakati wa sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China, kila familia ya Waqiang hutoa sadaka za ng'ombe na kondoo kwa kutambika kwa ajili ya mababu. Aidha, katika mkesha wa mwaka mpya, watu wote wa familia wanakaa pamoja na kuzunguka chungu cha pombe, mwenye umri mkubwa zaidi anakuwa wa kuanza kunywa pombe kwa kutumia mrija wa urefu wa moja halafu watu wa familia hiyo wanafyonza pombe kwa zamu toka kushoto hadi kulia kwa kutumia mrija.

    Wakati wa sikukuu ya mwaka mpya wa jadi, watoto wa kabila la Washui wanaweza kuomba peremende kwa wazazi wao, atakayepata peremende nyingi atachukuliwa kuwa ni mtoto mwenye heri na baraka zaidi, na siku za usoni atakuwa ni mwenye akili na afya nzuri.

    Asubuhi ya Tarehe 1 mwezi wa kwanza kwa kalenda ya kilimo ya kichina, Wabai wote wazee kwa watoto hunywa maji ya sukari yaliyotiwa mchele, hii inaonesha kuwa katika mwaka mpya wataishi maisha matamu.

    Katika sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa kichina, watu wa kabila la Wakorea wa wanabandika karatasi zilizoandikwa maneno ya kutakia heri na baraka mwaka mpya kwenye milango ya nyumba, na kupika vyakula vingi vya aina mbalimbali. Na asubuhi mapema ya tarehe 1 mwezi wa kwanza kwa kalenda ya kilimo, watu huamka na kuvaa nguo maridadi za sikukuu na kutoa kuwaamkia wazee na wazazi na kuwatakia heri na baraka ya mwaka mpya.

    Asubuhi ya tarehe 1 mwezi wa kwanza kwa kalenda ya kilimo,wavulana na wasichana wa kabila la Wamongolia wanaovaa nguo maridadi za aina mbalimbali na kupanda farasi kwenda nyumbani kwa wazazi wao kuwaamkia na kuwatakia heri na baraka ya mwaka mpya. Vilevile, kabila hilo hufanya tamasha kubwa la nyimbo na ngoma, ambapo watu wote wanavaa vibandiko kwenye nyuso zao, ili kuonesha kuagana na mwaka uliopita na kuukaribisha mwaka mpya.

    Wavulana na wasichana wa kabila la Wahani hukusanyika pamoja wakati wa mwaka mpya wa jadi wa China, kunywa pombe, kuimba, kucheza dansi na kuchagua wachumba.

    Katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa jadi ya kichina, watoto wa kiume wanaotimiza umri wa miaka 13 wanafanyiwa "sherehe ya kuvaa suruali" na watoto wa kike wanafanyiwa "sherehe ya kuvaa sketi", ikimaanisha kuwa watoto hao wameingia katika utu uzima.

    Asubuhi katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa jadi wa kichina watu wa kabila la Wapumi wanapiga mizinga na mbiu kusherehekea mwaka mpya.

    Katika siku ya mwaka mpya wa jadi wa China vijana wa kabila la Wabuyi huvaa mavazi ya sikukuu kusalimiana au kwenda kutalii, kuimba na kucheza ngoma vya kutosha, kisha wanarudi nyumbani.

    Asubuhi mapema katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa jadi wa China vijana wa kabila la Waoroqen huwamiminia wazee wa familia glasi nzima ya mvinyo wakionesha heshima, kisha vijana hao wanatakiana heri kwa kunywa mvinyo. Baada ya kifungua kinywa vijana hukusanyika na kufanya mashindano ya mbio za farasi na kulenga shabaha kwa mishale.

    Asubuhi mapema katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa jadi wa China vijana wa kabila la Wadaur wanapaka masizi usoni na kuwapaka wengine wakiwemo wasichana. Inasemekana kuwa kufanya hivyo kuna maana ya kuwatakia furaha na mavuno mazuri ya kilimo.

    Katika kalenda ya kilimo ya China, tarehe 15 mwezi wa kwanza ni "Sikukuu ya Taa" ya kichina, ambayo ni miongoni mwa sikukuu kubwa za jadi za kichina.

    Wachina walianza kusherehekea sikukuu hiyo tangu Enzi ya Han ya magharibi. Mfalme Han Wendi alikalia kiti cha ufalme tarehe ya 15 Januari kwa kalenda ya Kichina. Ili kuikumbuka siku hiyo ya kuwa mfalme, kila mwaka katika siku hiyo mfalme Han Wendi alijifanya raia na kutembelea mjini "kuburudika pamoja na raia" wake. Ingawa simulizi hiyo haijathibitishwa, lakini ukweli ni kwamba tangu Enzi ya Han siku hiyo imekuwa siku ya kufanya tambiko kwa mungu ili kuomba baraka.

    Binadamu walianza kutumia moto na taa kwa pamoja katika maisha yao. Simulizi kuhusu chanzo cha sikukuu ya taa iliyoenea zaidi ni kwamba, katika Enzi ya Han kulikuwa na mtu mmoja, aliyeitwa Dong Fangshuo, ambaye alikuwa mcheshi na mwerevu. Mfalme alimpenda sana kwa kuwa mara kwa mara alikuwa akimpatia ushauri na kumfurahisha. Mwaka fulani mwezi wa 12, katika majira ya baridi theluji kubwa ilianguka, Dong Fangshuo alipoona mfalme hana raha, alikwenda kwenye bustani ili amchumie maua. Alipokuwa bustanini alikutana na msichana mmoja wa mfalme aliyeitwa mtumishi msichana mmoja, jina lake Yuan Xiao akilia kwa huzuni, na machozi yakimtiririka kwenye mashavu yake. Baada ya kumwuliza sababu, akatambua kwamba msichana huyo alikuwa na wazazi wawili wakongwe. Msichana huyo hakuwaona wazazi wake tangu achaguliwe kuwa mtumishi kwenye kasri ya mfalme. Kila ilipofika sikukuu ya mwaka mpya alikuwa anawakumbuka sana wazazi wake. Baada ya Dong Fangshuo kumfariji kidogo alimwahidi kuwa atamsaidia ili atoke kwenye kasri akawaone wazazi wake.

    Baada ya kuachana na mtumishi huyo wa kike Dong Fangshuo alikwenda nyumbani kwa wazazi wake na kuandaa mpango kwa akili yake. Dong Fangshuo aliondoka nyumbani kwa wazee akarudi mjini, huku akijifanya mpiga ramli barabarani. Kila aliyekuja kwake kupigiwa ramli alimwambia kwamba tarehe 15 Januari ni siku ya mji "kuunguzwa kwa moto kutoka mbinguni", na dawa ya kukwepa janga hili ni kuwa, "tarehe 13 mungu wa moto atajifanya msichana mwenye kuvaa mavazi mekundu akiwa na punda wa rangi nyekundu hafifu atakuja mjini Chang An kukagua sura ya ardhi, wakati huo wenyeji waende kaskazini ya mji wajipange barabarani ambapo msichana huyo atapitia, wamsihi wakilia na hivyo watu wote wataokoka." Watu waliambizana hayo na wakisubiri siku ya tarehe 13 iwadie. Siku ilipowadia, Dong Fangshuo alimwambia msichana mmoja aigize kama alivyomtaka, aliingia mjini taratibu akiwa juu ya punda wake. Wenyeji walipomwona wote walimvamia wakimsihi huku wakilia machozi. Msichana akawaambia, "Kutokana na ombi lenu, basi mkabidhi mfalme wenu kadi hii nyekundu aisome." Kisha akaondoka. Mfalme alifungua kadi akaona juu yake imeandikwa "Tarehe 15 moto utaanguka toka mbinguni, na mji utaunguzwa." Baada ya kusoma hayo mfalme alitetemeka, asijue la kufanya. Kwa haraka akamwita Dong Fangshuo kumwomba ushauri wake. Kwa akili alimwambia mfalme, "Naomba mfalme wangu uwaambie raia wako waanze kutengeneza taa nyekundu toka leo na ifikapo siku ya tarehe 15 watundike barabarani, vichochoroni, milangoni, na kila mahali mjini; wawashe fataki na fashifashi na watu wa mjini na viungani watoke majumbani kuangalia; wewe mfalme na mkeo, mawaziri, masuria na watumishi wasichana, muende mjini pia mjumuike na raia kufurahia taa." Mfalme akatoa amri kama alivyoambiwa. Tarehe 15 usiku, taa ziling'ara kote mjini kama mchana, fataki na fashifashi zilikuwa zikiwake angani. Kama walivyopangiwa wazazi walimwona binti yao Yuan Xiao, na walipata nafasi ya kuongea nae kwa muda mrefu. Usiku wenye shamrashamra ulipita, mji mkuu wa Chang An ulisalimika, na mfalme akafurahi sana. Akatoa amri, kwamba kila mwaka katika siku hiyo sherehe ifanyike kwa kutundika taa nyekundu na kuwasha fataki na fashifashi.

    Siku hiyo taa hutengenezwa kwa aina na rangi mbalimbali, matengenezo ya taa ni sanaa maalumu za kichina na baadhi ya sehemu hufanya maonyesho, taa za mayungiyungi, za kuelea majini, zenye vivuli vya wanyama vinavyozunguka zunguka, za majoka na za barafu, zinavutia kwa ufundi mkubwa, watazamaji wanapostaajabu taa hizi huburudika na shamrashamra za michezo ya kuchezesha taa za majoka, ngoma ya ngongoti, mashua ya nchi kavu, na kuonja vyakula vya sehemu maalumu. Sikukuu ya Taa pia inamaanisha kumalizika kwa kipindi cha mwaka mpya wa Kichina.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako