• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mwigizaji kijana wa opera ya Beijing Bi. Jia Pengfei

    (GMT+08:00) 2009-08-10 15:55:20

    Bi. Jia Pengfei ni mwigizaji kijana wa Jumba la Taifa la Opera ya Beijing, katika michezo ya opera ya Beijing anaigiza wahusika wanawake mbalimbali waliojulikana katika hadithi, aliwahi kuigiza mara nyingi mchezo wa opera ya Beijing "Malaika Atawanya Maua" nchini na nje ya China ambao ulitungwa na msanii mkubwa wa opera ya Beijing Bw. Mei Lanfang, kutokana na maigizo yake mazuri na sauti yake nyororo, watu wanamwita "Malaika".

    Mliyosikia ni kipande cha ""Njia ya Mawingu" cha mchezo wa opera ya Beijing uitwao "Malaika Atawanya Maua" alichoimba Bi. Jia Pengfei. Kitambaa cha hariri chenye urefu wa mita 15 ni kifaa anachotumia katika maigizo ya kipande hiki cha mchezo. Katika Jumba la Taifa la Opera ya Beijing karibu kila siku unaweza kumwona msichana huyo mwenye kimo kirefu akipeperusha kitambaa hicho kwa kurukaruka na kuzungukazunguka, na sauti yake nyororo hunajaa ndani ya ukumbi wa mazoezi.

      " Malaika Atawanya Maua" ni mchezo uliotungwa na msanii mkubwa wa opera ya Beijing Bw. Mei Lanfang kwa mujibu wa hadithi ya dini ya Kibuddha. Kwa kipufi hadithi inaeleza kwamba Buddha mmoja alisoma sana msahafu usiku na mchana kwa muda mrefu na mwishowe akapofuka. Kusikia hayo Buddha mkuu alimwagiza malaika aende kwa Buddha huyo ili aone hali aliyokuwa nayo na kisha atawanye maua kwenye chumba cha Buddha. Kipande cha "Njia ya mawingu" katika mchezo wa opera hiyo kinaeleza mandhari nzuri aliyoiona malaika huyo wakati alipokwenda kwa Buddha huyo. Nyimbo alizoimba zilikuwa za taratibu na baadae kubadilika kuwa za haraka zikiambatana na vitendo alivyofanya kwa kuonesha mazingira jinsi alivyokuwa kwenye mawingu. Bi. Jia Pengfei alisema,

    "Kitambaa chenye urefu wa mita 15 kinamithilisha mawingu au kwa maneno ya dini ya Kibuddha ni mawimgu ya baraka, malaika huyo alishuka kutoka mbinguni akiwa juu ya mawingu hayo aliisifu mandhari nzuri ya duniani aliyoona kutoka mbinguni, alipotawanya maua alikuwepo mtoto mmoja aliyeshikilia kisusu cha maua, malaika huyo alichukua maua kutoka kwenye kisusu hicho na kuyatawanya."

    Kutokana na mwaliko, Mwishoni mwa mwezi Juni Bi. Jia Pengfei alipata nafasi ya kuonesha mvuto wa opera ya Beijing katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Kutokana na mwaliko huo wa Umoja wa Mataifa akiwa pamoja na wenzake alikwenda New York kufanya maonesho, maigizo yake ya "Malaika Atawanya Maua" yaliwapatia maofisa wa Umoja huo kumbukumbu nzuri sana. Bi. Jia Pengfei alisema,

    "Kwa kuwa 'Malaika Atawanya Maua" inaoneshwa kwa nyimbo na dansi, maofisa wa Umoja wa Mataifa wameweza kufahamu, makofi yalipigwa kwa muda mrefu. Ingawa opera ya Beijing inaoneshwa kwa lugha ya Kichina lakini ikiwa pamoja na vitendo vya mwili vinasaidia kuwafahamisha."

    Bi. Jia Pengfei alianza kujifunza opera ya Beijing alipokuwa na umri wa miaka 10 ambapo alisoma darasa la tatu katika shule ya msingi, aliwahi kupata tuzo katika mashindano ya waigizaji watoto wa mchezo wa opera hiyo, baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Tamthilia cha Beijing akafundishwa na walimu wawili waliokuwa wanafunzi wa msanii mkubwa wa opera ya Beijing Bw. Mei Lanfang. Alisema,

    "Opera ya Beijing ni sanaa inayofundishwa uso kwa uso, walimu wangu walinisaidia kuinua uwezo wangu wa kuimba na maigizo yangu yakiwa pamoja na namna ya kuonesha hisia kwa macho."

    Awali, Bi. Jia Pengfei alipenda opera ya Beijing kwa sababu waigizaji wanapambwa vizuri, lakini sasa ameshika kweli sanaa hiyo ya opera. Alisema,

    "Nilipokuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi nilianza kupenda opera ya Beijing nikifikiri nikiwa mwigizaji wa opera hiyo pia nitaweza kuigiza wahusika tofauti kwa sura mbalimbali, baadaye imenifanya niipende zaidi opera hiyo kadiri umri unavyoongezeka. Pengine unapoanza kujifunza Opera ya Beijing mwanzoni unakuwa huipendi sana, lakini unaipenda opera hiyo kadiri unavyozidi kujihusisha nayo na hatimaye mapenzi hayo hayawezi kukutoka. Nilipokuwa nyumbani nalijifunza kupitia DVD au naenda kutazama michezo ya opera inayooneshwa na waigizaji mashuhuri."

    Opera ya Beijing ni mkusanyiko wa sanaa za aina nyingi, Bi. Jia Pengfei aliwahi kucheza mara nyingi mchezo wa opera ya Beijing ya "Malaika Atawanya Maua", na kila mara kabla ya maonesho lazima afanye mazoezi pamoja na bendi. Alisema,

    "Kila mara kabla ya maonesho ni lazima nifanye mazoezi pamoja na bendi, bila kujali nimeigiza mchezo huo kwa miaka mingi, maana hairuhusiwi kutokea dosari yoyote jukwaani."

    Mwenzake Bw. Wang Haoqiang alisema.

    "Bi. Jia Pengfei ni msanii anayefanya bidii bila kujali uchovu, akiwa anaigiza mhusika mkuu katika mchezo, kimo chake kinafaa sana kuonesha uzuri wa vitendo. Kila mara baada ya muda wetu wa mazoezi kumalizika, yeye hubaki na kuendelea peke yake mpaka usiku sana."

    Bi. Jia Pengfei ana mpango wake wa kuendeleza usanii wake. Alisema, sasa yeye bado ni kijana, anaweza kuigiza mhusika mkuu msichana, lakini kadiri umri unavyoongezeka ataigiza wahusika wa aina nyingine katika mchezo wa opera ya Beijing, kwa hiyo licha ya kuigiza opera ya "Malaika Atawanya Maua" atajaribu kuigiza wahusika wanawake wa aina nyingine, na kujitahidi kuwavutia watazamaji.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako