• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maisha bora ya waislamu wa mtaa wa Niujie mjini Beijing

    (GMT+08:00) 2009-08-13 16:29:03

    Katika sehemu ya Xuanwu mjini Beijing, kuna mtaa mmoja maarufu uitwao "Niujie". Mtaa huo ni eneo kubwa zaidi la makazi ya waislamu mjini Beijing, na idadi ya waislamu wanaoishi huko imezidi elfu kumi. Waislamu hao wanaishi pamoja na watu wa makabila mengine kwa masikilizano.

    Ijumaa ni siku muhimu ya ibada ya sala kwa waumini wa dini ya kiislamu. Siku hiyo waislamu zaidi ya 1,000 wakazi wa mtaa wa Niujie hukusanyika kwenye Msikiti wa Niujie, ili kufanya ibada kwa pamoja. Bw. Yang Chongqing mwenye umri wa miaka 60 alianza kuishi kwenye mtaa wa Niujie tangu alipokuwa mdogo. Katika miaka zaidi ya kumi iliyopita baada ya kustaafu, anakwenda kwenye msikiti huo kufanya ibada kila siku, kwani msikiti huo ni nyumbani kwake kiroho. Alisema,

    "Naona kuwa Msikiti wa Niujie ni nyumba yangu nzuri, na kufanya ibada kwenye msikiti huo ni jambo ambalo haliwezi kufutika katika maisha yangu ya kila siku. Jambo hilo lilifanywa na babu na baba yangu, na sasa pia watoto wangu wanaendelea kufanya hivyo."

    Msikiti wa Niujie ni msikiti mkubwa na wenye historia ndefu zaidi mjini Beijing, pia ni jengo ambalo ni alama ya mtaa wa Niujie. Msikiti huo ulijengwa na msomi mmoja mwarabu aliyekuwa ofisa wa serikali ya China wakati wa enzi ya Liao, na ujenzi wake ulianza mwaka 996. Bw. Xue Tianli mwenye umri wa miaka 76 ni mkuu wa Shirikia la Dini ya Kiislamu la Beijing, ambaye pia ni imamu mkuu wa Msikiti wa Niujie. Alisema kutokana na sheria ya dini ya kiislamu, msikiti wa Niujie unaandaa ibada mara tano kwa siku, na kuwashirikisha waislamu zaidi ya 200. Alisema,

    "Haki ya kuabudu ya waislamu inalindwa kisheria. Wakati waislamu wengi wanapokusanyika kwa ajili ya kufanya ibada hasa katika sikukuu za Idd el Haji na Idd el Fitri, serikali hutoa msaada wa kuhakikisha usalama. Zaidi ya hayo, serikali ya China pia iliweka siku maalumu za mapumziko kwa waislamu katika sikukuu zao za kidini."

    Licha ya waislamu wa China, wageni kutoka nchi za nje pia wanakwenda kwenye msikiti huo. Wageni hao hasa ni kutoka Pakistan, Uturuki na nchi za Afrika na Asia ya Kati ambao wengi ni waislamu wanaofanya kazi na kuishi mjini Beijing. Aidha watalii pia wanapenda kutembelea msikiti huo. Bw. Mark Hartog kutoka Ujerumani alisema, msikiti huo umemwachia kumbukumbu kubwa, alisema, "Msikiti huo ni mzuri sana, hapa ni mahali pa tulivu sana, kila jambo linaendeshwa kwa utaratibu, na watu kwenye msikiti huo ni wema. Dini ya kiislamu ni dini ya inayopenda amani, na kila muamini wa dini hiyo anafuata dini yake kwa makini."

    Ndani ya msikiti wa Niujie, shughuli za kidini ambazo zimedumu kwa miaka elfu kadhaa zinaendelea, na nje ya msikiti huo, wakazi wa mtaa wa Niujie wanaishi maisha yao ya jadi. Kwa kuwa wakazi wengi wa mtaa huo ni waislamu, shule za msingi na sekondari, ofisi ya usimamizi wa mazishi, supamaketi, na hospitali maalumu kwa ajili ya waislamu zimejengwa katika mtaa huo. Bw. Xue Tianli aliyeishi kwenye mtaa huo kwa miaka zaidi ya 20 ameshuhudia mabadiliko makubwa ya mtaa wa Niujie katika miaka kadhaa iliyopita, alisema, "Zamani mtaa wa Niujie ulikuwa na hali ya uchafu na mwebamba kama kichochoro, na wakazi wengi waliishi kwenye nyumba ndogo mbovu. Sasa barabara imepanuliwa kuwa na upana wa mita 40, ambapo wakazi wa mtaa huo wamehamia kwenye nyumba mpya nzuri. Pia supamaketi iliyoanzishwa kwa ajili ya waislamu imeturahisishia katika maisha, na vyakula vya kiislamu vya aina mbalimbali vyote vinapatikana huko."

    Bw. Jin Shaochun mwenye umri wa miaka 59 kutoka kabila la Wahui ni mkazi wa mtaa wa Niujie aliwaambia waandishi wetu wa habari kuwa, serikali inafuatilia sana maisha ya waislamu, na uhusiano kati ya watu wa makabila tofauti pia ni mzuri sana. Alisema, "Waislamu wanaweza kufanya shughuli mbalimbali katika mtaa wa Niujie, miundo ya maisha hasa mikahawa yote ni ya kiislamu. Serikali pia imejenga hospitali maalumu kwa ajili ya waislamu, na mazingira ya matibabu ni mazuri sana. Zamani sisi watu wa kabila la Wahui tulikuwa tukiishi bila kujichanganya na makabila mengine, lakini sasa baadhi yetu tunaishi kwenye jengo moja na wakazi wa kabila la Wahan, na uhusiano kati yetu ni mzuri sana."

    Ikiwa alama ya mtaa wa Niujie, Msikiti wa Niujie pia unahifadhiwa vizuri. Imamu mkuu wa msikiti huo Bw. Xue Tianli alijulisha kuwa, katika miaka 60 tangu China mpya ianzishwe msikiti huo umekarabatiwa mara nne, hasa mwaka 2005, serikali ya mji wa Beijing ilitenga yuan milioni 25 kwa ajili ya ukarabati wa msikiti huo. Alisema, "Zamani eneo la msikiti huo lilikuwa mita za mraba elfu nne tu, baada ya kupanuliwa mwaka 2005, sasa eneo lake ni zaidi ya mita za mraba elfu kumi, na unaweza kupokea watu kati ya elfu nne na tano. Hali hii imeondoa kabisa tatizo la zamani kutokuwa na sehemu ya kutosha kwa waislamu wanaofanya ibada wakati wa sikukuu za kidini. Aidha sehemu maalumu kwa ajili ya waislamu wanawake pia imejengwa katika msikiti huo."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako