• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maisha mjini Beijing mwaka mmoja baada ya michezo ya Olimpiki

    (GMT+08:00) 2009-08-13 16:24:30

    Tarehe 8 Agosti mwaka huu ilikuwa siku ya maadhimisho ya mwaka mmoja ya kufanyika kwa michezo ya Olimpiki ya Beijing. Katika kipindi cha leo, wakazi wa Beijing wanaelezea jinsi maisha na mitizamo yao ilivyobadilika kutokana na mji wao kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki. Karibuni.

     Zhao Zi'ao alizaliwa alfajiri ya tarehe 8 Agosti mwaka 2008, siku ambayo ilikuwa ni ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya Beijing. Watoto waliozaliwa siku hiyo wanajulikana nchini China kama "watoto wa Olimpiki". Mama yake Bi. Li Yan alisema hakutarajia kumzaa mtoto mwaka huo ambao Beijing ilikuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki, wala hakutegemea kujifungua siku hiyo hiyo ya kufunguliwa kwa michezo ya Olimpiki. Mtoto huyo wa kike alipewa jina la Zi'ao, maana yake ni mtoto anayewaletea wazazi fahari, jina hilo pia linadokeza kuwa, huyo ni mtoto wa Olimpiki.

    Mama Li Yan alitoa ufafanuzi akisema  "Neno 'ao' linafanana na matamshi ya herufi ya kwanza ya neon Olimpiki, katika maandishi neno hilo kwa Kichina ni majivuno, tunatarajia motto huyu atuletee fahari katika siku za baadaye. Alizaliwa katika siku ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki, hali ambayo inaonesha uhusiano mkubwa kati ya mtoto wetu na michezo hiyo, ndiyo maana tulimpa jina hilo ili kuadhimisha michezo hiyo ya Olimpiki."

    Mtoto huyo wa kike alipotimia miezi 6, kwa mara ya kwanza wazazi wake walimchukua kutembelea uwanja mkuu wa michezo ya Olimpiki ya Beijing ambao unajulikana kwa jina la kiota.

    Mama Li Yan akikumbusha safari hiyo alisema"Tulimwambia, 'baby, siku ulipozaliwa michezo ya Olimpiki ilifunguliwa hapa uwanjani, baba na mama tutakupeleka uwanjani kutazama michezo mbalimbali siku za baadaye utakapokuwa mkubwa.' Tulimwambia kuwa hivi ni viti vya watazamaji, na kule ni sehemu ya wageni rasmi, na huku ni njia ya kukimbia mbio. Tuliposema mtoto alisikia na kuangalia kwa makini."

    Mama Li Yan aliongeza kuwa, anapenda mtoto wake avutiwe na shughuli za michezo tangu utotoni mwake, na kuelewa umuhimu wa kufanya mazoezi ya kujenga mwili.

    Wakazi wengi wa mji wa Beijing wana mtizamo unaofanana na huyu mama, hususan baada ya mji huu kuandaa kwa mafanikio michezo ya Olimpiki, wakazi wengi zaidi walijitokeza kushiriki kwenye michezo ya aina mbalimbali. Nyumba ya mzee Zhang Chonglu mwenye umri wa miaka 72 iko karibu na jumba la mchezo wa kuogelea la michezo ya Olimpiki ya Beijing. Mwezi Juni mwaka huu jumba hilo lilipoanza kufunguliwa kwa jamii, mzee Zhang alikwenda na mjukuu wake kutembelea jumba hilo la mchezo.

    Mzee Zhang alisema"Nimekuja na mjukuu ajionee jumba hilo lilivyo na vifaa vyake, kwani waogeleaji hodari walishindana kwenye jumba hilo wakati wa michezo ya Olimpiki."

    Mjukuu wake Zhang Mingyang mwenye umri wa miaka 13 alitoa maoni yake kuwa, kufunguliwa kwa jamii kwa viwanja na majumba ya michezo ya Olimpiki kunaweza kuwafanya wakazi wengi zaidi washiriki kwenye shughuli za michezo. Alisema "Kimsingi uwanja na majumba ya michezo ya Olimpiki yamejengwa kwa ajili ya kutumika katika shughuli za michezo, ni vizuri kuwaona watu wanafanya mazoezi ya kujenga mwili kwa pamoja. Hili ni jumba lililotumika wakati wa michezo ya Olimpiki, ambapo waogeleaji wengi walishindana hapa jumbani, kwa hakika lina vifaa vya kiwango cha juu, napenda kujionea jinsi hali ya ndani ya jumba hilo ilivyo."

    Bw. Li Zhaoqian mwenye umri wa miaka 32 ni mwajiriwa wa kampuni moja. Baada ya kazi anapenda kucheza mpira na marafiki. Alieleza mara ya kwanza alipocheza mpira wa wavu kwenye jumba la mchezo wa mpira wa wavu la chuo kikuu cha uhandisi ambalo pia lilitumika kwa ajili ya michuano ya michezo ya Olimpiki, alisema "Naona hilo si jumba la anasa, lakini linafaa kwa michuano."

    Katika maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing, licha ya ujenzi wa viwanja na majumba ya michezo, Beijing ilitumia fedha nyingi katika kuboresha miundo mbinu ya mji huu, na nusu ya fedha hizo zilitumika katika ujenzi wa reli, subway, barabara kuu na uwanja wa ndege. Hivi sasa mtandao rahisi wa mawasiliano umewapa urahisi mkubwa wa kusafiri wakazi wa mji wa Beijing baada ya michezo ya Olimpiki kumalizika.

    Mama Bi Yuzi ni mkazi wa Beijing, ambaye nyumba yake iko mbali na ofisi yake. Kabla ya kuzinduliwa kwa subway, mama huyo alipaswa kubadilisha mabasi mara mbili kutoka anakoishi hadi ofisini kwake, hata kama akiendesha gari alikumbwa na msongamano barabarani, katika hali ya kawaida ilimchukua saa 2 kufika ofisini. Hivi sasa subway mbili za No.5 na No.10 zimeunganisha nyumbani kwake na ofisini, hali ambayo iliinua kwa kiasi kikubwa ufanisi wa usafiri kwake.

    Mama Bi Yuzi alisema "Njia nyingi za subway zilijengwa kwa ajili ya michezo ya Olimpiki. Hivi sasa naweza kutumia subway No.5 na kubadilisha subway No.10 ambayo napanda kutoka nyumbani hadi sehemu ya karibu na ofisi yangu. Sasa mawasiliano ni rahisi sana, naona kumekuwa na urahisi mkubwa zaidi katika maisha, popote ninapokwenda natumia subway."

    Katika kipindi cha michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008, dunia ilivutiwa na uchangamfu na urafiki mkubwa wa watu wa China kutokana na malaki ya watu wanaojitolea ambao walitoa huduma nzuri na tabasamu nzuri. Baada ya kumalizika kwa michezo hiyo, baadhi ya watu hao waliendelea kutoa huduma ya kujitolea. Kijana Ji Peng ni miongoni mwa watu hao. Hivi sasa katika siku za mapumziko anatoa huduma ya kujitolea kwa watalii katika sehemu karibu na jumba la mchezo wa kuogelea.

    Kijana huyo alisema michezo ya Olimpiki ya Beijing ilienzi moyo wa kujitolea kuwahudumia wengine, kutokana na moyo huo, vijana wa Beijing wana upendo zaidi na kupenda kuchangia maendeleo ya jamii. Alisema  "Zamani nilijiona kuwa nazingatia tu maslahi yangu binafsi, hali ambayo ni kama walionayo vijana wengi waliozaliwa katika miaka ya 90. Lakini hivi sasa sina mitizamo finyu kuhusu mambo mengi, naweza kushughulikia baadhi ya masuala kwa mtizamo wa uvumilivu."

    Mbali na urahisi katika maisha ya kila siku, michezo ya Olimpiki iliwaletea zaidi wakazi wa Beijing mabadiliko ya mitizamo na mtindo wa maisha. Mazoezi ya kujenga mwili, mwamko wa kuhifadhi mazingira na moyo wa watu wa kujitolea, hivi sasa hayo yote yanapewa uzito mkubwa, hali ambayo haijawahi kutokea katika historia ya mji wa Beijing.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako