• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ujenzi wa miji midogo wachangia maendeleo ya sehemu za vijijini nchini China

    (GMT+08:00) 2009-08-27 17:40:43

    China ina wakulima wapatao milioni 900 ambao wanachukua theluthi mbili ya idadi ya wananchi wote wa China. Katika muda wa miaka 60 iliyopita, hususan katika miaka 30 iliyopita tangu China ianze kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, wakulima wamepata maendeleo makubwa na maisha yao yameinuka sana. Katika kipindi cha leo, tunakuletea maelezo kuhusu maisha ya wakulima wa wilaya ya Xuefu, mkoani Jiangsu, mashariki mwa China yalivyoboreshwa. Karibuni.

    Mzee Zhao Juming mwenye umri wa miaka 68 ni mkulima anayeishi wilayani Xuefu, mkoani Jiangsu, mashariki mwa China. Yeye alinunua gari lake la kwanza mwezi Januari mwaka huu lililomgharimu Yuan zaidi ya elfu 50, sawa na dola za kimarekani elfu 7. Mzee Zhao alipata utajiri kwa kutegemea kilimo cha miche ya miti. Katika hekta 5 hivi za mashamba yake, imepandwa miche ya miti ya aina kadha wa kadha.

    Alipozungumzia maisha ya hivi sasa, mzee Zhao alieleza kwa furaha kuwa, mbali na yeye, wakulima wenzake pia wamechuma pesa nyingi kutokana na kilimo cha miche ya miti.

    Mzee Zhao alisema "Katika kijiji chetu, wakulima wengi wanajishughulisha na kilimo cha miche ya miti, karibu kila familia inapanda miche ya miti kwenye mashamba yao, na pato la mwaka kwa kila familia linaweza kuwa Yuan elfu 80 hata laki 2. Wenzangu wengi wamenunua magari, vyombo vya umeme nyumbani, na nyumba za kisasa katika mji wa wilaya Xuefu."

    Hivi sasa wilaya Xuefu yenye eneo la kilomita za mraba 230 na wakazi karibu elfu 70 inajulikana kutokana na kilimo cha maua na miche ya miti. Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2008 hekta zaidi ya 1,500 za mashamba ambazo ni asilimia 30 ya mashamba wilayani humo zilipandwa maua na miche ya miti, na kuleta faida ghafi ya zaidi ya Yuan milioni 200, sawa na dola za kimarekani milioni 30.

    Mbali na kilimo cha maua na miche ya miti, nguzo nyingine za uchumi za wilaya hiyo ni viwanda vya vifaa vya ujenzi na vya nguo. Imefahamika kuwa mwaka 2008 thamani ya uzalishaji mali wa viwanda vyote wilayani humo ilikuwa Yuan bilioni 4.7, hili ni ongezeko la asilimia 18 kuliko mwaka 2007.

    Kuimarika kwa nguvu ya uchumi kunachangia utandawazi wa mji. Hivi sasa mji wa wilaya hiyo una eneo la kilomita za mraba 4.8 na wakazi zaidi ya elfu 10.

    Bi. Xu Luofeng ana duka moja katika mji wa wilaya hiyo. Yeye alianza kufanya biashara katika mji huo miaka 20 iliyopita, hivyo ameshuhudia mabadiliko makubwa yaliyotokea mjini humo. Alisema "Miaka 20 iliyopita, ilikuwa hakuna nyumba katika kando nyingine ya barabara hii, wakati huo nyumba yangu ilikuwa nyumba pekee kwenye kando ya barabara hiyo nzima. Nimeshuhudia jinsi nyumba nyingine zilivyojengwa moja baada ya nyingine. Hivi sasa watu wana uwezo mkubwa zaidi. Hapo zamani walifanya manunuzi wakati wa sikukuu, na katika siku za kawaida walinunua mahitaji ya lazima tu, kama vile mafuta ya kupikia na chumvi. Lakini hivi sasa hali imebadilika sana, watu wameanza kununua vitu vyenye thamani ya juu baada ya kujitosheleza kwa chakula na mahitaji mengine ya lazima."

    Katika kuharakisha utandawazi wa mji, serikali ya wilaya ya Xuefu ilitoa sera ya kuwahimiza wakulima wahamie kwa utaratibu kwenye mji. Katika miaka mitatu iliyopita, nyumba nyingi za makazi na miundo mbinu ya umma inayoambatana na makazi hayo ilijengwa, na miti mingi kupandwa mjini Xuefu. Hivi sasa asilimia 80 ya wakazi wa mjini humo wanaishi katika nyumba za kisasa.

    Bi. Xu Luofeng alisema "Kwa mfano wa kiwanja kilichopo nyuma ya hospitali, kutokana na mpangilio wa serikali, kiwanja hicho kilitumika katika ujenzi wa makazi ambao unatekelezwa kwa vipindi vitatu. Katika kipindi cha kwanza nyumba 60 hivi zilijengwa, ni nyumba nzuri sana, zina mazingira mazuri na kila nyumba ina ua. Kwa hiyo watu wengi walitaka kununua nyumba za kipindi cha pili. Watu wakipata uwezo mkubwa zaidi, wanapenda kuboresha mazingira ya kuishi. Nyumba hizo za kipindi cha pili ziliuzwa haraka, bado kuna watu wanaotaka kununua, kwa hiyo ujenzi wa kipindi cha tatu umeanza."

    Utandawazi wa mji pia umechangia maendeleo ya huduma za jamii katika wilaya Xuefu. Huduma ya afya na matibabu ni muhimu sana katika jamii, na katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya wilaya hiyo imetilia mkazo utoaji wa huduma hiyo. Hivi sasa wakulima wote wilayani humo wanalindwa na bima ya ushirikiano wa matibabu inayotekelezwa katika sehemu za vijijini. Kutokana na bima hiyo, kamati ya wanakijiji inalipa sehemu kubwa ya bima, kila mkulima analipa kiasi kidogo tu cha Yuan 10, sawa na dola za kimarekani 1.5, hatua ambayo inawanufaisha sana wakulima.

    Mzee Zhao Juming alipotaja bima hiyo ya matibabu, alisema  "Inapaswa kulipa bima ya ushirikiano wa matibabu, kila mwaka kamati ya wanakijiji inatoa sehemu ya bima, na wakulima binafsi walitoa sehemu nyingine. Mwaka jana nilitoa Yuan 10 wa bima, lakini nilirudishiwa nusu ya malipo ya matibabu, nilirudishiwa malipo ya matibabu kwenye hospitali ya mji wa wilaya. Hii ni bima nzuri. Nikiugua sana narudishiwa malipo ya matibabu, nafurahia sana bima hiyo. Sasa kila mtu ana kadi ya bima ya matibabu ya ushirikiano, tukiwa na kadi hiyo tunakwenda kutibiwa kwenye hospitali ya mji wa wilaya, na baadaye tunarudishiwa malipo ya matibabu."

    Ofisa wa serikali ya China anayeshughulikia mambo ya sehemu za vijijini Bw. Chen Xiwen alisema, utandawazi wa mji unatokana na maendeleo makubwa ya uchumi wa sehemu za vijijini, na unaleta manufaa ya kuchangia maendeleo ya viwanda na kilimo chenye umaalumu, kusaidia uhifadhi wa mazingira ya asili, na kuinua kiwango cha huduma za jamii. Kutokana na utandawazi wa mji, nguvu kazi inayobaki vijijini inaweza kuingia mijini.

    Ofisa huyo alisema (sauti 7) "Nchini China utandawazi wa mji unazingatia maendeleo ya uwiano kati ya miji mikubwa, yenye ukubwa wa wastani na midogo. Kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu nchini China, haiwezekani kutegemea tu miji mikubwa kuwapokea wakulima wanaopenda kuhamia na kuishi mijini, ndiyo maana kujenga na kukuza miji midogo ni hatua muhimu sana katika mchakato wa utandawazi wa mji nchini China."

    Hivi sasa China ina miji midogo ipatayo 18,000. Ujenzi na ustawi wa miji midogo una umuhimu mkubwa katika kuchangia maendeleo ya uchumi na huduma za jamii katika sehemu za vijijini. Lakini kutokana na kukosa hali ya uwiano katika maendeleo ya uchumi katika sehemu mbalimbali za China, miji midogo iliyopo sehemu za katikati na za magharibi zenye uwezo mdogo wa kiuchumi bado ipo katika hali duni ya kimaendeleo, ikilinganishwa na ile iliyopo sehemu za mashariki zenye maendeleo makubwa kiuchumi. Kutokana na hali hiyo, bado kuna njia ndefu katika ujenzi na ustawi wa miji midogo nchini China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako