
"Hamjambo wasikilizaji wa Radio China Kimataifa. Mimi ni Ahn Jung-Kwan."
Mwaka 1999, Ahn Jung-Hwan alichaguliwa kuwa mwanasoka bora kwenye Ligi ya soka ya Korea ya Kusini, na mwaka 2000 alikwenda kuichezea timu ya Perugia na kuwa mwanasoka wa kwanza wa Korea ya Kusini anayeingia kwenye Ligi huu ya Italia. Pia aliisaidia timu ya Korea ya Kusini kupata nafasi ya nne katika Fainali za Kombe la Dunia la mwaka 2002. Mwezi Machi mwaka huu, mchezaji huyo alijiunga na timu ya Shi De ya Dalian kwenye Ligi kuu ya China, na kuwa mmoja wa wanasoka nyota kwenye soka ya China. Ingawa wakati ule timu ya Ligi kuu ya Japan pia ilitaka kumsajili, lakini Ahn Jung-Hwan aliamua kujiunga na timu ya Shi De ya Dalian, China.
Ahn Jung-Hwan akizungumzia sababu ya kuchagua kuichezea timu ya Shi De ya Dalian alisema:
"Nimeamua kucheza soka nchini China, kwa sababu naona hii ni changamoto mpya kwangu. Nataka kupata uzoefu wa kushiriki kwenye Ligi ya soka nchini China, na kupata ubingwa wa ligi hiyo. Tangu zamani nilikuwa nikijua timu ya Shi De ya Dalian kuwa ilishika nafasi ya pili katika Mashindano ya kombe la klabu za Asia. Si mimi binafsi, watu wengi wa Korea ya Kusini wanafahamu kuwa timu ya Dalian ni hodari. Hii ni sababu muhimu kwangu kuchagua kuichezea timu hiyo."
Dalian iliyoko kaskazini mashariki nchini China, ni mji wenye mandhari nzuri, na ni mji maarufu wenye vivutio vingi vya utalii. Lakini kwa Ahn Jung-Hwan, muhimu zaidi kwake ni kuwa mji huu uko karibu sana na nyumbani kwake Korea ya Kusini, na inamchukua saa moja tu kufika Seoul kutoka Danlian kwa ndege, hali ambayo inamrahisishia Ahn Jung-Hwan kukutana na jamaa zake wakati wa mapumziko. Aidha, kuna mikahawa mingi ya kikorea mjini Dalian, na hana wasiwasi wa kutozoea vyakula vya kichina.
Kutokana na maandalizi mazuri ya klabu ya Shi De ya Dalian kwa ajili ya Ahn Jung-Hwan, hakuna tatizo lolote kwenye maisha yake, tatizo kubwa zaidi linalomkabili ni lugha ya kichina. Akizungumzia suala hilo alisema:
"Tatizo kubwa kwangu ni lugha ya kichina. Nimekaa nchini China kwa miezi mitatu, sasa naweza kufahamu maneno machache ya kichina. Lakini jambo la kufurahisha ni kuwa najua kuwasiliana na wenzangu kwa lugha ya kiingereza na pia kwa vitendo."
Ahn Jung-Hwan alisaini mkataba wa miezi mitatu na timu ya Shi De ya Dalian, hadi sasa muda wa mkataba huo utamalizika mapema. Wakati Ahn Jung-Hwan na timu ya Shi De zilipojadili kuongeza muda wa mkataba huo, timu za Ligi ya J ya Japan na Ligi ya K ya Korea ya Kusini kwa mara nyingine tena zilitoa mwaliko wa kutaka kumsajili. Vyombo vingi vya habari vya China vinaona kuwa Ahn Jung-Hwan ataondoka timu ya Shi De, kwani hali ya timu hiyo imeshuka, na haipo kwenye nafasi juu kwenye Ligi ya soka ya China. Lakini jambo ambalo haikutarajiwa na watu ni kuwa Ahn Jung-Hwan aliamua kubaki kwenye timu hiyo, alisema:
"Klabu ya Shi De, wenzangu wa timu hiyo na wakazi wa Dalian walinipa misaada mikubwa, mashabiki wa hapa pia ni wakarimu sana, na wamenipa uungaji mkono mkubwa kuliko wale wa nchi nyingine duniani. Nataka kutoa shukrani zangu kwa vitendo vyangu, na kuwachezea soka."
Hivi sasa An Jung-Hwan mwenye umri wa miaka 33 amesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu na timu ya Shi De, na anatumai kumaliza maisha yake ya soka mjini humo.
"Ingawa sijakuwepo kwa muda mrefu nchini China, lakini nimepata uungaji mkono mkubwa kutoka kwa wachina, na washukuru sana! Nitafanya juhudi kubwa zaidi kuwaletea furaha kubwa zaidi. Asante sana! "
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |