• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Sikukuu ya Shoton ya kabila la Watibet

    (GMT+08:00) 2009-09-03 17:07:28

    Mkoa unaojiendesha wa Tibet ulioko kusini magharibi mwa China unajulikana duniani kama ni sehemu nzuri yenye miujiza. Mkoa huo una kilele cha Chomolangma, milima na maziwa mazuri yenye mvuto, utamaduni wenye historia ndefu na wanyama na mimea ya ajabu ya uwanda wa juu. Mbali na hayo, mila na desturi maalumu za wakazi wa mkoa huo pia zinawavutia watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani.

    Sikukuu ya Shoton ni moja kati ya sikukuu muhimu zaidi za jadi mkoani Tibet. Sikukuu hiyo inaanza tarehe 30 Juni kila mwaka kutokana na kalenda ya kitibet, na kusherehekewa kwa siku kati ya 6 na 7. Kwa lugha ya kitibet, maana ya Sho ni mtindi, na maana ya Ton ni kula. Hivyo sikukuu ya Shoton pia inajulikana kama ni sikukuu ya kunywa mtindi. Kwa mujibu wa mila na desturi za jadi za kitibet, sikukuu hiyo inaanza kwa sherehe ya kuonesha picha ya Budha.

    Wakati kunapambazuka na jua linapochomoza kwenye mlima wa Kanpeiwuzi, kwa kufuata sauti ya taadhima ya honi ya kidini, picha kubwa mno ya Budha inainushwa katika mlima ulioko nyuma ya Hekalu la Drepung. Picha hiyo ina urefu kama jumba lenye ghorofa 6, katika picha hiyo, Budha mwenye sura ya upole anatazama waumini wake juu ya mlima. Wakati huo huo, waumini na watalii wanaokusanyika chini ya picha hiyo wanarusha Hatta ambayo ni kitambaa cha kuonesha heshima kwa mujibu wa mila na desturi za baadhi ya makabila ya China kwa Budha, ili kuonesha matumaini yao mazuri. Waumini wa dini ya kibudha wanaamini kuwa, ni majaliwa yao kwa kuweza kuona sherehe ya kuonesha picha ya Budha, na hii pia ni fursa yao nzuri ya kumwabudu Budha, kufanya maombi, na kuomba baraka. Sufii wa kike Qichangcuo kutoka mji wa Beijing alisema,

    "Nina furaha kubwa, kwani ndoto yangu imetimia. Baada ya kurudi Beijing, nitajitakasa zaidi, na kufanya juhudi zaidi za kutukuza dini ya kibudha."

    Bibi. Gabriella anatoka Italia, na aliwahi kutembelea mkoani Tibet mara nne. Alisema,

    "Watu walioniachia kumbukumbu zaidi ni watibet waliokuja kumwabudu Budha. Baadhi yao walitoka Lhasa na Shigatse, wengine walitoka wilaya ya Aba, na inawachukua wiki mbili tatu kufikia mwisho wa safari. Naona kuwa kuamini dini ni jambo muhimu zaidi kwenye maisha yao. Sisi tukiwa wageni kutoka sehemu za nje, tunapaswa kuheshimu mazingira ya utakatifu ya hapa."

    Ikiwa alama ya utamaduni wa kitibet, sikukuu ya Shoton ina historia ya miaka karibu 1,000. Sikukuu hiyo ilianza karne ya 11, na zamani ilikuwa ya kidini tu. Lakini kuanzia nusu ya pili ya karne ya 17, sikukuu ya Shoton ilibadilika kuwa sikukuu muhimu ya umma, na mbali na sherehe ya kuonesha picha ya Budha, maonesho ya opera ya kitibet pia yanafanyika. Hivyo sikukuu hiyo pia inajulikana kama sikukuu ya maonesho ya opera ya kitibet, na sikukuu ya kuonesha picha ya Budha. Mwaka 1994, serikali ya mji wa Lhasa ilianza kubeba wajibu wa kuandaa sikukuu ya Shoton, shughuli mbalimbali za jadi katika sikukuu hiyo zote zimerithiwa vizuri, licha ya hayo, mambo mapya ya kisasa yakiwemo maonesho ya sanaa, utalii na mazungumzo ya biashara pia yanafanyika katika sikukuu hiyo. Wakati wa sikukuu ya Shoton, wakazi wa Lhasa wana siku kati ya 6 na 7 za mapumziko. Mwanafunzi wa shule ya sekondari ya 8 ya Lhasa Tsering Chokyi anaona kuwa, sikukuu hiyo ni tamasha kubwa, alisema,

    "Wakati wa sikukuu ya Shoton, tuna siku nyingi za mapumziko. Siku ya kwanza tunakwenda kutazama sherehe ya kuonesha picha ya Budha, baadaye tunakwenda kutazama maonesho ya opera ya kitibet yanayofanyika katika Kasri la Norbulingka na Longwangtan."

    Hivi sasa sikukuu ya Shoton imechanganya mambo mengi zaidi kuliko zamani. Kwa waumini wa dini ya kibudha, sikukuu hiyo ni fursa nzuri ya kumwabudu Budha, kwa watoto sikukuu hiyo ni siku zenye furaha za kucheza ngoma na kuimba nyimbo, na kwa upande wa mji wa Lhasa, kuandaa sikukuu hiyo ni njia muhimu ya kupata marafiki na kuhimiza maendeleo ya uchumi na jamii.

    Baada ya maendeleo ya miaka 1,000, sikukuu ya Shoton si kama tu sikukuu ya jadi ya watu wa Tibet na nchi nzima, bali pia ni sikukuu ya watalii kutoka nchi mbalimbali duniani. Bw. Bessey kutoka Ufaransa, alisema ana bahati sana kwa kuwa amekuta sikukuu ya Shoton anapotembelea Tibet kwa mara ya kwanza. Alisema,

    "Watu wa hapa ni wachangamfu sana. Tumetakiana kila la heri."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako