• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Urithi wa Utamaduni Usioonekana wa China"-Picha zinazochorwa Ndani ya chupa katika Mji wa Hengshui China

    (GMT+08:00) 2009-09-07 17:46:13

    Picha zilizochorwa kwenye sehemu ya ndani ya chupa ni sanaa ya kipekee nchini China, picha hizo zinazochorwa kwenye tabakero kwa ndani ni pamoja na picha za watu, mandhari ya mazingira ya asili, maua, ndege na sanaa ya maandiko ya Kichina. Tabakero ni kichupa kidogo kinachotengenezwa kwa kioo, fuwele au kaharabu. Picha hizo zinazochorwa ndani ya chupa zinaweza kuonekana kwa nje na kuvutia. Kutokana na umaarufu wa sanaa hiyo, mji wa Hengshui ulioko mkoani Hebei, kaskazini mwa China, umepewa jina la "Maskani ya Sanaa ya Picha za ndani ya chupa" na Wizara ya Utamaduni ya China, na mwaka 2006 sanaa hiyo iliwekwa kwenye orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana wa China. Mwanzilishi wa sanaa hiyo ya mji wa Hengshui Bw. Wang Xisan pia alichaguliwa kuwa ni mrithi wa sanaa hiyo.

    Bw. Wang Ziyong ni mtoto wa mwanzilishi wa sanaa hiyo Bw Wang Xisan. Bw. Wang Ziyong bado anakumbuka vizuri kwamba alipokuwa na umri wa miaka 15 mzee mmoja wa Marekani alitumia dola za Marekani laki 1.2 kununua seti moja ya tabakero zenye picha za wafalme wote wa Enzi ya Qing kwenye sehemu za ndani ambazo zilichorwa na baba yake. Mzee huyo wa Marekani alikuja China kwa ajili ya tu kuonana na Bw. Wang Xisan. Tokea hapo Bw. Wang Ziyong alitambua thamani kubwa ya sanaa hiyo, na mbele yake baba yake akawa mtu hodari na mwenye thamani kubwa.

    Sanaa ya kuchora picha kwenye sehemu ya ndani ya tabakero ilianza Enzi ya Qing, sanaa hiyo imegawanyika katika mitindo minne katika maeneo manne tofauti, moja kati ya mitindo hiyo ni mtindo wa mji wa Hengshui, mwanzilishi wa mtindo huo Bw. Wang Xisan amechanganya uchoraji wa Kimagharibi pamoja na uchoraji wa jadi wa kichina. Picha alizochora kwa mchanganyiko wa uchoraji wa kimagharibi na wa kichina zinavutia zaidi.

    Mwaka 1991, Bw. Wang Ziyong aliyekuwa na umri wa miaka 22 alihitimu kwenye kitivo cha sanaa katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Mkoa wa Hebei. Ili apate ufundi wa kuchora picha kwenye sehemu ya ndani ya tabakero, kwa hiari aliacha nafasi aliyopewa ya kubaki chuoni kuwa mwalimu na akaanza kuchora picha za sanaa hiyo. Kutokana na msingi wa ufundi aliopata kutoka kwa baba yake, Bw. Wang Ziyong alivumbua mtindo wake wa uchoraji. Alisema,

      "Nimebuni vifaa vya kuchorea kwa teknolojia ya kisasa, hivyo picha za watu kama wenye ndevu, nyusi na mvi naweza kuzichora kama za picha za kupigwa, na nimeendeleza zaidi uchoraji wa jadi namna ya kuonesha mazingira ya asili ya karibu na ya mbali pamoja na kivuli cha mandhari hayo kwenye maji."

    Mwaka 2001 Bw. Wang Ziyong aliombwa achore picha za marais wa nchi sita walioshiriki kwenye mkutano wa APEC ili kuwazawadia marais hao. Bw. Wang Ziyong anaona hii ni fursa nzuri ya kuitangaza duniani sanaa ya picha ndani ya tabakero, alisema,

    "Baba yangu aliwahi kusema, uchoraji wa 'picha ndani ya tabakero' ni mimi niliyeuvumbua, siwezi kuona sanaa hiyo ikitoweka katika uhai wangu.' Maneno yake hayo yana maana kuwa nijifunze vizuri na kurithi sanaa hiyo. Naona jukumu langu ni kubwa ambalo licha ya kurithi sanaa hiyo tena nawajibika kuiendeleza na kuwafundisha wengine ili idumishwe kizazi hadi kizazi."

    Licha ya kuchora picha Bw. Wang Ziyong anaona ana jukumu lingine ambalo ni muhimu zaidi. Mwaka 1997 alisajili "Kampuni ya Picha za Ndani ya Xisan" kwa kutumia jina la baba yake. Baada ya kuanzisha kampuni hiyo Bw. Wang Ziyong alifanya juhudi nyingi kueneza biashara yake katika soko la bidhaa za zawadi na kutangaza thamani ya bidhaa hizo. Alisema,

    "Kadiri maisha ya watu yanavyozidi kuwa bora ndivyo watu wanavyozidi kuhitaji vitu vya sanaa vyenye ufundi mkubwa wa kisanii ili wapambe maisha yao. Sanaa ya picha ndani ya tabakero itapata nguvu kubwa za uhai kutokana na jinsi maisha yanavyobadilika."

    Mwanzilishi sanaa hiyo Bw. Wang Xisan alichora picha zaidi ya elfu mbili, lakini picha hizo karibu zote zimekuwa mali za masoko machache kabisa duniani yenye uwezo mkubwa na ya kiwango cha juu zaidi, watu wa kawaida hawakupata fursa hata kuiona sanaa hiyo. Kwa hiyo kueneza sanaa hiyo hadi majumbani kwa watu wa kawaida limekuwa lengo la Bw. Wang Ziyong.

    Mwaka 2003 Bw. Wang Ziyong alijenga Jumba la Makumbusho la Picha zinazochorwa Ndani ya chupa za Xisan ili kuonesha sanaa hiyo. Jumba hilo lina ghorofa mbili, ghorofa ya chini ni maonesho na mauzo ya tabakero zilizochorwa picha na kwenye mlango wa jumba hilo kuna meza mbili ambazo wachoraji wawili wanaonesha ufundi wa kuchora picha, ghorofa ya kwanza ni maonesho kuhusu historia ya sanaa hiyo na kwenye ghorofa ya pili ni maonesho mengine husika.

    Baada ya jumba hilo la makumbusho kufunguliwa, kila siku wanakuja washabiki wengi kuangalia na kutoa mapendekezo yao. Katika miaka ya hivi karibuni Bw. Wang Ziyong amesanifu picha zaidi ya 50, hivi sasa kwenye mji wa Hengshui kuna watu zaidi ya elfu 8 wanaoshughulika na sanaa hiyo, na thamani ya kazi zao inafikia Yuan bilioni moja kwa mwaka. Kutokana na juhudi nyingi, urithi wa utamaduni usioonekana wa sanaa ya kuchora picha kwenye sehemu ya ndani ya tabakero unadumishwa na bidhaa za sanaa hiyo zimepata hali nzuri katika soko. Bw. Wang Ziyong anasema ingawa tabakero ni kichupa kidogo, lakini ana furaha kubwa kutoka sanaa hiyo, kwa hiyo hataiacha sanaa hiyo maishani mwake.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako