• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Nyimbo za kilimo wa Jiashan, urithi wa utamaduni usioonekana nchini China

    (GMT+08:00) 2009-09-10 16:46:21

    China ni nchi yenye ustaarabu wa kilimo wenye historia ya zaidi ya miaka 6,000, katika maendeleo ya jamii ya kilimo, kuna mambo mengi ya kufurahisha ya utamaduni wa kilimo, miongoni mwake, kuna nyimbo za kilimo. Nyimbo za kilimo ziliimbwa na wakulima walipofanya kazi za kilimo. Mwanzoni, zilikuwa zinaimbwa kwa ajili ya kuondoa uchovu, lakini kadiri ustaarabu wa binadamu unavyoendelezwa na kubadilika, ndivyo nyimbo hizo zinavyokuwa burudani katika kazi na sehemu ya maisha ya wakulima. Nyimbo za kilimo za Jiashan ni nyimbo maalum zinazoimbwa katika miji ya Jiashan, Qingpu na Luxu, kusini mwa China, na zinahifadhiwa vizuri. Mwaka 2008 nyimbo za kilimo za Jiashan ziliwekwa na baraza la serikali kwenye orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana wa ngazi ya taifa.

    Mliosikia ni wimbo uitwao Msichana wa Tano, ambao unaimbwa sana wilayani Jiashan. Wimbo huo ni mzuri, sauti yake ni nyororo na inasikika vizuri, na unaimbwa kwa lugha ya huko, ukieleza mambo mengi, na unaonesha maisha ya vijiji vya eneo la Ziwa Taihu. Kwa kuwa sauti ya wimbo wa aina hiyo ni ya juu, na unabadilika unapoimbwa, hivyo ni vigumu kuimba, hivi sasa kuna watu wachache sana wanaoweza kuimba wimbo huo, lakini Bibi Yang Lingzhen mwenye umri wa miaka 63 ni mmoja kati ya watu hao. Alisema,

    "Nilianza kujifunza nyimbo za kilimo nilipokuwa na umri wa miaka 11 au 12, mama yangu anajua kuimba, katika majira ya joto, tulipopumzika, mama yangu aliimba nilimsikia na nilijua kuimba."

    Kuanzia umri wa miaka zaidi ya 10 hadi umri wa miaka wa 60, Bibi Yang Lingzhen ameimba nyimbo za kilimo kwa miongo kadhaa. Hadi sasa, Bibi Yang Lingzhen bado anaimba nyimbo za kilimo anapofanya kazi za nyumbani.

    Hivi sasa, huko Jiashan wanaojua kuimba nyimbo za kilimo ni wazee wenye raika moja na Bibi Yang Lingzhen, wimbo wa aina hiyo hauwavutii sana vijana. Mtaalam maarufu wa nyimbo za kilimo Bw. Han Jinmei, ambaye pia ni mwanachama wa shirikisho la wanamuziki wa China alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hali hii sio tu inatokea hapa China, pia inatokea katika nchi nyingine nyingi. Alisema,

    "Nilipotoa mafunzo katika chuo kikuu cha muziki cha taifa la Korea ya Kusini, niliambiwa kuwa Korea ya Kusini pia inaathiriwa na utamaduni wa nchi za magharibi, vijana wanapokea muziki wa "rock na roll" kwa haraka, lakini hawataki kujifunza mila, desturi na utamaduni wao wa kikabila, wanaona kuwa umepitwa na wakati, hivyo waliniuliza kuwa sisi tunatatua suala hilo vipi, naona kuwa, ni lazima kuendeleza, kurithisha kwenye msingi wa kuendeleza, na kuendeleza urithi mzuri kabisa."

    Kwa hiyo, ili kuendana na zama mpya, waimbaji na wataalam wa wimbo wa kilimo wanafanya uvumbuzi, na kutunga nyimbo mpya kwenye msingi wa nyimbo za zamani. Nyimbo hizo mpya sio tu zimeendelea kuwa na mtindo mzuri wa zamani, bali pia zimeingizwa mambo mapya, ili kuenzi utamaduni wa kikabila na kuonesha sura mpya na mvuto wa zama tulizo nazo.

    Mliosikia ni wimbo uliotungwa upya uitwao "mji mdogo wenye historia ya miaka elfu moja ni mahala panapovutia". Katika miaka ya hivi karibuni, kadiri maendeleo ya shughuli za utalii yanavyotokea huko Xitang wilayani Jiashan, ndivyo watalii wengi zaidi wa nchini na nchi za nje wanavyokwenda kuutembelea mji huo mdogo. Wimbo huo ulitungwa kwa ajili ya kuambatana na kazi ya kuendeleza shughuli za utalii za Xitang. Unaimbwa hivi "upepo mwororo unapovuma katika majira ya mchipuko, bora twende tukafanya utalii. Ingawa vivutio ni vingi kote nchini, lakini Xitang ni mahali pazuri zaidi. Mji mdogo huo wenye historia ya zaidi ya miaka elfu moja ni mahali panapovutia, unifuate na usikilize wimbo wangu, tutembelee kwanza kwenye kichochoro cha Shipi katika mtaa wa magharibi, halafu tutembelee jumba la Zhongfu."

    Licha ya kukusanya, kuratibisha na kutunga nyimbo za zamani za kilimo, ili kuenzi sanaa hiyo ya zamani, kituo cha utamaduni cha wilaya ya Jiashan pia kinafanya shughuli za aina nyingi za kufundisha nyimbo za kilimo katika shule na mitaa.

    Ili kufufua sanaa hiyo, warithi wa nyimbo za kilimo pia wanatiliwa mkazo na kuungwa mkono na idara ya utamaduni ya serikali. Mwaka 2008, Bibi Yang Lingzhen akiwa mwimbaji wa nyimbo za kilimo aliwekwa kwenye orodha ya wasanii wa mji wa Jiaxing. Kadiri nguvu za kuuhifadhi wimbo wa kilimo zinavyoimarishwa, ndivyo nyimbo za kilimo za Jiashan zinavyorudisha uhai wake wa zamani.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako