• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mwanafasihi mkubwa katika Enzi ya Song Kaskazini, Ouyang Xiu

    (GMT+08:00) 2009-09-14 10:15:02
    Ouyang Xiu alikuwa ni mwanasiasa na mwanafasihi mkubwa katika Enzi ya Song Kaskazini ya zama za kale nchini China, na ni mmoja kati ya wanafasihi wakubwa wanane katika enzi za Tang na Song. Baba yake alifariki dunia wakati Ouyang Xiu alipokuwa na umri wa miaka minne tu, kutokana na umaskini, mama yake alimfundisha kuandika kwenye mchanga kwa bua la mtete badala ya kutumia karatasi, na alipokuwa na umri wa miaka 23 alifaulu mtihani wa mwisho wa kifalme.

    Kuhusu mtindo wa uandishi, Ouyang Xiu alipinga mtindo wa kuchezea maneno bila maana na kutetea kufanya mageuzi katika uandishi wa makala na mashairi. Harakati za mageuzi ya uandishi wa fasihi katika enzi za Tang na Song zililenga kuhuisha fikra za Confucius na kupinga mtindo wa kuchezea maneno na kutetea kufuata kanuni kwa uhuru, kutetea kuenzi "maandishi ya kale" ya enzi za Qin na Han, ambayo yalisaidia kuonesha maisha ya hali halisi na kueleza fikra.

    Bw. Ouyang Xiu alitetea sana mtindo wa "maandishi ya kale" usiokuwa na miiko mingi na kuandika makala kwa mtindo unaofaa wa kueleza fikra kwa mtiririko. Mtindo wa maandishi yake ulifuatwa na wasomi wengi wa zama za wakati wake na zama za baadaye. Katika maandishi yake ya aina mbalimbali, Ouyang Xiu alisimulia mambo mengi kwa kwa maana ya kina, maneno aliyotumia yalichaguliwa kwa makini na kueleza hoja kwa mtiririko na kueleza mambo yanayoweza kugusa hisia za watu. Bw. Ouyang Xiu ameacha johari kubwa katika historia ya fasihi ya China.

    Katika mambo ya siasa, Ouyang Xiu aliwahi kuwa ofisa katika serikali kuu na mitaa, kutokana na kuwalilia watu maskini na kuwa mkweli na muwazi, mara nyingi aliondolewa madarakani, na pia mara nyingi alirudishwa kazini. "Kumbukumbu za Mzee aliyelewa katika Kibanda" ni makala iliyompatia Ouyang Xiu umaarufu zaidi. Makala hiyo ilionesha hisia zake zisizo za kawaida kwa kueleza mazingira mazuri ya asili na hali nzuri ya jamii, kwamba ingawa hakuweza kutimiza matumaini yake alipokuwa ofisa mkubwa wa serikali kuu, lakini amepata mafanikio ya kiasi fulani baada ya kuvuliwa wadhifa mkubwa na kuwa ofisa wa mji mdogo wa Chuzhou, na mafanikio hayo kwa Ouyang Xiu ni faraja kubwa alipokuwa hoi baada ya shughuli nyingi.

    Katika makala hiyo, Ouyang Xiu alijifanya kama mzee aliyelewa, alikuwa ni mtu mwenye kifua kipana kwenye kibanda kimoja katika mazingira ya asili yenye mandhari nzuri mbali na mji wenye ghasia, katika mazingira hayo alijawa na raha na kuona ridhaa ya moyo.

    Kwa kueleza mandhari nzuri ya mazingira na mambo yaliyomkuta, mzee huyo alieleza yaliyokuwa moyoni mwake. Hisia zake hazikuandikwa moja kwa moja bali zilioneshwa kwa kueleza mandhari aliyoiona, hii iliifanya makala yake iwe ya kuvutia zaidi. Katika makala hiyo aliandika "Mzee anayekunywa pombe hayumo katika jambo hili, bali kwenye mandhari nzuri ya mito na milima" ni sentensi inayojulikana na kutumika sana.

    Ouyang Xiu alisifiwa zaidi kutokana na mandishi yake mengi yanayoeleza mandhari ya mazingira, vitu na watu. Maishani mwake aliandika makala 500 zikiwa ni pamoja na makala zinazohusu mambo ya siasa, masimulizi ya mambo na maelezo ya hisia. Makala hizo zote ziliandikwa bila kuachana na maudhui, makala za kueleza hoja zilielezwa vya kutosha na zinavutia, na makala zilizoeleza hisia au mandhari zinagusa hisia za wasomaji na kuwapelekea kwenye mazingira halisi.

    Mashairi ya Ouyang Xiu pia yana mtindo wake maalumu ambao ni kama mchanganyiko wa mitindo ya mashairi halisi na makala ya kawaida. Shairi lake lililo maarufu zaidi ni "Sauti ya Autumn", kwenye shairi hilo alitumia mifano mingi akieleza hali ilivyo wakati wa majira ya Autumn, na wasomaji wanaposoma wanajihisi kama wapo kwenye mazingira halisi. Mashairi yake yaliyo mengi yalieleza maisha magumu ya raia na kufichua giza la jamii, na katika mashairi hayo huzungumzia mambo ya siasa na kuponda upotovu wa kisiasa na mashairi yaliyoeleza hisia zake kwa kueleza mandhari ya asili pia yalikuwa mengi. Bw. Ouyang Xiu ni mwanafasihi mkubwa katika historia ya fasihi ya China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako