• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tamasha la sanaa la nchi za Asia mjini Erdos China

    (GMT+08:00) 2009-09-19 17:01:11

    Tamasha la 11 la sanaa la nchi za Asia ambalo linafanyika katika mji wa Erdos mkoani Mongolia ya Ndani China limeanza tarehe 18 Agosti na litamalizika tarehe 26. Ujumbe ulioongozwa na mawaziri wa utamaduni kutoka nchi 16, maofisa wa tume za nchi 28 nchini China na wasanii wa makundi ya kiserikali kutoka nchi 18 walishiriki kwenye tamasha hilo kwa nia ya kuimarisha maelewano, ushirikiano na kutunza tamaduni za jadi za aina mbalimbali za Asia.

    Mliosikia ni mchezo uliyooneshwa na wasanii kutoka Nepal na Afghanistan jioni ya tarehe 18 katika uwanja wa mji wa Erdos. Siku hiyo kutokana na mvua maonesho yaliyopangwa kufanyika uwanjani humo yaliahirishwa kwa saa mbili, hata hivyo wasanii na watazamaji hawakupungukiwa na hamasa zao.

    Lengo la kufanyika kwa tamasha hilo ni kuwaletea wasanii wa nchi za Asia fursa za maingiliano na kuonesha sura mpya ya tamaduni za Asia. Tokea Wizara ya Utamaduni ya China ianzishe tamasha hilo mwaka 1998, katika miaka 11 iliyopita, tamasha hilo limekuwa likistawi kutoka maonesho ya michezo ya sanaa tu ya hapo awali hadi shughuli za aina nyingi za hivi sasa zikiwemo ziara za maofisa waandamizi wa serikali, makongamano ya wataalamu, maonesho ya michezo ya sanaa na maonesho ya vitu vya sanaa.

    Waziri wa Utamaduni wa China Bw. Cai Wu alisema, sababu ya kuongezeka haraka kwa kiwango cha tamasha hilo ni kutokana na mahitaji ya pamoja ya nchi za Asia kuwa na ushirikiano mkubwa. Alisema,

    "Katika miaka ya hivi karibuni, tamasha hili limepata maendeleo ya haraka na kiwango chake kimekuwa cha juu zaidi, washiriki wamekuwa wengi na nchi zinalithamini zaidi tamasha hilo. Hali hiyo inatokana na mazingira ya utandawazi ya nchi za Asia kuwa yamezidi kutambua umuhimu wa ushirikiano na mshikamano wa bara hilo, kwa hiyo licha ya kuimarisha uchumi na biashara na ushirikiano wa kiteknolojia, maendeleo ya utamaduni pia yanatakiwa yawe ya haraka. Asia ni chanzo cha tamaduni nyingi duniani, hivyo kuimarisha maingiliano na ushirikiano wa kiutamaduni na kuwa na nia na fikra za namna moja ni suala muhimu la kuleta ustawi wa pamoja kwa nchi zote za bara hilo."

    Mkazi Ding Yajuan wa mji wa Erdos alimwambia mwandishi wa habari akisema, yeye na wanafamilia yake waliwahi kutalii Thailand na nchi nyingine nyingi za Asia, kwa hiyo anafahamu kwa kiasi fulani sanaa zao lakini anaona si nyingi kama zilizopo nyumbani kwake. Alisema,

    "Nilipotembelea katika nchi hizo sikuweza kufahamu mambo mengi kuhusu utamaduni wa nchi hizo, kwasababu wakati ulikuwa hautoshi lakini sasa nimeelewa mambo ya utamaduni wao niliyokuwa siyafahamu. Kwa mfano maonesho ya mavazi yaliyofanywa na wasanii wa Thailand na Malaysia yananivutia sana, sikupata kuona wakati nilipotembelea katika nchi hizo."

    Bila shaka wasanii wote wanataka kuonesha utamaduni mahususi wa nchi zao ili watazamaji wa China na wageni washuhudie utamaduni wao wa jadi. Kiongozi wa kundi la wasanii kutoka Kampuchea ambaye pia ni ofisa wa Wizara ya Utamaduni ya nchi hiyo Bw. Chan-Ninmenth alisema ametembelea China mara nyingi, lakini hii ni mara ya kwanza kuja kwenye sehemu ya makabila madogo madogo iliyoko kaskazini magharibi mwa China, kwa hiyo anaona ni fursa nzuri ya kutangaza utamaduni wa nchi yake sehemu hiyo. Alisema,

    "Tunaona fahari kwa kukaribishwa vizuri na wenyeji wa China. Hapa tumeleta utamaduni wetu wa jadi, tunatumai utamaduni huu wenye historia ndefu utavutia."

    Katika tamasha la mwaka huu serikali ya China imeshirikisha vikundi vya maonesho vya aina nyingi. Tarehe 19 asubuhi wageni kutoka nchini na nchi za nje walitizama maonesho kwenye sherehe kubwa ya "Nadam" ambayo ni ya jadi ya kabila la Wamongolia, sherehe hiyo ilifanyika katika uwanda wa majani, wachezaji zaidi ya elfu mbili walishiriki kwenye maonesho hayo wakionesha michezo yao ya ngoma na umahiri wa kupanda farasi. Mzee mwenye umri wa miaka 54 Bi. Narenhua ni mmoja katika kundi la wasanii wazee la kabila la Wamongolia, mzee huyo pamoja na wenzake walifanya mazoezi kwa siku kumi ili waweze kuonesha adabu kwa wageni. Alisema,

    "Leo asubuhi tulipanda jukwaani kuwatunukia wageni 'Hada' kitambaa cheupe cha hariri ambacho ni ishara ya kuwatakia wageni baraka. Kwa hiyo sisi wazee zaidi ya 100 tulifanya mazoezi kwa siku 10 kwa ajili ya kitendo hicho cha adabu."

    Katika uwanda wa majani vijana wa kabila la Wamongolia zaidi ya 500 walionesha michezo ya jadi ikiwa ni pamoja na mashindano ya mwereka, kulenga shabaha kwa mishale, umahiri wa kupanda farasi na mashindano ya mbio za ngamia.

    Katika siku za tamasha hilo, wakazi wa mji wa Erdos na wasanii wa nchi za nje pia walifanya michezo ya sanaa huku wakiwa wanatembea barabarani. Tarehe 19 jioni wasanii kutoka nchi 16 walionesha tamaduni za nchi hizo wakiwa ndani ya malori 33.

    Kadhalika, tamasha hili pia limewapatia washiriki wa nchi mbalimbali nafasi ya kubadilishana fikra za namna ya kutunza na kuendeleza utamaduni wa jadi wa nchi zao. Waziri wa utamaduni wa Japan Bw. Tamai Hideo anaona kwamba nchi za Asia zinatakiwa zishirikiane ili kukabiliana na changamoto na kuimarisha taathira ya utamaduni. Alisema,

    "Mfano mzuri ni mkutano wa majadiliano, nchi zinatakiwa ziimarishe uelewano, zikubaliane kimawazo na zitunze kwa pamoja utamaduni wa aina tofauti. Na juu ya msingi huo tuimarishe nguvu za kiutamaduni katika kukuza uchumi na kukabiliana na msukosuko wa kiuchumi kwa mshikamano."

    Naibu waziri wa utamaduni wa nchi ya Mongolia Bi. Chonoi Kulanda alisema nchi yake imenufaika sana kutokana na tamasha hili na hasa ushirikiano kati ya nchi yake na China. Alisema,

    "Ninaona kwamba nchi yetu inaweza kujifunza mengi kutoka utamaduni wa jadi wa kabila la Wamongolia nchini China, naona utamaduni wa Kimongolia umeenziwa vizuri nchini China. Ili kudumisha utamaduni huo ambao ni wetu wa pamoja inatupasa tuimarishe ushirikiano katika nyanja mbalimbali za utamaduni, China na nchi nyingine za Asia."

    Katika siku za tamasha hili, China, Japan, Viet Nam, Singapore na nchi nyingine jumla 17 zilitia saini taarifa ya pamoja ya "Mapendekezo ya Erdos" ambayo inazitaka nchi za Asia zienzi utamaduni wao wa aina tofauti.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako