• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Hoteli iliyo karibu zaidi na majumba ya wafalme wa zamani wa China

    (GMT+08:00) 2009-09-21 14:26:49

    Majumba ya wafalme wa China yaliyoko mjini Beijing yalikuwa ni mahali penye heshima kubwa na yenye mambo mengi yasiyofahamika kwa watu wengine katika enzi zile. Hivi sasa kuna hoteli moja, ambayo inawezesha kumfanya mtu ahisi hali ya umaalumu wa kuwa jirani na mfalme. Kama ukikaa kwenye hoteli hiyo, basi mawazo yako yanaweza kukupotosha, na kukufanya udhani uko kwenye enzi ya kifalme, na raha unayopata ukiwa kwenye hoteli hiyo pengine ni zaidi ya waliyokuwa wakipata wafalme wa zamani.

    Hoteli hiyo ya kifalme iko kwenye upande wa mashariki wa mto unaoyazunguka majumba ya wafalme wa zamani, na ni jirani na majumba hayo. Asubuhi unaweza kula chakula huku ukiburudishwa kwa mandhari ya majumba ya wafalme, bustani ya Jingshan na bustani ya Beihai; jioni unaweza kuoga kwenye bafu lenye maji yenye vipande vya maua, wakati wazee wanaoishi kwenye nyumba za zamani za wakazi wa Beijing, Hutong, ambayo ni mitaa midogo, wanajitokeza majumbani wakiwa wamebeba viota vya ndege mikononi, na watoto wakiwa wanachezacheza kwa furaha………raha ya mji wa kifalme wa nchi ya kale iko katika maisha ya Hutong ya wenyeji wa Beijing, ambayo inawavutia sana watu. Mwanzilishi wa hoteli hiyo, ambaye sasa ni mkurugenzi mkuu Bw Liu Shaojun alisema, sababu kubwa iliyomfanya aanzishe hoteli huko, kwanza kabisa ni mahali pazuri na pekee panapowawezesha wageni waone vizuri majumba ya wafalme kutoka kwa juu. Alisema:

    "Hii ni sehemu isiyo kelele kwenye mji huu wenye pilikapilika nyingi, sehemu hii iko katikati ya mji, lakini ni sehemu isiyo na kelele. Kwani majengo unayoyaona hapa ni majumba ya wafalme yaliyokuwepo zaidi ya miaka 700 iliyopita, lakini unapogeuka na kuangalia upande wa mashariki, unaweza kuona majengo mengi ya kisasa yaliyoko kwenye mtaa wa Wangfujing. Ingawa makundi hayo mawili ya majengo yana tofauti ya zaidi ya miaka 700 au miaka 800 hivi, lakini yako pamoja kwa mapatano. Wakati mwingine tofauti hii inaweza kumfanya mtu ajiulize mimi ni nani, ninatoka wapi, na ninakwenda wapi? Kwa hiyo ninaipenda sana sehemu hii."

    Unaposikia jina la Royal Inn, pengine unaweza kudhani kuwa hii ni hoteli ya kifahari, ya kale na yenye umaalumu wa jadi ya China. Lakini unapoingia kwenye mlango mkubwa wa hoteli hiyo, bila shaka utaona mbele kuna mwanga bila wewe kutarajia. Mkurugenzi mkuu wa hoteli hiyo Bw Liu Shaojun alitufahamisha kuwa, hoteli hiyo ilisanifiwa na kampuni ya GRAF, ambayo ni kampuni maarufu ya usanifu wa majengo nchini Ujerumani, hoteli hiyo imebakiza kuta za matofali na paa la jengo la zamani, isipokuwa ndani kumerekebishwa na kuwa na mtindo wa kisasa kabisa. Kampuni ya mawasiliano na watu ya Walter Junger ilisaidia kubuni chapa, wazo la uvumbuzi na maandalizi ya uendeshaji wa shughuli za hoteli. Hiyo ni hoteli pekee nchini China, ambayo usanifu wake na nia ya uvumbuzi wake una lengo la kutafsiri utamaduni wa China kwa lugha ya kimataifa. Alisema,

    "ndiyo maana ulipoingia kwenye mlango wa hoteli uliona mbele yako kuna mwanga: mahali ninapofika ni China? Hii ni hoteli ya kifalme? Hiyo kabisa ni hoteli ya kisasa na ni hoteli maridadi sana. Vitu vya kichina si kitu kingine, bali ni kitu kimoja machoni pa wageni kinachowasaidia wageni kuielewa China. Tunatafuta kiunganisho kati ya mashariki na magharibi, kati ya China ya kale na ya jadi pamoja na China ya kisasa."

    Hoteli hiyo ya kifalme ina sehemu tatu za bwalo la chini ya ardhi, vyumba vya kulala na sehemu ya juu ya jengo. Kati ya sehemu hizo, bwalo la chini ya ardhi na sehemu ya chini ya jengo la hoteli ni ya rangi ya chungwa, ghorofa ya kwanza ina rangi ya kijani, ghorofa ya pili ina rangi ya buluu nzito, mtu akisimama na kuangalia mbele kwenye ukumbi wa hoteli kupitia vioo vikubwa maalumu, anaweza kuona kuta za rangi nyekundu za majumba ya wafalme, ambazo sehemu yake ya chini imepakwa rangi ya manjano, na paa lililoezekwa kwa vigae vinavyong'aa kama kioo; na kama ukitupia macho ndani ya jengo, zinaonekana rangi tatu za manjano, kijani na buluu, ambazo zote ni rangi za jadi zilizotumika katika majumba ya wafalme ya China katika zama za kale. Msanifu anaona kuwa, "rangi hizo zina uhai mkubwa na zinavutia, na ni sehemu ya utamaduni wa China".

    Katika hoteli ya kifalme, vyumba 55 vinawakilisha wafalme 55 wa China, wageni wanapotafuta vyumba vyao kwa kufuata kadi za vyumba walizopewa, pengine wanaweza kuwa na mashaka, kwani kwenye kadi zao hakuna namba ya chumba isipokuwa kuna mchoro rahisi wa mfalme unaolingana na mchoro ule uliochorwa kwenye mlango wa chumba. Mgeni anapoondoka hotelini, atapata mhuri wa kichina uliochongwa mchoro wa mfalme ulioko katika chumba alicholala. Mkurugenzi mkuu Liu anaona kuwa, mbali na kujitahidi kupamba vizuri hoteli yao, wanatarajia zaidi kuonesha utamaduni wa jadi wa China kwa huduma wanazotoa. Alisema

    "Kwa mfano, kila mgeni anapoingia katika chumba chake, tutamwambia, simu ya kwanza anayopiga iwe kwa sehemu yoyote duniani, malipo ya dakika tatu za mwanzo yanasamehewa. Pengine ataniuliza kwa nini? Mimi nitamweleza, hii ni desturi ya sisi wachina, kwani sisi wachina bila kujali mtu anasafiri kwenda wapi, tunawatumia ujumbe watu wa familia kuwa tumefika salama, kwa hiyo simu ya kutoa habari ya kuwa umefika salama haitozwi malipo. 'Mtoto hawezi kusafiri kwenda mbali kama anatakiwa kuwatunza wazazi wake, endapo analazimika kusafiri ni lazima awaambie wazazi wake mahali anapokwenda'. Wewe umefika katika hoteli yetu, ninatarajia uwajulishe ndugu zako kuwa umefika salama, na ninatarajia kumfikishia mgeni sehemu hiyo nzuri ya utamaduni wa China kutokana na mabadiliko ya huduma zetu, na kutaka mgeni aone nchi yetu China kweli ni nchi yenye ustaarabu."

    Katika muda usiofikia mwaka mmoja tangu hoteli ya kifalme ianze shughuli zake, wageni wake waliotoka sehemu mbalimbali za dunia wanaisifu sana. Mwezi Novemba mwaka 2008, jarida maarufu la Marekani linaloitwa "Forbes" lilitoa orodha ya hoteli 12 za kiwango cha juu kabisa za duniani zinazochaguliwa na wafanyabiashara, hoteli ya kifalme ya Beijing iko kwenye orodha hiyo. Maelezo ya jarida hilo yanasema, "kukusanyika kwa lugha ya usanifu ya kisasa na umaalumu wa jadi ya China. Usanifu wa hoteli ya kifalme ya Beijing, ambayo iko kwenye upande wa mashariki wa majumba ya wafalme wa zamani na iko karibu na uwanja wa Tiananmen, ni wa ujasiri mkubwa, kulala katika vyumba 55 vyenye majina ya wafalme wa enzi mbalimbali wa China, kunamfanya mgeni ajihisi kama yeye ni mfalme anayetawala nchi hiyo."

    Kijana Michael Schaible kutoka Ujerumani ni msaidizi wa meneja mkuu wa hoteli hii. Anaona kinachovutia zaidi cha hoteli ya kifalme ni mahali wa kipekee na usanifu maalumu, kuna wageni wengi kutoka nchi za nje, waliovutiwa na kufika kwenye hoteli hii bila kujali umbali. Alisema

    "Wageni wengi wanapenda usanifu maalumu wa hoteli hii, kwani tunachofuatilia si mtindo wa kawaida wa hoteli peke yake. Ikilinganishwa na kazi za hoteli kubwa kubwa, hapa pananifurahisha zaidi, kwa sababu katika hoteli kubwa, ninazungukazunguka kwenye meza ya kaunta ya mbele tu. Lakini katika hoteli yetu hii, ambayo ni ndogo kiasi, ninapata muda mwingi zaidi wa kuwa pamoja na wageni. Katika kazi yangu za kila siku, zaidi ya nusu ya muda wangu nautumia kuwa na wageni katika eneo la wazi za hoteli hiyo."

    Bi Renate Muniz na mumewe kutoka Hispania, waliokuja kutalii mjini Beijing, wanaona kuwa ni furaha kulala kwenye hoteli ya kifalme ya Beijing, tena muhimu zaidi kwao ni kuweza kuhisi utamaduni wa China kwa karibu zaidi. Alisema,

    "Hoteli hii iko kwenye sehemu maalumu sana, mara baada ya kutoka kwenye mlango wa hoteli hii, tunaona majumba ya wafalme. Vilevile tunaona makazi ya Hutong ya sehemu hii yamehifadhiwa na kutunzwa vizuri. Ninaona kulala katika hoteli hii ya kisasa, kunaniwezesha kuona vizuri maisha ya wakazi wenyeji. Unapoingia kwenye Hutong, unaweza kushuhudia maisha ya kweli ya watu wa China, ambayo hapo zamani tuliweza kuyafahamu kwa kusoma vitabu tu.

    Mbali na mazingira mazuri ya kupumzika, hoteli ya kifalme ina bwalo moja linalopika vitoweo vilivyobuniwa vya kifalme; wakati wa usiku, unaweza kuangalia mandhari ya majumba ya wafalme, bustani ya Jingshan au kunywa vinywaji na marafiki kwenye baa la sehemu ya juu ya jengo. Mkurugenzi mkuu Bw Liu Shaojun anatarajia kuwa wageni wanaolala kwenye hoteli ya kifalme wataona ufahari wa kifalme, huku wakiweza kuona furaha na upendo wa nyumbani. Alisema, "ukilala kwenye hoteli ya kifalme, utaona mwili wako uko katika mazingira ya kifalme, na mawazo yako pia yatakuwa katika mazingira ya kifalme.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako