• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Milima, mito na mbuga nzuri ya wilaya ya Keshiketeng

    (GMT+08:00) 2009-09-28 20:39:45

    Katika miaka ya hivi karibuni, kadiri hatua za ufunguaji mlango zinavyoharakishwa katika mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, ndivyo mkoa huo unavyofahamika zaidi kwa watu wengi. Kila kipindi cha majira ya joto kinapofika, ukanda wa mbuga huwa unaonekana unapendeza zaidi, ambapo idadi ya watalii wanaokwenda huko kuangalia mbuga, anga ya buluu na mawingu meupe inaongezeka kwa mfululizo. Katika kipindi hiki cha leo, tutawafahamisha kuhusu wilaya ya Keshiketeng, ambayo ni mahali pazuri penye furaha na vivutio vingi.

    Wilaya ya Keshiketeng ina makabila 10 yakiwa ni pamoja na Wahan, Wahui, Waman na kabila la Wamongolia ambalo lina watu wengi zaidi kuliko ya makabila mengine katika wilaya hiyo. Wilaya hii iko kwenye mji wa Chifeng, mashariki mwa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, na iko umbali wa zaidi ya kilomita 600 kutoka mji mkuu Beijing. Idadi ya watu wa Keshiketeng ni karibu laki 2.5, eneo lake ni kiasi cha kilomita elfu 20 za mraba. Wilaya ya Keshiketeng iko kwenye sehemu yenye makutano ya milima ya Yanshan, milima ya Daxinganling na jangwa la Hunshandake, hivyo hali maalumu ya kijiografia na muundo maalumu wa kijiolojia ya sehemu hii, vinaifanya sehemu hii iwe na mandhari ya kipekee ya kimaumbile na kusifiwa kama ni hazina ya Mongolia ya ndani.

    Keshiketeng ni sehemu inayowavutia sana watu, kila mwaka kuna idadi kubwa ya watalii wa nchini na kutoka nchi za nje wanaotembelea sehemu hiyo. Katika ardhi ya eneo hili kuna vivutio vingi vya utalii vikiwa ni pamoja na misitu ya mawe, mbuga, jangwa, misitu ya asili na ziwa lenye maji chumvi. Eneo hili lina sehemu kadhaa zenye mandhari nzuri za ngazi ya kitaifa na kimataifa, wilaya ya Keshiketeng ilipewa jina la "bustani ya kijiolojia ya kimataifa" na shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa mwaka 2005. Mkurugenzi wa idara ya utalii ya Keshiketeng Bw Sun Mingyu alisema,

    "Hapa kuna vivutio vingi vya utalii, vivutio vya utalii vya aina zote vilivyoko katika mkoa wa Mongolia ya ndani, zinapatikana Keshiketeng. Kutokana na kuwepo kwa vivutio vingi namna hii kwenye eneo hili lenye kilomita elfu 20 tu za mraba, tunaiita wilaya ya Keshiketeng kuwa ni "mfano wa Mongolia ya ndani."

    Hapa kuna mbuga nzuri, misitu minene, maskani ya ndege yenye ziwa kubwa, unapoingia kwenye wilaya ya Keshiketeng utafurahi sana, uwe umepanda farasi na kukimbia kwenye mbuga, iwe ni kuoga kwenye chemchemi ya maji moto, kukamata samaki ziwani, kuwinda msituni, au kutalii kwenye mji wa kale, ilimradi unajishirikisha na shughuli hizo utakuwa na furaha. Kwenye mkutano wa kwanza wa mazungumzo ya shughuli za utalii wa Asia na Pasifiki, mji wa Keshiketeng uliteuliwa kuwa ni "sehemu nzuri ya kutalii nchini China". Kwa hiyo ukienda kwenye mkoa wa Mongolia ya ndani, usikose kutembelea Keshiketeng.

    Keshiketeng haiko mbali, tena kuna njia nyingi za reli na barabara zinazofika huko, licha ya hayo treni maalumu ya kwenda kutalii Keshiketeng kutoka Beijing ilizinduliwa mwaka jana. Ili kuinua uchumi wake kwa kutumia rasilimali za utalii za huko, wilaya ya Keshiketeng pia imechukua hatua mbalimbali kuimarisha ujenzi wa miundombinu ili kuunganisha sehemu nane muhimu za utalii. Mkurugenzi Bw. Sun Mingyu alisema,

    "Sehemu 8 za bustani ya kimataifa ya kijiolojia ziko kwenye eneo la kilomita za mraba 5,000, kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ya eneo hilo si mbali, lakini zamani njia zilizozifika kwenye sehemu hizo hazikuwa nzuri, kwa hiyo watalii walisumbuka sana. Kuanzia mwaka 2005, serikali ya huko ilitenga kiasi cha Yuan milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na sehemu zenye mandhari nzuri. Hivi sasa sehemu zote zenye vivutio za eneo hilo la utalii zimeunganishwa kwa barabara."

    Takwimu zinaonesha kuwa katika miaka minne iliyopita, idadi ya watalii waliotembelea wilaya Keshiketeng iliongezeka kwa 20% kwa mwaka, hususan mwaka jana idadi ya watalii ilifikia milioni 1.65, hivi sasa shughuli za utalii zimekuwa nguzo muhimu ya uchumi wa wilaya hiyo.

    Mkurugenzi wa idara ya utalii ya Keshiketeng Bw Sun Mingyu alisema mazingira ya asili ya wilaya ya Keshiketeng ni dhaifu, mbinu za jadi za kilimo na ufugaji zinaharibu vibaya mazingira ya viumbe. Katika jitihada za kuendeleza shughuli za utalii, serikali ya huko imepiga marufuku kufuga mifugo kwenye eneo la utalii, baada ya kuendeleza utalii kwenye mazingira ya asili katika wilaya ya Keshiketeng, shughuli za utalii zimekuzwa kwa mfululizo, vivutio vya utalii na mazingira ya asili zote zimehifadhiwa vizuri. Mkurugenzi Bw Sun Mingyu alisema,

    "Kuendeleza utalii kwenye mazingira ya asili kwa upande mwingine ni kubadilisha mawazo wa wakulima na wafugaji wa huko, tunatoa wito wa kuwataka wahifadhi mazingira ya ikolojia, pia wabadilishe mitazamo ya watu na mtindo wa uzalishaji mali, tunataka watu wengi zaidi watoke katika shughuli za kilimo na ufugaji na kujiunga na sekta ya utoaji huduma."

    Hivi sasa, wafugaji wengi licha ya kushughulikia ufugaji wa mifugo, wanaanzisha shughuli za utalii kwenye malisho yao. Katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kutekelezwa utaratibu wa kandarasi mbili kuhusu mifugo na majani malishoni, mabadiliko makubwa yametokea katika shughuli za uzalishaji mali na maisha ya wafugaji, kama mkienda kuwatembelea wafugaji kwenye mbuga, mtafurahishwa sana na mtindo wa maisha, kazi na mavazi ya wakazi wa huko.

    Keshiketeng ni sehemu nzuri na yenye mambo mengi ambayo bado hayafahamiki, Keshiketeng ni kama lulu inayong'ara sana kwenye ukanda wa mbuga wa Mongolia ya ndani, inawavutia wageni wa nchini na wa kutoka nchi za nje kwa utamaduni na mila ya kikabila na mandhari nzuri ya kimaumbile.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako