• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Bw. Anura, kijana wa Sri Lanka anayeipenda China

    (GMT+08:00) 2009-10-16 16:08:02

    "Jina langu ni Anura, ninatoka Sri Lanka, nchi iliyopo Asia ya kusini, ambayo ina hazina nyingi, zikiwemo chai nyeusi, nazi na manukato yenye sifa nzuri." Kijana huyo anayeongea vizuri lugha ya Kichina alipokuwa anafahamisha chai, alisema,

    "Tutazame rangi ya majani ya chai ya Kandy. Kwa kawaida, tukimimina chai nyeusi kwenye kikombe, hatumimini nyingi, kwani baadaye tunapaswa kuweka maziwa kidogo." Mwandishi wetu wa habari alimwona Bw. Anura katika sehemu ya Xuanwu mjini Beijing, akiwa anawaelekeza wateja njia ya kutengeneza chai nyeusi ya Lanka katika duka lake la chai. Bw. Anura alisema sera ya China ya mageuzi na ufunguaji mlango imeanzisha mawasiliano kati ya China na dunia, ambayo inawawezesha wageni wengi kama yeye wanaoipenda China na utamaduni wa China kuja China, kujifunza utamaduni wa China na kujionea wenyewe maendeleo ya uchumi na jamii ya China. Alisema China inampa fursa nyingi za kujifunza kwa kina na kujiendeleza siku hadi siku. Bw. Anura ambaye alikuwa na umri wa miaka 19 alikuja hapa China kwa mara ya kwanza miaka 14 iliyopita, na kuanzia hapo hakuondoka tena China. Bw. Anura alisema, anapenda sana Wushu ya China, ndiyo maana alikuja China, ambapo maisha yake yakabadilika. Alisema,

    "Nilikuja hapa Beijing kutokana na kupenda Gongfu ya China. Kabla ya hapo, nilijifunza Wushu kwa miaka mitatu na nusu nchini Sri Lanka. Mwaka 1995, serikali ya China iliipa Sri Lanka nafasi moja ya udhamini wa masomo ya Wushu, halafu nilipitia mitihani mbalimbali, na kwa bahati nzuri nilipata nafasi hiyo ya kuja China kusoma." Bw. Anura ana ndugu watano, wote wanajifunza Wushu. Kutokana na ushawishi wa familia yake, Bw. Anura alipenda kutazama filamu za Bruce Lee kuanzia utotoni, na kuwa na ndoto ya kwamba siku moja atakuwa "mtu wa kuruka" kama Bruce Lee. Kabla ya kuja China, Bw. Anura alidhani kuwa kila Mchina anajua kucheza Gongfu. Hivyo "alisikitika" kidogo baada ya kuja hapa Beijing, kwani alikuta si wote wanaweza kucheza Gongfu. Lakini majengo marefu hapa na pale na magari mengi barabarani hapa Beijing yalimpa picha nzuri. Katika miaka mitatu ya mafunzo ya Wushu katika Chuo Kikuu cha Michezo cha China, Bw. Anura alithamini sana fursa hii na kujifunza kwa bidii. Kwa miaka miwili tu, Bw. Anura alipata ngazi ya kwanza ya kitaifa ya mchezo wa Wushu, na hivyo kuwa Msri Lanka wa kwanza kupata sifa hiyo. Wakati huo, kijana huyo wa Sri Lanka pia alianza kuupenda utamaduni wa China. Mwaka 2000 Bw. Anura alikuwa mwanafunzi wa msanii maarufu wa Ngonjera wa China Bw. Ding Guangquan, na kufanya maonesho na mwalimu wake mwezi Oktoba mwaka huohuo, baadaye alijifunza opera ya kibeijing na Kuaiban kutoka kwa mwalimu wake. Baada ya kujifunza kutoka kwa mwalimu Ding, Bw. Anura anashiriki mara kwa mara kwenye maonesho na mashindano mbalimbali makubwa, kwa kuwa anaongea vizuri lugha ya Kichina, anacheza vizuri Gongfu na anafanya maonesho mazuri, hivyo anasifiwa sana na watazamaji wa China. Licha ya kupata heshima, Bw. Anura pia amepata zawadi yenye thamani kubwa zaidi katika maisha yake, yaani alipata mapenzi ya msichana wa China. Kutokana na wote wawili kuipenda Wushu na utamaduni wa China, vijana hao wawili walifahamiana na kupendana. Kutokana na kuipenda Wushu na kumpenda msichana huyo, Bw. Anura aliacha mpango wake wa kurudi nchini Sri Lanka, na kuamua kubaki nchini China. Mwaka 2003, Bw. Anura alimaliza masomo yake ya shahada ya pili katika Chuo Kikuu cha Umma cha China, na kuoana na msichana huyo. Alipokumbuka miaka 14 ya masomo, maisha na kazi nchini China, Bw. Anura alisema, China inampa nafasi na fursa ya kukua kwa pande zote. Katika miaka 14 iliyopita, China pia imekuwa na mabadiliko makubwa, na mabadiliko hayo yanamfurahisha sana. Alisema,

    "Katika miaka 14 iliyopita, China imekuwa na mabadiliko makubwa. Kwa mfano Beijing ya hivi sasa na niliyoiona miaka 14 iliyopita ni tofauti. Sasa Beijing imejenga barabara 6 zinazozunguka mji, pia imejenga majengo marefu mengi……ni vigumu kueleza mabadiliko hayo kwa maneno machache. Kwa ujumla, watu wote wa China wametoa mchango wao kwa ustawi wa China." Hivi sasa, mkwe huyo wa China kutoka Sri Lanka amekuwa Mbeijing halisi. Anashughulikia biashara ya chai nyeusi ya Sri Lanka hapa China. Bw. Anura alisema, China ni nchi inayozalisha kwa wingi chai ya kijani, na Sri Lanka ni nchi inayozalisha kwa wingi chai nyeusi, chai sio tu ni bidhaa, bali pia inabeba utamaduni wa chai. Alisema anataka kuwa mfanyabiashara anayefanya biashara ya chai, huku akieneza utamaduni wa chai, ili kuhimiza mawasiliano ya uchumi, biashara na utamaduni kati ya China na Sri Lanka. Tarehe 6 Machi mwaka 2009, kwenye maadhimisho ya miaka 52 tangu China na Sri Lanka zianzishe uhusiano wa kibalozi yaliyoandaliwa na ubalozi wa Sri Lanka nchini China, Bw. Anura alipewa "tuzo ya biashara na uwekezaji kati ya China na Sri Lanka". Alisema,

    "Nina matumaini kuwa katika siku za usoni, kampuni yangu itakuwa na fursa kubwa zaidi ya kujiendeleza. Nataka kuzitangaza sanaa za jadi za mikono za Lanka na pombe ya mnazi kwa China. Mkoa wa Hainan pia unazalisha pombe ya mnazi, lakini pombe nzuri zaidi ya mnazi inazalishwa huko Lanka. Nitaendelea kushughulikia biashara kati ya China na Sri Lanka." Alipoulizwa kuwa ni kwa nini anataka kushughulikia biashara kati ya nchi hizo mbili, Bw. Anura alisema,

    "Sri Lanka ni taifa langu, nilizaliwa nchini Sri Lanka; lakini China pia ni taifa langu, ninaishi hapa China. Baada ya miaka mitano, muda wangu wa kuishi nchini China utakuwa sawa na ule nilioishi nchini Sri Lanka. Nayapenda mataifa haya mawili. Kusema kweli, naipenda zaidi China, kwa sababu hapa kuna mke na watoto wangu, na familia yangu." Bw. Anura alisema, ataendelea kuishi nchini China, kwa sababu mke wake, shughuli zake, Wushu, ngonjera, Kuaiban na Opera ya kibeijing anazozipenda zote ziko nchini China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako