• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 1027

    (GMT+08:00) 2009-10-26 14:59:44

    Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa SLP.161 Bariadi Shinyanga Tanzania ametutumia barua akisema, ni miaka 45 sasa imepita tangu nchi zetu mbili tukufu, Jamhuri ya watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilipoanzisha uhusiano wa kibalozi mnamo tarehe 26 mwezi April mwaka 1964. Tarehe hiyo ni siku ambayo nchi yetu pia iliandika historia ya pekee barani Afrika ambapo Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuzalisha nchi mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

    Mintaarafu ya makala, kipindi hicho cha miaka 45 ya uhusiano na ushirikiano wa nchi zetu China na Tanzania, mambo mengi mazuri na yenye manufaa makubwa yamefanyika na hivyo kujenga misingi imara na ya kudumu ya mawasiliano na ushirikiano huu usio na mashaka. Niseme mapema tu kwamba, mustakabali wa ushirikiano kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mzuri na umejikita katika dhamira njema na ipo mikakati mizuri na sera mwafaka zenye ubunifu na ugunduzi wa kiwango cha juu na msisitizo wa nguvu ya hoja inayokubalika kwa pande zote mbili, ili kuendeleza uhusiano huu wa kindugu ulioanza tangu enzi na dahari hata kabla ya taifa letu halijajikomboa kutoka kwa ukoloni.

    Viongozi waasisi wa nchi zetu tunaowaenzi na kuwakumbuka sana Hayati mwenyekiti Mao Zedong wa China na Hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanazania ni viongozi mashuhuri wa kukumbukwa na kuenziwa daima kwa heshima zote na vizazi vyote katika historia ya nchi zetu mbili China na Tanzania. Mwaka 1965 waziri mkuu wa China Hayati Komredi Chou Enlai alitembelea Tanzania na kushangiliwa sana na wananchi, viongozi wa ngazi za juu na maafisa waandamizi wa chama na serikali na taasisi muhimu kutoka China walifanya ziara ili kuhakikisha kwamba mambo yanakuwa sawa sawia ili nchi zetu ziweze kushirikiana na kusaidiana kadri iwezekanavyo.

    Rais wa kwanza wa Tanzania ambaye pia ni Baba wa taifa letu, Hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa uhai wake alizuru China mara nyingi sana, lengo likiwa ni kujenga na kuimarisha urafiki na ushirikiano mkubwa kabisa kati ya China na Tanzania. Juhudi na malengo ambayo yameleta matunda mengi hadi sasa na leo hii tunashuhudia ushirikiano wa namna kwa namna wa serikali zetu pamoja na wananchi wa China na Tanzania kwa kiwango cha juu sana kisichoweza kulinganishwa. Jamhuri ya watu wa China imeisaidia sana Tanzania katika mipango na miradi mingi ya maendeleo ikiwemo miundo mbinu ya barabara, usafiri, viwanda, shule, afya, miradi ya maji, viwanja vya michezo, majengo, reli na hata wataalamu wa fani mbalimbali na kadhalika. Mfano ujenzi wa reli ya Tanzania na Zambia-Tazara na uwanja mkubwa kabisa wa taifa wa michezo uliojengwa mjini Dar es Salaam Tanzania ambao mheshimiwa Rais Hu Jintao wa China aliukabidhi kwa serikali ya Tanzania mwezi Februari mwaka huu wa 2009.

    Kwa hakika ziara ya kiserikali aliyoifanya rais wa China mheshimiwa Hu Jintao nchini Tanzania mwezi huo wa Februari ni tukio kubwa na ziara ya kihistoria kwa mkuu huyo wa nchi na imefungua ukurasa mpya wa kidiplomasia na ushirikiano baina ya Jamhuri ya watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika ziara yake rais Hu Jintao alifanya mazungumzo na mheshimiwa rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete. Aidha mheshimiwa rais Hu Jintao alipowahutubia wananchi wa Tanzania katika uwanja mpya na wa kisasa kabisa wa michezo, kila mara alishangiliwa na wananchi na viongozi wa Tanzania kwa kupigiwa makofi, nderemo na vigeregere vingi wakifurahia ugeni kutoka China ulioongozwa na mheshimiwa rais Hu Jintao.

    Lilikuwa ni tukio lenye msisimko mkubwa na thamani kubwa sana. Viongozi hao wa juu kabisa wa China na Tanzania walishuhudia utiwaji saini wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi zteu mbili China na Tanznia. Tunavishukuru sana vyombo vya habari, ikiwemo Radio China Kimataifa na shirika la utangazaji la Tanzania-T.B.C, kwa waandishi wa habari na watangazji wote kwa kutupasha matukio mengi na habari motomoto kuhusu miaka 45 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania wakati ule, wakati wa sasa na wakati ujao, ambapo ni uhusiano imara na uliokamili na madhubuti kabisa.

    Kwa moyo wa furaha, heshima na taadhima tunauombea ushirikiano huu wa kindugu na kirafiki uimarike zaidi na zaidi na kudumu milele na milele.

    Tunamshukuru sana Bw. Kilulu Kulwa kwa barua yake kuhusu maadhimisho ya miaka 60 tangu Jamhuri ya watu wa China ianzishwe na maadhimisho ya miaka 45 tangu Jamhuri ya watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zianzishe uhusiano wa kibalozi. Barua yake inatuvutia ambayo imeonesha hisia zake za urafiki kwa watu wa China na kutarajia uhusiano kati ya China na Tanzania uendelezwe siku hadi siku.

    Msikilizaji wetu Paul Mungai Mwangi wa S.L.P 69 Injinia-North Kinangop Kenya, yeye anasema kwanza pokeeni salamu zangu za dhati ya moyo wangu enyi watangazaji, wahariri, wasimamizi na wasikilizaji wa CRI. Ni matumaini yangu kwamba nyote mbuheri wa afya, nawaombea dua mwenyezi mungu awape subira na fadhila mnapoendelea kutekeleza shughuli zenu za kila siku.

    Kwa muda sijajisikia kwenye kipindi hiki mufti cha sanduku la barua, ila mwenyewe nimekuwa nikisikiliza kwa makini barua zikisomwa kutoka kwa wasikilizaji mbalimbali. Nachukua fursa hii kueleza furaha tele niliyonayo kwa ushindi nilioupata wa nafasi ya kwanza katika mashindano ya chemsha bongo kuhusu 'vivutio vya utalii mkoani Sichuan' yaliyoandaliwa na CRI mwaka 2008.

    Hofu yangu ni kwamba bado sijapata zawadi inayoambatana na nafasi hiyo ya kwanza, naomba wanaohusika na mashindano ya chemsha bongo katika CRI walishughulikie jambo hili. Aidha nawaomba watangazaji wanijulishe kupitia kipindi hiki cha sanduku la barua kama zawadi hiyo imeshatumwa.

    Mwisho naomba niwasalimie wafuatao-:

    Mutanda Ayub Shariff wa Bungoma Kenya, Martin.Y. Nyatundo wa Kisii Kenya, Stephen Magoye Kumalija wa Kahama Tanzania na Ali Khamis Kimani wa Ndori Kenya.

    Kwanza tunakupa pole sana msikilizaji wetu Paul Mungai Mwangi kwa kuchelewa kuipata zawadi yako, tunapenda kukueleza kwamba hivi sasa tunafuatilia ili tujue tatizo liko wapi na zawadi yako imekwama wapi tutakapopata ufumbuzi tutakujulisha.

    Msikilizaji wetu Stephen Mgoye Kumalija wa S.L.P 1067 Kahama Tanzania, anasema ni matumaini yangu makubwa kuwa hamjambo sana wafanyakazi wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa kutoka mjini Beijing China, mimi huku ni mzima wa afya njema na ninaendelea kuitegea sikio sanjari na kawasiliana mara kwa mara kwa njia ya barua.

    Ni dhahiri kwamba naomba kuchukua fursa hii ili kumpa pole saana rais wa Marekani Barack Hussen Obama pamoja na wananchi wake kwa kuondikewa na mpendwa wao na kwa dunia nzima ambaye alikuwa mwanasiasa mashuhuri na mkongwe Edward Tedy Kennedy ambaye alifariki tarehe 25/8/2009 kwa ugonjwa wa saratani ya ubongo huko Boston Marekani, mwanasiasa huyu mashuhuri alikuwa mtetezi wa haki za binaadamu, alikuwa akitetea watu wanyonge duniani hatutamsahau kwa mchango wake jinsi alivyokuwa akitetea haki za binaadamu duniani. Marehemu Kennedy ambaye alikuwa mdogo wa rais wa zamani wa Marekani hayati John Kennedy hatasahaulika kwa ni alikuwa ni mtu shupavu na mnyenyekevu, tulikuwa tunampenda lakini mungu amempenda zaidi, kweli kazi ya Mungu haina makosa, mungu aiweke roho yake mahali pema peponi amin.

    Na katika barua yake nyingine Bw Kumalija anasema naomba kuchukua fursa hii kuipongeza serikali ya Jamhuri ya watu wa China ambapo mwaka inatimiza miaka 60 tangu ianzishwe tarehe 1/10/1949 chini ya uongozi wa aliyekuwa rais na mwenyekiti wa chama cha kikomunisti cha China Mao tse Tung.

    Ni dhahiri kuwa katika miaka 60 iliyopita serikali ya Jamhuri ya watu wa China pamoja na wananchi wake wamefanya juhudi kubwa za kujenga nchi na kuinua sana nguvu na uwezo wa jumla wa nchi nzima ambapo maisha ya wananchi yameboreshwa siku hadi siku na mafanikio makubwa yamepatikana katika viwanda, kilimo, sayansi na teknolojia ambapo uchumi wa China umekuwa na kufikia asilimia 7.2 kwa mwaka huu. Hata hivyo viongozi pamoja na wananchi wote wa serikali ya Jamhuri ya watu wa China ninawatakia sherehe njema yenye mafanikio mema.Kwa kumalizia naomba munitumie magazeti mbalimbali ya China today.

    Tunakushukuru sana Stephen Magoye Kumalija kwa barua zako, tuna imani kuwa wananchi wa Marekani pamoja rais wao wameshapona maumivu ya kuondokewa na mpendwa wao Kennedy, hiyo ni kazi ya mungu na kama ulivyosema haina makosa, pia tunashukuru sana kwa pongezi ulizotoa za maadhimisho ya miaka 60 tangu Jamhuri ya watu wa China ianzishwe, China ikiwa nchi iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo inajivunia sana miaka hiyo 60 ya mafanikio.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako