• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 1110

    (GMT+08:00) 2009-11-10 17:01:12

    Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161 Bariadi Shinyanga Tanzania hivi karibuni ametuandikia barua kwa mfululizo, ambapo ameeleza maoni yake kuhusu mambo mbalimbali.

    Katika barua yake inayohusu Makala maalum ya Rafiki wa China kuhusu miaka 60 tangu Jamhuri ya watu wa China ianzishwe, Bw. Kulwa anasema, mwaka huu wa 2009 ni mwaka wa 60 tangu Jamhuri ya watu wa China ianzishwe. Hakika wananchi wa China wakiongozwa na Chama tawala cha Kikomunisti cha China na serikali yao wana furaha kubwa kwa nchi yao inapoadhimisha miaka 60 tangu ilipoanzishwa. Miaka 60 kwa umri wa binadamu ni mtu mzima, pengine wengine watasema ni mzee, lakini hebu tujiulize kama kweli kuna binadamu ambao huishi zaidi ya miaka 100. Je, miaka 60 kweli ni umri wa uzee? Au ni umri wa kati na ukomavu! Kwa mtazamo wangu mtu anaweza kuzeeka hata akiwa na miaka 20 kutegemea na mtindo wake wa maisha anayoishi na kusongwa na magonjwa mbalimbali sugu katika maisha yake na hivyo kuchakaa sana kumpita hata mzee wa miaka 70. Huo ndio ukweli wa mambo hata kama wengine watakataa.

    Kabla ya kuanzishwa kwa China mpya yaani Jamhuri ya watu wa China, China ya kale ilipitia katika vipindi vigumu sana, iliwahi kuvamiwa na kupigana vita vya kibeberu vya wavamizi, mikataba ya kikasumba na kitapeli ya waliovamia na kuwafanya wananchi waishi maisha ya unyonge ya wasiwasi na mashaka makubwa. Wavamizi wa nje walivuruga ustawi wa China ya kale na hivyo kuwafanya wananchi washindwe kutumia fursa za kujiendeleza na kujiletea maendeleo ya mafanikio yao na nchi yao. Kiongozi mwanzilishi wa China mpya-hayati mwenyekiti Mao Zedong, aliongoza mapinduzi na harakati zote za ukombozi dhidi ya uonevu na uvamizi, alishirikiana na wanaharakati wengine chini ya vuguvugu la chama imara cha kikomunisti cha China na jeshi jekundu la China ili kuikomboa nchi na wanachi wake na hatimaye kupata ushindi wa kushindo na kuanzishwa kwa Jamhuri ya watu wa China tarehe 1 Oktoba mwaka 1949.

    Tangu kuundwa kwa Jamhuri ya watu wa China, pamoja na vikwazo vya hapa na pale, China imeaminiwa na kutumainiwa na nchi na mataifa mengi humu duniani, ikiwa ni mjumbe wa kudumu wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, China ni nchi kubwa inayoendelea yenye idadi ya watu wanaofikia bilioni 1.3 hivi sasa, ina sauti kubwa na nguvu kubwa itayaoweza kwa namna ya pekee kabisa kutetea, kusimamia na kulinda maslahi na haki ya nchi na mataifa yanayoendelea. China imepitia pia katika changamoto nyingi na matatizo kadha wa kadha yakiwemo ya upungufu wa chakula, majanga ya kimaumbile kama vile ukame, mafuriko na hata matetemeko ya ardhi, lakini kutokana na uongozi imara, mshikamano na uzalendo mkubwa walio nao wananchi wa China, China imesimama imara na kushinda taabu na matatizo yaliyowahi kuikabili na inaendelea mbele kwa kasi bila kusita. Sera ya ufunguaji mlango kwa nchi za nje na sera ya diplomasia ya China ni mipango mkakati ulioleta matokeo bora na kuzaa matunda mengi kwa medani ya kimataifa kwa nchi hii tukufu ya China na wananchi wake.

    China inashikilia kanuni tano za kuishi pamoja kwa amani; inaheshimu na kuzingatia sana mamlaka ya nchi yoyote ile iwe kubwa ama ndogo. China imekuwa ikipinga njama au mipango yoyote ya ufarakanishaji taifa la China na kupinga kwa nguvu zote hadaa yoyote ya kuligawa taifa ikihimiza na kutetea msimamo wake wa China moja, ambapo sisi marafiki wa China tunaiunga mkono sana kwa kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

    Tunapoadhimisha tukio hili kubwa la miaka 60 tangu nchi nzuri ya China ilipoanzishwa ninaweza kuandika mambo mengi mazuri sana kiasi kwamba wasioifahamu vizuri China wanaweza kusema kwamba nimetia chumvi mno katika makala yangu hii. Ukweli ni kwamba hakuna cha kutia chumvi wala mafuta ya kupikia. Mafanikio ya China katika nyanja zote na sekta zote yako dhahiri kote duniani. Zaidi ya hayo bara la Afrika na nchi nyingi za Afrika zinatambua na kuthibitisha vyema mchango na msimamo wa China tangu taifa hili kubwa lililopo barani Asia lilipoanzishwa. Jamhuri ya watu wa China iliziunga mkono sana nchi za kiafrika zilipokuwa zinadai uhuru wao kutoka kwa wakoloni.

    Nchi ya China imeweza kuzisaidia nchi za Afrika kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ambapo baadhi ya miradi hiyo ilionekana ni kama maajabu au miujiza tu kuikamilisha. Lakini kwa hakika miradi iliyoanzishwa na China iliweza kukamilika kwa wakati na kwa sifa ya kiwango cha juu. China imeonesha mshikamano na nchi nyingine washirika zinazoendelea wakati wa raha na wakati wa taabu, katika neema na wakati mgumu pia. Kweli tunaiona China kama mdau mkubwa kabisa kwa maendeleo na ustawi wa nchi zetu. Na ninaitakia kheri na mafanikio makubwa sana katika sera zake na mipango yake yote ya ujenzi na ustawishaji wa nchi yao. Tunaishukuru sana Radio China Kiataifa kwa kututangazia vipindi na makala kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya watu wa China. Ninaipenda sana nchi hii nzuri ya China na watu wake. Idumu milele na milele.

    Tunamshukuru sana Bw. Kilulu Kulwa kwa barua yake kuhusu maadhimisho ya miaka 60 tangu Jamhuri ya watu wa China ianzishwe. Kweli barua yake imeeleza mengi kuhusu China, ambayo inaweza kuwasaidia wasikilizaji wale ambao wanataka kujua mengi kuhusu China. Bw. Kulwa kweli ni mfuatiliaji wetu mkubwa, mbali na kuchapa kazi katika ujenzi wa nchi yake, yeye anapenda sana kusikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa, na tangu zamani sana amekuwa msikilizaji wetu mtiifu, anasikiliza matangazo yetu kwa makini na pia ametuletea barua kutoa maoni na mapendekezo yake, kila mara barua yake inatutia moyo sana. Asante sana.

    Msikilizaji wetu Paul Weezy wa S.L.P 5, Kenya anasema nachukua fursa hii kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya huko China na hata sisi pia twaisikia, wafanyakazi mmefanya kazi kubwa hadi nimewaandikia shairi la kuwapongeza na hili ndilo shairi lenyewe

    Enyi watangazaji wapendwa, pongezi kwenu nyote

    Kwa kazi nzuri mnayoifanya, mwahubiri kila upande

    Wazi mnafanya mambo yakawa, hadi mwapatikana kote

    Asanteni kwa hayo tunawashukuru watangazaji wa CRI

    Kila asubuhi na mapema, mwaamka kutujulia hali

    Mara matangazo mkatupa, yenye ukweli dhahiri

    Mwatangaza kwa ustadi sana, hata nami nawasihi muendelee zaidi

    Asanteni kwa hayo tunawashukuru watangazaji wa CRI

    Asanteni nyote kwa hayo, twawapongeza watangazaji wapendwa

    Mutie bidii zaidi nayo, kwa kazimbi si mchezo mwema

    Muwe na ujasiri kano, kwasababu mwasikika kote duniani

    Asanteni kwa hayo tunawashukuru watangazaji wa CRI

    Mwatenda yenye sifa, kwa sifa iliyonzuri

    Sifa ya kukuza taifa, naya kuleta kheri

    Mwasema yatendekayo, kote hapa duniani

    Asanteni kwa hayo tunawashukuru watangazaji wa CRI

    Shairi hili linazungumzia jinsi mnavyofanya kazi na vile tunavyo yasikia mambo na pia inatusaidia kujua yanayotendeka duniani kote.

    Shukrani sana msikilizaji wetu Paul Weezy kwa barua yako ambayo imejaa pongezi nyingi tu kwa wafanyakazi wa idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa hasa watangazaji, sisi tunasema tumezipokea pongezi hizo kwa mikono miwili na tunakuahidi kama ulivyosema kwenye shairi lako kwamba tutaongeza bidii ili tuwaridhishe wasikilizaji wetu wa kila pembe.

    Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa S.L.P 1067 Kahama Shinyanga Tanzania naye anasema salamu zangu nyingi ziwafikie hapo Beijing China, mimi huku ni mzima wa afya njema na ninaendelea kuyategea sikio matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa

    Nachukua fursa hii ili kuwapa pongezi marais wawili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuzindua mkonga wa mawasiliano ya internet mjini Dar es salaam Tanzania hivi karibuni ambapo mawasiliano ya internet yamepitishwa chini ya bahari kutoka nchi za Umoja wa falame za kiarabu, kupitia nchini India, bahari ya Hindi, Msumbiji, Swaziland mpaka Afrika ya Kusini. Hata hivyo ninayapongeza sana mashirika mbalimbali yaliyosimamia mpango huo wa mkonga wa mawasiliano ya internet ambao utaweza kupunguza gharama ya matumizi ya internet kwa watumiaji wake, pia wasikilizaji wa CRI kama mimi tutaweza kuwasiliana kwa haraka zaidi na washirika wetu walioko sehemu mbalimbali duniani hususan nchini China. Pongezi zangu za mwisho naomba kuzituma kwa rais wa Jamhuri ya kiislam ya Iran Bw. Mahmoud A hmednejad kwa kuchaguliwa tena kwa mara ya pili na wananchi wa Iran, na nikimtakia heri pamoja na ungozi bora ili kutekeleza majukumu aliyopewa na Mungu katika kuliongoza taifa hilo la Jamhuri ya kiislamu ya Iran.

    Na barua yake nyingine Stephen Mgoye anasema kwa kweli ni dhahiri kuwa serikali ya Jamhuri ya watu wa China pamoja na wananchi wake ambao idadi yao ya jumla ni bilioni 1.3, kutoka jumla ya makabila yote ya China yapatayo 56, ambapo jamii nzima ya China katika miaka 60 iliyopita imefanya juhudi kubwa sana ambayo imejenga nchi na kuinua nguvu na uwezo wa jumla wa nchi nzima na maisha ya wananchi wote yanaendelea kuboreshwa siku hadi siku, ni dhahiri kuwa mafanikio makubwa pamoja na ujuzi unaendelea kupatikana siku baada ya siku katika viwanda, kilimo, sayansi pamoja na teknolojia, ambapo China katika miongo sita iliyopita ikiwa inalisha watu wake ambao idadi yao inachukua 22% ya watu wote duniani kwa mashamba yake yanayochukua 7% ya eneo la mashamba duniani. Pia ni dhahiri kuwa uzalishaji wa nafaka katika mwaka 2008 ulikuwa ni tani milioni 500. Na kwa mwaka huu uchumi wake unachukua 7 % hivi kutokana na msukomsuko ulioikumba dunia aidha thamani ya jumla ya uchumi wa China inachukua nafasi ya pili baada ya Marekani na Japani, hata hivyo kwa mwaka ujao China itakuwa mwenyeji wa maonesho ya kimataifa ya mwaka 2010 yatakayofanyika Shanghai. China ikiwa ni nchi iliyorudishiwa kiti chake halali kwenye umoja wa mataifa mwaka 1971 hadi hivi sasa ina uhusiano wa kibalozi na nchi zipatazo 171 duniani Russia ikiwa ni nchi ya kwanza kuwa na uhusiano wa kibalozi na China. Anamalizia kwa kusema hayo ni maoni yangu kuhusu chemsha bongo ya ujuzi wa miaka 60 tangu Jamhuri ya watu wa China iasisiwe.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Stephen Mgoye kwa pongezi ulizozitoa kwa rais wa Tanzania na kiongozi wa Iran pamoja na maoni yako ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa miaka 60 tangu Jamhuri ya watu wa China iasisiwe. Nasi tunakupongeza sana kwa maoni yako hayo mazuri kabisa kuhusu China. Ila tu tunakuomba usisite kutuandikia maoni mbalimbali uliyonayo kuhusu China na hata dunia.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako