• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maisha ya msanifu wa majengo kutoka Brunei mjini Beijing

    (GMT+08:00) 2009-11-12 14:48:17

    Bw. Fu Mingwen anatoka Brunei, yeye ni msanifu wa majengo ambaye hivi sasa anaishi na kuendesha kampuni ya "Arkiteknique" ya utoaji ushauri kuhusu usanifu wa majengo mjini Beijing. Kwa kuwa utamaduni wenye historia ndefu wa Beijing na majengo mbalimbali ya kale vinamvutia sana, hivyo alikuja na kuamua kuishi nchini China.

    "Nilikuja China kwa bahati tu, sikutarajia naweza kupata maendeleo kama ya sasa. Nafurahi kuja hapa, kusema kweli, sikuchuma pesa nyingi, lakini pesa hizo zinatosha kutalii kwangu, nimetembelea sehemu mbalimbali nchini China, na kujionea pande mbalimbali za nchi hii."

    Bw. Fu Mingwen alipata stashahada katika Chuo cha majengo cha London mwaka 1986, ambacho ni chuo maarufu duniani, na mwaka 1990 alikuwa msanifu wa majengo wa Taasisi ya usanifu wa majengo ya Uingereza. Kabla ya kuanzisha kampuni yake ya kwanza ya Arkiteknique nchini Brunei mwaka 1991, Bw. Fu Mingwen alikuwa amefanya kazi katika nchi nyingi za Ulaya na Asia, hivyo alipata uzoefu mkubwa na ujuzi mwingi wa kitaaluma.

    Mwaka 1993 alipokuja mjini Beijing kwa mara ya kwanza, hakutarajia kuwa ataendesha shughuli zake hapa Beijing, na wala hakutarajia kama atakuwa na ofisi kwenye nyumba nzuri ya kale katika kichochoro cha mjini Beijing. Mwaka ule, Bw. Fu Mingwen alikuja mjini Beijing kutalii kwa ndege kutoka Brunei, ambapo kwenye ndege hiyo kulikuwa na abiria wawili tu yeye na rafiki yake.

    Mji wa Beijing wa wakati ule haukuwa na majengo mengi marefu, wala hakukuwa na magari mengi. Lakini sehemu zinazoonesha utamaduni maalum wa jadi za mji huo kama vile Tian'anmen, kasri la kale la wafalme, Ziwa Houhai na Ukuta Mkuu zilimvutia sana. Kwa hiyo mwaka 2001 rafiki yake alipomwalika Bw. Fu Mingwen kuja China kushiriki kwenye mradi, alikubali kwa furaha na akaishi mjini Beijing kwa miaka 8. Alisema,

    "Kukaa tu hakuna maana, kwa hiyo niliamua kufanya mambo kadhaa. Ingawa mambo hayo sio makubwa, lakini ni yale ninayopenda kufanya siku zote. Niligundua nyua hizi na utamaduni huu, kwa sababu sikujua vitu hivyo zamani, kwa hiyo nazipenda na kutaka kujifunza. Kwa hiyo nikaamua kuanzia hapa."

    Mradi wa kwanza alioshughulikia baada ya kuja China ni Bustani ya Huabin iliyoko kwenye sehemu ya Changping mjini Beijing. Ili kufanya vizuri kazi ya ujenzi wa mradi huo wenye uwanja wa mpira wa golf, hoteli na uwanja wa mchezo wa polo, Bw. Fu Mingwen alileta kundi la wataalam wengi kutoka Brunei ambao waliwahi kufanya pamoja ujenzi wa miradi ya ukoo wa mfalme wa Uingereza. Baada ya ujenzi wa miezi 10, klabu ya golf ikakamilika.

    Kadiri shughuli zake zinavyoendelezwa, mwaka 2003 Bw. Fu Mingwen alianzisha kampuni ya Arkiteknique ya utoaji ushauri kuhusu usanifu wa majengo, ambayo inashughulikia huduma za kutoa ushauri kuhusu usanifu wa majengo. Kuanzia hapo Bw. Fu Mingwen alianza shughuli zake nchini China.

    Mradi unaomfanya Bw. Fu Mingwen afurahi na kuona fahari ni mradi wa nyumba za Siheyuan. Mwaka 2003 ugonjwa wa SARS ulipotokea, wenzake kutoka Brunei wote walirudi nchini Brunei, lakini yeye peke yake alibaki mjini Beijing akitembelea vichochoro mbalimbali. Muda huu hatausahau, nyumba za Siheyuan ambazo ni nyumba za jadi za mjini Beijing, zinasahauliwa na watu wa zama hizi zinamvutia sana Bw. Fu Mingwen.

    Mwanzoni mwa mwaka 2004, aligundua kuwa hekalu moja lenye historia ya miaka 600 katika kichochoro cha Zhangwang lilikuwa linatumiwa kuwa nyumba ya kiwanda, na sura yake ya asili haikuonekana. Alisikitika sana, hivyo alitumia muda mwingi kuwasiliana na wenye kiwanda hicho na serikali ya mtaa, na hatimaye alikodi hekalu hilo. Alitumia muda wa miaka miwili kulikarabati hekalu hilo kwenye msingi wa kuhifadhi muundo wa zamani wa ujenzi wa hekalu hilo, baadaye aliweka samani za kawaida kama meza na viti, na nyumba hiyo ikawa nyumba ya ofisi yake ya sasa.

    Alipozungumzia kukarabati nyumba za Siheyuan, Bw. Fu Mingwen ana kanuni yake, alisema,

    "Haina haja ya kubadili sura yake ya asili na mtindo wake, sehemu zilizoharibika zinapaswa kukarabatiwa, na kuhifadhi sura yake ya zamani kadiri tuwezavyo, naona ni vizuri kuhifadhi historia ya nyumba hiyo."

    Kutokana na kuheshimu sura ya asili ya majengo, Bw. Fu Mingwen anafikiria kwa makini kuhusu kuhifadhi au kutohifadhi kila tofali na kigae. Ukarabati wa Bw. Fu Mingwen kwa nyumba za jadi za mjini Beijing, unahifadhi sura za asili za nyumba. Ingawa nyumba hizo kwa nje bado ni ya kale, lakini baada ya kuingia ndani, zinaonekana mpya kabisa. Mtindo huo maalum na rahisi unawavutia watu wengi wanaopenda usanifu wa majengo.

    Kutokana na kukarabati na kuhifadhi nyumba nyingi za Siheyuan, Bw. Fu Mingwen anafuatiliwa na watu wengi. Bw. Fu Mingwen alisema, utamaduni wa vichochoro mjini Beijing unamvutia sana, kwa hiyo alitumia mapato yote ya kampuni katika kazi hiyo anayopenda. Ana matumaini kuwa kila mradi anaofanya utaongoza ujuzi wake. Kabla ya kuja mjini Beijing, Bw. Fu Mingwen alikuwa na ujuzi kidogo kuhusu ujenzi na utamaduni wa China. Sasa ni miaka minane imepita, kutokana na kujifunza kwa bidii, amepata maendeleo makubwa.

    Katika miaka hiyo 8 mjini Beijing, Bw. Fu Mingwen amebahatika kujionea mabadiliko ya kasi ya Beijing kutokana na maandalizi ya Michezo ya Olimpiki. Alisema,

    "Wachina wamekuwa na mtazamo wa wazi siku hadi siku, wanapokea utamaduni wa nchi nyingine duniani, China ina mabadiliko makubwa, na inaendelezwa kwa kasi."

    Bw. Fu Mingwen anaona kuwa, kuna fursa nyingi za kujiendeleza mjini Beijing. Anataka kuwavutia watu wengi zaidi wa Brunei waje hapa kuwekeza, na kuwafanya watu wengi zaidi wa Brunei waifahamu China.

    Bw. Fu Mingwen ana matumaini kuwa ataweza kushiriki kwenye mradi wa kukarabati na kuhifadhi majengo ya kale ya China. Alisema kuendeleza kadiri ipasavyo majengo hayo sio tu kunaweza kuwafanya watu wengi zaidi wafahamu historia na jadi, na kuwafanya watu wayahifadhi majengo hayo, bali pia kunaweza kukusanya fedha kwa ajili ya kuyahifadhi vizuri zaidi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako