• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Michezo bora kabisa ya sanaa katika Tamasha la Kimataifa la michezo ya sanaa la Shanghai, China

    (GMT+08:00) 2009-11-16 15:44:01

    Tamasha la Kimataifa la 11 la michezo ya sanaa lilifanyika mwezi Oktoba mjini Shanghai, China. Tamasha hilo lilifunguliwa kwa mchezo wa ballet wa hadithi ya kale ya China iitwayo "Wang Zhaojun". Wasanii kutoka nchi 23 walikusanyika katika tamasha hilo na michezo mingi kama vile mchezo wa ballet wa "Wang Zhaojun" uliooneshwa na Kundi la Ballet la Mkoa wa Hubei na mchezo wa ballet wa "Dansi ya Wanawake Machoni mwa Wanaume" uliooneshwa na Kundi la Ballet la Monte-Carlo la Monaco, yote ni michezo iliyovutia watazamaji katika tamasha hilo.

      Kama ilivyokuwa kwenye tamasha la kimataifa la michezo ya sanaa la Shanghai la awamu zilizopita, tamasha hilo la mwaka huu pia lilisisitiza michezo iwe mipya na yenye mitindo ya kitaifa. Mchezo wa Ballet wa "Wang Zhaojun" ni wa mtindo wa Kichina kabisa, ambao unaeleza hadithi kuhusu Bi. Wang Zhaojun aliyekuwa mmoja kati ya warembo wanne mashuhuri katika historia ya China ya zama za kale, Bi. Wang Zhaojun aliozwa na mfalme wake kwa mfalme wa dola ya jirani ili kuweka urafiki na dola hiyo. Hii ni hadithi ya kweli katika historia ya China na anasifiwa kutokana na uzalendo wake. Ili kuonesha vilivyo hisia nyingi alizo nazo mrembo huyo, mchezo huo wa ballet unatumia dansi ya Kichina ya kale na ya sasa. Mwongoza wa mchezo huo Bw. Mei Changsheng alisema,

      "kwanza kabisa mtindo wa mchezo huo wa Ballet ni wa kitaifa, huu ni msingi wa mchezo huo wa dansi. Lakini kwa sababu hadithi yenyewe ilianza zamani sana inatupasa tuingize dansi ya ballet na ya kisasa ili vijana waelewe na kuona ni ya kisasa na pia ya jadi ya Kichina."

      Katika kipindi cha tamasha hilo, michezo mingi ya sanaa ya China ilikuwa mipya na ilivutia kutokana na utamaduni mkubwa wa China. Michezo ya wasanii wa mji wa Chongqing imeonesha kiwango cha juu kilichopatikana katika miaka ya hivi karibuni mjini humo, moja kati ya michezo yao ni simfoni yenye kwaya kubwa iitwayo "Mto Changjiang", kwa kutumia muziki wa simfoni na nyimbo za kwaya za aina ya kichina na kimagharibi, imeelezea vilivyo uzuri wa mto Changjiang.

      Tamasha la Kimataifa la michezo ya sanaa la Shanghai lilianza kufanyika mwaka 1999, mpaka sasa limefanyika mara 10. Kauli mbiu ya tamasha la mwaka huu ni "Tumulike Moyo kwa michezo ya sanaa". Katika muda wa mwezi mmoja wa tamasha hilo, michezo 55 ya sanaa iliyochaguliwa kwa makini ilioneshwa, kati ya michezo hiyo 28 ni ya nchi za nje na 27 ni ya China. Kuonesha michezo hiyo ya sanaa iliyo bora na kujaribu kuwa na uvumbuzi mpya ni lengo lililofuatiliwa zaidi kwenye tamasha hilo. Mwenyekiti wa tamasha hilo Bw. Chen Shenglai alisema,

    "Tamasha hilo ni la kiwango cha juu kwa sababu michezo yote ya sanaa inaoneshwa na makundi makubwa ya wasanii, licha ya michezo ya sanaa ya kisasa na ya aina mpya inayovumbuliwa, pia kuna michezo ya sanaa iliyotungwa kwa ushirikiano kati ya China na nchi nyingine. Na ili kuifanya michezo ya sanaa ya China iwe na mtindo wa kimataifa pia, tumeingiza utamaduni wa nchi za nje na kuuunganisha na utamaduni wetu wa China, kama uchumi wa China unavyoingiliana na uchumi wa dunia."

    Katika tamasha hilo mchezo wa ballet wa "Msichana Cinderella", kwa mara ya kwanza ulioneshwa na Kundi la Ballet la Monte Carlo la Monaco nchini China, na mchezo mwingine wa kundi hilo "Dansi ya Wanawake Machoni mwa Wanaume" pia ulioneshwa kwa mara ya kwanza kabisa. Mkuu wa kundi hilo alisema,

    "Tumeandaa michezo miwili ya ballet kwa ajili ya tamasha hili, wa kwanza ni 'Msichana Cinderella' na mwingine ni 'Dansi ya Wanawake Machoni mwa Wanaume', nina uhakika kwamba michezo hiyo miwili itagusa sana hisia za watazamaji."

    Aidha, mchezo uliochezwa kwa dansi ya aina ya Tango ya Argentina uitwao "Malaika Amekuja mjini Buenos Aires", tamthilia ya "Kijiji cha Mbwa" ya Ujerumani na tamthilia ya "Mpira wa Theluji" ya Ubelgiji, yote ni michezo ya sanaa iliyooneshwa kwa mara ya kwanza barani Asia katika tamasha hilo la michezo ya sanaa.

      Kwaya ya Wavulana na Wasichana ya Harlem kutoka Marekani kwa mara ya kwanza imeonesha nyimbo zake katika tamasha hilo. Kwaya hiyo licha ya kuimba wimbo wa taifa wa China na kushangiliwa sana pia iliimba wimbo maarufu sana nchini China uitwao "Mama ni Mtu Mwema Kabisa Duniani". Mkuu wa kwaya hiyo alisema,

    "Tamasha hili ni zuri sana! Tunafurahi kufanya maonesho yetu hapa, tumekutana na wasanii wengi wa Ujerumani, China, Poland, Italia na nchi nyingine na tumejionea utamaduni wa taifa la China. Tumefurahi kuona Wachina wengi wanapenda muziki. Hii ni mara yetu ya kwanza kuja hapa, tutakuja tena katika kipindi cha Maonesho ya Kimataifa ya Shanghai mwaka 2010."

      Tamasha la Kimataifa la michezo ya sanaa la Shanghai limewaletea fursa nzuri wasanii kuweza kubadilishana maoni, na maonesho ya biashara ya michezo ya sanaa yanayofanyika kila mwaka yamewavutia sana wafanyabiashara wengi. Mwaka huu wasanii walioshiriki kwenye maonesho hayo wanatoka katika nchi 30. Meneja wa kampuni ya biashara ya michezo ya sanaa kutoka Canada alisema,

      "Kwenye maonesho ya biashara tumeonesha michezo ya aina tano ikiwemo dansi, tamthilia, sarakasi na jazz. Kutokana na tamasha hilo tumeweza kugundua wasanii wengi wapya na tumeona michezo mingi inayovutia sana, na pia tumeona majumba mengi ya hali ya juu ya michezo ya sanaa."

    Katika muda wa Tamasha la Kimataifa la michezo ya sanaa la Shanghai pia kulikuwa na shughuli nyingi za utamaduni, kwa mfano, mashindano ya muziki wa piano, wiki ya utamaduni wa Korea ya Kusini, maonesho ya hazina ya Misri n.k. Tamasha hili lilikuwa sikukuu kubwa ya wasanii na wapenzi wa michezo ya sanaa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako