• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mwandishi wa habari wa China anayetoa mchango mkubwa kwenye kuongeza urafiki kati ya China na Afrika

    (GMT+08:00) 2009-11-16 17:08:57

    Hivi karibuni sherehe ya utoaji wa tuzo kwa watu waliotoa mchango mkubwa kwenye kuimarisha urafiki kati ya China na Afrika ilifanyika hapa Beijing. Na Bw. Ding Bangying, ambaye ni mkurugenzi wa ofisi kuu ya Redio China Kimataifa barani Afrika, amekuwa mmojawapo wa watu waliopewa tuzo hiyo.

    Bw. Ding ni mwandishi wa habari wa China aliyewahi kuwahoji marais na maofisa waandamizi wengi zaidi wa nchi za Afrika. Akitumia lugha za Kiingereza na Kiswahili kuwahoji marais wanane wa nchi za Afrika, pia ni rafiki wa baadhi ya viongozi wa Afrika. Amesema:

    "Kufany mahojiano na marais pamoja na viongozi wa hali ya juu ni kazi ngumu na yenye maana pia. Ufunguo wa kufanikisha mahojiano kama hayo ni kuwasiliana na kuelewana vizuri na wafuasi wa marais. Kwa kutumia ufunguo ipasavyo nikafanikiwa kufanya mahojiano na marais wanne kutoka Zimbabwe,Zambia.Sudan na Uganda katika siku tatu tu wakati mkutano wa biashara wa Afrika mashariki na ya kusini ulipofanywa mjini Kampala. Jambo la kunifurahisha zaidi ni kwamba kwa kupitia mahojiano hayo nikarafikiana na baadhi ya viongozi hao, kama Rais Nyerere wa Tanzania, Katibu Mkuu wa OAU (UA kwa sasa)Bw. Salimu na kadhalika. Yote hayo yakanipa kumbukumbu ya furaha mpaka leo hii."

    Mwezi Desemba mwaka 1988, bila kutarajia, Bw. Ding alipokea barua ya mwaliko kutoka ikulu ya Kenya, akialikwa kuhudhuria sherehe ya maadhimisho ya miaka 25 ya uhuru wa Jamhuri ya Kenya akiwa mgeni maalum, na hali hii ilimfanya awe mwandishi wa habari wa kwanza wa China kupata mwaliko kama huo. Bw. Ding amesema:

    "Balozi wa Kenya katika China aliponipatia barua ya mwaliko kutoka ikulu ya Kenya nikashangaa sana maana sikutegemea kabisa kupata heshima kama hiyo. Naona mwaliko huo nadhani ulitokana na sababu tatu: kwanza ni mafanikio ya mahojiano niliyofanya na Rais Moi mjini Beijing; pili ni lugha ya kiswahili ambayo ilisaidia kuelewana na kurafikiana; na tatu ni kama shukrani kwa kutukuza matembezi ya Rais Moi katika China, Maana nilifanya ripoti 8 zinazohusiana na matembezi ya Mai wakati alipotembelea China kwa siku chache tu, na ripoti hizo zote nikampatia Rais Moi kwa kuptia balozi wa Kenya nchni China. Wakat nilipofika Kenya ,Rais Moi alinipokea tena kwa urafiki, na nikasisimka sana mpaka sasa."

    Mwaka 1983 wakenya walishangaa sana kusikia habari kuhusu mchina akipata nafasi ya kwanza katika mashindano ya lugha ya Kiswahili, na mchina huyu ni Bw. Ding. Ushindi huo ulizungumziwa sana na wachina walioishi nchini Kenya hata mpaka sasa. Bw. Ding amesema:

    "Kusema kweli, kujiunga na mashindano hayo kwangu mimi sio kwa ajili ya ushindi wowote bali ni kama starehe tu .Hivyo hata mimi mwenyewe nikashangaa wakati matokeo ya mashindano yalipotanggazwa hadharani. Nikiwa mgeni nilipata ushindi wa kwanza katika mashindano ya Kiswahili,waandishi wa habari wa Kenya walifululiza kufanya mahojiano nami na habari hiyo ilijulikana kote nchini Kenya. Balozi wa China katika Kenya alinipa hongera akasema kwamba matokea hayo yalitukuza jina la China.Mpaka leo hii bado naona kuwa matokeo hayo ni kwa bahati tu wala sio kweli Kiswahili changu ni kizuri sana .Hata hivyo hapa ningependa kuwashukuru walimu wangu wa China na Tanzania."

    Bw. Ding amewafahamisha waafrika mambo kuhusu China, huku akiwafahamisha wachina mambo kuhusu Afrika, makala zake nyingi zinazohusu Afrika zilichapishwa kwenye magazeti na majarida mbalimbali nchini China, na baadhi ya makala hizo zinachukuliwa kuwa ni za kwanza za aina yake katika utafiti husika, hasa ripoti alizoandika wakati alipokwenda kukusanya habari nchini Somalia mwaka 1992. Bw. Ding amesema:

    "Mnamo mwaka 1992 hali ya kivita nchini Somali ilivutia vyombo vya habari vya kote ulimwenguni hasa vile vya nchi za magharibi. Radio China kimataifa ikiwa chombo muhimu cha habari katika China na hata dunia, waandishi wake wa habari ni lazima kujiingiza wenyewe nchini Somalia na kuripoti hali ilivyo nchini humo kwa wasililizaji wetu wa China na walimwengu wala sio tu kukopisha ripoti kutoka Magharibi.Kutokana na mawazo hayo ,ndiyo nikaamua kwenda Somalia kufanya matembezi bila ya kuzingatia hatari. Nilipokuwa huko nikahudhuria mkutano wa habari wa jeshi la Marekani, kutembelea mji mkuu Mogadisho na Kisimayo pia, mwishowe nikatuma ripoti nyingi kuhusu hali ilivyo ya kivta nchini Somalia na ripoti hizo zilikaribishwa sana na wasikilizaji wetu pamoja na wasomaji wa China. Bila shaka hatari ilikuwepo, lakini naona matembezi hayo yalistahili kweli kweli."

    Mwaka 2006 Bw. Ding alipelekwa tena na CRI kufanya kazi nchini Kenya. Bw. Jacob Mugoa ni mmoja wa waandishi wa habari anayefanya kazi pamoja na Bw. Ding Bangying huko Nairobi, mtangazaji huyo anayejulikana nchini Kenya alipokutana na Bw. Ding kwa mara ya kwanza, walionekana kama ni marafiki makubwa ambao hawakuonana kwa muda mrefu. Bw. Mugoa amesema:

    "Bw. Ding amekuwa mkubwa wangu kazini. Naweza kusema ana utu wa kipekee. Kwa sababu tumekuwa tukichapa kazi sana mpaka tumesahau kula chakula cha mchana. Ukifanya kazi vizuri, Bw. Ding mara kwa mara huonesha furaha yake na kukupatia hongera na kukuambia kutia bidii zaidi."

    Shirika la Utangazaji la Kenya lina ushirkiano na CRI kwa muda mrefu. Mkurugenzi wa shirika hilo Bw. David Waweru alipopata habari kwamba rafiki yake Bw. Ding amepewa tuzo kutokana na mchango alioutoa kuimarisha urafiki kati ya China na Afrika, alifurahi sana. Bw. Waweru amesema:

    "Bw. Ding ni ndugu yangu. Yeye ni mtu anayechapa kazi na mwenye ufanisi wa kazi, kutokana na juhudi zake, KBC na CRI zimepata kuendesha miradi mbalimbali ya kunufaishana. Bw. Ding ana marafiki wengi nchini Kenya. Nampongeza sana Bw. Ding kwa kupata tuzo ya 'mchango kwa urafiki kati ya China na Afrika', naona kutunukiwa kwake ni jambo linalostahili. Naamini kwamba kutokana na juhudi za Bw. Ding, urafiki na ushirikiano kati ya KBC na CRI utaendelezwa zaidi."

    Bw. Ding mwenye umri wa zaidi ya miaka 60, ametoa matumaini yake kwamba vijana wengi zaidi wanaweza kutoa mchango katika ushirikiano kati ya China na Kenya, na hata kati ya China na Afrika. Amesema:

    "Tumepata mafanikio ya kikazi, na hiyo ni kweli. Mafanikio hayo yote yanategemea uongozi wa Radio China Kimataifa,pia yanategemea usaidizi na ushirikiano kutoka serikali ya kenya pamoja na marafiki wa hali mbali mbali nchini Kenya. Kazi zetu zinazidi, na bidii za kikazi pia zinatakiwa kuzidishwa. Hivyo tutaendelea kufanya kazi kwa juhudi zaidi ili kusaidia maelewano na ushirikiano kati ya serikali ya China na Kenya pamoja na wananchi wao."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako