• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mchoraji anayechangia maingiliano ya utamaduni kati ya China na nchi za nje Bw. Wang Peidong

    (GMT+08:00) 2009-11-23 17:11:57

      

    Bw. Wang Peidong wa wilaya ya Wuyang ya mkoa wa Henan ni mchoraji mahiri wa picha za maua na ndege kwa mtindo wa jadi wa Kichina, picha zilizochorwa naye mara nyingi zilipata tuzo kubwa nchini China na nchi za nje. Mwaka 2007 alichaguliwa kuwa ni mmoja kati ya wachoraji 30 wa picha zinazonunuliwa sana nchini China katiza zama za hivi leo. Bwana huyo pia ni mwanaharakati wa maingiliano ya utamaduni kati ya China na nchi za nje.

      Bw. Wang Peidong alizaliwa mwezi Machi mwaka 1941, baba yake Bw. Wang Zhujiu alikuwa ni mwanafunzi wa mchoraji mashuhuri wa picha za maua na ndege Bw. Qi Baishi. Bw. Wang Peidong alikuja Beijing na baba yake wakati alipokuwa mtoto, na alikuwa jirani wa mchoraji mkubwa Qi Baishi. Bw. Wang Peidong na mtoto wa Qi Baishi walikuwa marafiki. Kutokana na kuishi kwenye mazingira ya uchoraji Bw. Wang Peidong bila kukusudia alianza kuchorachora picha kwa brashi ya wino.

    Mwaka 1961 baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu, alisomea shahada ya uzamili katika Chuo cha Uchoraji cha Beijing akifundishwa na Bw. Wang Xuetao aliyekuwa mwanafunzi wa mchoraji mkubwa Qi Baishi, mwalimu huyo anazingatia sana jinsi mwanafunzi wake anavyotumia brashi na kuchora vitu halisi na kufundisha namna ya kuiga picha zilizochorwa na wasanii mashuhuri wa kale. Bw. Wang Peidong alisema,

    "Mwalimu wangu Bw. Wang Xuetao aliazima picha kubwa ya asili ya bata maji iliyochorwa na Lu Ji wa Enzi ya Ming ili niigize, nilichora mpaka usiku wa manane na siku ya pili mwalimu alipobisha hodi chumbani kwangu nilikuwa bado nimelala. Baada ya kuiangalia picha niliyochora mwalimu alitabasamu na kusema, si vibaya."

    Bw. Wang Peidong anapendelea zaidi kuiga uchoraji wa picha za maua na ndege wa Wu Changshuo, Qi Baishi, na Wang Xuetao, na kila alipokuwa anachora picha, baba yake pia alikuwa pembeni akimwelekeza. Hivyo Bw. Wang Peidong ameweka msingi imara wa kuchora picha za maua na ndege kwa brashi ya wino na kupata njia yake maalumu. Alisema,

    "Picha zilizochorwa na mchorani huonesha jinsi mchoraji alivyo, baada ya kufikia kiwango fulani picha alizochora hakika zitaonesha hisia zake ambazo zitakuwa tofauti na picha zilizochorwa na watu wengine."

    Bw. Wang Peidong aliwahi kutembelea sehemu mbalimbali zenye milima na mito mikubwa ikiwa ni pamoja na uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet, ili ajipatie msukumo wa kuchora. Alisema,

    "Mkoani Tibet kuna milima iliyofunikwa na theluji, uwanda mkubwa usio na upeo wa macho, hewa safi, mbingu ya kibuluu na mawingu meupe, ambapo ni mazingira yanayosafisha roho, ingawa siku ya kwanza baada ya kufika Tibet nilipata shida ya kupumua kutokana na kutokuwepo oksijeni ya kutosha, lakini siku ya pili nilipotembelea sehemu mbalimbali nilivumilia. Matatizo yalikuwa mengi lakini nikiwa na wakati nitakwenda tena huko."

    Mchoraji akiwa na nia thabiti kama hiyo hakika anapata uwezo mkubwa wa kuchora picha kama anavyotaka. Bw. Wang alisema,

    "Nakumbuka nilipokuwa na umri wa miaka 40 nilichora picha moja ya mayungiyungi yenye urefu wa mita kadhaa nikitaka kuonesha mandhari nzuri ya ziwa. Nilizifunga brashi kadhaa za wino kwa pamoja na kuchora majani ya mayungiyungi, picha ya kwanza sikuridhika nayo, baada ya kunywa pombe nikachora picha ya pili nikakamilisha picha hiyo kwa pumzi moja, majani yalikuwa makubwa, na kila ua lilikuwa kubwa sawa na beseni, picha hiyo ilipooneshwa katika Jumba la Sanaa ya uchorani la Beijing ilivutia watazamaji wengi."

    Bw. Wang Peidong aliipatia picha hiyo jina la "Hewa Safi Idumu". Katika maonesho ya picha za Chuo cha Uchoraji cha Beijing na Chuo cha Uchoraji cha Japan ya mwaka 1982, picha hiyo ya mayungiyungi ilisifiwa sana na wachoraji na watazamaji wa China na Japan. Tokea hapo picha anazochora mara nyingi zinapata tuzo kubwa nchini China na nchi za nje na zimekusanywa kwenye kitabu cha picha. Mwaka 2007 alichaguliwa kuwa mmoja kati ya wachoraji 30 wa picha za maua na ndege zinazonunuliwa kwa wingi kaktika zama za hivi leo.

    Bw. Wang Peidong akiwa msanii mkubwa katika Shirikisho la Urafiki wa Watu wa China na Nchi za Nje aliwahi kutembelea Japan, Korea ya Kusini, Marekani na Ufaransa na kufanya maingiliano ya utamaduni. Mwezi Aprili mwaka 2009 akiwa na watu wengine alikwenda Nepal kuchora picha za mazingira ya asili. Alisema,

    "Baada ya kurudi nyumbani kutoka Nepal tulichora picha kadhaa, tulipokuwa huko tulifanya maonesho ya picha katika ubalozi wa China nchini humo, balozi alifurahi sana na kutualika tufanye maonesho huko Nepal."

    Kuhusu maingiliano na nchi za nje Bw. Wang Peidong alikumbuka mawasiliano kati yake na wake wa mabalozi wa nchi mbalimbali nchini China katika kipindi cha Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008, alisema,

    "Mwaka jana wake kadhaa wa mabalozi wa nchi mbalimbali walizuru chuo chetu cha uchoraji, ambapo walitaka kujaribu kuchora picha, niliwafundisha kidogo, nilisema mzee Qi Baishi alikuwa hodari wa kuchora kamba, nikachora kuwaonesha, kisha mmoja kati yao alijaribu nikamsaidia, basi kwa ushirikiano tulikamilisha picha ya kamba mmoja, alifurahi sana na baadaye aliichukua picha hiyo na kuihifadhi."

    Kila mwaka Bw. Wang Peidong anafundisha wanafunzi 20 hivi wanaosomea shahada ya uzamili, kati yao kuna wanafunzi kutoka nchi za nje. Kwenye chumba cha kuchora picha mwanafunzi mmoja wa Korea ya Kusini alichora picha ya maua na ndege, mwanafunzi huyo amekuwa mchoraji mashuhuri katika nchi yake. Bw. Wang Peidong alisema,

    "Amekuja China kujifunza kuchora maua na ndege, kutokana na kipaji chake amepata maendeleo ya haraka."

    Bw. Wang Peidong anafurahi kwa kuwa wanafunzi wake wametapakaa katika sehemu mbalimbali duniani.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako