• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Biashara ya huduma ni nguvu mpya ya kuongoza kufufuka kwa uchumi wa dunia

    (GMT+08:00) 2009-11-25 17:04:14

    Mkutano wa kimataifa wa kujadili biashara ya huduma umefungwa tarehe 25 hapa Beijing. Maofisa na wataalamu waliohudhuria mkutano huo wamekubaliana kuwa, biashara ya huduma ni nguvu mpya ya kuongoza kufufuka kwa uchumi wa dunia. Waziri wa biashara wa China Bw. Chen Deming alitoa makadirio kuwa, katika miaka mitano ijayo, China itaagiza kutoka nchi za nje huduma zenye thamani ya dola za kimarekani trilioni moja, hali ambayo italeta fursa kubwa kwa maendeleo ya sekta za huduma za nchi mbalimbali duniani. 

    Mkutano huo uliwashirikisha viongozi husika wa shirika la biashara duniani, benki ya dunia, baraza la biashara na maendeleo la Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa ya ushirikiano wa kiuchumi. Viongozi hao walieleza kuwa, kutokana na sifa yake maalumu, biashara ya huduma iliathiriwa kwa kiasi kidogo zaidi kuliko biashara ya bidhaa katika msukosuko wa fedha duniani, hivi sasa sekta ya huduma na biashara ya huduma ni nguvu mpya katika juhudi za kukabiliana na msukosuko huo na kuleta ongezeko la uchumi duniani.

    Naibu mkurugenzi mkuu wa shirika la biashara duniani Bw. Alejandro Jara alitoa takwimu zilizokusanywa na shirika hilo zikionesha kuwa, mwaka 2008 nchi mbalimbali duniani zilisafirisha nje huduma zenye thamani ya dola za kimarekani trilioni 3.7, ambalo lilikuwa ni ongezeko la asilimia 11 kuliko mwaka 2007.

    Alisema , "Katika msukosuko wa fedha duniani, biashara ya huduma ilikumbwa na athari ndogo zaidi kuliko biashara ya bidhaa. Msukosuko huo ulipoibuka, sekta za huduma za fedha, mawasiliano na utalii ziliathiriwa vibaya, lakini sekta nyingine za huduma zimekuwa zikidumisha maendeleo yaliyowafurahisha watu katika uchumi wa nchi moja moja na biashara ya kimataifa. Uzoefu tuliopata umethibitisha kuwa, katika hali ya kudidimia kwa uchumi, sekta za huduma zinaweza kufufuka kwa haraka zaidi kuliko sekta nyingine, zaidi ya hayo kufufuka kwa sekta za huduma kutachangia ongezeko la uzalishaji mali."

    Waziri wa biashara wa China Bw. Chen Deming alieleza kukubaliana na maoni hayo. Alisema mwaka 2008 China ilisafirisha nje huduma zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 146.5, tangu mwaka 1982 thamani ya usafirishaji nje wa huduma wa China ilidumisha ongezeko la wastani la asilimia 17 kwa mwaka, na thamani ya uagizaji wa huduma kutoka nchi za nje iliongezeka kwa wastani wa asilimia 14.8 kwa mwaka. Waziri Chen Deming alisema, 

     "China itaimarisha sifa yake katika biashara ya huduma katika sekta za mawasiliano, utalii na ujenzi, China pia itajitahidi kukuza sekta za upashanaji habari, huduma za fedha, huduma zinazohusu kompyuta, uchapishaji vitabu, vyombo vya habari na huduma za kutoa ushauri. Pia itapanua wigo wa uagizaji huduma kutoka nchi za nje, na inakadiriwa kuwa, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, China itaagiza kutoka nchi za nje huduma zenye thamani zaidi ya dola za kimarekani trilioni moja. Kwa uhakika italeta nafasi kubwa kwa maendeleo ya sekta za huduma za nchi mbalimbali duniani."

    Watalaamu waliohudhuria mkutano huo pia walitoa tahadhari kuhusu mwelekeo wa kujilinda kibiashara katika biashara ya huduma duniani. Bw. Chen Deming alisema, kutokana na athari za msukosuko wa fedha, hali ya kujilinda kibiashara imeenea kwenye biashara ya huduma, ndiyo maana nchi mbalimbali duniani zinapaswa kuwa macho dhidi ya hali hiyo. Alisisitiza kuwa, China ni mtetezi imara wa biashara huria na biashara rahisi, inajikita kwenye kuanzisha mfumo wa biashara wa pande nyingi ulio wa haki na usio na ubaguzi.

    Bw. Chen Deming aliongeza kuwa, biashara ya huduma ni moja ya ajenda muhimu kati ya ajenda 8 za mazungumzo ya biashara ya raundi ya Doha, China inapenda kushirikiana na pande mbalimbali katika kusukuma mbele mazungumzo hayo, ili yapate mafanikio yenye uwiano mapema iwezekanavyo na kutimiza malengo ya maendeleo ya mazungumzo hayo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako