• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mtengeneza nywele maarufu kutoka kijijini

    (GMT+08:00) 2009-11-26 16:21:27

    Tarehe 1 Novemba ni "siku ya wafanyakazi vibarua" mjini Chongqing, China. Mioyoni mwa Wachina wengi, wakulima wako mbali na jukwaa la mitindo, lakini Bw. He Xianze kutoka mji wa Chongqing amefanikiwa kupiga hatua hiyo. Alisema,

    "Huenda wengine wanaona haiwezekani, lakini tukijitahidi tunaweza kutimiza lengo letu."

    Bw. He Xianze alizaliwa miaka 40 iliyopita katika kijiji cha Yanglu wilayani Banan mjini Chongqing, ambacho ni kijiji cha mlimani. Kuanzia utotoni mwake Bw. He Xianze alifuatana na wazazi wake kufanya kazi za mashambani na kufuga ng'ombe, wakati huo alikuwa hawezi kujua mambo ya nje ya nyumbani kwake. Lakini baada ya kuhitimu kutoka shule ya sekondari, alikuwa amejifunza mambo mengi mapya kutoka kwenye vitabu. Baadaye Bw. He Xianze alikuwa mfanyakazi wa posta wa muda. Ingawa kulikuwa na kazi nyingi na zenye kuchosha, lakini Bw. He Xianze na wazazi wake waliridhika na kazi hiyo. Alisema,

    "Kusema kweli, nina bahati zaidi kuliko wenzangu, nilipata fursa ya kuwa mfanyakazi wa posta, naona kazi hiyo ni nzuri, hivyo niliifanya kwa bidii, wakati ule niliona fahari."

    Miaka mitatu ikapita, Bw. He Xianze hakufanya makosa yoyote, viongozi na wenzake walimsifu sana. Lakini wakati huo, Bw. He Xianze alikuwa na wazo jingine. Aliona kuwa akiendelea kutuma na kupokea barua, hawezi kujiendeleza sana.

    Siku moja alikwenda kwenye saluni ya kinyozi ya rafiki yake. Alisema,

    "Niliona kuwa kila siku alikuwa anahudumia wateja 50 au 60, kila mmoja alilipa Yuan 1, lakini wakati huo mshahara wangu wa kila mwezi ulikuwa Yuan 57.5 tu, hivyo niliamua kuwa mtengeneza nywele."

    Katika vijiji vya China, zamani kazi ya kinyozi ilichukuliwa kuwa ni kazi ya kiwango cha chini. Kwa hiyo, wazazi wa Bw. He Xianze walipinga sana uamuzi huo wa Bw. He, na jamaa na marafiki zake pia walimbembeleza mara kwa mara asifanye kazi hiyo, lakini Bw. He Xianze alikuwa amefanya uamuzi, hivyo alijiuzulu kazi ya posta, na kujifunza kazi ya kinyozi na utengenezaji wa nywele kutoka kwa mwalimu mzuri kabisa wa huko wa utengenezaji nywele.

    Bw. He Xianze alipata ujuzi wa kinyozi baada ya kujifunza kwa nusu mwaka tu, baadaye alichunguza saluni za vinyozi za kijiji cha Yanghe, na akaamua kuanzisha shughuli zake mwenyewe. Baada ya kufanya juhudi, Bw. He Xianze alikopa Yuan 300 kutoka benki, na kuanzisha saluni yake ya kwanza ya kinyozi. Alisema,

    "Mteja wangu wa kwanza alikuwa mwenzangu, kwa sababu kabla ya hapo sikuwahi kukata watu nywele, nilikata kutokana na kumbukumbu niliyopata kutoka kwa mwalimu wangu akikata watu nywele, nikafanya hivyo, niliridhika na matokeo, mwenzangu pia aliridhika, na wengine walipoona walisifu, hivyo nilikuwa najiamini."

    Hatua kwa hatua Bw. He Xianze alijulikana katika kijiji chake kutokana na ufundi wake mzuri na mitindo ya kisasa ya unyoaji wa nywele. Baadhi ya wakati aliwahudumia wateja zaidi ya 100 kwa siku. Lakini Bw. He Xianze hakuridhika na mafanikio aliyopata, baada ya kufikiri kwa makini, aliuza saluni yake ya kinyozi, na kuondoka kutoka kijijini kwao kwa mara ya kwanza, na kuanza safari yake nje ya nyumbani kwake kwenye sehemu ya milimani.

    Bw. He Xianze alitembelea mikoa ya Shenzhen, Zhejiang, Fujian, Shanghai na mji wa Beijing. Ingawa aliishiwa kabisa pesa, lakini aliongeza ufahamu wake na kuimarisha imani yake. Baada ya kuja mjini Beijing, Bw. He Xianze alivutiwa na tangazo la shule ya saluni ya urembeshaji.

    Kila asubuhi Bw. He Xianze aliamka mapema, na kupanda basi kwa saa tatu kwenda shuleni. Wakati ule yalikuwa ni majira ya baridi, hakuwa na nguo nzito, alivaa nguo zake zote za majira ya joto; alipokuwa na njaa, alinunua mikate tu. Bw. He Xianze alijitahidi kujifunza kutengeneza nywele, na kiwango chake cha ufundi kiliinuka siku hadi siku, na aliipenda zaidi shughuli hiyo siku hadi siku. Siku chache baadaye alipata ajira katika saluni moja ya vinyozi mjini Beijing. Wakati wa baada ya kazi, alitumia muda wake wote na pesa zake zote katika kufanya mazoezi.

    Wenye subira wanapata mafanikio, ufundi wa utengenezaji wa nywele wa Bw. He Xianze umekubaliwa na wataalam wa kazi hiyo. Mwaka 2001, alichaguliwa na shirikisho la utengenezaji nywele la China kwenye timu ya taifa kushiriki kwenye mashindano ya kombe la Asia kwa ajili ya kushiriki kwenye mashindano ya ubingwa wa mitindo ya nywele ya kombe la dunia, na alipata matokeo mazuri. Sasa Bw. He Xianze amekuwa mwamuzi wa mashindano ya ufundi wa kazi hiyo, na mwalimu wa mashindano ya mitindo ya nywele ya taifa. Ingawa amepata heshima kubwa, lakini Bw. He Xianze ana matarajio moyoni mwake. Alisema,

    "Nataka sana kufanya juhudi ili kuifanya Chongqing iwe mji mkubwa wa kisasa wenye ufundi mwingi katika kazi ya kinyozi. Nataka kuandika ukurasa wangu mpya katika shughuli hiyo."

    Ili kutimiza matumaini yake, mwaka 2004 Bw. He Xianze aliacha ajira yenye mshahara mkubwa mjini Beijing, akarudi mjini Chongqing. Alianzisha saluni zake za vinyozi, na kutoa mafunzo bure kuhusu utengenezaji wa nywele. Watengenezaji nywele wengi wa Chongqing wakajulikana chini ya uongozi wake. Ingawa anashughulikia mambo ya kisasa kwa muda mrefu, lakini hakusahau kuwa yeye ni mtoto wa mkulima. Alisema,

    "Kwa kuwa mimi ni mtoto wa mkulima, hivyo ninafanya juhudi na kushikilia bila kulegalega ili kupata mafanikio. Nimeongeza imani na kazi yangu. Napenda usemi usemao Ukishikilia bila kuogopa taabu utapata ushindi."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako