• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mwanasarakasi Mashuhuri wa China Bibi Deng Baojin

    (GMT+08:00) 2009-11-30 16:43:19

    Bibi Deng Baojin mwenye umri wa miaka 51 amefanya maonesho ya sarakasi kwa miaka zaidi ya 30 nchini China na nchi za nje. Licha ya kuwa amepata tuzo nyingi za dhahabu katika mashindano mengi ya kimataifa na kupewa heshima ya daima ya mafanikio katika michezo ya sarakasi na serikali ya China, pia alikuwa mjumbe wa Bunge la Umma la China katika vipindi vitatu mfululizo na sasa anapewa ruzuku maalum na serikali ya China. Hivi sasa akiwa naibu mwenyekiti wa Shirikisho la Wanasarakasi la China na mkuu wa Kundi la Sarakasi la Mji wa Jinan mkoani Shandong, Bibi Deng amejikita kwenye shughuli za kuvumbua michezo ya aina mpya, kustawisha biashara ya michezo ya kundi lake akiwa na matumaini kuwa ataweza kuifanya sarakasi ambayo imekuwa na historia ndefu sana nchini China iwe ya kuvutia zaidi.

    Bibi Deng Baojin anaonekana kama amezaliwa kwa ajili ya michezo ya sarakasi. Ingawa hivi sasa amekuwa mtu wa makamo, lakini mwili wake bado ni mwembamba na wenye unyumbufu, anaweza kufanya vitendo vyote vya viungo kama zamani. Tangu ajiunge na kundi la sarakasi alipokuwa na umri wa miaka 13 mpaka sasa,ameshiriki kwenye michezo ya sarakasi kwa miongo kadhaa, na kama asingekuwa mkuu wa kundi la sarakasi huenda angeendelea kucheza jukwaani, kwa kuwa yeye anapenda sana sarakasi. Alisema,

    "Nilipokuwa nikicheza sarakasi nilikuwa mchezaji mkuu, katika muda wa miaka zaidi ya 20 iliyopita nilitembelea nchi hamsini hivi duniani, kwa hiyo msingi wangu wa michezo ya sarakasi ni imara. Napenda sarakasi, na nafasi yangu niliyocheza katika michezo inawaachia watazamaji kumbukumbu nyingi kutokana na kutafakari namna ya kucheza vizuri."

    Bibi Deng Baojin alianza kujihusisha na sarakasi kwa bahati tu. Alipokuwa mtoto alikuwa mchezaji wa jimnestiki, baadaye hakuweza kuendelea na mchezo wa jimnestiki kutokana na kupungua uwezo wa mwili wake, wakati huo kundi la wanasarakasi liliandikisha wanafunzi, na vitendo alivyofanya viliwavutia sana watahini. Lakini wazazi wake hawakukubali, walielewa kwamba akiwa mchezaji wa sarakasi ataumia mara kwa mara, lakini watahini waling'ang'nia na kuwashawishi, mwishowe wazazi wake walikubali, basi tokea hapo alipokuwa na umri wa miaka 13 amejihusisha na sarakasi maishani mwake. Bi. Deng Baojin alisema,

      "Wakati huo umri wangu ulikuwa mkubwa, mwalimu wangu aliniambia ninatakiwa nifanye juhudi mara dufu kuliko wengine, kwa hiyo kila siku nilikuwa nafanya mazoezi kwa saa kadhaa zaidi kuliko wengine, baadaye niliweza kucheza michezo zaidi ya kumi na mara nyingi nilishiriki kwenye matamasha ya michezo ya sanaa na mashindano ya taifa."

      Wachina wanasema mtu anapofanya maandalizi ya kutosha ndipo anapoweza kuwa na mafanikio, Bibi Deng Baojin alifanya hivyo. Alifanya mazoezi bila kujali uchovu, alipokuwa na umri wa miaka 18 alipata tuzo ya kwanza katika mashindano ya taifa ya michezo ya sarakasi, tokea hapo alipata tuzo mbalimbali katika mashindano. Miaka ya 80 na 90 ya karne iliyopoita ilikuwa ni kipindi ambacho maisha yake ya sarakasi yamepamba moto, na alipata tuzo kwa mfululizo katika maonesho aliyofanya nchini Uingereza, Ufaransa na Korea ya Kaskazini na nchi nyingi nyingine, na kuwa nyota mkubwa.

    Mwaka 1992 Bibi Deng Baojin alipewa tuzo ya "heshima ya daima ya mafanikio" katika michezo ya sarakasi nchini China, heshima hiyo inatokana na juhudi alizofanya kwa miaka mingi. Katika miongo kadhaa iliyopita aliyokuwa anashiriki kwenye michezo ya sarakasi aliumia mara nyingi hapa na pale, lakini anaona huo ni uchungu wenye ladha nzuri kama kahawa nyeusi. Alisema,

      "Mambo mengi yanafanikiwa kwa kutegemea nia na upendo. Niliumia kiuno, mabega na miguu mara nyingi, mpaka sasa nyonga yangu bado ina matatizo, lakini nashikilia kufanya mazoezi, nasikia maumivu, lakini ni lazima nifurahie maumivu kama watu wanapokunywa kahawa nyeusi, wengine wanaona uchungu, na wengine wanafurahia uchungu huo."

      Mwaka 2000 Bibi Deng Baojin alistaafu kutoka kwenye jukwaa la uchezaji wa sarakasi na kuwa mkuu wa Kundi la Sarakasi la Mji wa Jinan, tokea aliposhika wadhifa huo alikuwa na matumaini ya kulisukuma mbele kundi lake kwa uwezo wake. Akiwa pamoja na wachezaji wake walitunga michezo ya aina mbalimbali inayoonesha utamaduni wa China na michezo hiyo ilioneshwa katika nchi za Hispania, Marekani, Japan na iliwavutia sana watazamaji. Kutokana na kuhamasishwa na michezo waliyotunga, Bibi Deng Baojin alitunga mchezo mwingine uitwao "Opera ya Sarakasi" ambao ulichanganya sarakasi, opera ya kibeijing na dansi ya kisasa kutokana na kusaidiwa na wanamuziki, wachezaji wa dansi na wasanifu wa jukwaa la maonesho. Bibi Deng Baojin alisema,

      "Kabla ya kutunga mchezo wa 'Opera ya Sarakasi' tulifanya utafiti kwa muda mrefu, kuhusu aina gani inafaa ili mchezo uvutie watazamaji, kwanza tulitunga michezo kadhaa mifupi kwa ustadi wa baiskeli, na bembea za angani ikiwa ni kama majaribio, watazamaji wanapenda sana, kisha tukaamua kukamilisha mchezo huo wa 'Opera ya Sarakasi."

    Mchezo wa "Opera ya Sarakasi" ulianza kuoneshwa mwaka jana, mwanzoni ulioneshwa bila tikiti kwa lengo la kuwapa watazamaji fursa ya kutoa maoni yao. Ustadi mkubwa wa sarakasi na hadithi yenyewe ya opera hiyo ilisifiwa. Bibi Deng Baojin alisema katika mwaka mmoja uliopita mchezo huo ulioneshwa mara 280, na pia uliwekwa katika maonesho ya sherehe ya michezo ya Olimpiki mwaka 2008, na hivi sasa mchezo huo unatarajiwa kuoneshwa katika nchi za nje. Bi. Deng Baojin anajivunia sana kwa mafanikio ya mchezo huo.

     Bibi Deng Baojing anapenda kuimba na kucheza dansi, na sasa amejikita kwenye elimu ya uendeshaji wa biashara, anatumia kila fursa aliyonayo kujifunza elimu ya uendeshaji wa biashara na kutangaza maonesho yao, maneno anayosema mara kwa mara ni namna ya kujitangaza kibiashara. Alisema,

      "Naona ni rahisi kuwa mchezaji, lakini si rahisi kuwa mkuu wa kundi la sarakasi, kwani mkuu anatakiwa awe na akili nyepesi ya kutumia fursa inayoonekana katika soko na awe na elimu ya biashara, kwa sababu usipokuwa na elimu hiyo utakufa."

      Bibi Deng Baojin anaona kwamba hivi sasa soko la maonesho ya michezo ya sanaa linaendelea kwa kasi, kwa hiyo mageuzi ya kibiashara kwa kundi lake yanapaswa yafanyike, mafanikio daima yatakuwa kwa watu wenye ujasiri na kuthubutu kufanya majaribio.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako