• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Waislamu wa China washerehekea sikukuu ya Eid al-Haji

    (GMT+08:00) 2009-12-03 14:27:49

    Tarehe 28 ilikuwa ni sikukuu ya Eid al-Haji kwa waislamu wote duniani. Kuanzia siku hiyo, waislamu kwenye mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uyghur na mkoa unaojiendesha wa kabila la Wahui la Ningxia nchini China wamekuwa na mapumziko ya siku tano. Kwa mujibu wa mila na desturi, alfajiri ya siku hiyo waislamu wanaoga na kubadilisha nguo, halafu wanakwenda msikiti kufanya ibada. Baada ya kurejea nyumbani wanachinja kondoo kuwakarimu wageni, licha ya hayo wanasalimiana na kufanya shughuli mbalimbali za kusherehekea sikukuu.

    Eid al-Hajj ni sikukuu kubwa ya dini ya kiislamu kwa waislamu zaidi ya milioni 20 kutoka makabila ya Wahui, Wauighur, na Wakazakh nchini China. Msikiti wa mtaa wa Niujie, ambao unachukua nafasi ya kwanza kwa kuwa na waislamu wengi mjini Beijing, tarehe 28 uliandaa sherehe kubwa, ambapo waislamu zaidi ya 6,000 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo China, Malaysia, Pakistan na Misri walikwenda kwenye msikiti huo kufanya ibada.

    Mtaa wa Niujie ni eneo maarufu la makazi ya watu kutoka makabila madogo madogo mjini Beijing, na makabila hayo ni pamoja na Wahui, Waman, na Wauyghur. Kila ifikipo sikuku ya Eid al-Haji, waislamu wanaoishi kwenye mtaa huo watakusanyika msikitini kufanya ibada na sherehe ya sikukuu. Saa 3 asubuhi ya tarehe 28, Novemba mwaka huu, sherehe ilianza rasmi. Kwanza imamu alisoma kurani kwa waislamu waliopo msikitini, halafu walifanya ibada kwa pamoja. Wafanyakazi wa msikiti huo pia walichinja ng'ombe na kondoo zaidi ay 50 ili kutoa mhanga kwa Mungu.

    Kwenye mkoa unaojiendesha wa kabila la Wahui la Ningxia wenye idadi ya waislamu zaidi ya milioni mbili walisherehekea sikukuu kwa njia ya jadi. Kwa wakulima wa kijiji cha Najiahu mkoani humo, sikukuu ya Eid al-Haji ya mwaka huu ni tofauti na miaka iliyopita, kwani hii ni mara yao ya kwanza kusherehekea sikukuu hiyo katika nyumba zao mpya zilizojengwa chini ya msaada wa serikali.

    Hali mbaya ya hewa haikupunguza furaha ya wanakijiji wa Najiahu hata kidogo, alfajiri na mapema ya tarehe 28, wakivaa nguo nzuri walikusanyika kwenye msikiti wa kijiji hicho ili kufanya ibada kwa pamoja. Bw. Na Jincheng ni mmoja kati yao. Zamani familia yake waliishi pamoja na wazazi wake na familia za ndugu zake wawili katika nyumba ndogo. Mwaka huu familia hizo nne zote zilipata nyumba mpya nzuri kutokana na msaada wa serikali. Bw. Na Jincheng alichinja kondoo wawili ili kusherehekea sikukuu ya kwanza ya Eid al-Haji katika nyumba yake mpya. Alisema,

    "Nafurahi sana, kwani nimepata nyumba mpya nzuri, na jamaa na marafiki zangu wote wamekuja kunipongeza."

    Wanaume wa kijiji cha Najiahu walifanya ibada katika msikiti, ambapo wanawake walikuwa wakiandaa vyakula vya sikukuu nyumbani. Imamu kutoka kabila la Wahui Bi Ma Xueyi alisema,

    "Tunaandaa vyakula vingi zaidi mwaka hadi mwaka wakati wa Eid al-Haji. Familia zenye uwezo wa kiuchumi pia zinachinja mifugo ili kusherehekea sikukuu hiyo."

    Kwenye mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uighur wenye waislamu zaidi ya milioni 11 ambao ni wengi zaidi nchini China, waislamu waliovalia nguo za sikukuu wa sehemu mbalimbali wa mkoa huo walikusanyika mapema kwenye misikiti ili kufanya ibada ya pamoja. Habari zilizotolewa na shirika la habari la Xinhua la China zinasema, ili kusherehekea sikukuu, teksi karibu 300 za mji wa Urumchi zilijitolea kuwabeba watu bila kulipa pesa. Huko Urumuqi, mji mkuu wa mkoa huo, vyakula vya kutosha vya kiislamu vinatolewa kwenye supamaketi na masoko. Katika soko maarufu la Dabazha, waislamu wengi walikwenda kununua nguo na vyakula. Bibi Maisihan kutoka kabila la Wauyghur aliyekuwa akinunua vyakula sokoni alisema,

    "Nimenunua vitu vyote vinavyohitajika katika sikukuu. Wajukuu wangu wamepewa siku za mapumziko, na jamaa wote wa familia yangu watakutana na kula chakula kwa pamoja."

    Kutokana na kuongezeka kwa uwezo wa kiuchumi, familia nyingi za waislamu mjini Urumuqi zinakwenda kula chakula katika mikahawa ili kusherehekea sikukuu. Inakadiriwa kuwa thamani ya mauzo ya mikahawa mjini Urumuqi wakati wa Eid al-Haji ni mara tano kuliko ile katika siku za kawaida.

    Shirikisho la Dini ya Kiislamu la China siku hiyo pia liliandaa tamasha hapa Beijing kwa ajili ya mabalozi na watalaamu waislamu kutoka nchi za nje.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako