• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Nyumba ya walemavu mjini Beijing

    (GMT+08:00) 2009-12-03 14:35:24

    Kadiri China inavyoendelezwa kwa kasi, ndivyo maisha ya walemavu nchini China yanavyoboreshwa kwa kiasi kikubwa. Lakini namna ya kujiunga na jamii, na kuwasiliana na wengine, bado ni tatizo kwa walemavu wengi. Katika eneo la Xicheng mjini Beijing, kuna kituo cha utoaji huduma kwa walemavu, ambacho kinafanya juhudi ili kuwafanya walemavu waweze kujiunga na jamii zaidi.

    Siku moja mchana, katika kituo cha kuwasaidia walemavu kupona, Bw. Zhang Liqun na wenzake walifanya kazi kama kawaida. Walipowaona waandishi wa habari wa nchini na wa nchi za nje, waliimba wimbo wa "moyo uliojaa shukrani".

    Bw. Zhang Liqun mwenye umri wa miaka 22 ni mlemavu wa mtindio wa ubongo, na amefanya kazi katika kituo hicho kwa zaidi ya miaka miwili. Kazi yake ya kila siku ni kuweka seti ya sahani zilizosafishwa kwa dawa za kuua vijidudu kwenye mfuko wa plastiki unaofungwa. Kutokana na kazi hiyo, Bw. Zhang Liqun sio tu anapata mapato kila mwezi, bali pia ameimarisha uwezo wake wa kujitunza mwenyewe, kazi hiyo vilevile inamwondolea kikwazo cha kuwasiliana na wengine.

    Bw. Zhang Liqun alisema, anapenda maisha yake katika kituo cha utoaji huduma. Katika kumbukumbu zake, jambo ambalo hatalisahau ni kuzungumza na kutengeneza Jiaozi pamoja na rais Hu Jintao wa China wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008. Alisema,

    "Tarehe 20 Agosti mwaka 2008, rais Hu alikuja hapa, sote tulifurahi sana. Rais Hu na sisi tulitengeneza Jiaozi kwa pamoja."

    Kituo cha utoaji huduma kwa walemavu cha eneo la Xicheng kinatoa nafasi kadhaa za ajira kwa walemavu, walimu wa kituo hicho pia wanawafundisha walemavu hao wa mtindio wa ubongo uwezo wa kimsingi wa kumudu maisha, ili kuwasaidia waweze kujiunga na jamii kwa urahisi zaidi. Katika darasa moja lililoko kwenye ghorofa ya pili ya kituo hicho, ambalo linapambwa kama jiko, mwalimu Wu Meijuan alikuwa anawafundisha wasichana watatu walemavu wa mtindio wa ubongo kutengeneza Jiaozi. Mwalimu Wu alisema,

    "Katika miaka hiyo miwili mitatu, wamejua kutengeneza pizza, Jiaozi, kukatakata na kupika mboga, na kutengeneza vyakula vya baridi. Pia wanajifunza namna ya kutumia vyombo mbalimbali vya umeme nyumbani vya hapa, hivi sasa wamejua kutumia vyombo hivyo vya kawaida, na uwezo wao wa kujitunza wenyewe umeimarishwa."

    Kabla ya kwenda kwenye kituo hicho, mwalimu Wu alikuwa mfanyakazi wa kushona nguo. Alisema kabla ya hapo hakufahamu sana mambo ya walemavu, lakini baada ya kufanya kazi kwenye kituo hicho, aliwapenda wanafunzi hawa maalum, na anatafuta njia zinazofaa watoto hao katika mafunzo yake ya kila siku. Alisema,

    "Baadhi ya watoto hawawezi kuelewa kwa haraka, tunapaswa kuwafundisha polepole na mara nyingi. Baadaye wataweza kutengeneza wenyewe, na kazi zetu ni kuwasaidia."

    Baada ya kufanya juhudi kwa zaidi ya miaka miwili, mwalimu Wu alifurahi kuona mabadiliko mazuri yanayotokea kwa wanafunzi wake. Aligundua kuwa watoto hao wanafungua mioyo yao siku hadi siku, na kupenda maisha yao katika kituo cha utoaji huduma, pia wanapenda kuwasiliana na wenzao. Alisema,

    "Walipokuja hapa hawakuwasiliana na wengine. Baada ya kupewa mafunzo ya miaka miwili mitatu, sasa wanaishi vizuri na wengine."

    Kikiwa ni idara pekee ya utoaji huduma kwa walemavu katika eneo la Xicheng, kituo hicho kilijengwa na kuanza kutumiwa mwaka 2007, kinatoa huduma mbalimbali kwa walemavu, zikiwemo utoaji mafunzo ya ufundi, matibabu ya kuwasaidia walemavu kupunguza hali ya ulemavu, ushauri kuhusu kazi, na shughuli mbalimbali za utamaduni. Naibu mkurugenzi wa shirikisho la walemavu la sehemu ya Xicheng Bw. Guo Xin alisema, kituo cha utoaji huduma sio tu kinapaswa kutoa mafunzo ya ufundi kwa walemavu, bali pia kinapaswa kuimarisha uwezo wao wa kujitunza, ili kupunguza vikwazo kwa wao kujiunga na jamii. Bw. Guo alisema,

    "Matatizo makubwa kwa walemavu ni kuwasiliana na wengine na ufundi. Kwa hiyo utoaji mafunzo unapaswa kuwa na sehemu mbili, yaani kuwafundisha ufundi na kuimarisha uwezo wao wa kujitunza wenyewe. Kama hawana uwezo huo, hawawezi kujiunga na jamii, wala hawawezi kuwa na maisha mazuri na kuhakikisha maslahi yao ya kimsingi."

    Bw. Guo Xin alisema, hivi sasa mafunzo ya ufundi yanatolewa kwa kufuata hali ya kila mlemavu, ili kuhakikisha wanaweza kufanya kazi. Aidha, kituo cha utoaji huduma pia kinawasaidia walemavu kutafuta ajira. Alifahamisha kuwa baada ya kuhitimu mafunzo ya kompyuta, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wahandisi wa kompyuta, na kila mwezi wanaweza kupata mshahara wa Yuan zaidi ya 5,000.

    Licha ya kutoa mafunzo ya ufundi, kuwasaidia walemavu wa viungo vya mwili kupunguza hali ya ulemavu wao pia ni kazi muhimu ya kituo hicho.

    Mzee Liu Daen mwenye umri wa miaka 71 ni mgonjwa anayotibiwa na daktari Liao Zhengyi, hivi sasa kila siku anakwenda kwenye kituo hicho kupokea matabibu. Mwaka 2001 mzee Liu alikuwa amepooza nusu ya mwili wake, na maisha yake yaliathiriwa sana. Lakini baada ya kutibiwa na daktari Liu kwenye kituo hicho, anaridhika na hali yake ya sasa.

    Vifaa vizuri katika kituo hicho pia viliwapa waandishi wa habari wa nchini na wa nchi za nje kumbukumbu nzuri, na Bw. Katou Harunobu kutoka kituo cha televisheni cha NHK cha Japan pia alishangazwa na alivyoona katika kituo hicho. Alisema,

    "Vifaa vya hapa vya kuwasaidia walemavu visivyo na vikwazo ni vizuri kama vya Japan. Walemavu wanaweza kushinda matatizo yao wenyewe, kusaidiana na kufanya kazi pamoja, hayo yananipa kumbukumbu nyingi. Kituo cha utoaji huduma kwa walemavu cha eneo la Xicheng kimeonesha juhudi za China kuwasaidia walemavu. Wazo wa kujenga jamii yenye masikilizano lililotolewa na viongozi wa China linaoneshwa vizuri hapa."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako