• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Balozi Liu Guijin: Naipenda sana Afrika

    (GMT+08:00) 2009-12-04 16:56:17

    Mkutano wa nne wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika ulifanyika mwanzoni mwa mwezi Novemba huko Sham el Sheikh, Misri. Miaka 9 imepita tangu baraza hilo lianzishwe mwaka 2000, na limekuwa ni baraza muhimu linalosukuma mbele urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika, linafuatiliwa sana na pande hizo mbili na hata dunia nzima. Lakini je, ni nani alianzisha na kuandaa baraza hilo? Mwaka 2000 aliyekuwa mkuu wa idara ya Afrika katika wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Liu Guijin aliongoza wenzake kufanya maandalizi kwa makini na kuuwezesha mkutano wa kwanza wa mawaziri wa baraza hilo ufanyike kwa mafanikio mwaka huo hapa Beijing. Ofisa aliyewahi kufanya kazi pamoja na Liu Guijin kwa miaka mingi Konsela Wang Shiting ndiye anayefahamu zaidi mchango uliotolewa na Bw. Liu Guijin kwa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika. Konsela Wang Shiting alisema:

    "Mchango uliotolewa na Bw. Liu Guijin kwa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika ni mkubwa zaidi, kwa kuwa kuanzishwa kwa baraza hilo kulitokana na mapendekezo yake Bw. Liu. "

    Baada ya mkutano wa kwanza wa baraza hilo kufanyika, Bw. Liu Guijin aliendelea na juhudi zake katika kufanya uratibu na majadiliano na pande mbalimbali, na hatimaye kuthibitisha utaratibu wa baraza hilo wa kufanya mkutano kila baada ya miaka mitatu. Mwaka 2006 viongozi wa nchi zaidi ya 40 za Afrika walikuja Beijing kuhudhuria mkutano wa mwaka huo wa baraza hilo. Wakati ule Liu Guijin alikuwa balozi wa China nchini Afrika Kusini, na alirudi nyumbani akiambatana na rais wa wakati ule wa Afrika Kusini Bw. Thabo Mbeki kuhudhuria mkutano huo. Alikumbusha akisema:

    "Wakati huo rais Thabo Mbeki aliniambia kuwa 'hata mikutano ya wakuu ya Umoja wa Afrika huwa haihudhuriwi na viongozi wengi namna hii wa nchi za Afrika, lakini safari hii niliwaona baadhi ya viongozi ambao hawakuhudhuria mikutano ya wakuu ya Umoja wa Afrika kwa miaka mingi ambao wamekuja kuhudhuria mkutano wa Beijing wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika.'"

    Katika mika karibu 30 iliyopita, akiwa mwanadiplomasia Bw. Liu Guijin amekuwa anashughulikia mambo ya Afrika karibu siku zote, akisema:

    "Tangu mwaka 1981 nilipoanza kufanya kazi katika ubalozi wa China nchini Kenya mpaka sasa, sijajitoa katika kazi yangu inayohusu mambo ya Afika, sijaacha kuifuatilia Afrika, na kila siku naifuatilia na kuzingatia masuala kuhusu Afrika."

    Bw. Liu Guijin amesema ni lazima kulinda uhusiano kati ya China na Afrika kama anavyolinda macho yake mwenyewe. Alipokuwa balozi wa China nchini Afrika Kusini, thamani ya biashara kati ya China na Afrika Kusini iliongezeka kwa mara 7 hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 14 katika mwaka 2007, huku thamani ya uwekezaji kati ya nchi hizo mbili ikiongezeka maradufu. Bidii ya kazi ya Bw. Liu Guijin imewapatia wenzake kumbukumbu nyingi. Ofisa Wang Sheng wa idara ya Afrika ya wizara ya mambo ya nje ya China ni mmoja kati ya wafanyakazi hao, na anaona kuwa amejifunza mengi kutoka kwa Bw. Liu Guijin, akisema:

    "Anapofanya kazi ya kidiplomasia, anachapa kazi sana bila kulegalega. Anasema mara kwa mara kwamba kazi ya kidiplomasia ina sehemu mbili, ya kwanza ni kupata ufahamu kuhusu watu wengine, na ya pili ni kutangaza hali ya China. Naona Balozi Liu ameonesha uhodari wake katika kazi hiyo."

    Wakati Bw. Liu Guijin alipomaliza muda wake wa ubalozi nchini Afrika Kusini mwaka 2007, alikuwa ametimiza umri wa kustaafu. Lakini aliacha fursa hiyo ya kupumzika na kuishi maisha ya starehe ya uzeeni, na kukubali bila kusitasita kushika wadhifa wa mjumbe maalum wa serikali ya China anayeshughulikia mambo ya Afrika na suala la Darfur. Alisema hajutii hata kidogo uamuzi huo, akisema:

    "Nchi yangu inanitaka nibebe jukumu hili. Nimetumia maisha yangu yote katika kazi inayohusiana na Afrika, lakini naona bado naweza kufanya kazi, bado nina uwezo wa kutoa mchango wangu katika kazi inayohusiana na Afika, napenda kufanya mambo halisi kadha wa kadha kwa ajili ya kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano kati ya China na Afrika."

    Katika miaka miwili iliyofuata, Balozi Liu Guijin alitembelea sehemu ya Darfur mara 9, na kutembelea mara nyingi katika nchi za Misri, Ethiopia na Chad ambazo ni nchi jirani za Sudan, na alihudhuria mikutano ya kimataifa iliyofanyika katika sehemu mbalimbali duniani. Kila baada ya ziara yake Balozi Liu Guijin alikuwa anaitisha mkutano na waandishi wa habari kufahamisha vyombo vya habari vya nchi mbalimbali hali ya Darfur na ya nchini Sudan na kujibu lawama zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za magharibi dhidi ya China. Waafrika wanamfahamu balozi huyo maalum wa China na kumsifu sasa. Bw. Usama Mukhtar kutoka Sudan alisema:

    "Mjumbe maalum wa China Bw. Liu Guijin anaheshimiwa sana nchini Sudan, kwa kuwa yeye ni mmoja kati ya watu waliotoa mchango mkubwa kwa mchakato wa amani ya Darfur. Kama tujuavyo Sudan na China zinaendesha miradi mingi ya kiuchumi kwa ushirikiano, hii inatokana na kazi kubwa alizofanya mjumbe maalum Balozi Liu na mchango wake katika kuhimiza yatatuliwe suala la Darfur."

    Sasa Balozi Liu Guijin amekuwa na umri wa zaidi ya miaka 60, lakini bado yupo mstari wa mbele katika mambo ya kidiplomasia kuhusu Afrika. Alisema:

    "Naipenda sana Afrika, ingawa bara hili limekumbwa na majanga mbalimbali na liko nyuma kimaendeleo, lakini nina imani kubwa juu ya maendeleo ya Afrika, naamini kuwa katika siku za usoni Afrika itakuwa na sura mpya, na itapata maendeleo makubwa zaidi."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako