• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Shi Zhangyuan, Mwanamuziki Mkulima aliyetunga Nyimbo Zaidi ya 2000

    (GMT+08:00) 2009-12-07 17:08:32

    Katika wilaya ya Xiyang mkoani Shanxi, kaskazini mwa China, kuna mzee mmoja anayeitwa Shi Zhangyuan. Mzee huyo mwenye umri wa miaka 90, hafahamu namna ya kuonesha sauti kwenye mistari mitano ya kuandikia noti, kwa kuwa katika maisha yake yote anaishi vijijini, lakini kutokana na kupenda maisha na uzalendo alionao, katika muda wa miaka hamsini iliyopita ametunga nyimbo zaidi ya 2000. Katika miaka ya 50 ya karne iliyopita wimbo aliotunga unaoitwa "Furaha Yaangukia Kila Mahali" ulikuwa unaimbwa kote nchini China, na wimbo huo ulitafsiriwa kwa lugha za kigeni na kuimbwa katika nchi nyingi nyingine. Kutokana na utungaji wake mkubwa alipokelewa na viongozi wa taifa wa wakati huo mwenyekiti Mao Zedong na waziri mkuu Zhou Enlai, na Wizara ya Utamaduni ya China ilimpa sifa ya "Mwanamuziki Mkulima".

      Tarehe mosi Oktoba, Jamhuri ya Watu wa China iliposherehekea maadhimisho ya miaka 60 tangu ianzishwe, wimbo huo ulianza kuimbwa kwa mara nyingine tena kote nchini, na mtunzi wa wimbo huo mzee Shi Zhangyuan pia anafuatiliwa tena na watu. Mzee Shi Zhangyuan hakuwahi kuondoka kijijini kwake, miaka nenda miaka rudi hivi sasa amekuwa na kibyongo na matege, mzee huyo alikuwa na furaha kubwa na hata alitokwa machozi kwa kuweza kushuhudia maadhimisho ya miaka 60 tokea China mpya ianzishwe. Alisema,

    "Naweza kuishi katika zama hizi za furaha, nina bahati sana."

    Mzee huyo alisema, mwanamuziki mkulima anatakiwa kwanza awe mkulima bora, asiache ardhi yake iliyomlea. Rafiki yake wa miaka mingi ambaye pia ni mwanamuziki mzee Lu Zhongqi alisema,

    "Mzee Shi Zhangyuan ni mwanamuziki wa kijijini hasa, nyimbo zake licha ya kuimbwa kote nchini pia zinaimbwa katika nchi za nje. Ingawa amekuwa mtu mashuhuri, lakini bado yuko kama alivyokuwa zamani, hasahau alikotoka, sababu ya kuwa hivyo alivyo ni upendo wake wa maisha."

    Mandhari ya mazingira ya asili na maisha ya wenyeji wenzake, yote ni chimbuko lake la kutunga nyimbo. Mzee huyo licha ya kutunga nyimbo pia anashiriki kwenye shughuli za utamaduni kijijini, ambapo anawaongoza wenzake kuimba nyimbo baada ya kazi, ili kupata furaha na kusahau uchovu.

    Mzee Shi Zhangyuan ana watoto kumi na wawili, watu 14 wa familia yake wanaishi kwa kutegemea shamba moja dogo lisilo na rutuba. Watoto wanakula sana kwa hiyo familia yake haiwezi kuondokana na umaskini. Katika majira ya joto watu wote wanabanana wakati wa kulala katika kitanda kimoja cha udongo, joto linakuwa kali, hayo ndio mazingira aliyoishi, na nyimbo zaidi ya 2000 alizitunga katika mazingira hayo. Rafiki yake Lu Zhongqi alisema,

    "Nilimwuliza, mchana kutwa unalima kwa ajili ya kulisha watoto 12, unapataje nafasi ya kutunga nyimbo badala ya kupumzika? Aliniambia 'nafurahia'."

    Mwaka 1959 Wizara ya Utamaduni ilifanya mashindano ya waimbaji wa ridhaa, masharti ya nyimbo zilizoimbwa katika mashindano hayo yalikuwa ni lazima ya mashairi ya nyimbo yachaguliwe kutoka kwenye kitabu cha mashairi kilichoandikwa na washairi Guo More na Zhou Yang. Mzee Shi Zhangyuan alipekuapekua kitabu hicho na mwishowe alichagua shairi linaloitwa "Furaha Yaangukia Kila Mahali".

    Baada ya kuchagua maneno ya wimbo, mzee huyo alianza kutunga sauti ya wimbo wakati wote alipokuwa shambani, na baada ya kutoka kazini aliandika wimbo aliotunga na kuanza kuimbaimba, mwishowe alikamilisha wimbo huo kwa mtindo wa kuchangamsha. Alisema,

    "Nilichagua mtindo wa kuchangamsha kwa kuiga mtindo wa nyimbo za aina moja zilizoenea katika mkoa wetu."

    Baada ya kukamilisha wimbo huo, kwanza aliimba mbele ya wenyeji wa kijiji chake ili kuomba ushauri, wenyeji walisema wimbo huo ni mzuri! Baadaye aliimba wimbo huo wakati aliposhiriki katika mashindano ya waimbaji wasiolipwa mkoani, kisha wimbo huo ulitangazwa katika radio ya serikali kuu na kuchapishwa kwenye magazeti. Wakati huo watu zaidi ya milioni 400 waliimba wimbo huo na kumfahamu mzee huyo kwa kupitia matangazo ya radio.

    Miaka ya 60 ya karne iliyopita ilikuwa ni kipindi ambacho mzee huyo alitunga nyimbo nyingi kwa mfululizo zilizovutia na kuimbwa sana, na Wizara ya Utamaduni ya China ilimpa sifa ya "mwanamuziki mkulima".

    Baada ya mwaka 1960 Mzee Shi Zhangyuan alialikwa mara mbili kuhudhuria kwenye mikutano iliyofanyika mjini Beijing, ambapo alipokelewa na viongozi wa taifa, mwenyekiti Mao Zedong na waziri mkuu Zhou Enlai. Siku moja kwenye mkutano Shi Zhangyuan alijitolea kuimba wimbo mmoja aliotunga ili kuonesha furaha yake, wimbo huo unaitwa "Karibu Kijijini kwetu". Alisema,

    "Nilisimama na kusema, nimetunga wimbo mmoja hivi karibuni, na nitauimba sasa. Baada ya kuimba mara waziri mkuu Zhou Enlai alisimama na kunipigia makofi."

    Mwezi Septemba mwaka 2005 kitabu chenye mkusanyiko wa nyimbo zote alizotunga Shi Zhangyuan kilichapishwa na kuitwa "Nyimbo Mpya za Wakulima". Kitabu hicho kimekusanya nyimbo zake zaidi ya elfu mbili alizotunga chini ya kibatari, mzee huyo ametimiza tumaini lake alilokuwa nalo miaka yote.

    Katika miaka kadhaa iliyopita, maonesho ya uimbaji wa nyimbo za mzee Shi Zhangyuan yalifanyika mjini Shanghai na mzee huyo alilipwa Yuan laki moja ambapo hakuwahi kuona donge nono la fedha kama hilo maishani mwake, lakini siku ya pili alichangia fedha hizo kwenye mradi wa kujenga shule moja ya msingi, na yeye anaendelea kuishi katika hali ya kawaida. Mzee huyo kila alipoulizwa kama ana matumaini yoyote maishani mwake, alijibu bila kusita kwamba matumaini yake ni kuwa maonesho ya uimbaji wa nyimbo zake yatafanyika tena wakati bado yuko hai.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako