• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • He Liehui: Balozi anayehimiza mawasiliano kati ya Wachina na Waafrika

    (GMT+08:00) 2009-12-11 15:20:09

    Bw. He Liehui ni mfanyabiashara wa China nchini Nigeria. Katika miaka kadhaa iliyopita, alitumia mamilioni ya pesa kuandaa makongamano mbalimbali yaliyoshirikisha makampuni ya China na makampuni ya Afrika, ili makampuni hayo yakae pamoja na kutafuta fursa za biashara, pia anafanya juhudi kwa moyo wote katika kusukuma mbele maendeleo ya uchumi na biashara ya Nigeria.

    .

    Bw. He Liehui alihitimu masomo kwenye Chuo Kikuu cha Mambo ya Bahari cha Shanghai mwaka 1999, na mwaka huo huo alipata ajira kwenye mahakama ya sehemu moja nchini China. Kutokana na mvuto wa kazi ya baba yake, ambaye alikuwa anafanya biashara nchini Botswana, mwaka 2000 Bw. He Liehui alijiuzulu nafasi yake na kuamua kwenda Afrika kumsaidia baba yake. Alisema:

    "Nilipohitimu masomo katika chuo kikuu baba yangu alinitaka niende Afrika kumsaidia, kwa kuwa hajui Kiingereza na mdogo wangu mvulana aliyekwenda na baba yangu pia hajui sana Kiingereza. Kutokana na shinikizo kutoka kwao, nilijiuzulu kazi yangu kwenye mahakama, na kwenda Afrika kumsaidia baba yangu."

    Lakini kutokana na sababu ya viza, badala ya kwenda Botswana alifika nchini Nigeria na kuanzisha kampuni ya Touchroad nchini humo, ambayo biashara yake kuu ni ya nguo. Katika siku za awali alitembeza bidhaa zake mwenyewe kutoka duka moja hadi lingine kwenye soko la Nigeria, ambapo karibu wafanyabiashara wenyeji wote sokoni walimfahamu mchina huyo mchapa kazi. Kutokana na msaada wa wafanyabiashara wenyeji na juhudi zake mwenyewe, kampuni ya Touchroad ilipata maendeleo ya kasi. Lakini wakati huohuo jambo moja lilitokea bila kutarajia.

    Asubuhi ya siku moja ya mwaka 2001 Bw. He Liehui alipata oda yenye thamani ya dola za kimarekani laki 7, hata mpaka sasa bado anakumbuka jinsi alivyofurahi kuhusu biashara hiyo. Lakini baadaye mteja huyo alisema kitambaa kinachotumiwa kushonea nguo hizo kina tatizo na alianza kudai fidia. Kutokana na sababu mbalimbali, Bw. He Lihui aliona kuwa kuna uwezekano kwamba sifa ya kitambaa hicho ina tatizo, kwa hiyo alibeba wajibu huo. Baada ya mazungumzo Bw. He Liehui aikubali kutoa fidia ya dola za kimarekani laki 2. Lakini hakuweza kukusanya pesa nyingi namna hii kwa mara moja, kwa hiyo walikubaliana kwamba fidia hiyo itolewe hatua kwa hatua katika biashara zilizofuata. Kutokana na udhati wake, alipata nafasi ya kufanya ushirikiano wa muda mrefu na mteja huyo, na mteja huyo pia aliwafahamisha wateja wengine wengi kuhusu mfanyabiashara huyo mchina anayeaminika.

    Kuishi nchini Nigeria kwa muda mrefu na kuwa na marafiki wengi nchini humo, kumemfanya Bw. He Liehui awe na hisia maalum kuhusu nchi hiyo, na kuichukulia kama ni nyumbani kwake. Alianza kufikiri namna ya kuwa daraja kati ya makampuni ya China na ya Afrika ili kutafuta fursa za biashara kwa ajili yao. Alisema:

    "Mwaka 2000 niliwaalika maofisa wa ubalozi wa Ghana nchini China kutembelea viwanda vilivyo kwenye maskani yangu, ambapo kila sehemu mimi na marafiki zangu waafrika wanne watano tulipokwenda, ilijaa watu wengi, kwa kuwa hapo awali kulikuwa hakuna mwafrika yeyote aliyetembelea maskani yangu. Mwaka huo huo nilipofika Nigeria, wenyeji waliniangalia kama walivyoangalia wanyama adimu, hii ilimaanisha kwamba mawasiliano kati ya China na Afrika yalikuwa machache sana."

    Bw. He Liehui anaamini kwamba China inaweza kuisaidia Afrika kwa uzoefu wake wa kujiendeleza, kwa hivyo mwaka 2008 Bw. He Liehui alitumia yuan za Renminbi zaidi ya milioni moja kuanzisha Kongamano la Uwekezaji kati ya China na Afrika, na kuandaa mkutano wa kwanza mwaka huo. Kongamano hilo lililotoa fursa kwa makampuni ya China na ya Afrika kuwasiliana na kujadili kuhusu biashara, na lilifuatiliwa sana na serikali na makampuni ya nchi nyingi za Afrika, ambapo mashirika ya kimataifa na na makampuni 18 yalishiriki kwenye mkutano wa kwanza wa kongamano hilo. Ofisa wa ofisi ya Benki ya Maendeleo ya Afrika nchini Burundi Bw. Mabuga amesema, kutokana na kongamano hilo, ameongeza ufahamu wake kuhusu China uliongezeka. Alisema:

    "Urafiki kati ya China na Afrika ni wa muda mrefu, maendeleo ya uchumi wa pande hizo mbili yamesukuma mbele maendeleo ya urafiki kati ya pande hizo. Katika miaka ya hivi karibuni uwekezaji wa China barani Afrika katika miundo mbinu na shughuli nyingine mbalimbali umesukuma mbele maendeleo ya huko."

    Wakati mkutano wa pili wa Kongamamo la Uwekezaji kati ya China na Afrika ulipofanyika mwaka 2009, ujumbe wa nchi zaidi ya 40 za Afrika, wajumbe wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Umoja wa Nchi za Kiarabu, mashirika mengine ya kimataifa, na wajasiriamali zaidi ya 500 walikuja China kuhudhuria mkutano huo, na hii iliimarisha nia ya Bw. He Liehui ya kuhimiza mawasiliano kati ya watu wa China na Afrika.

    Baada ya hapo Bw. He Liehui aliyaalika makampuni mengi zaidi ya China na Afrika kutembeleana. Kutokana na juhudi zake, katika miaka kadhaa iliyopita waafrika zaidi ya 700 na makampuni zaidi ya 200 ya Afrika yamefanya ziara nchini China, wakiwemo mamia ya wajasiriamali kutoka Nigeria, huku idadi ya wafanyabiashara wachina waliotembelea Afrika ikiendelea kuongezeka.

    Bw. He Liehui anaona kuwa maendeleo ya kampuni yake yanategemea sera za nchi, mazingira ya jumla ya ushirikiano kati ya China na Afrika, na uungaji mkono wa marafiki zake waafrika wa hali mbalimbali, ndiyo sababu atabeba wajibu mwingi zaidi wa kijamii bila kusitasita. Alisema:

    "Tangu safari yangu ya kwanza barani Afrika, nimetembelea nchi zaidi ya 20 barani humo, ambapo niliaminiwa na kutambuliwa na serikali za nchi hizo. Kama watu wa nchi hizo wakija nchini China nitawasaida pia kujenga uhusiano na makampuni na serikali ya China."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako