• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Urithi wa Utamaduni Usioonekana wa China"-Opera ya Su

    (GMT+08:00) 2009-12-21 17:09:52

      

    Opera ya Su ni mchezo wa sanaa unaoenea katika mikoa ya Jiangsu na Zhejiang, katika sehemu ya kusini mwa Mto Changjiang nchini China. Mwaka 1941 Kundi la Opera ya Su ya Guofeng ambalo ni la kwanza kabisa la opera hiyo, liliundwa katika mji wa Shanghai, hii ilikuwa na maana ya kuanza rasmi kwa opera hiyo nchini China. Muziki unaotumika katika opera hiyo ni mchanganyiko wa muziki wa aina kadhaa ambao umeenea katika sehemu ay kusini mwa Mto Changjiang nchini China, na ala ya muziki inayotumika zaidi ni erhu, kinanda cha muziki huo kinapigwa kwa upinde na michezo inayojulikana sana ya opera hiyo ni "Mlevi akirudi Nyumbani" na "Kumsindikiza mtoto anayekwenda Safari". Kutokana na juhudi za watu wa vizazi viwili, sasa opera hiyo imepata maendeleo makubwa.

      Mliyosikia ni sauti ya Bi. Wang Fang akiimba katika mchezo wa opera ya Su inayoitwa "Mlevi akirudi Nyumbani", kutokana na uhodari wake katika uchezaji wake Bibi huyo amepata tuzo ya kwanza katika mashindano ya opera nchini China. Lakini ustadi wake kwenye uchezaji asingeupata bila msaada kutoka kwa mwalimu wake Bibi Jiang Yufang ambaye anasifiwa kuwa ni msanii wa kwanza wa opera ya Su. Katika mchezo unaoitwa "Mlevi akirudi Nyumbani" aliigiza kama msomi mmoja mwanaume. Ingawa yeye anajulikana kwa uhodari wa kuigiza wahusika wanaume, lakini pia ni hodari wa kuwaigiza wahusika wanawake. Bi. Wang Fang alisema,

      "Sijui nimwelezee vipi, maana anaimba vizuri sana na sauti yake inavutia kweli kweli, uigizaji wake unalingana sana na hali ilivyokuwa ya mhusika katika mchezo na hadi sasa hakuna mtu anayeweza kufikia kiwango chake cha uigizaji. Nilipokuwa mwanafunzi wake alinieleza tena na tena jinsi mchezo wa 'Mlevi akirudi Nyumbani' ulivyo, ili niweze kuigiza kwa hisia za ndani."

      Bibi Jiang Yufang ni msanii wa opera ya Su wa kizazi cha kwanza. alianza kujifunza opera hiyo alipokuwa na umri wa miaka 12 huku akifundishwa na mwalimu wake Yin Zhongqiu. Wakati huo opera ya Su ilikuwa bado haijulikani rasmi katika jamii bali ilikuwa ni usanii wa Sutan wa kusimulia hadithi kwa kuimba huku wasanii kadhaa wakiwa wamekaa, baadaye kutokana na juhudi za Bibi Jiang Yufang na wenzake usanii huo wa Sutan ukageuzwa na kuwa "Opera ya Su".

      Kwa kuwa jamii iliendelea na uwezo wa watazamaji kupima uwezo wa wasanii uliongezeka, Bibi Jiang Yufang alichemsha bongo ili kuifanyia mageuzi opera hiyo na kuifanya iwe ni opera inayochezwa kwa kuimba huku wasanii wakifanya vitendo mbalimbali badala ya kukaa tu. Wazo hilo liliungwa mkono na wasanii wenzake. Msanii mzee mwenye umri wa miaka 89 Bi. Yin Simin alipokumbuka hali ilivyokuwa wakati huo alisema,

    "Kabla ya hapo tulifanya maonesho kwa kukaa tu bila kufanya vitendo vyovyote, sasa tumeingiza vitendo ili kueleza jinsi wahusika walivyo."

    Baadaye Bibi Jiang Yufang alichanganya muziki wa aina mbalimbali ulioenea katika sehemu ya kusini mwa Mto Changjiang nchini China na kuifanya opera hiyo iwe ya aina ya kipekee nchini China. Bibi Jiang Yufang alitumia muziki tofauti ili kufanya maonesho vizuri kuhusu wahusika wa aina tofauti, ingawa hakusomea kutunga muziki lakini muziki aliotunga unafaa kuonesha vizuri jinsi wahusika walivyo, na hii ndio sababu ya kupewa sifa nyingine ya "Mtunzi wa Muziki".

      Bi. Wang Fang akiwa ni mwanafunzi hodari wa bibi Jiang Yufang, Bi Wang anamsifu na kumheshimu sana jinsi mwalimu Jiang alivyokuwa mwalimu mzuri. Alisema Bibi Jiang Yufang alimtendea kama ndugu yake, licha ya kumfundisha usanii pia alimfundisha maadili ambayo waigizaji wanapaswa kuwa nayo. Alisema,

    "Nilipojiunga na kundi hilo tayari alikuwa msanii mashuhuri, akiwa na wenzake walioweka msingi wa kundi letu, tulikuwa tunawaheshimu sana kama wazee wetu."

      Katika jumba la maonesho ya opera mjini Suzhou, kuna picha moja ambayo watu wengi akiwemo Bibi Jiang walipigwa pamoja na waziri mkuu Zhou Enlai, hii ni picha iliyopigwa mwezi Aprili mwaka 1959. Bibi Jiang Yufang alisema, "Picha hiyo ni fahari ya Opera ya Su, na inastahili kukumbukwa katika historia ya Opera ya Su!"

      Mwezi Januari mwaka 2008 Mzee Jiang Yufang alifariki akiwa na umri wa miaka 87, kwenye ukumbi wa kutoa heshima za mwisho hakukupigwa muziki wa maombolezo bali ni wimbo alioimba katika opera ya Su. Wang Fang alisema, "Niliposikia sauti yake nilihisi kama vile yeye bado yuko nami."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako