• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Makazi ya ukoo wa Lu mjini Dongyang

    (GMT+08:00) 2009-12-21 17:07:53

    Mkoa wa Zhejiang ulioko sehemu ya mashariki ya China una nyumba nyingi za kale za wakazi zenye mandhari nzuri ya bustani. Miongoni mwa nyumba hizo, nyumba za makazi ya ukoo wa Lu zilizoko mjini Dongyang, ni za kipekee kati ya majengo ya kale yaliyoko kwenye sehemu ya kusini ya China kutokana na hali yake ya kifahari na kupambwa vizuri, nyumba hizo zimekusanya uzuri wa majengo ya miaka elfu moja iliyopita.

    Nyumba za ukoo wa Lu ni mahali wanapokaa kwa wingi watu wa ukoo huo, majengo yaliyojengwa katika enzi za Ming na Qing kwenye sehemu ya kusini ya China yamehifadhiwa vizuri, mwaka 1988 majengo hayo yaliwekwa kwenye orodha ya tatu ya vitu muhimu vya kiutamaduni vinavyohifadhiwa kitaifa. Juni mwaka 2008, ufundi wa ujenzi wa majengo ya nyumba za makazi ya ukoo wa Lu uliwekwa kwenye orodha ya pili ya urithi wa utamaduni usio wa vitu. Naibu mkuu wa ofisi ya hifadhi na usimamizi wa nyumba za ukoo wa Lu Bw Wu Xinlei alisema "Vijiji vingine havina majengo makubwa kama hayo, tena vichochoro vyake ni vyembamba sana. Kwa sababu watu wa ukoo huo mkubwa walikuwa na fedha nyingi sana, hivyo walijali sana hali ya ufahari. Nyumba za makazi za ukoo wa Lu zilitumiwa na jeshi la kimwinyi kama ngome, na nyumba nyingi ziliteketezwa."

    Nyumba za Ukoo wa Lu ziko kwenye sehemu ya mashariki ya mji wa Dongyang zikiwa eneo karibu hekta mbili, na ni kundi la majengo yenye mtindo wa enzi za Ming na Qing. Kitabu cha ukoo wa Lu kinaonesha kuwa, katika enzi za Ming na Qing, watu wengi wa ukoo huu walikuwa maofisa wenye vyeo vya juu, na ukoo huo ulikuwa ukoo mashuhuri wenye heshima.

    Kutokana na ustawi wa ukoo huu, majengo ya nyumba za ukoo wa Lu ni tofauti na nyumba za wakazi wa kawaida wa sehemu ya kusini ya China, nyumba hizo zilijengwa kwa mfano wa majumba ya maofisa wakubwa, baadhi ya watu waliziita nyumba hizo kuwa ni "jumba la mfalme la kienyeji". Kwa sababu nyumba za ukoo wa Lu ni sawa na jumba la mfalme wa zamani, nyumba za zilizojengwa kwenye sehemu ya kati zinapangana kwenye mstari, na nyumba zilizojengwa kwenye pande mbili ya mstari wa katikati zinalingana kabisa, hata mpango wa makazi unafanana na ule wa kasri la zamani la mfalme, nyumba zilizoko sehemu ya mbele ni kumbi za kufanya shughuli mbalimbali, na nyumba zilizoko sehemu ya nyuma ni kwa ajili ya kulala. Kwenye sehemu ya mbele kuna ukumbi mmoja, ambao ulitumiwa na watu wa ukoo huu kufanya matambiko, kujumuika, kufanya mazungumzo, kutoa mafunzo na kwa mambo ya burudani. Nyumba ya sehemu ya nyuma ni nyumba za kuishi wake na watoto wao pamoja na watumishi, kuna mlango mmoja wa mawe kati ya sehemu za mbele na nyuma, na mlango huu hufungwa katika nyakati za kawaida, na watu wa nje hawaruhusiwi kuigia. Katika nyumba za ukoo wa Lu kuna nyua 9 zilizojengwa kutoka sehemu ya mbele hadi sehemu ya nyuma kwenye urefu wa mita 320, na hakuna nyumba nyingine zilizojengwa kwa mpango kama huu isipokuwa majumba ya zamani ya mfalme na hekalu la Confucius.

    Baada ya kuingia kwenye nyumba za makazi ya ukoo wa Lu, mlango wa kwanza unaitwa mlango wa kuleta habari nzuri, mtu akisimama na kutizama upande wa nyuma yake, anaweza kuona mlima kwa mbali, ambao unafanana sana na chombo cha kuwekea kalamu. Mfanyakazi wa ofisi ya uhifadhi wa vitu vya kiutamaduni kwenye makazi ya ukoo wa Lu, Fu Minfang alisema "Kivutio kikubwa cha nyumba za makazi ya Lu ni kuhusu utamaduni wa majengo, elimu na sanaa ya ufundi, ambao unawakilisha utamaduni wa sehemu ya kati ya mkoa wa Zhejiang. Kitu kingine muhimu ni desturi ya jadi ya wachina ya kuchagua mahali pa kujenga, mkabala wa makazi ya ukoo wa Lu kuna mlima wa chombo cha kuwekea kalamu, watu wanaamini kuwa "kama nje ya nyumba kuna mlima wa chombo cha kuwekea kalamu, basi wanajitokeza maofisa wakubwa kizazi hadi kizazi".

    Inasemekana kuwa wakati ule mzee wa ukoo wa Lu aliamua kujenga nyumba yao kule kutokana na kuweko kwa mlima unaofanana na chombo cha kuwekea kalamu, kwa kujaliwa na kulindwa na mungu wa mlima, walijitokeza maofisa wakubwa na wasomi wengi katika vizazi ya ukoo wa Lu.

    Mlango wa pili kwenye nyumba za Lu ni mlango wa heshima, ambao ni mahali pa kuwalaki na kuagana na wageni. Mlango mkuu wa sehemu ya kati ni mlango wa jemadari, zamani za kale mlango huu ulikuwa unafungwa daima isipokuwa katika wakati usio wa kawaida. Wageni wanapotembelea huko waliingia kwenye mlango wa mashariki na kutokea kwenye mlango wa magharibi, isipokuwa wakati muhimu kama ofisa mwenye cheo cha juu anapofika, mlango mkuu unafunguliwa kwa kuonesha heshima. Baada ya kuingia kwenye mlango huu kuna ua mmoja wenye eneo la kiasi cha mita za mraba 400, chini vilevile yalitandikwa mawe ya mango, na kwenye kona moja kuna ujia wenye upana wa mita 2 unaozunguka, ambao unaenda katika ukumbi wa Xiaoyong ulioko upande wa kaskazini.

    Mtu akifika kwenye nyumba za ukoo wa Lu, asikose kufika kwenye ukumbi Xiaoyong, kwa kuwa jengo hilo lililoko katikati ni jengo kuu la nyumba zilizoko kwenye makazi hayo. Taa moja ya jadi iliyotundikwa kwenye ukumbi huu ni maridadi na ya kuvutia sana, katikati kuna taa tatu zilizounganishwa kutoka juu hadi chini, pamoja na taa ndogo 24 zilizotundikwa kwenye minyororo 6 iliyoko kwenye sehemu za nje za taa ile kubwa ya katikati. Taa hiyo nzima ina kimo cha mita 4.5 na uzito wa kilo 127.

    Mbali na ukumbi wa Xiaoyong kuna nyumba nyingi kwenye eneo hilo. Iwe kwa eneo au vyombo vilivyoko ndani ya nyumba, ukumbi wa Xiaoyong unachukua nafasi ya kwanza miongoni mwa nyumba za makazi za nchini China.

    Ikilinganishwa na ukubwa wa kundi la nyumba za ukoo wa Dong mkoani Yunnan na nyumba ya ukoo wa Qiao mkoani Shanxi, nyumba zakani ya ukoo wa Lu bado ni ndogo sana. Lakini nyumba hizo zikilinganishwa kwa ufundi wa ujenzi wa nyumba na mapambo ya nyumba, nyumba za ukoo wa Lu zinatia fora kabisa. Naibu mkuu wa ofisi ya hifadhi ya mabaki ya kiutamaduni ya nyumba za makazi ya ukoo wa Lu Bw Wu Xinlei alisema, "Toka zamani za kale mji wa Dongyang unasifiwa kuwa na mafundi hodari wa kila aina, nyumba za ukoo wa Lu zilitumia ufundi wa uchongaji wa mbao kwenye nguzo na majengo mengine ya nyumba pamoja na ufundi wa ufinyanzi na uchoraji michoro ya rangi."

    Tukichukulia majengo kama mfano wa mchoro, nyumba za ukoo wa Lu ni kama mchoro uliochorwa kwa makini sana. Ingawa nyumba za ukoo wa Lu ni makazi ya ofisa wa serikali mwenye cheo cha juu, lakini vigae vya kuezekea mapaa vyenye rangi ya kijivu iliyokolea na njia za mawe ya mango kwenye nyumba hizo, ni vitu vilivyo karibu sana kwenye maisha ya watu wa kawaida na vinaonekana ni vya kudumu. Mtalii kutoka Shanghai Bw Li Herong alisema, "Nyumba zinapendeza sana, maboriti yalichongwa nakshi na kuchorwa michoro ya rangi, ni nzuri sana."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako